MAZISHI YA MTU MZIMA

Generic placeholder image

Hatua ya kwanza


NYUMBANI KWA MAREHEMU

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

Mhudumu awape pole wanaohuzunika kwa msiba huu, kama ilivyo desturi ya mahali hapo. Halafu anaweza kusema maneno kama haya:
Ndugu na jamaa mliopo hapa, naomba sana tushirikiane kumwombea huyu ndugu yetu aliyeaga dunia, apate kusamehewa na kuondolewa dhambi zake. Mungu ampokee kwake mbinguni aweze kufurahi pamoja na Malaika na Watakatifu na jamaa zake waliomtangulia. Nasi tutakapoaga dunia tumkute huko mbinguni.

Wimbo
(K) Ninakulilia, katika unyonge wangu, ewe kinga yangu.

1. Toka vilindini nakulilia ee Bwana, Uisikie sauti yangu, sikiliza sauti ya dua zangu. (K)

2. Kama wewe ungehesabu maovu, kama usingerehemu, kati yetu sote nani angesimama. (K)

3. Kwako msamaha ni mwingi, na neema zote na fadhili, kwako Bwana, ukombozi wazidi.(K)

4. Nimemgoja Bwana, roho yangu imemgoja, neno lake nimelitumainia. (K)

Tumwombe sasa Mungu atutie nguvu ya kupokea msiba huu kwa imani kuu.
(Hapa anasubiri kidogo)
Bwana wetu Yesu Kristo uliyetuonesha njia iendayo kwa Baba yetu wa mbinguni.
Bwana tuhurumie W. Bwana utuhurumie.

Bwana wetu Yesu Kristo uliyeleta uzima duniani kwa kifo chako.
Kristo utuhurumie W. Kristo utuhurumie.

Bwana wetu Yesu Kristo uliyetayarisha makao yetu mapya katika nyumba ya Baba.
Bwana utuhurumie W. Bwana utuhurumie.

Tuombe. Ee Bwana, usikilize sala zetu. Sisi tunaokuomba sana huruma yako Kwa ajili ya mtumishi wako F. Tunakuomba pia, uwatazame hawa watumishi wako wanaoomboleza. Uwape nguvu za kuvumilia msiba huu kwa imani. Utujalie sisi sote tuliokutanika hapa, tukutane siku moja na ndugu zetu mahali ambapo machozi yote hufutwa. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

MAANDAMANO
Kanisa likiwa karibu, ingefaa sana kupeleka maiti mahali ambapo marehemu alizoea kusali. Kanisa ni mfano wa 'Yerusalemu mpya' ndio mbingu, tutakapokaa na Mungu, Baba yetu. Njiani wote wanaweza kuimba Zab. 91 au 6; au wimbo mwingine ufaao.

Hatua ya pili

KANISANI MLANGONI

Baba yetu...(wote wanasali)

Mhudumu anamnyunyuzia maiti maji ya baraka, na kumfukizia ubani.
Mhudumu:
Bwana awe nanyi.
Wote: Na awe rohoni mwako.

Tuombe. Ee Bwana usikilize sala zetu. Sisi tunakuomba sana huruma yako, ili marehemu mtumishi wako F. uliyemhamisha hapa duniani, umweke katika amani na mwanga pamoja na watakatifu wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

M. Raha ya milele umpe, ee Bwana.
W. Na mwanga wa milele umwangazie.
M. Apumzike kwa amani.
W. Amina.

Wakati wa kuingia kanisani watu wanaweza kuimba wimbo unaofaa, kwa mfano:
(K) Ee Bwana wa rehema, uwajalie raha.
1. Ee Bwana umjalie / pumziko la milele
2. Na mwanga wa milele/ umwangazie.
3. Ee Mungu wastahili/ kuimbiwa Sayuni.
4. Na kutimiziwa/ nadhiri Yerusalemu.
5. Wewe unayesikiliza sala,/ kila mwanadamu aje kwako.

MASOMO YA NENO LA MUNGU
Iwapo Misa inaadhimishwa, (tazama link ya misa ya mazishi), Antifona ya Mwanzo na Kolekta vinaachwa, na Masomo yanaanza mara moja. Mhudumu anaweza kusema maneno haya kabla ya somo.

Ndugu zangu mliokusanyika hapa, Bwana wetu Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, alipokaa hapa duniani, alilia machozi kwenye kaburi la rafiki yake Lazaro. Huyu Yesu aliyeshinda mauti, yupo sasa hivi kati yetu tunapotangaza matendo yake makuu tunaposoma Maandiko Matakatifu.

Masomo ya Biblia
Wimbo wa katikati:

(K) Tumaini letu ni kwa Bwana.

SALA YA WAAMINI
Tumwombee huyu ndugu yetu kwa Bwana wetu Yesu Kristo aliyesema: “Mimi ndimi ufufuo na uzima” Twakuomba umweke miongoni mwa watakatifu na wateule wako, huyu ndugu yetu aliyesafishwa kwa maji ya Ubatizo na kupakwa mafuta matakatifu.
W. Twakuomba utusikie.

Twakuomba umpokee mbinguni, huyu ndugu yetu aliyekula karamu ya Mwili na Damu yako.
W. Twakuomba utusikie.

Tusali kwa ajili ya wale wote wanaoteswa, ili wasifikiri hata mara moja kwamba wameachwa na Mungu.
W. Twakuomba utusikie.

Tusali kwa ajili ya ndugu zetu marehemu ili Mungu mwenyezi apende kuwapokea katika ufalme wa mbinguni.
W. Twakuomba utusikie.

Ee Mungu, Muumba wetu na Mkombozi wa waamini wote, uzijalie roho za marehemu maondoleo ya dhambi zao zote. Kwa maombezi yetu wapate msamaha walioutumainia daima. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

MAOMBI YA MWISHO
NA KUMPA BURIANI MAREHEMU

Misa, au adhimisho bila Misa, ikiisha, hufuata sala ya kumpa buriani marehemu kama ifuatavyo:
Leo tunamsindikiza ndugu yetu katika safari yake ya mwisho ya hapa duniani, Mungu alimpa maisha ya duniani, na sasa amemwita ili ampe maisha ya mbinguni yasiyo na mwisho. Mwili wake tunauweka ardhini kama mbegu ya mwili utakaotukuka, na roho yake iingie katika raha ya milele. Twakuomba ee Bwana, umpokee huyu ndugu yetu katika uzima wa milele na utawala wako, apate furaha isiyo na mwisho na kukaa miongoni mwa watakatifu wote, milele na milele.
W. Amina.

Mhudumu anamnyunyizia maiti maji ya baraka, na kumfukizia ubani bila kusema neno lolote.

MAANDAMANO YA KWENDA MAKABURINI
Mhudumu aweza kuwaalika wote kumsindikiza marehemu.
Sasa tumpeleke ndugu yetu makaburini. Twatumaini kuwa siku moja tutakutana naye katika uzima mpya.
Wakati wa kwenda makaburini wanaosindikiza maiti husali Rozari (matendo ya utukufu) au kuimba nyimbo zinazofaa.

Hatua ya tatu:


KWENYE KABURI

Mhudumu anasimama karibu na jeneza akiwaelekea watu. Watumishi wanasimama kando yake wakiwa na maji ya baraka na chetezo. Kama maiti hakupelekwa kanisani, wala maneno ya buriani hayajasemwa bado, yaweza kusemwa sasa.

KUBARIKI KABURI
Tuombe: Ee Mungu, ulibariki kaburi hili, umweke na Malaika wako mtakatifu alilinde. Na huyu, ambaye mwili wake utazikwa humu, roho yake ifurahi kwako mbinguni pamoja na watakatifu wako bila mwisho. Tunaomba hayo, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Analinyunyizia kaburi maji ya baraka.

KUWAOMBEA WAZIMA NA WAFU
Ndugu zangu, tumwombe kwa unyenyekevu Mungu Baba wa rehema kwa ajili ya ndugu zetu waliofariki:
W. Twakuomba utusikie.

Ee Bwana, uwasamehe kwa wema dhambi zao:
- Uzipokee kazi zao njema.
W. Twakuomba utusikie.

Tuwaombee wote wanaohuzunika kwa kifo cha ndugu huyu:
-Ee Bwana uwatulize wote waliofiwa.
W. Twakuomba utusikie.

Tuombeane sisi wenyewe ambao tu wasafiri hapa duniani:
- Mungu atuimarishe na kutudumisha katika utumishi wake mtakatifu.
W. Twakuomba utusikie.

Mungu Mwenyezi, kwa imani tunasadiki kifo na ufufuko wa Mwanao. Tunaomba utujalie sisi na ndugu zetu marehemu tufufuke katika furaha. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. W. Amina.

MAITI ANAWEKWA KABURINI
Mwenyezi Mungu amependa kumwita kwake huyu ndugu yetu toka uzima huu. Tunauweka mwili wake udongoni, urudie ulikotoka. Kristo amefufuka wa kwanza kutoka wafu. Tunamkabidhi huyu ndugu yetu kwa Bwana. Bwana ampokee katika amani yake na mwili wake aufufue siku ya mwisho.

Mhudumu anamnyunyizia maiti maji ya baraka.
Katika maji ulibatizwa. Mungu akamilishe ndani mwako aliyoanzisha katika Ubatizo.

Maiti anapofukiziwa ubani:
Mwili wako ulikuwa hekalu la Mungu. Tunaomba akupe furaha ya milele.

Wakati wa kutupa udongo kaburini:
Wewe ni mavumbi,
utarudia kuwa mavumbi.
Lakini Bwana atakufufua siku ya mwisho.

SALA YA MWISHO
Ee Mungu, siku zako hazina mwisho, na rehema zako hazina idadi. Utukumbushe daima, kwamba maisha ya hapa duniani ni mafupi, na ya kwamba hatujui tutakufa lini. Roho wako Mtakatifu atuongoze katika utakatifu na haki siku zote za maisha yetu. Tufike salama katika ufalme wako, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

M. Raha ya milele umpe, ee Bwana.
W. Na mwanga wa milele umwangazie.
M. Apumzike kwa amani.
W. Amina.

Mhudumu anaweza kuchora alama ya msalaba juu ya kaburi.
Uandikwe ishara ya Bwana, + Mkombozi wetu Yesu Kristo, aliyekukomboa kwa ishara hii. Upumzike kwa Amani.
W. Amina.