10

Kifo cha mfalme Sauli
(1Sam 31:1-13)
1 Basi, Wafilisti walipigana vita dhidi ya Waisraeli; nao Waisraeli walikimbia mbele ya Wafilisti na kuuawa katika mlima wa Gilboa.
2 Lakini Wafilisti wakamzingira Sauli na wanawe, kisha wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-shua wana wa Sauli.
3 Vita vilikuwa vikali sana dhidi ya Sauli. Wapiga mishale walipomwona walimjeruhi.
4 Ndipo Sauli alipomwambia mtu aliyembebea silaha, “Chomoa upanga wako unichome nife, ili watu hawa wasiotahiriwa wasije wakanidhihaki.” Lakini huyo aliyembebea silaha hakuthubutu; kwa sababu aliogopa sana. Hivyo, Sauli alichukua upanga wake mwenyewe akauangukia.
5 Halafu yule aliyembebea silaha alipoona kuwa Sauli amekufa, naye pia akauangukia upanga wake, akafa.
6 Hivyo ndivyo Sauli alivyokufa, yeye na wanawe watatu, na jamaa yake yote.
7 Nao watu wa Israeli walioishi bondeni walipoona jeshi limewakimbia maadui, na ya kuwa Sauli na wanawe wamekufa, waliihama miji yao wakakimbia. Wafilisti wakaenda na kukaa katika miji hiyo.
8 Kesho yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa, waliikuta maiti ya Sauli na wanawe mlimani Gilboa.
9 Walimvua mavazi, wakachukua kichwa chake pamoja na silaha zake, halafu walituma wajumbe katika nchi yote ya Filistia kutangaza habari njema kwa sanamu zao na watu.
10 Waliziweka silaha za Sauli katika hekalu la miungu yao; kisha wakakitundika kichwa chake katika hekalu la Dagoni.
11 Lakini watu wa Yabesh-gileadi waliposikia yote Wafilisti waliyomtendea Sauli,
12 mashujaa wote waliondoka na kuuchukua mwili wa Sauli na miili ya wanawe, wakaileta mpaka Yabeshi. Wakaizika mifupa yao chini ya mwaloni huko Yabeshi, nao wakafunga kwa muda wa siku saba.
13 Sauli alikufa kwa sababu ya kutokuwa mwaminifu; hakuwa mwaminifu kwani hakutii neno la Mwenyezi-Mungu na alikwenda kwa mwaguzi kumtaka shauri,
14 badala ya kumwendea Mwenyezi-Mungu ili kumtaka shauri. Kwa sababu hiyo Mwenyezi-Mungu akamuua, na ufalme wake akampa Daudi mwana wa Yese.

Generic placeholder image