KUSIMIKA MSALABA KABURINI

Generic placeholder image

SEHEMU YA KWANZA


Nyumbani kwa marehemu

Padri au katekista anayeongoza anasema:
Bwana sikiliza sala yangu.
Na mlio wangu ukufikie.

Tuombe. Ee Mungu unayewajalia waliopo mbinguni na walio bado duniani ushirika katika Mwanao Yesu Kristo, twakuomba utupatie leo baraka zako sisi tunaofanya kumbukumbu ya ndugu yetu marehemu J. ili nasi pia tuishi katika imani hadi tuweze kuungana naye nyumbani kwako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

Mwenye kuhusika anachukua msalaba mikononi na anauinua ili wote wauone.
Ndugu, wote tuliopo hapa, tuandamane sasa wote pamoja kuelekea kaburini, ili tusimike msalaba huu ulio ishara ya imani yetu. Imani tuliyo nayo ni kwamba ndugu zetu marehemu wana maisha ng'ambo walikokwenda, tena, kuwa Yesu Kristo, kwa kifo chake msalabani, ametupatia matumaini ya kupokelewa katika furaha ya mbinguni.

SEHEMU YA PILI
Maandamano kuelekea kaburini

Wimbo: Msalaba wako, ee Mwokozi wangu.
Sala ya Rozari

SEHEMU YA TATU
Kaburini

Somo la Neno la Mungu:
chagua mojawapo ya masomo yafuatayo.

INJILI Mt.5:1-12
Furahini na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,
Heri walio maskini wa roho;
Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri wenye huzuni;
Maana hao watafarijika.
Heri wenye upole;
Maana hao watairithi nchi.
Heri wenye njaa na kiu ya haki;
Maana hao watashibishwa.
Heri wenye rehema;
Maana hao watapata rehema.
Heri wenye moyo safi;
Maana hao watamwona Mungu.
Heri wapatanishi;
Maana hao wataitwa wana wa Mungu.
Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki;
Maana Ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri nyinyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako, ee Kristo

AU
INJILI Mt.11:25-30
Watoto ni wale wenye moyo mnyenyekevu, wanaomsadiki.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Yesu alipaza sauti, akasema, Nakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako, ee Kristo

AU
INJILI Mt.25:1-13
Haya, Bwana arusi anakuja; tokeni mwende kumlaki. Kila wakati sisi tuwe tayari kumlaki Yesu kwa mawazo na matendo yetu.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano huu: Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. Hata bwana harusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao, Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika. Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie. Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa. Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie. Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi. Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako, ee Kristo

Kisha hufuata maelezo na mafundisho ya Padri au Katekista kufuatana na somo lenyewe.

SEHEMU YA NNE
Kusimika msalaba

Wimbo. Zaburi 130:
Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia;*
Bwana, uisikie sauti yangu.

Masikio yako na yaisikilize*
sauti ya dua zangu.

Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,*
Ee Bwana, nani angesimama?

Lakini kwako kuna msamaha,*
ili Wewe uogopwe.

Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja,*
na neno lake nimelitumainia.

Nafsi yangu inamngoja Bwana,+
kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,*
naam, walinzi waingojao asubuhi.

Ee Israeli, umtarajie Bwana;*
maana kwa Bwana kuna fadhili,

na kwake kuna ukombozi mwingi.*
Yeye atamkomboa Israeli na maovu yake yote.

K. Raha ya milele uwape Ee Bwana
W. Na mwanga wa milele uwaangazie
K. Wastarehe kwa amani.
W. Amina

Tuombe. Ee Bwana, uipokee roho ya huyu mtumishi wako J. uliyependa kumwita kwako kutoka ulimwengu huu, ili akishafunguliwa kifungo cha dhambi zote, ajaliwe raha na mwanga wa milele, tena astahili kufufuliwa katika utukufu pamoja na watakatifu na wateule wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.