47

Tamko la Mwenyezi-Mungu juu ya Filistia
1 Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaushambulia mji wa Gaza:
2 Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Tazama! Maji yanapanda kutoka kaskazini, nayo yatakuwa mto uliofurika; yataifunika nchi nzima na vyote vilivyomo, mji na wakazi na wanaoishi humo. Watu watalia, wakazi wote wa nchi wataomboleza.
3 Watasikia mshindo wa kwato za farasi, kelele za magari ya vita, na vishindo vya magurudumu yao. Kina baba watawasahau watoto wao, mikono yao itakuwa imelegea mno.
4 Hiyo ni siku ya kuwaangamiza Wafilisti wote, kukomesha msaada uliobakia kutoka Tiro na Sidoni. Maana Mwenyezi-Mungu anawaangamiza Wafilisti, watu waliosalia wa kisiwa cha Kaftori.
5 Watu wa Gaza wamenyoa upara kuomboleza; mji wa Ashkeloni umeangamia. Enyi watu wa Anakimu mliobaki mpaka lini mtajikatakata kwa huzuni?
6 Ee upanga wa Mwenyezi-Mungu! Utachukua muda gani ndipo utulie? Ingia katika ala yako, ukatulie na kunyamaa!
7 Lakini utawezaje kutulia, hali Mwenyezi-Mungu ameupa kazi? Ameuamuru ushambulie mji wa Ashkeloni na watu wanaoishi pwani.”

Generic placeholder image