2

Sala ya Yona
1 Basi, Yona, akiwa tumboni mwa samaki huyo, akawa akimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake,
2 akisema: “Kwa sababu ya taabu yangu, nilikuomba, ee Mwenyezi-Mungu, nawe ukanisikiliza; toka chini kuzimu, nilikulilia, nawe ukasikiliza kilio changu.
3 Ulinitupa katika kilindi, katikati ya bahari, gharika ikanizunguka, mawimbi na gharika vikapita juu yangu.
4 Nilidhani kwamba nimetengwa nisiwe mbele yako; nisiweze kuliona tena hekalu lako takatifu.
5 Maji yalinizunguka na kunisonga; kilindi kilinifikia kila upande, majani ya baharini yakanifunika kichwa.
6 Niliteremka hadi kwenye misingi ya milima, katika nchi ambayo milango yake imefungwa milele. Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umenipandisha hai kutoka humo shimoni.
7 Roho yangu ilipoanza kunitoka, nilikukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu, sala yangu ikakufikia, katika hekalu lako takatifu.
8 Watu wanaoabudu sanamu za miungu batili, huutupilia mbali uaminifu wao kwako.
9 Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani, nitakutolea sadaka, na kutimiza nadhiri zangu. Mwenyezi-Mungu, ndiye aokoaye.”
10 Basi, Mwenyezi-Mungu akamwamuru yule samaki, naye akamtapika Yona kwenye nchi kavu.

Generic placeholder image