KOMUNYOPAMBA
(VIATIKO)

Generic placeholder image
Kumunyopamba
(VIATIKO):

Kila inapowezekana Padri amwungamishe mgonjwa kabla ya kutoa Komunyopamba. Kama mgonjwa haungami, tendo la toba laweza kufanywa wakati wa kutoa Komunyopamba, kama ilivyo katika kanuni ya Misa.

MWANZO WA ADHIMISHO
P. Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu:
W. Amina.

Padri anamsalimu mgonjwa kirafiki. Anaweza kutumia salamu hii:
Amani kwa nyumba hii, na kwa wote wanaokaa humu.

Halafu, anamnyunyizia mgonjwa na chumba maji ya baraka, akisema:
Maji haya yatukumbushe Ubatizo wetu katika Kristo, aliyetukomboa kwa kifo na ufufuko wake.

Kisha anaweka Hostia takatifu juu ya meza na wote wanaiabudu.
Baada ya hayo, Padri anaweza kutumia maneno yafuatayo au mengine yanayofaa kadiri ya hali ya mgonjwa.

Ndugu zangu, Bwana Yesu Kristo, kabla ya kuihama dunia hii na kwenda kwa Baba, alituachia Sakramenti ya Mwili na Damu yake ili, saa ya kuhama kwetu toka maisha haya kwenda kwake, baada ya kupewa nguvu katika Komunyopamba ya Mwili na Damu yake, tulindwe kwa amana ya ufufuko. Tumwombee ndugu (dada) yetu tunayeunganika naye katika upendo.

Tendo la toba
Iwapo mgonjwa hakuungama mwanzoni, Padri anawaalika mgonjwa na wale waliopo washiriki tendo la toba:
Ndugu zangu, tukiri dhambi zetu, ili tupate kustahilishwa kuadhimisha mafumbo matakatifu.
Husubiri kidogo
Namwungamia Mungu mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo, na kwa kutotimiza wajibu: nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana namwomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.

Padri anaendelea:
Mungu mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele.
W. Amina.

Rehema kamili
Sakramenti ya Kitubio au Tendo la toba huweza kumalizika kwa rehema kamili ambayo Padri anaweza kutoa kwa watu wanaoingia katika hatari ya kufa.

Au (1)
Mimi, kwa mamlaka niliyopewa na Baba Mtakatifu, ninakupa rehema kamili na maondoleo ya dhambi zako zote, kwa jina la Baba, na la Mwana + na la Roho Mtakatifu.
W. Amina.

Au (2)
Kwa njia ya mafumbo matakatifu sana ya fidia ya binadamu, Mungu Mwenyezi akuondolee adhabu zote za maisha ya sasa, yajayo, na akufungulie malango ya paradiso.
W. Amina.

Neno la Mungu
Yafaa sana, Padri au mmojawapo waliopo asome walau somo fupi lifuatalo:
SOMO: Yn.6:54-59

Yesu alisema: "Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufufa siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele. Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu".

Ungamo la Imani na Litania
Ni jambo la kufaa kama mgonjwa anatoa ungamo la imani yake. ya Ubatizo kabla hajapokea Komunyopamba. Padri anaweza kumpa mgonjwa maelezo mafupi kabla ya kumuuliza maswali yafuatayo:
Je, unasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, Muumba mbingu na dunia?
Mgonjwa anajibu: Ninasadiki.

Je, unasadiki kwa Yesu Kristo, Mwanae pekee, Bwana wetu, aliyezaliwa na Bikira Maria, akateswa, akafa, akazikwa, akafufuka katika wafu, amekaa kuume kwa Baba?
Mgonjwa anajibu: Ninasadiki.

Je, unasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu Katoliki, Ushirika wa watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa mwili na uzima wa milele?
Mgonjwa anajibu: Ninasadiki.

Iwapo hali ya mgonjwa inaruhusu, Litania fupi yaweza kusemwa. Mgonjwa akiweza anaitikia pamoja na watu waliopo.
Ndugu zangu, kwa moyo mmoja tumwombe Bwana Yesu Kristo. Kwa ajili ya ndugu (dada) yetu, tunakuomba wewe, Bwana, uliyetupenda sisi mpaka mwisho na ukajitoa mwenyewe kufa ili utujalie sisi uzima.
W. Ee Bwana utusikie.

Kwa ajili ya ndugu (dada) yetu, tunakuomba, wewe Bwana, uliyesema: aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu ana uzima wa milele.
W. Ee Bwana utusikie.

Wewe ee Bwana, unatualika sisi kwenye karamu ile ambako hakutakuwa tena na mateso wala majonzi, wala huzuni, wala mtengano. Tunakuomba kwa ajili ya ndugu (dada) yetu.
W. Ee Bwana utusikie.

KOMUNYOPAMBA (VIATIKO)
Padri anawaalika wote kwa maneno kama haya:
Na sasa tumwombe Mungu kwa pamoja kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyotufundisha kusali.

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

Padri anamwonesha mgonjwa Hostia takatifu akisema:
Tazama, Mwanakondoo wa Mungu,
tazama, aondoaye dhambi za ulimwengu.
Heri yao walioalikwa kwenye karamu ya Mwanakondoo.

Mgonjwa akiweza, anasema pamoja na wale waliopo:
Ee Bwana, sistahili uingie kwangu,
lakini sema neno tu, na roho yangu itapona.

Padri anamkomunisha mgonjwa, akisema:
Mwili wa Kristo
Mgonjwa anajibu: Amina.

Hapo Padri anaendelea kusema:
Yesu mwenyewe akulinde na kukufikisha katika uzima wa milele.
W. Amina.

MWISHO WA ADHIMISHO
Padri anamalizia kwa sala ifuatayo:
Tuombe.
Ee Mungu, Mwana wako ni Njia yetu, Ukweli na Uzima, umtazame kwa upole mtumishi wako F. na umjalie aufikie Ufalme wako katika amani, kwa amani, kwa maana amejikabidhi kwa ahadi zako na ameburudishwa kwa Mwili na Damu ya Mwana wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

Mwisho, Padri anatoa baraka, na wote waliopo wanaweza kumtakia mgonjwa amani.
Awabariki Mungu Mwenyezi, Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu. W. Amina.