MAZISHI YA MTOTO ALIYEBATIZWA

Generic placeholder image

Hatua ya kwanza


NYUMBANI KWA MAREHEMU

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

Mhudumu awape pole wanaohuzunika kwa msiba huu. Labda inafaa kutaja umri wa mtoto aliyekufa, Ubatizo wake na sababu ya kifo chake, na kumalizia kwa maneno kama haya.
Mtoto huyu ametuacha mapema amekwenda kwa Muumba wake. Sasa yuko mbinguni akifurahi na ndugu zetu waliotutangulia huko. Tumzike kwa heshima anayostahili, naye atuombee kwa Mungu tupate kutulia.
W. Amina

Tuombe. Ee Bwana, tunakukabidhi kwa unyenyekevu huyu mtoto uliyempenda sana. Umempokea kwako mbinguni. Huko hakuna uchungu, wala taabu yoyote, bali amani na furaha pamoja na Mwanao na Roho Mtakatifu, milele na milele.
W. Amina.

Wimbo
(K) Tumaini letu ni kwa Bwana.
1. Heri walio kamili njiani mwao, wakitembea katika sheria ya Bwana. (K)
2. Heri wanaoshika mafundisho yake, wanaomtafuta kwa moyo wote. (K)
3. Kijana atatunzaje njia yake iwe safi? Kwa kushika neno lako. (K)
4. Wao wasiotenda uovu, wanakwenda katika njia za Bwana. (K)
5. Mimi nitashangilia hata milele, nitamwimbia sifa Mungu.(K)

Imani yetu yatuambia kuwa Mungu amekamilisha uzima wa mtoto huyu aliyekwisha ingia mbinguni. Katika tumaini hilo tusali:
Bwana wetu Yesu Kristo, ulikubali kuzaliwa kama mtoto mchanga.
Bwana utuhurumie. W. Bwana utuhurumie.

Bwana wetu Yesu Kristo, uliwapenda sana watoto, uliwaita waje kwako ukawabariki.
Kristo utuhurumie. W. Kristo utuhurumie.

Bwana wetu Yesu Kristo, uliwaahidia mbingu wote wapokeao ufalme wa Mungu kama watoto.
Bwana utuhurumie. W. Bwana utuhurumie.

Tuombe. Ee Mungu, usikilize sala zetu. Tunajua mtoto huyu alitakaswa kwa maji ya Ubatizo. Umemshirikisha uzima wa mbinguni. Tunaomba uwafariji kwa wema watumishi wako waliopata msiba. Utujalie sisi pia tushiriki siku moja pamoja naye furaha za milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

MAANDAMANO KWENDA KANISANI
Njiani wanaweza kuimba Zab. 91 au 6, au nyimbo nyingine za kufaa.

Hatua ya pili

KANISANI MLANGONI

Baba yetu... (wote wanasali)

M. Bwana awe nanyi
W. Na awe rohoni mwako.
Tuombe. Ee Mungu, unajua jinsi gani mioyo yetu inavyosongwa na uchungu kwa kifo cha mtoto huyu. Tunamlilia mtoto huyu aliyefariki dunia kwa maongozi yako. Tunaamini kwamba amekwisha pata makao ya milele mbinguni. Utujalie nasi siku moja tushiriki naye uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

M. Bwana amempokea katika raha ya milele.
W. Tumshukuru Mungu.
Wakati wa kuingia kanisani watu wanaweza kuimba wimbo unaofaa.

MASOMO YA NENO LA MUNGU
Iwapo Misa inaadhimishwa, (tazama link ya misa ya mazishi), Antifona ya Mwanzo na Kolekta vinaachwa, na Masomo yanaanza mara moja.

Mhudumu anaweza kusema maneno kama haya kabla ya Somo:
Ndugu, zangu, Yesu ni rafiki wa wenye moyo safi kama watoto. Alipoishi hapa duniani mara kwa mara aliwakaribisha akawabariki. Watoto wanakubali kwa urahisi Neno la Mungu, kwa hiyo wao ni mfano kwetu sisi.

Masomo kwa Mazishi ya mtoto.
Wimbo wa katikati unaofaa, kwa mfano:

(K) Huo ndio ni mwanzo wa Ufalme wa Mungu.
1. Umpende Mungu kwa moyo wote maana ndiye Baba yako.
2. Heri ukiwa maskini moyoni maana ufalme wa mbinguni ni wako.
3. Heri ukiwa mpole maana utapata nchi.
4. Heri ukiona huzuni maana utatulizwa.
5. Heri ukiona njaa na kiu ya kupata utakatifu maana utashibishwa.
6. Heri ukiwa na huruma maana utahurumiwa.
7. Heri ukiwa na moyo safi maana utamwona Mungu.

SALA ZA WAAMINI
Tumwombe sasa Mungu, Baba yetu awajalie watoto baraka nyingi. Ee Mungu uwajalie watoto wote wapate kuzaliwa mara ya pili katika uzima wa kimungu kwa Ubatizo.
W. Twakuomba utusikie.

Ee Mungu uwajalie watoto wetu afya ya mwili na roho ili waweze kukutumikia maisha yao yote.
W. Twakuomba utusikie.

Utujalie nasi tukumbuke daima kuwa sisi sote tu wanao kutokana na Ubatizo wetu. Unayeishi na kutawala milele na milele.
W. Amina.

MAOMBI YA MWISHO
NA KUMPA BURIANI MAREHEMU.

Baada ya Misa, au adhimisho bila Misa, hutolewa maombi na kumpa buriani marehemu kama ifuatavyo:
Leo tunatimiza kazi ya kuzika mwili wa mtoto ilivyo desturi ya waamini. Tunaomba kwa matumaini, Mungu aufufue mwili wa mtoto huyu siku ya mwisho. Mtoto huyu alizaliwa upya kwa Ubatizo. Tunasadiki kwamba amekwisha ingia katika makao ya Baba yake wa mbinguni. Nasi kwa tumaini thabiti la uzima huo, tumwombe Mungu awafariji wazazi wake na jamaa zake, atufanye sote kutamani mambo ya mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Mhudumu ananyunyizia maiti maji ya baraka, na kumfukizia ubani bila kusema neno lolote.

MAANDAMANO YA KWENDA MAKABURINI
Mhudumu anaweza kuwaalika wote kumsindikiza marehemu.
Sasa tumsindikize marehemu makaburini. Twatumaini siku moja tutakutana naye katika uzima mpya.

Wakati wa kwenda makaburini waamini husali Rozari (matendo ya utukufu) au kuimba wimbo kama huu iwapo ni desturi ya mahali hapo:
(K) Ni wapi kwangu? Siyo chini.
Ndiyo kwa Mungu, ndiyo uwinguni. (x2)
1. Mji wa heri, makao ya milele, Jumba kuu akaapo Mungu,
Siku moja nifike mimi kule, Ndilo neno, ndiyo nia yangu.

2. Duniani, tazama mambo gani, Taabu nyingi, wingi wa uchungu;
Siyo sawa mambo ya uwinguni, Kwenye raha, na kumwona Mungu.

3. Walioko hawaogopi uovu; Wamefika, milele wakaaga;
Mwili wao ni mwepesi, mwangavu, Kama jua mweupe wang'aa.

Hatua ya tatu

KWENYE KABURI

Mhudumu anasimama karibu na jeneza akiwaelekea watu. Watumishi wanasimama kando yake wakiwa na maji ya baraka na chetezo. Iwapo maiti hakupelekwa Kanisani, wala maneno ya buriani hayajasemwa bado, yanaweza kusemwa sasa.

KUBARIKI KABURI
Tuombe. Ee Mungu, twakuomba ulibariki kaburi hili, umweke na Malaika wako mtakatifu alilinde. Sisi tunazika leo mwili wa mtoto huyu F. katika kaburi hili. Roho yake ifurahi kwako mbinguni pamoja na watakatifu wako bila mwisho. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Analinyunyizia kaburi maji ya baraka.

KUWAOMBEA NDUGU WA MAREHEMU
Ndugu zangu, Yesu alisema: Mimi ni ufufuo na uzima. Anisadikiye mimi atakuwa mzima hata baada ya kufa. (Yn.11:25).

Bwana utuhurumie. W. Bwana utuhurumie.
Kristo utuhurumie. W. Kristo utuhurumie.
Bwana utuhurumie. W. Bwana utuhurumie.
Uwatulize ndugu zetu waliofiwa.
W. Twakuomba utusikie.
Uwaepushe na kila chuki.
W. Twakuomba utusikie.
Udumishe kati yetu uhusiano mwema.
W. Twakuomba utusikie.
Utuimarishe katika njia zako takatifu.
W. Twakuomba utusikie.
Uinue mioyo yetu itamani kufika mbinguni.
W. Twakuomba utusikie.

Tuombe.
Ee Bwana, umemwita mtoto huyu F. ukampokea katika jamaa ya wateule wa Mungu. Huko amepata furaha isiyo na mwisho pamoja na wenzake; ataishi raha mustarehe siku zote. Tunakuomba sasa uwatulize wazazi wake na ndugu zake wote hadi watakapoonana naye tena kwako katika utukufu wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

MAITI ANAWEKWA KABURINI
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amependa kumwita kwake huyu mtoto wetu, tunauweka mwili wake udongoni. Tuna hakika mtoto huyu hakuzaliwa bure. Mungu ameisha kumpokea na kumjalia heri ya mbinguni.

Mhudumu anamnyunyizia maiti maji ya baraka akisema:
Katika maji ulibatizwa; Mungu akamilishe ndani mwako aliyoanzisha katika Ubatizo.

Anapomfukizia maiti ubani, mhudumu anasema:
Mwili wako ulikuwa hekalu la Mungu, Bwana amekupa furaha ya milele.

Wakati anapotupa udongo kaburini, mhudumu anasema:
Wewe ni mavumbi,
utarudi kuwa mavumbi.
Lakini Bwana atakufufua siku ya mwisho.

SALA YA MWISHO
Ee Mungu, siku zako hazina mwisho, na rehema zako hazina idadi. Utukumbushe daima, kwamba maisha ya hapa duniani ni mafupi, na ya kwamba hatujui tutakufa lini. Roho wako Mtakatifu atuongoze katika utakatifu na haki siku zote za maisha yetu, ili siku moja tufike salama katika Ufalme wako mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

M. Bwana amempokea katika raha ya milele.
W. Tumshukuru Mungu.

Mhudumu anaweza kuchora alama ya msalaba juu ya kaburi (kwa mkono au kwa kutumia fimbo).

Uandikwe ishara ya Bwana, + Mkombozi wetu Yesu Kristo, aliyekukomboa kwa ishara hii. Upumzike kwa amani.
W. Amina.