MISA YA MAZISHI

Generic placeholder image

Kabla ya Misa Padri anakwenda kuilaki maiti penye mlango wa kanisa. Anawapa pole waliopo. halafu anaanza kuadhimisha Mazishi. Kwa kuwa MWANZO na SALA zimekwisha kusemwa mwanzoni mwa Mazishi, Padri anaanza mara moja na Somo la kwanza la Misa mojawapo katika hizi zifuatazo. Baada ya Injili huwa na homilia fupi, siyo hotuba ndefu ya kumsifia marehemu. Halafu husemwa sala ya waamini. Kisha hufuata Liturujia ya Ekaristi kama kawaida.

C. KIPINDI CHA PASAKA
ANTIFONA YA KUINGIA 1The.4:14;1Kor.15:22
Kama Yesu alivyokufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa, aleluya.

Utukufu husemwa.

KOLEKTA
Ee Bwana, tunakuomba usikilize kwa wema sala zetu, ili, kama vile imani yetu katika Mwanao mfufuka kutoka wafu inavyoimarishwa, vivyo hivyo tumaini letu la kutazamia ufufuko wa mtumishi wako J. lithibitishwe. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
W. Amina.

SOMO 1 Rum.5:5-11
Tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.
Somo la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi.
Tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; Zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.
Neno la Bwana
W. Tumshukuru Mungu

WIMBO WA KATIKATI Zab.42:1-2,4;43:3-5(K)42:2
1. Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji,
vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku,
ee Mungu.

(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu, Mungu aliye hai?

2. Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu,
Mungu aliye hai,
lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? (K)

3. Nayakumbuka hayo
nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu,
jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano,
na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu,
kwa sauti ya furaha na kusifu,
mkutano wa sikukuu. (K)

4. Niletewe nuru yako na kweli zako ziniongoze,
zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu
na hata maskani yako (K).

5. Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu,
kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu;
nitakusifu kwa kinubi, ee Mungu,
Mungu wangu.(K).

6. Nafsi yangu, kwa nini kuinama,
na kufadhaika ndani yangu?
Umtumaini Mungu; kwa maana nitakuja kumsifu,
aliye afya ya uso wangu, na Mungu wangu.(K)

SHANGILIO Yn.3:16
Aleluya, aleluya!
Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye, awe na uzima wa milele.
Aleluya!

INJILI Mt.25:1-13
Haya, Bwana arusi anakuja; tokeni mwende kumlaki. Kila wakati sisi tuwe tayari kumlaki Yesu kwa mawazo na matendo yetu.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano huu: Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. Hata bwana harusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao, Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika. Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie. Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa. Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie. Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi. Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako, ee Kristo

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, uwe radhi kuvipokea vipaji vyetu, ili huyu mtumishi wako J. apokelewe katika utukufu pamoja na Mwanao, ambaye, kwa njia ya Sakramenti yake kuu ya upendo, wote tunaunganishwa naye. Anayeishi na kutawala milele na milele.

UTANGULIZI WAFU
WAFU I: Tumaini la ufufuko katika Kristo.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Katika Yeye tumaini la ufufuko wenye heri liliangaza kwetu, ili sisi, tunaosikitika kwa sababu tunajua kwamba lazima tutakufa, tufarijiwe kwa ahadi ya uzima wa milele. Maana, uzima wa waamini wako, ee Bwana, hauondolewi, ila unageuzwa tu, na hao wanapata makao ya milele mbinguni, yakiisha bomolewa makao ya hapa duniani.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na pamoja na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

WAFU II: Kristo alikufa ili sisi tupate uzima.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye ndiye yule mmoja aliyepokea mauti, ili sisi sote tusije tukafa; ila mmoja tu alikubali kufa, kusudi sote tupate kuishi kwa ajili yako milele.
Kwa hiyo, pamoja na Malaika wa mbinguni, tunakusifu tukiungama kwa furaha:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

WAFU III: Kristo ndiye wokovu na uzima.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye ndiye wokovu wa ulimwengu, uzima wa wanadamu, ufufuko wa wafu.
Kwa njia yake majeshi ya Malaika husujudia adhama yako, wakifurahi daima na milele mbele ya uso wako. Tunakusihi, utujalie tujiunge nao kwa wimbo wa sifa, tukishiriki kusema kwa shangwe:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

WAFU IV: Kutoka maisha ya duniani kufika kwenye utukufu wa mbinguni.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Kwa amri yako twazaliwa. kwa matakwa yako twaongozwa, na kwa agizo lako tunakombolewa na sheria ya dhambi, inayoturudisha katika udongo, ambamo tulichukuliwa kwanza. Nasi tuliokombolewa kwa njia ya kifo cha Mwanao, kwa ishara yako tunaamshwa kwenye utukufu wa ufufuko wake.
Kwa hiyo, sisi pamoja na umati wa Malaika na Watakatifu, tunakuimbia utenzi wa sifa, tukisema bila mwisho:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

WAFU V: Ufufuko wetu huja kwa ushindi wa Kristo.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Ingawa tunastahili kufa, lakini unatuhurumia kwa neema yako kwamba, tukiisha kuangamizwa na mauti kwa sababu ya dhambi, tunakombolewa kwa njia ya ushindi wa Kristo, na kuitwa tena pamoja naye kwenye uzima.
Kwa hiyo, sisi pamoja na Nguvu za mbinguni, tunakutukuza daima hapa duniani tukisifu bila mwisho adhama yako kwa sauti kuu:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

---------

SALA YA EKARISTI II

UTANGULIZI
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Baba uliye mtakatifu, kwa njia ya Mwanao mpenzi, Yesu Kristo, Neno wako, ambaye kwa njia yake uliumba vitu vyote.
Ndiye uliyemtuma kwetu kama Mwokozi na Mkombozi, akafanyika mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira. Kwa kuwa alitaka kutimiza mapenzi yako na kukupatia taifa takatifu alipanua mikono yake alipoteswa msalabani, ili aangamize mauti na kudhihirisha ufufuko.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Watakatifu wote tunatangaza utukufu wako, tukisema kwa sauti moja:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

kuhani, hali amefumbua mikono, anasema.
KK. Ee Bwana, kweli u Mtakatifu, na chemchemi ya utakatifu wote.

Anafumba mikono, na kuitandaza juu ya mkate na divai, akisema:
KW. Tunakuomba uvitakatifuze vipaji hivi kwa nguvu ya Roho wako,

Anafumba mikono, na kufanya ishara ya msalaba mara moja tu juu ya mkate na kalisi, akisema:
ili viwe kwetu Mwili na + Damu
ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Anafumba mikono.
Yeye alipotolewa na kuingia kwa hiari katika Mateso yake,
alitwaa mkate, akashukuru, akaumega, na akawapa wafuasi wake, akisema:

TWAENI, MLE NYOTE:
HUU NDIO MWILI WANGU,
UTAKAOTOLEWA KWA AJILI YENU.


Anawaonesha waamini hostia takatifu, na kuiweka kwenye Patena, na, kwa kupiga goti, anaabudu.
Vivyo hivyo, baada ya kula,
akitwaa kikombe,
na kukushukuru tena,
aliwapa wafuasi wake, akisema:

TWAENI, MNYWE NYOTE:
HIKI NDICHO KIKOMBE CHA DAMU YANGU,
DAMU YA AGANO JIPYA NA LA MILELE,
ITAKAYOMWAGIKA KWA AJILI YENU
NA KWA AJILI YA WENGI
KWA MAONDOLEO YA DHAMBI.
FANYENI HIVI KWA UKUMBUSHO WANGU.


Anawaonesha waamini kalisi, anaiweka juu ya korporale, na, akipiga goti, anaabudu. Halafu anasema:
KK. Fumbo la imani.
W. Ee Bwana, tunatangaza kifo chako, na kutukuza ufufuko wako, mpaka utakapokuja.

Au:
W.
Ee Bwana, kila tunapokula mkate huu na kukinywea kikombe hiki, tunatangaza kifo chako, mpaka utakapokuja.

Au.
W.
Ee Mwokozi wa ulimwengu, utuokoe, Wewe uliyetukomboa kwa msalaba na ufufuko wako.

Halafu kuhani, hali amefumbua mikono, anasema:
Kwa hiyo, ee Bwana, tunapoadhimisha ukumbusho wa kifo na ufufuko wake Mwanao, tunakutolea mkate wa uzima na kikombe cha wokovu.

Tunakushukuru kwa kuwa umetustahilisha kusimama mbele yako na kukutumikia. Pia tunakusihi kwa unyenyekevu ili, kwa kushiriki Mwili na Damu ya Kristo, tukusanywe na Roho Mtakatifu tupate kuwa jamaa moja.

K1. Ee Bwana, ulikumbuke Kanisa lako lililoenea popote duniani, ulikamilishe katika mapendo, pamoja na Baba mtakatifu wetu J. na Askofu wetu J., na Waklero wote.

--------------
Katika Misa kwa wafu inawezekana kuongeza:
Umkumbuke mtumishi wako J., uliyemwita kwako (leo) kutoka dunia hii. Ujalie, ili, yeye aliyeshirikishwa kifo cha Mwanao kwa Ubatizo, ashiriki pia ufufuko wake.
----------------

K2. Uwakumbuke pia ndugu zetu, waliofariki dunia wakiwa na tumaini la ufufuko, na marehemu wote, waliofariki dunia katika huruma yako, uwapokee kwenye nuru ya uso wako.

K3. Tunakuomba, utuhurumie sisi sote, ili, pamoja na Maria Bikira mwenye heri Mama wa Mungu, na mtakatifu Yosefu, mume wake huyo Bikira, Mitume wenye heri na Watakatifu wote waliokupendeza tangu kale, tustahili kushiriki uzima wa milele, na kukusifu na kukutukuza

anafumba mikono
kwa njia ya Mwanao Yesu Kristo.

Anatwaa patena yenye hostia takatifu na kalisi, na akiviinua vyote viwili, anasema:
Kwa njia yake,
na pamoja naye na ndani yake,
wewe, Mungu Baba mwenyezi,
katika umoja wa Roho Mtakatifu,
unapata heshima yote na utukufu
milele na milele.

W. Amina.

------------

SALA YA EKARISTI III

Kuhani, hali amefumbua mikono, anasema:
KK.
Ee Bwana, kweli u Mtakatifu, na kila kiumbe kilichoumbwa nawe kinakusifu kwa haki. Maana, kwa njia ya Mwanao, Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa uwezo tendaji wa Roho Mtakatifu, unavitia uzima vitu vyote na kuvitakatifuza, wala huachi kukusanya watu kwako, ili, toka maawio ya jua hata machweo yake, dhabihu safi itolewe kwa jina lako.

Anafumba mikono, na kuitandaza juu ya mkate na divai, akisema:
KW. Basi, ee Bwana, tunakusihi kwa unyenyekevu, vipaji hivi, ambavyo tumekutolea ili uvitakase, upende kuvitakatifuza kwa Roho huyo huyo,

anafumba mikono na kufanya ishara ya msalaba mara moja tu juu ya mkate na kalisi, akisema:
ili viwe Mwili na + Damu
ya Mwanao, Bwana wetu Yesu Kristo,

anafumba mikono
aliyetuamuru tuadhimishe mafumbo haya.

Maana, Yeye mwenyewe, usiku ule alipotolewa, alitwaa mkate, na akikushukuru, aliubariki, akaumega, na akawapa wafuasi wake, akisema:

TWAENI, MLE NYOTE:
HUU NDIO MWILI WANGU,
UTAKAOTOLEWA KWA AJILI YENU.


Anawaonesha waamini hostia takatifu, na kuiweka kwenye patena, na, akipiga goti, anaabudu. Halafu anaendelea akisema:
Vivyo hivyo, baada ya kula,
akitwaa kikombe, na kukushukuru, alikibariki, na akawapa wafuasi wake, akisema:

TWAENI, MNYWE NYOTE:
HIKI NDICHO KIKOMBE CHA DAMU YANGU,
DAMU YA AGANO JIPYA NA LA MILELE,
ITAKAYOMWAGIKA KWA AJILI YENU
NA KWA AJILI YA WENGI
KWA MAONDOLEO YA DHAMBI.
FANYENI HIVI KWA UKUMBUSHO WANGU.


Awaonesha waamini kalisi, anaiweka juu ya korporale, na, akipiga goti, anaabudu.

KK. Fumbo la imani.
W. Ee Bwana, tunatangaza kifo chako, na kutukuza ufufuko wako, mpaka utakapokuja.

Au:
W.
Ee Bwana, kila tunapokula mkate huu na kukinywea kikombe hiki, tunatangaza kifo chako, mpaka utakapokuja.

Au:
W.
Ee Mwokozi wa ulimwengu, utuokoe, Wewe uliyetukomboa kwa msalaba na ufufuko wako.

KW. Kwa hiyo, ee Bwana, tunapoadhimisha ukumbusho wa mateso ya Mwanao yaletayo wokovu, pamoja na ufufuko wake wa ajabu na kupaa kwake mbinguni, na tunapoutazamia ujio wake wa pili, tunakutolea, kwa shukrani, sadaka hii iliyo hai na takatifu.

Tunakuomba, uyaangalie matoleo ya Kanisa lako, na kwa kumtambua Yeye, aliye Kafara ambaye ulitaka kutulizwa kwa sadaka ya kifo chake, utujalie sisi tunaotiwa nguvu kwa Mwili na Damu ya Mwanao, na kujazwa Roho wake Mtakatifu, tupate kuwa mwili mmoja na roho moja katika Kristo.

K1. Yeye atufanye sisi tuwe kwako sadaka timilifu ya milele, ili tuweze kupata urithi pamoja na wateule wako: kwanza kabisa pamoja na Bikira Maria, mwenye heri, Mama wa Mungu, na mtakatifu Yosefu, mume wake huyo Bikira, na Mitume wako wenye heri na Mashahidi wako watukufu, (pamoja na Mtakatifu J.: Mtakatifu wa siku au Msimamizi) na Watakatifu wote, ambao tunategemea kupata daima msaada wa maombezi yao mbele zako.

K2. Tunakuomba, ee Bwana, huyu aliye Kafara na upatanisho wetu alete amani na wokovu duniani kote. Upende kuliimarisha katika imani na mapendo Kanisa lako, linalosafiri hapa duniani, pamoja na mtumishi wako Baba Mtakatifu wetu J. na Askofu wetu J., pamoja na Maaskofu wote, Waklero wote, na watu wote unaowafanya kuwa taifa lako.

K3. Usikilize kwa wema sala za jamaa hii uliyoiita hapa mbele yako. Ee Baba uliye mtakatifu, kwa huruma yako uwakusanye kwako wanao wote waliotawanyika popote duniani.

-------
katika Misa kwa wafu:
Umkumbuke mtumishi wako J., uliyemwita kwako (leo) kutoka dunia hii. Umjalie kwamba, yeye ambaye alishirikishwa kifo cha Mwanao kwa Ubatizo, hali kadhalika ashiriki ufufuko wake, siku ambapo atawafufua wafu katika miili yao kutoka ardhini. Hapo, ataufananisha mwili wa unyonge wetu na mwili wa utukufu wake.

Pia uwapokee kwa wema katika ufalme wako ndugu zetu marehemu na wote walioaga dunia wakiwa wamekupendeza.

Nasi tunatumaini kufika katika ufalme huo ili pamoja tushibishwe milele kwa utukufu wako. Ndipo utakapofuta kila chozi katika macho yetu; maana kwa kukuona wewe, Mungu wetu, kama ulivyo, tutafanana nawe milele yote, na tutakusifu bila mwisho,

Anafumba mikono
kwa njia ya Kristo Bwana wetu, ambaye kwa njia yake unaujalia ulimwengu mema yote.

Anatwaa patena yenye hostia takatifu na kalisi, na akiviinua vyote viwili, anasema:
Kwa njia yake,
na pamoja naye na ndani yake,
wewe, Mungu Baba mwenyezi,
katika umoja wa Roho Mtakatifu,
unapata heshima yote na utukufu
milele na milele.

W. Amina.
------------


C. KOMUNYO


Baada ya kuweka altareni kalisi na patena, kuhani, hali amefumba mikono, anasema:
Kwa kulitii agizo la Mwokozi wetu, na tukifuata mafundisho yake ya kimungu, tunathubutu kusema:

Anafumbua mikono na anaendelea kusema, pamoja na waamini:
Baba yetu, uliye mbinguni, jina lako litukuzwe; ufalme wako ufike; utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kila siku; utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni.

amefumbua mikono:
KK. Ee Bwana, tunakuomba utuopoe katika maovu yote, utujalie kwa wema amani maishani mwetu, kusudi, kwa msaada wa huruma yako, tuopolewe daima na dhambi wala tusifadhaishwe na jambo lolote, tunapotazamia tumaini lenye heri, na ujio wa Mwokozi wetu Yesu Kristo.

W. Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele.

amefumbua mikono
KK. Ee Bwana Yesu Kristo, uliyewaambia Mitume wako, “Amani nawaachieni, amani yangu nawapa”,usizitazame dhambi zetu, ila tu imani ya Kanisa lako; upende kulijalia amani na umoja, kama yalivyo mapenzi yako.

Anafumba mikono.
Unayeishi na kutawala milele na milele.

W. Amina.

huku akifumbua na kufumba mikono, anaendelea kusema:
KK.
Amani ya Bwana iwe daima nanyi.

W. Na iwe rohoni mwako.

KK. Mpeane amani.

Kisha, anachukua hostia takatifiu na kuimega juu ya patena, halafu anakitia kipande ndani ya kalisi, akisema kwa sauti isiyosikika:
KK. Huku kuchanganya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo kutupatie uzima wa milele sisi tunaopokea.

MWANAKONDOO
Mwanakondoo wa Mungu,
uondoaye dhambi za ulimwengu: utuhurumie.
Mwanakondoo wa Mungu,
uondoaye dhambi za ulimwengu: utuhurumie.
Mwanakondoo wa Mungu,
uondoaye dhambi za ulimwengu: utujalie amani.

Halafu kuhani, hali amefumba mikono, anasema kwa sauti isiyosikika:
KK.
Ee Bwana Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, kadiri ya mapenzi ya Baba, na kwa kutenda kazi pamoja na Roho Mtakatifu, uliupatia ulimwengu uzima kwa njia ya kifo chako. Uniokoe kwa Mwili na kwa Damu yako hii takatifu sana, katika maovu yangu yote na mabaya yote; unifanye niambatane daima na amri zako, wala usiruhusu nitengane nawe kamwe.

Au:
Ee Bwana Yesu Kristo, huku kupokea Mwili na Damu yako kusiwe kwangu hukumu na adhabu, bali, kwa huruma yako, kunifae mimi kwa kunilinda akili na mwili na kuwa dawa ya kuniponya.

Kuhani anapiga goti, halafu anachukua hostia takatifu na kuiinua kidogo juu ya patena au juu ya kalisi, na, akiwaelekea waamini, anasema kwa sauti ya kusikika:

KK. Tazama, Mwanakondoo wa Mungu, tazama, aondoaye dhambi za ulimwengu. Heri yao walioalikwa kwenye karamu ya Mwanakondoo.

Na anaendelea kusema, pamoja na waamini:
Ee Bwana, sistahili uingie kwangu, lakini sema neno tu, na roho yangu itapona.

Na kuhani, akiielekea altare, anasema kwa sauti ndogo:
KK.
Mwili wa Kristo unilinde nipate uzima wa milele.

Na kwa heshima anakula Mwili wa Kristo. Halafu anatwaa kalisi na kusema kwa sauti ndogo:
KK. Damu ya Kristo inilinde nipate uzima wa milele.

Na kwa heshima anakunywa Damu ya Kristo. Halafu anatwaa patena au siborio na anakwenda kukomunisha waamini, akiinua kidogo hostia na kumwonesha kila anayepokea, na kumwambia:

Mwili wa Kristo.

Mwenye kukomunika anaitikia:
Amina.

ANTIFONA YA KOMUNYO Flp.3:20-21
Tunamtazamia Mwokozi, Bwana wetu Yesu Kristo, atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu.

wakati vyombo vikiendelea kusafishwa, kuhani anasema kwa sauti isiyosikika:
Ee Bwana, tulichopokea kinywani, tukishike kwa moyo safi; na tulichopewa kama zawadi hapa duniani kiwe kwetu dawa ya kutuponya milele.

SALA BAADA YA KUMONYO
Ee Bwana, tumeadhimisha Sakramenti ya Pasaka kwa ajili ya mtumishi wako J.. Tunakuomba, umjalie aingie katika makao ya mwanga na amani. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

Sala baada ya Komunyo ikiisha semwa, Padri anatoa maombi ya mwisho, amevaa kasula au joho. Sala hii huweza kufanywa kanisani au makaburini.