KOMUNYO YA WAGONJWA
Kumunyo ya Wagonjwa
Chumba cha mgonjwa kiwe safi. Iwekwe meza au sanduku
lililofunikwa kwa kitambaa safi cheupe cha kuwekea Sakramenti.
Maji ya baraka yakitumiwa, pawepo na chombo, mrashi au kitawi
kidogo. Ni vema pia kuwasha mishumaa miwili.
P: Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu:
W: Amina.
Kusalimu
Padri anamsalimu mgonjwa na wote waliopo kwa kufuata mazingira:
Amani kwa nyumba hii na kwa wote wanaokaa humu.
Halafu, anamnyunyizia mgonjwa na chumba maji ya baraka,
akisema:
P: Maji haya yawe ukumbusho wa Ubatizo uliopokelewa na yawe ukumbusho
wa Kristo aliyetukomboa sisi kwa Mateso na Ufufuko wake.
Kisha anaweka Hostia takatifu juu ya meza na wote wanaiabudu.
Majuto
Tendo la toba linafanyika kama ilivyo katika kanuni ya Misa.
P: Ndugu zangu, tukiri dhambi zetu, ili tupate kustahilishwa kuadhimisha
mafumbo matakatifu.
Husubiri kidogo. Kisha wanasema pamoja:
Namwungamia Mungu mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno kwa mawazo, kwa maneno, kwa
matendo, na kwa kutotimiza wajibu: nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana
namwomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi, ndugu zangu, niombeeni
kwa Bwana Mungu wetu.
P: Mungu mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye
uzima wa milele.
W: Amina.
Sala ya Bwana
P: Kwa kulitii agizo la Mwokozi wetu, na tukifuata
mafundisho yake ya kimungu, tunathubutu kusema:
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe;
ufalme wako ufike;
utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.
Usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni.
Amina.
Sehemu ya maandiko matakatifu yaweza kusomwa na Padri au mtu mwingine.
MASOMO YA BIBLIA
1: Mt.11:25-30
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Wakati ule Yesu alijibu akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya
uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyo kupendeza mbele zako. Akasema, nimekabidhiwa vyote na Baba yangu;
wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda
kumfunulia.
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu,
mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa
maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo.
2: Mt.25:31-40
Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye,
ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye
atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa
kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.
Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni mliobarikiwa na Baba yangu, urithini
ufalme, mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa
na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja
kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.
Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu
tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena
tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri
mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo.
3: Mk.16:15-20
Wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Marko.
Yesu akawaambia wafuasi wake, Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye
na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina
langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha,
hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu.
Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno
kwa ishara zilizofuatana nalo.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo
4: Lk.10:5-6,8-9
Wapozeni wagonjwa
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Luka.
Na nyumba yoyote mtakoyoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani,
amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha,
vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu
umewakaribia.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo.
5: Lk.10:25-37
Ni nani aliyekuwa jirani?
Somo la Injili Takatifu ilvyoandikwa na Luka.
Na tazama, mwanasheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi
uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende
Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili
zako zote; zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.
Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema,
Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang'anyi; wakamvua nguo,
wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia
ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando.
Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia
akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka
nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni,
akisema, Mtunze huyu, na chochote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.
Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia katika wanyanganyi?
Akasema ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo.
6: Lk.11:5-10
Nami nawaambia, ombeni nanyi mtapewa; kwa kuwa kila aombaye hupokea.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Luka.
Akawaambia, ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu,
nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha
kuweka mbele yake; na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe mlango umekwisha fungwa, nasi
tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe? Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa
haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa
kadiri ya haja yake.
Nami nawaambia, ombeni nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa
kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo.
KOMUNYO
Kisha Padri anamwonesha mgonjwa Hostia takatifu, akisema:
Tazama, Mwanakondoo wa Mungu,
tazama, aondoaye dhambi za ulimwengu.
Heri yao walioalikwa kwenye karamu ya Mwanakondoo.
Mgonjwa na wale waliopo wanasema mara moja:
Ee Bwana, sistahili uingie kwangu,
lakini sema neno tu, na roho yangu itapona.
Hapo Padri anamwendea mgonjwa, anamwonesha Hostia takatifu anayoishika
mkononi ameinua juu kidogo, akisema:
Mwili wa Kristo
Mgonjwa anajibu: Amina.
na kupokea Komunyo. Halafu wengine wanaotaka wanapokea
Komunyo kama kawaida.
Sala ya kumalizia
Baada ya kusafisha vyombo, Padri anasema sala.
Tuombe. Ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu
Mwenyezi wa milele, tunakuomba kwa imani, ili Mwili
mtakatifu sana (na Damu takatifu sana) ya Bwana wetu
Yesu Kristo, Mwanao, aliopokea ndugu yetu (dada)
umfae kwa mwili na roho kuufikia uzima wa milele.
Tunaomba hayo kwa imani na kwa jina la Yesu Kristo,
anayeishi na kutawala pamoja nawe milele na milele.
W: Amina.
Baraka
Kisha Padri anambariki mgonjwa na hao waliopo, kama
kawaida:
Awabariki Mungu mwenyezi, Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W: Amina.