Tafuta:
Neno unalotafuta:
linapatikana sura zifuatazo:
1Mwanzo. 1:1>>
Hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na dunia.
2Mwanzo. 1:2>>
Dunia ilikuwa bila umbo na tupu. Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji na roho ya Mungu ilikuwa ikitanda juu ya maji.
3Mwanzo. 1:3>>
Mungu akasema, “Mwanga uwe.” Mwanga ukawa.
4Mwanzo. 1:4>>
Mungu akauona mwanga kuwa ni mwema. Kisha Mungu akautenganisha mwanga na giza,
5Mwanzo. 1:5>>
mwanga akauita “Mchana” na giza akaliita “Usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya kwanza.
6Mwanzo. 1:6>>
Mungu akasema, “Anga liwe katikati ya maji, liyatenge maji sehemu mbili.”
7Mwanzo. 1:7>>
Mungu akalifanya anga, akayatenga maji yaliyo juu ya anga na yale yaliyo chini ya anga hilo. Ikawa hivyo.
8Mwanzo. 1:8>>
Mungu akaliita anga “Mbingu.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya pili.
9Mwanzo. 1:9>>
Mungu akasema, “Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, nchi kavu itokee.” Ikawa hivyo.
10Mwanzo. 1:10>>
Mungu akapaita mahali pakavu “Nchi” na kusanyiko la maji akaliita “Bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.
11Mwanzo. 1:11>>
Kisha Mungu akasema, “Nchi na ioteshe mimea. Mimea izaayo mbegu, na miti izaayo matunda yenye mbegu.” Ikawa hivyo.
12Mwanzo. 1:12>>
Basi, nchi ikaotesha mimea izaayo mbegu kwa jinsi yake, na miti izaayo matunda yenye mbegu kwa jinsi yake. Mungu akaona kuwa ni vyema.
13Mwanzo. 1:13>>
Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tatu.
14Mwanzo. 1:14>>
Mungu akasema, “Mianga na iweko angani, itenge mchana na usiku, ioneshe nyakati, majira, siku na miaka,
15Mwanzo. 1:15>>
na ingae angani na kuiangazia dunia.” Ikawa hivyo.
16Mwanzo. 1:16>>
Basi, Mungu akafanya mianga miwili mikubwa; ule mkubwa utawale mchana na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia.
17Mwanzo. 1:17>>
Mungu akaiweka mianga hiyo angani iiangazie dunia,
18Mwanzo. 1:18>>
ipate kutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akaona kuwa ni vyema.
19Mwanzo. 1:19>>
Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya nne.
20Mwanzo. 1:20>>
Mungu akasema, “Maji na yatoe makundi ya viumbe hai na ndege waruke angani.”
21Mwanzo. 1:21>>
Basi, Mungu akaumba wanyama wakubwa sana wa baharini na aina zote za viumbe vyote hai viendavyo na kujaa majini; akaumba na aina zote za ndege wote. Mungu akaona kuwa ni vyema.
22Mwanzo. 1:22>>
Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni, muongezeke, muyajaze maji ya bahari; nao ndege waongezeke katika nchi.”
23Mwanzo. 1:23>>
Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tano.
24Mwanzo. 1:24>>
Mungu akasema, “Nchi na itoe aina zote za viumbe hai, wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo na wanyama wa porini wa kila aina.” Ikawa hivyo.
25Mwanzo. 1:25>>
Basi, Mungu akafanya aina zote za wanyama wa porini, wanyama wa kufugwa, na viumbe vitambaavyo. Mungu akaona kuwa ni vyema.
26Mwanzo. 1:26>>
Kisha Mungu akasema, “Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa, dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo.”
27Mwanzo. 1:27>>
Basi, Mungu akaumba mtu kwa mfano wake; naam, kwa mfano wake Mungu alimuumba. Aliwaumba mwanamume na mwanamke.
28Mwanzo. 1:28>>
Mungu akawabariki na kuwaambia, “Zaeni muongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki; muwatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kitembeacho duniani.”
29Mwanzo. 1:29>>
Kisha Mungu akasema, “Tazama, nawapeni kila mmea duniani uzaao mbegu, na kila mti uzaao matunda yenye mbegu; mbegu zao au matunda yao yatakuwa chakula chenu.
30Mwanzo. 1:30>>
Nao wanyama wote duniani, ndege wote wa angani, viumbe vyote vitambaavyo, naam, kila kiumbe chenye uhai, chakula chao kitakuwa majani yote ya mimea.” Ikawa hivyo.
31Mwanzo. 1:31>>
Mungu akaona kila kitu alichokifanya kuwa ni chema kabisa. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya sita.
32Mwanzo. 2:1>>
Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyokamilika pamoja na vitu vyote vilivyomo.
33Mwanzo. 2:2>>
Siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyofanya; siku hiyo ya saba Mungu akapumzika baada ya kazi yake yote aliyofanya.
34Mwanzo. 2:3>>
Mungu akaibariki siku ya saba na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote ya kuumba.
35Mwanzo. 2:4>>
Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyoumbwa.
36Mwanzo. 2:5>>
Hapakuwa na mimea juu ya nchi wala miti haikuwa imechipua kwani Mwenyezi-Mungu hakuwa ameinyeshea nchi mvua, wala hapakuwa na mtu wa kuilima.
37Mwanzo. 2:6>>
Hata hivyo, maji yalitoka ardhini yakainywesha ardhi yote.
38Mwanzo. 2:7>>
Basi, Mwenyezi-Mungu akamfanya mwanamume kwa mavumbi ya udongo, akampulizia puani pumzi ya uhai, na huyo mwanamume akawa kiumbe hai.
39Mwanzo. 2:8>>
Kisha Mwenyezi-Mungu akapanda bustani huko Edeni, upande wa mashariki, na humo akamweka huyo mwanamume aliyemuumba.
40Mwanzo. 2:9>>
Mwenyezi-Mungu akaotesha kutoka ardhini kila aina ya miti mizuri izaayo matunda yafaayo kwa chakula. Katikati ya bustani hiyo kulikuwa na mti wa uhai na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
41Mwanzo. 2:10>>
Kulikuwa na mto huko Edeni uliotiririka maji na kuinywesha hiyo bustani; kutoka huko mto huo uligawanyika kuwa mito minne.
42Mwanzo. 2:11>>
Jina la mto wa kwanza ni Pishoni; huo waizunguka nchi yote ya Hawila ambako kuna dhahabu.
43Mwanzo. 2:12>>
Dhahabu ya nchi hiyo ni safi kabisa. Huko pia kuna marashi yaitwayo bedola na vito viitwavyo shohamu.
44Mwanzo. 2:13>>
Jina la mto wa pili ni Gihoni; huo waizunguka nchi yote ya Kushi.
45Mwanzo. 2:14>>
Jina la mto wa tatu ni Tigri, nao watiririkia upande wa mashariki wa nchi ya Ashuru; na jina la mto wa nne ni Eufrate.
46Mwanzo. 2:15>>
Basi, Mwenyezi-Mungu akamtwaa huyo mwanamume, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.
47Mwanzo. 2:16>>
Mwenyezi-Mungu alimwamuru huyo mwanamume, “Waweza kula matunda ya mti wowote katika bustani;
48Mwanzo. 2:17>>
lakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, usile, maana siku utakapokula matunda ya mti huo, hakika utakufa.”
49Mwanzo. 2:18>>
Kisha Mwenyezi-Mungu akasema, “Si vizuri huyu mwanamume kuwa peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.”
50Mwanzo. 2:19>>
Basi, kutoka katika udongo, Mwenyezi-Mungu akaumba kila mnyama wa porini na kila ndege wa angani, halafu akamletea huyo mwanamume aone atawapa majina gani; na majina aliyowapa viumbe hao, yakawa ndio majina yao.
51Mwanzo. 2:20>>
Basi, huyo mwanamume akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, wanyama wa porini na ndege wote wa angani. Lakini hakupatikana msaidizi yeyote wa kumfaa.
52Mwanzo. 2:21>>
Basi, Mwenyezi-Mungu akamletea huyo mwanamume usingizi mzito, na alipokuwa usingizini, akatwaa ubavu wake mmoja na kupafunika mahali pale kwa nyama.
53Mwanzo. 2:22>>
Na huo ubavu Mwenyezi-Mungu alioutoa kwa yule mwanamume akaufanya kuwa mwanamke, akamleta kwa huyo mwanamume.
54Mwanzo. 2:23>>
Ndipo huyo mwanamume akasema, “Naam! Huyu ni mfupa kutoka mifupa yangu, na nyama kutoka nyama yangu. Huyu ataitwa ‘Mwanamke’, kwa sababu ametolewa katika mwanamume.”
55Mwanzo. 2:24>>
Ndiyo maana mwanamume humwacha baba yake na mama yake, akaambatana na mkewe, nao wawili huwa mwili mmoja.
56Mwanzo. 2:25>>
Huyo mwanamume na mkewe wote walikuwa uchi, lakini hawakuona haya.
57Mwanzo. 3:1>>
Nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini walioumbwa na Mwenyezi-Mungu. Basi, nyoka akamwambia huyo mwanamke, “Ati Mungu alisema msile matunda ya mti wowote bustanini?”
58Mwanzo. 3:2>>
Mwanamke akamjibu huyo nyoka, “Twaweza kula matunda ya mti wowote bustanini;
59Mwanzo. 3:3>>
lakini Mungu alisema, ‘Msile matunda ya mti ulio katikati ya bustani, wala msiuguse, msije mkafa.’”
60Mwanzo. 3:4>>
Nyoka akamwambia mwanamke, “Hamtakufa!
61Mwanzo. 3:5>>
Mungu alisema hivyo kwa sababu anajua kwamba mkila matunda ya mti huo mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
62Mwanzo. 3:6>>
Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumewe, naye pia akala.
63Mwanzo. 3:7>>
Mara macho yao yakafumbuliwa, wakatambua kwamba wako uchi; hivyo wakajishonea majani ya mtini, wakajifanyia mavazi ya kiunoni.
64Mwanzo. 3:8>>
Jioni, wakati wa kupunga upepo, huyo mwanamume na mkewe wakasikia hatua za Mwenyezi-Mungu akitembea bustanini, nao wakajificha kati ya miti ya bustani, Mwenyezi-Mungu asipate kuwaona.
65Mwanzo. 3:9>>
Lakini Mwenyezi-Mungu akamwita huyo mwanamume, “Uko wapi?”
66Mwanzo. 3:10>>
Naye akamjibu, “Nimesikia hatua zako bustanini, nikaogopa na kujificha, maana nilikuwa uchi.”
67Mwanzo. 3:11>>
Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umekula tunda la mti nililokuamuru usile?”
68Mwanzo. 3:12>>
Huyo mwanamume akajibu, “Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala.”
69Mwanzo. 3:13>>
Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza huyo mwanamke, “Umefanya nini wewe?” Mwanamke akamjibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”
70Mwanzo. 3:14>>
Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hivyo, umelaaniwa kuliko wanyama wote wa kufugwa, na kuliko wanyama wote wa porini. Kwa tumbo lako utatambaa, na kula vumbi siku zote za maisha yako.
71Mwanzo. 3:15>>
Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, kati ya uzawa wako na uzawa wake; yeye atakiponda kichwa chako, nawe utamwuma kisigino chake.”
72Mwanzo. 3:16>>
Kisha akamwambia mwanamke, “Nitakuzidishia uchungu wa kuzaa, kwa uchungu utazaa watoto. Hata hivyo utakuwa na hamu na mumeo, naye atakutawala.”
73Mwanzo. 3:17>>
Kisha akamwambia huyo mwanamume, “Kwa kuwa wewe umemsikiliza mkeo, ukala matunda ya mti ambayo nilikuamuru usile; kwa hiyo, kwa kosa lako ardhi imelaaniwa. Kwa jasho utajipatia humo riziki yako, siku zote za maisha yako.
74Mwanzo. 3:18>>
Ardhi itakuzalia michongoma na magugu, nawe itakubidi kula majani ya shambani.
75Mwanzo. 3:19>>
Kwa jasho lako utajipatia chakula mpaka utakaporudi udongoni ulimotwaliwa; maana wewe ni mavumbi, na mavumbini utarudi.”
76Mwanzo. 3:20>>
Adamu akampa mkewe jina “Hawa”, kwani alikuwa mama wa binadamu wote.
77Mwanzo. 3:21>>
Mwenyezi-Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.
78Mwanzo. 3:22>>
Kisha Mwenyezi-Mungu akasema, “Sasa, binadamu amekuwa kama mmoja wetu, anajua mema na mabaya. Lazima kumzuia kula lile tunda la mti wa uhai, kwani akilila ataishi milele!”
79Mwanzo. 3:23>>
Basi, Mwenyezi-Mungu akamfukuza Adamu nje ya bustani ya Edeni, ili akailime ardhi ambamo alitwaliwa.
80Mwanzo. 3:24>>
Alimfukuza nje, na kuweka mlinzi upande wa mashariki wa bustani ya Edeni na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia iendayo kwenye mti wa uhai.
81Mwanzo. 4:1>>
Adamu akalala na Hawa mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Nimepata mtoto wa kiume kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu!”
82Mwanzo. 4:2>>
Halafu akamzaa Abeli nduguye. Abeli alikuwa mfugaji kondoo na Kaini alikuwa mkulima.
83Mwanzo. 4:3>>
Baada ya muda fulani, Kaini alimtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kutokana na mazao ya shambani,
84Mwanzo. 4:4>>
naye Abeli akamtolea Mungu sadaka ya wazawa wa kwanza wa kondoo wake na nyama nono. Mwenyezi-Mungu akapendezwa na Abeli na tambiko yake,
85Mwanzo. 4:5>>
lakini hakupendezwa na Kaini wala na tambiko yake. Basi, Kaini akakasirika sana na uso wake ukakunjamana.
86Mwanzo. 4:6>>
Mwenyezi-Mungu akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika, na kwa nini uso wako umekunjamana?
87Mwanzo. 4:7>>
Je, ukitenda vyema hutakubaliwa? Na usipotenda vyema, basi, dhambi inakuvizia mlangoni; inakutamani, lakini unapaswa kuishinda.”
88Mwanzo. 4:8>>
Baadaye, Kaini akamwambia Abeli nduguye, “Twende nje shambani” Basi, walipokuwa shambani, Kaini akamvamia Abeli nduguye, akamuua.
89Mwanzo. 4:9>>
Mwenyezi-Mungu akamwuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Kaini akamjibu, “Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
90Mwanzo. 4:10>>
Mwenyezi-Mungu akasema, “Umefanya nini? Damu ya ndugu yako yanililia kutoka udongoni.
91Mwanzo. 4:11>>
Sasa wewe umelaaniwa! Hutailima tena ardhi yenye rutuba ambayo kama kinywa imeipokea damu ya nduguyo uliyemuua.
92Mwanzo. 4:12>>
Ukiilima ardhi haitakupatia tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani.”
93Mwanzo. 4:13>>
Kaini akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Adhabu yangu ni kubwa mno; siwezi kuistahimili.
94Mwanzo. 4:14>>
Leo umenifukuza kutoka ardhi yenye rutuba na mbali nawe. Basi, nitakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani, na yeyote atakayeniona ataniua.”
95Mwanzo. 4:15>>
Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sivyo! Atakayekuua wewe Kaini atalipizwa mara saba.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamtia Kaini alama ya tahadhari, ili yeyote atakayemwona asimuue.
96Mwanzo. 4:16>>
Kisha Kaini akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawa anaishi katika nchi ya Nodi, upande wa mashariki wa Edeni.
97Mwanzo. 4:17>>
Kaini akalala na mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Henoki. Kaini akajenga mji akauita kwa jina la Henoki mwanawe.
98Mwanzo. 4:18>>
Henoki akamzaa Iradi, naye Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, naye Methushaeli akamzaa Lameki.
99Mwanzo. 4:19>>
Lameki alioa wanawake wawili, mmoja aliitwa Ada na mwingine Sila.
100Mwanzo. 4:20>>
Ada alimzaa Yabali ambaye alikuwa baba yao wafugaji waishio mahemani.
101Mwanzo. 4:21>>
Ndugu yake alikuwa Yubali; huyo alikuwa baba yao wanamuziki wote wapigao zeze na filimbi.
102Mwanzo. 4:22>>
Sila naye alimzaa Tubal-kaini, ambaye alikuwa mhunzi wa vyombo vyote vya shaba na chuma. Dada yake Tubal-kaini alikuwa Naama.
103Mwanzo. 4:23>>
Lameki akawaambia wake zake,“Ada na Sila sikieni sauti yangu!Sikilizeni nisemayo enyi wake za Lameki.Mimi niliua mtu kwa kunijeruhi,naam, nilimuua kijana kwa kuniumiza.
104Mwanzo. 4:24>>
Ikiwa Kaini atalipizwa mara saba,kweli Lameki atalipizwa mara sabini na saba.”
105Mwanzo. 4:25>>
Adamu akalala tena na Hawa mkewe, naye akazaa mtoto wa kiume, akamwita Sethi akisema, “Mungu amenijalia mtoto mahali pa Abeli aliyeuawa na Kaini.”
106Mwanzo. 4:26>>
Sethi naye alipata mtoto wa kiume, akamwita Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kumwomba Mwenyezi-Mungu kwa jina lake.
107Mwanzo. 5:1>>
Ifuatayo ni orodha ya wazawa wa Adamu. Wakati Mungu alipomuumba binadamu, alimuumba kwa mfano wake.
108Mwanzo. 5:2>>
Aliwaumba mwanamume na mwanamke, kisha akawabariki na kuwapa jina “Binadamu.”
109Mwanzo. 5:3>>
Adamu alipokuwa na umri wa miaka 130, alipata mtoto aliyefanana naye, na mwenye sura kama yake; akamwita Sethi.
110Mwanzo. 5:4>>
Baada ya kumzaa Sethi, Adamu aliishi miaka 800, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
111Mwanzo. 5:5>>
Adamu alifariki akiwa na umri wa miaka 930.
112Mwanzo. 5:6>>
Sethi alipokuwa na umri wa miaka 105, alimzaa Enoshi.
113Mwanzo. 5:7>>
Baada ya kumzaa Enoshi, Sethi aliishi miaka 807, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
114Mwanzo. 5:8>>
Sethi alifariki akiwa na umri wa miaka 912.
115Mwanzo. 5:9>>
Enoshi alipokuwa na umri wa miaka 90, alimzaa Kenani.
116Mwanzo. 5:10>>
Baada ya kumzaa Kenani, Enoshi aliishi miaka 815 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
117Mwanzo. 5:11>>
Enoshi alifariki akiwa na umri wa miaka 905.
118Mwanzo. 5:12>>
Kenani alipokuwa na umri wa miaka 70, alimzaa Mahalaleli.
119Mwanzo. 5:13>>
Baada ya kumzaa Mahalaleli, Kenani aliishi miaka 840 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
120Mwanzo. 5:14>>
Kenani alifariki akiwa na umri wa miaka 910.
121Mwanzo. 5:15>>
Mahalaleli alipokuwa na umri wa miaka 65, alimzaa Yaredi.
122Mwanzo. 5:16>>
Baada ya kumzaa Yaredi, Mahalaleli aliishi miaka 830 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
123Mwanzo. 5:17>>
Mahalaleli alifariki akiwa na umri wa miaka 895.
124Mwanzo. 5:18>>
Yaredi alipokuwa na umri wa miaka 162, alimzaa Henoki.
125Mwanzo. 5:19>>
Baada ya kumzaa Henoki, Yaredi aliishi miaka 800 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
126Mwanzo. 5:20>>
Yaredi alifariki akiwa na umri wa miaka 962.
127Mwanzo. 5:21>>
Henoki alipokuwa na umri wa miaka 65, alimzaa Methusela.
128Mwanzo. 5:22>>
Henoki alikuwa mcha Mungu. Baada ya kumzaa Methusela, Henoki aliishi miaka 300 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
129Mwanzo. 5:23>>
Henoki aliishi miaka 365.
130Mwanzo. 5:24>>
Alikuwa mcha Mungu, akatoweka, kwa maana Mungu alimchukua.
131Mwanzo. 5:25>>
Wakati Methusela alipokuwa na umri wa miaka 187, alimzaa Lameki.
132Mwanzo. 5:26>>
Baada ya kumzaa Lameki, Methusela aliishi miaka 782, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
133Mwanzo. 5:27>>
Methusela alifariki akiwa na umri wa miaka 969.
134Mwanzo. 5:28>>
Wakati Lameki alipokuwa na umri wa miaka 182, alimzaa mtoto wa kiume.
135Mwanzo. 5:29>>
Alimwita mtoto huyo Noa, akisema, “Mtoto huyu ndiye atakayetufariji kutokana na kazi yetu ngumu tunayofanya kwa mikono yetu katika ardhi aliyoilaani Mwenyezi-Mungu.”
136Mwanzo. 5:30>>
Baada ya kumzaa Noa, Lameki aliishi miaka 595 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
137Mwanzo. 5:31>>
Lameki alifariki akiwa na umri wa miaka 777.
138Mwanzo. 5:32>>
Noa alipokuwa na umri wa miaka 500, alimzaa Shemu na Hamu na Yafethi.
139Mwanzo. 6:1>>
Binadamu walipozidi kuongezeka duniani na kuzaa wasichana,
140Mwanzo. 6:2>>
watoto wa kiume wa Mungu waliwaona hao wasichana wa watu kuwa ni wazuri, wakawachukua wale waliowapenda kuwa wake zao.
141Mwanzo. 6:3>>
Hapo Mwenyezi-Mungu akasema, “Roho yangu haitakaa ndani ya binadamu milele, maana yeye ni wa kufa tu. Basi, hataishi zaidi ya miaka 120.”
142Mwanzo. 6:4>>
Nyakati hizo na hata baadaye, kulikuwa na majitu duniani ambao walikuwa wazawa wa watoto wa kiume wa Mungu na wasichana wa watu. Hao ndio watu waliokuwa mashujaa na wenye sifa enzi hizo, nao waliitwa Wanefili.
143Mwanzo. 6:5>>
Mwenyezi-Mungu alipoona wingi wa uovu wa binadamu duniani, na kwamba kila analokusudia binadamu moyoni mwake ni ovu daima,
144Mwanzo. 6:6>>
Mwenyezi-Mungu alisikitika sana kwa kumuumba binadamu duniani. Mwenyezi-Mungu alihuzunika sana moyoni mwake,
145Mwanzo. 6:7>>
hivyo akasema, “Nitamfuta kabisa duniani binadamu niliyemuumba; nitafutilia mbali pia wanyama wa porini, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Ninasikitika kwamba niliwaumba duniani.”
146Mwanzo. 6:8>>
Lakini Noa alipata fadhili mbele ya Mwenyezi-Mungu.
147Mwanzo. 6:9>>
Ifuatayo ni habari juu ya Noa ambaye alikuwa ndiye mwadilifu pekee na ambaye hakuwa na lawama nyakati zake. Alikuwa mcha Mungu.
148Mwanzo. 6:10>>
Noa alikuwa na watoto watatu wa kiume: Shemu, Hamu na Yafethi.
149Mwanzo. 6:11>>
Mungu aliiona dunia kuwa imeharibika na kujaa ukatili.
150Mwanzo. 6:12>>
Naam, Mungu aliiangalia dunia, akaona kuwa imeharibika kabisa, kwa maana kila mtu alifuata njia yake mbovu.
151Mwanzo. 6:13>>
Mungu akamwambia Noa, “Nimeamua kuwaangamiza binadamu wote kwa sababu wameijaza dunia ukatili. Naam, nitawaangamiza kabisa pamoja na dunia!
152Mwanzo. 6:14>>
Kwa hiyo, jitengenezee safina kwa mbao za mpingo. Gawa vyumba ndani yake na ipake lami ndani na nje.
153Mwanzo. 6:15>>
Utaitengeneza hivi: Urefu wake mita 139, upana wake mita 25 na kimo chake mita 15.
154Mwanzo. 6:16>>
Safina hiyo iwe ya ghorofa tatu na yenye mlango pembeni. Itengenezee paa, kisha acha nafasi ipatayo nusu mita kati ya paa na dari.
155Mwanzo. 6:17>>
Nitaleta gharika ili kuangamiza viumbe vyote hai duniani. Kila kiumbe hai duniani kitakufa.
156Mwanzo. 6:18>>
Lakini nitafanya agano nawe. Utaingia katika safina, wewe pamoja na mkeo, wanao na wake zao.
157Mwanzo. 6:19>>
Nawe utaingiza katika safina jozi ya kila aina ya viumbe, wa kiume na wa kike, ili kuwahifadhi hai pamoja nawe.
158Mwanzo. 6:20>>
“Utaingiza kila aina ya ndege wa angani, kila aina ya mnyama, kila aina ya kiumbe kitambaacho, wawiliwawili, ili kuwahifadhi hai.
159Mwanzo. 6:21>>
Pia chukua aina zote za vyakula vinavyolika, uvihifadhi kwa ajili ya chakula chenu na viumbe hao.”
160Mwanzo. 6:22>>
Noa akafanya yote kama Mungu alivyomwamuru.
161Mwanzo. 7:1>>
Mwenyezi-Mungu akamwambia Noa, “Ingia ndani ya safina wewe pamoja na jamaa yako yote, kwa maana, kati ya watu wote wanaoishi nyakati hizi zako, nimekuona wewe peke yako kuwa mwadilifu mbele yangu.
162Mwanzo. 7:2>>
Chukua pamoja nawe wanyama wote walio safi, dume na jike, saba saba; lakini wanyama walio najisi, chukua dume na jike, wawiliwawili.
163Mwanzo. 7:3>>
Vilevile chukua ndege wa angani dume na jike, saba saba, ili kuzihifadhi hai aina zao duniani.
164Mwanzo. 7:4>>
Baada ya siku saba, nitanyesha mvua nchini siku arubaini mchana na usiku, na kila kiumbe hai nilichokiumba duniani nitakiangamiza.”
165Mwanzo. 7:5>>
Noa akafanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru.
166Mwanzo. 7:6>>
Noa alikuwa na umri wa miaka 600 wakati gharika ilipotokea nchini.
167Mwanzo. 7:7>>
Noa, mkewe, wanawe na wake zao wakaingia ndani ya safina ili kuiepa gharika.
168Mwanzo. 7:8>>
Wanyama walio safi, wanyama walio najisi, ndege na viumbe vyote vitambaavyo,
169Mwanzo. 7:9>>
wawiliwawili, dume na jike, wakaingia ndani ya safina pamoja na Noa kama Mungu alivyomwamuru.
170Mwanzo. 7:10>>
Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaanza kuifunika nchi.
171Mwanzo. 7:11>>
Noa alipokuwa na umri wa miaka 600, mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili, siku hiyo chemchemi zote za vilindi vya nchi zikabubujika maji, na madirisha ya mbinguni yakafunguka.
172Mwanzo. 7:12>>
Mvua ikanyesha nchini siku arubaini mchana na usiku.
173Mwanzo. 7:13>>
Siku hiyohiyo mvua ilipoanza kunyesha, Noa, mkewe na wanawe, Shemu, Hamu na Yafethi, pamoja na wake zao, waliingia ndani ya safina.
174Mwanzo. 7:14>>
Waliingia wao wenyewe pamoja na aina zote za wanyama wa porini, wanyama wafugwao, wanyama watambaao na ndege wa kila aina.
175Mwanzo. 7:15>>
Waliingia ndani ya safina pamoja na Noa wiliwawili wa kila aina ya viumbe hai.
176Mwanzo. 7:16>>
Kila aina yao waliingia, dume na jike, kama Mungu alivyomwamuru Noa. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaufunga mlango wa safina nyuma yake Noa.
177Mwanzo. 7:17>>
Gharika ilidumu nchini kwa muda wa siku arubaini. Maji yakaongezeka na kuiinua safina, ikaelea juu ya ardhi.
178Mwanzo. 7:18>>
Maji yakaendelea kuongezeka zaidi nchini na safina ikaelea juu yake.
179Mwanzo. 7:19>>
Maji hayo yakawa mengi sana juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu katika nchi.
180Mwanzo. 7:20>>
Yaliongezeka hata kuifunika milima kiasi cha mita saba na nusu.
181Mwanzo. 7:21>>
Viumbe wote hai katika nchi wakafa. Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama wa porini, makundi ya viumbe wote katika nchi kavu na wanadamu wote;
182Mwanzo. 7:22>>
naam, kila kiumbe hai katika nchi kavu kilikufa.
183Mwanzo. 7:23>>
Mungu akaangamiza kila kiumbe kilichokuwa hai duniani: Binadamu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Vyote viliangamizwa duniani. Noa tu ndiye aliyesalimika na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina.
184Mwanzo. 7:24>>
Maji hayo yalidumu katika nchi siku 150.
185Mwanzo. 8:1>>
Kisha Mungu akamkumbuka Noa na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Basi, Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakaanza kupungua.
186Mwanzo. 8:2>>
Chemchemi za maji ya vilindi na madirisha ya mbinguni yakafungwa. Mvua ikazuiwa,
187Mwanzo. 8:3>>
maji yakaendelea kupungua polepole katika nchi. Baada ya siku 150, maji yakawa yamepungua sana.
188Mwanzo. 8:4>>
Mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua juu ya milima ya Ararati.
189Mwanzo. 8:5>>
Maji yakaendelea kupungua polepole, na siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana.
190Mwanzo. 8:6>>
Baada ya siku arubaini, Noa alifungua dirisha alilokuwa ametengeneza katika hiyo safina,
191Mwanzo. 8:7>>
akamtoa kunguru nje, naye hakurudi bali aliruka huko na huko mpaka maji yalipokauka nchini.
192Mwanzo. 8:8>>
Kisha Noa akamtoa njiwa apate kuona kama maji yalikuwa yamepungua juu ya nchi.
193Mwanzo. 8:9>>
Lakini, kwa vile maji yalikuwa bado yameifunika nchi yote, huyo njiwa hakupata mahali pa kutua, akamrudia Noa katika safina. Noa akanyosha mkono, akamtwaa na kumrudisha ndani ya safina.
194Mwanzo. 8:10>>
Noa akangoja siku nyingine saba, kisha akamtoa tena huyo njiwa.
195Mwanzo. 8:11>>
Njiwa huyo akamrudia Noa saa za jioni akiwa na tawi bichi la mzeituni mdomoni mwake. Kwa hiyo Noa akajua kwamba maji yalikuwa yamepungua katika nchi.
196Mwanzo. 8:12>>
Kisha akangoja siku nyingine saba, akamtoa tena yule njiwa; safari hii njiwa hakurudi kabisa.
197Mwanzo. 8:13>>
Noa alipokuwa na umri wa miaka 601, siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, maji yalikuwa yamekauka katika nchi. Noa akafunua kifuniko cha safina na alipotazama, akaona kwamba nchi ilikuwa imekauka.
198Mwanzo. 8:14>>
Siku ya 27 ya mwezi wa pili, nchi ilikuwa imekauka kabisa.
199Mwanzo. 8:15>>
Hapo, Mungu akamwambia Noa,
200Mwanzo. 8:16>>
“Toka katika safina, wewe pamoja na mkeo, wanao na wake zao.
201Mwanzo. 8:17>>
Toa pia viumbe wote hai wa kila aina waliokuwa pamoja nawe, ndege na wanyama na kila kiumbe kitambaacho, wapate kuzaa kwa wingi duniani, waongezeke na kuenea kila mahali duniani.”
202Mwanzo. 8:18>>
Basi, Noa akatoka katika safina pamoja na wanawe na mkewe pamoja na wake za wanawe.
203Mwanzo. 8:19>>
Wakatoka kufuatana na jamii zao, wanyama wote wa porini, viumbe wote watambaao, ndege wote na wanyama wote hai duniani.
204Mwanzo. 8:20>>
Noa akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu, akatwaa mmoja katika kila aina ya wanyama walio safi na ndege walio safi, akamtolea Mungu sadaka za kuteketezwa.
205Mwanzo. 8:21>>
Harufu nzuri ya tambiko hiyo ikampendeza Mwenyezi-Mungu, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena nchi kwa sababu ya binadamu; najua kwamba mawazo yake ni maovu tangu utoto wake. Wala sitaangamiza tena viumbe wote kama nilivyofanya.
206Mwanzo. 8:22>>
Kadiri itakavyodumu nchi majira ya kupanda na kuvuna, ya baridi na joto, ya masika na kiangazi, usiku na mchana, hayatakoma.”
207Mwanzo. 9:1>>
Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni, muongezeke, mkaijaze nchi.
208Mwanzo. 9:2>>
Wanyama wote, ndege wote wa angani, viumbe wote watambaao juu ya nchi na samaki wote wa baharini watakuwa na hofu na kuwaogopa nyinyi. Wote wamewekwa chini ya mamlaka yenu.
209Mwanzo. 9:3>>
Wanyama wote hai watakuwa chakula chenu kama vile nilivyowapa mimea kuwa chakula chenu.
210Mwanzo. 9:4>>
Lakini msile nyama yenye damu, kwani uhai uko katika damu.
211Mwanzo. 9:5>>
Damu ya uhai wenu nitaidai; nitaidai kutoka kwa kila mnyama na binadamu. Atakayemuua binadamu mwenzake, nitamdai uhai wake.
212Mwanzo. 9:6>>
Amwagaye damu ya binadamu, damu yake itamwagwa na binadamu; maana binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu.
213Mwanzo. 9:7>>
Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni kwa wingi, mkaongezeke nchini.”
214Mwanzo. 9:8>>
Kisha Mungu akamwambia Noa na wanawe,
215Mwanzo. 9:9>>
“Ninaweka agano langu nanyi na wazawa wenu
216Mwanzo. 9:10>>
na viumbe vyote hai: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wa porini, wote waliotoka katika safina pamoja nanyi.
217Mwanzo. 9:11>>
Nathibitisha agano langu nanyi, kwamba, kamwe viumbe vyote hai havitaangamizwa kwa gharika, wala haitatokea tena gharika kuiharibu nchi.”
218Mwanzo. 9:12>>
Tena Mungu akasema, “Hii ndiyo alama ya agano ninalofanya kati yangu nanyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi kwa vizazi vyote vijavyo.
219Mwanzo. 9:13>>
Naweka upinde wangu mawinguni, nao utakuwa ishara ya agano kati yangu na dunia.
220Mwanzo. 9:14>>
Kila nitakapoifunika dunia kwa mawingu, na huo upinde wa mvua utakapoonekana katika mawingu,
221Mwanzo. 9:15>>
nitalikumbuka agano langu nanyi na viumbe vyote hai. Kamwe maji hayatageuka kuwa gharika ya kuviangamiza viumbe vyote hai.
222Mwanzo. 9:16>>
Huo upinde utakapotokea mawinguni, nitauona na kulikumbuka agano hilo la milele kati yangu na viumbe vyote hai duniani.”
223Mwanzo. 9:17>>
Mungu akamwambia Noa, “Hii ndiyo ishara ya agano ambalo nimefanya na viumbe vyote hai duniani.”
224Mwanzo. 9:18>>
Watoto wa Noa waliotoka katika safina walikuwa Shemu, Hamu na Yafethi. Hamu alikuwa baba yake Kanaani.
225Mwanzo. 9:19>>
Hao ndio watoto watatu wa Noa, na kutokana nao watu walienea duniani kote.
226Mwanzo. 9:20>>
Noa alikuwa mkulima wa kwanza. Alilima shamba la mizabibu,
227Mwanzo. 9:21>>
akanywa divai, akalewa, kisha akalala uchi hemani mwake.
228Mwanzo. 9:22>>
Hamu, baba yake Kanaani, aliuona uchi wa baba yake, akatoka nje na kuwaambia ndugu zake wawili.
229Mwanzo. 9:23>>
Lakini Shemu na Yafethi wakatwaa nguo, wakaitanda mabegani mwao, wakaenda kinyumenyume na kuufunika uchi wa baba yao. Waliangalia pembeni, wala hawakuuona uchi wa baba yao.
230Mwanzo. 9:24>>
Noa alipolevuka na kujua alivyotendewa na mwanawe mdogo,
231Mwanzo. 9:25>>
akasema, “Kanaani na alaaniwe! Atakuwa mtumwa wa watumwa kwa ndugu zake.”
232Mwanzo. 9:26>>
Tena akasema, “Shemu na abarikiwe na Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu! Kanaani na awe mtumwa wake.
233Mwanzo. 9:27>>
Mungu na amkuze Yafethi, aishi katika hema za Shemu; Kanaani na awe mtumwa wake.”
234Mwanzo. 9:28>>
Baada ya gharika, Noa aliishi miaka 350,
235Mwanzo. 9:29>>
kisha akafariki akiwa na umri wa miaka 950.
236Mwanzo. 10:1>>
Baada ya gharika, watoto wa Noa, Shemu, Hamu na Yafethi, walipata watoto wa kiume na wa kike. Hii ndiyo orodha ya wazawa wao:
237Mwanzo. 10:2>>
Watoto wa kiume wa Yafethi walikuwa Gomeri, Magogu, Madai, Yavani, Tubali, Mesheki na Tirasi.
238Mwanzo. 10:3>>
Watoto wa kiume wa Gomeri walikuwa Ashkenazi, Rifathi na Togama.
239Mwanzo. 10:4>>
Watoto wa kiume wa Yavani walikuwa Elisha, Tarshishi, Kitimu na Dodanimu.
240Mwanzo. 10:5>>
Hawa ndio asili ya watu walioenea sehemu za pwani, kila watu kwa lugha yao, kwa jamaa zao na kufuata mataifa yao.
241Mwanzo. 10:6>>
Watoto wa kiume wa Hamu walikuwa Kushi, Misri, Puti na Kanaani.
242Mwanzo. 10:7>>
Watoto wa kiume wa Kushi walikuwa Seba, Hawila, Sabta, Raama na Sabteka. Watoto wa kiume wa Raama walikuwa Sheba na Dedani.
243Mwanzo. 10:8>>
Kushi alikuwa baba yake Nimrodi ambaye alikuwa shujaa wa kwanza duniani.
244Mwanzo. 10:9>>
Alikuwa mwindaji shujaa mbele ya Mwenyezi-Mungu, ndiyo maana kuna msemo usemao, “Kama Nimrodi mwindaji shujaa mbele ya Mwenyezi-Mungu.”
245Mwanzo. 10:10>>
Miji ya kwanza ya utawala wake ilikuwa Babuloni, Ereki na Akadi, katika nchi ya Shinari.
246Mwanzo. 10:11>>
Kutoka huko, Nimrodi alikwenda Ashuru, akajenga miji ya Ninewi, Rehoboth-iri, Kala na
247Mwanzo. 10:12>>
Reseni ulioko kati ya Ninewi na mji mkubwa wa Kala.
248Mwanzo. 10:13>>
Misri alikuwa babu wa Waludi, Waanamu, Walehabi, Wanaftuhi,
249Mwanzo. 10:14>>
Wapathrusi, Wakasluhi (ambao ndio asili ya Wafilisti), na Wakaftori.
250Mwanzo. 10:15>>
Kanaani alikuwa babu yake Sidoni, mzaliwa wake wa kwanza, na Hethi,
251Mwanzo. 10:16>>
na pia babu yao Wayebusi, Waamori, Wagirgashi,
252Mwanzo. 10:17>>
Wahivi, Waarki, Wasini,
253Mwanzo. 10:18>>
Waarvadi, Wasemari na Wahamathi. Baadaye watu wa jamii mbalimbali za Kanaani walitawanyika,
254Mwanzo. 10:19>>
hata eneo la nchi yao likawa toka Sidoni kuelekea kusini, hadi Gerari mpaka Gaza, na kuelekea mashariki hadi Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu hadi Lasha.
255Mwanzo. 10:20>>
Hao ndio wazawa wa Hamu kadiri ya makabila yao, lugha zao, nchi zao na mataifa yao.
256Mwanzo. 10:21>>
Shemu, mkubwa wa Yafethi, alikuwa baba yao Waebrania wote.
257Mwanzo. 10:22>>
Watoto wa kiume wa Shemu walikuwa Elamu, Ashuru, Arfaksadi, Ludi na Aramu.
258Mwanzo. 10:23>>
Watoto wa kiume wa Aramu walikuwa Usi, Huli, Getheri na Mashi.
259Mwanzo. 10:24>>
Arfaksadi alimzaa Shela, Shela akamzaa Eberi.
260Mwanzo. 10:25>>
Eberi alikuwa na watoto wa kiume wawili; wa kwanza akamwita Pelegi kwa sababu wakati huo watu duniani waligawanyika, na wa pili akamwita Yoktani.
261Mwanzo. 10:26>>
Yoktani alikuwa baba wa Almodadi, Shelefu, Hasarmawethi, Yera,
262Mwanzo. 10:27>>
Hadoramu, Uzali, Dikla,
263Mwanzo. 10:28>>
Obali, Abimaeli, Sheba,
264Mwanzo. 10:29>>
Ofiri, Hawila na Yobabu. Hao wote walikuwa watoto wa Yoktani.
265Mwanzo. 10:30>>
Nchi walimokaa ilienea toka Mesha mpaka Sefari katika nyanda za juu za mashariki.
266Mwanzo. 10:31>>
Hao ndio wazawa wa Shemu, kadiri ya makabila yao, lugha zao, nchi zao na mataifa yao.
267Mwanzo. 10:32>>
Hao ndio jamaa za watoto wa Noa, kadiri ya vizazi vyao na mataifa yao. Kutokana nao mataifa yote yalienea duniani baada ya gharika.
268Mwanzo. 11:1>>
Kwanza, watu wote duniani walikuwa na lugha moja na walitumia maneno yaleyale.
269Mwanzo. 11:2>>
Basi, ikawa watu waliposafirisafiri kutoka mashariki, walifika katika nchi tambarare huko Shinari, wakakaa.
270Mwanzo. 11:3>>
Kisha wakaambiana, “Haya! Na tufyatue matofali, tuyachome moto vizuri.” Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa.
271Mwanzo. 11:4>>
Wakasema, “Na tujijengee mji na mnara ambao kilele chake kitafika mbinguni ili tujipatie jina, tusije tukatawanyika duniani kote.”
272Mwanzo. 11:5>>
Ndipo Mwenyezi-Mungu akashuka chini kuuona mji huo na mnara walioujenga binadamu.
273Mwanzo. 11:6>>
Mwenyezi-Mungu akasema, “Tazama, watu hawa ni taifa moja na wote wana lugha moja; huu ni mwanzo tu wa yale watakayoyafanya. Lolote wanalokusudia kulifanya watafanikiwa.
274Mwanzo. 11:7>>
Haya, na tushuke chini na kuivuruga lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.”
275Mwanzo. 11:8>>
Hivyo, Mwenyezi-Mungu akawatawanya mahali pote duniani, nao wakaacha kuujenga ule mji.
276Mwanzo. 11:9>>
Mji huo ukaitwa Babeli, kwa sababu huko ndiko Mwenyezi-Mungu alikoivuruga lugha ya dunia yote, na kutoka huko akawatawanya watu kila mahali duniani.
277Mwanzo. 11:10>>
Wafuatao ni wazawa wa Shemu. Miaka miwili baada ya ile gharika, Shemu akiwa na umri wa miaka 100, alimzaa Arfaksadi.
278Mwanzo. 11:11>>
Baada ya kumzaa Arfaksadi, Shemu aliishi miaka 500 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
279Mwanzo. 11:12>>
Arfaksadi alipokuwa na umri wa miaka 35, alimzaa Shela.
280Mwanzo. 11:13>>
Baada ya kumzaa Shela, Arfaksadi aliishi miaka 403 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
281Mwanzo. 11:14>>
Shela alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Eberi.
282Mwanzo. 11:15>>
Baada ya kumzaa Eberi, Shela aliishi miaka 403 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
283Mwanzo. 11:16>>
Eberi alipokuwa na umri wa miaka 34, alimzaa Pelegi.
284Mwanzo. 11:17>>
Baada ya kumzaa Pelegi, Eberi aliishi miaka 430 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
285Mwanzo. 11:18>>
Pelegi alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Reu.
286Mwanzo. 11:19>>
Baada ya kumzaa Reu, Pelegi aliishi miaka 209 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
287Mwanzo. 11:20>>
Reu alipokuwa na umri wa miaka 32, alimzaa Serugi.
288Mwanzo. 11:21>>
Baada ya kumzaa Serugi, Reu aliishi miaka 207 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
289Mwanzo. 11:22>>
Serugi alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Nahori.
290Mwanzo. 11:23>>
Baada ya kumzaa Nahori, Serugi aliishi miaka 200 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
291Mwanzo. 11:24>>
Nahori alipokuwa na umri wa miaka 29, alimzaa Tera.
292Mwanzo. 11:25>>
Baada ya kumzaa Tera, Nahori aliishi miaka 119, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
293Mwanzo. 11:26>>
Tera alipokuwa na umri wa miaka 70, alimzaa Abramu na Nahori na Harani.
294Mwanzo. 11:27>>
Wafuatao ni wazawa wa Tera, baba yao Abramu, Nahori na Harani. Harani alikuwa baba yake Loti.
295Mwanzo. 11:28>>
Huyo Harani alifariki wakati Tera baba yake alikuwa anaishi huko Uri alikokuwa amezaliwa.
296Mwanzo. 11:29>>
Abramu na Nahori walioa. Mke wa Abramu aliitwa Sarai. Mke wa Nahori aliitwa Milka, binti Harani ambaye pia alikuwa baba yake Iska.
297Mwanzo. 11:30>>
Sarai hakuwa na mtoto kwa sababu alikuwa tasa.
298Mwanzo. 11:31>>
Tera akamchukua Abramu mwanawe, Loti mjukuu wake aliyekuwa mwanawe Harani, na Sarai mkewe Abramu, wakaondoka wote pamoja toka Uri, mji wa Wakaldayo, wakaenda katika nchi ya Kanaani. Lakini walipofika Harani, wakakaa.
299Mwanzo. 11:32>>
Tera alifariki huko Harani akiwa na umri wa miaka 205.
300Mwanzo. 12:1>>
Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, acha jamaa yako na nyumba ya baba yako, uende katika nchi nitakayokuonesha.
301Mwanzo. 12:2>>
Nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, nitakubariki na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka.
302Mwanzo. 12:3>>
Anayekubariki, nitambariki; anayekulaani, nitamlaani. Kwako wewe, nitayabariki mataifa yote ya dunia.”
303Mwanzo. 12:4>>
Kwa hiyo, Abramu akaondoka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru; na Loti akaenda pamoja naye. Abramu alikuwa na umri wa miaka 75 alipotoka Harani.
304Mwanzo. 12:5>>
Alimchukua Sarai mkewe, na Loti mwana wa ndugu yake, pamoja na mali yao yote na watu wote waliokuwa wamejipatia huko Harani, wakaondoka kuelekea nchi ya Kanaani. Walipoingia nchini Kanaani,
305Mwanzo. 12:6>>
Abramu akapita katikati ya nchi mpaka Shekemu, mahali patakatifu, penye mti wa mwaloni wa More. Wakati huo, Wakanaani walikuwa ndio wenyeji wa nchi hiyo.
306Mwanzo. 12:7>>
Ndipo Mwenyezi-Mungu akamtokea Abramu, akamwambia, “Wazawa wako nitawapa nchi hii.” Basi, Abramu akajenga madhabahu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu aliyemtokea.
307Mwanzo. 12:8>>
Baadaye Abramu akaondoka, akaelekea mlimani mashariki ya Betheli akapiga hema kati ya mji wa Betheli, upande wa magharibi, na mji wa Ai upande wa mashariki. Hapo pia akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu na kumwomba kwa jina lake.
308Mwanzo. 12:9>>
Kisha Abramu akaendelea kusafiri kuelekea upande wa Negebu.
309Mwanzo. 12:10>>
Wakati huo, njaa ilitokea nchini. Njaa hiyo ilikuwa kali, hivyo Abramu akalazimika kwenda Misri kukaa huko kwa muda.
310Mwanzo. 12:11>>
Alipokaribia Misri, Abramu alimwambia Sarai mkewe, “Najua kuwa wewe ni mwanamke mzuri na wa kuvutia.
311Mwanzo. 12:12>>
Wamisri watakapokuona watasema, ‘Huyu ni mkewe,’ kisha wataniua lakini wewe watakuacha hai.
312Mwanzo. 12:13>>
Basi, waambie kuwa wewe ni dada yangu ili mambo yaniendee vema, niachwe niishi kwa ajili yako.”
313Mwanzo. 12:14>>
Basi, Abramu alipowasili nchini Misri, wenyeji wa huko walimwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana.
314Mwanzo. 12:15>>
Maofisa wa Farao walipomwona Sarai, wakamsifia kwa Farao. Basi, Sarai akapelekwa nyumbani kwa Farao.
315Mwanzo. 12:16>>
Basi, kwa ajili yake, Farao alimfadhili Abramu, akampa kondoo, ngômbe, punda dume, watumishi wa kiume na wa kike, punda jike na ngamia.
316Mwanzo. 12:17>>
Lakini Mwenyezi-Mungu akamtesa Farao na watu wote wa nyumba yake kwa mapigo makali kwa sababu ya Sarai, mkewe Abramu.
317Mwanzo. 12:18>>
Farao akamwita Abramu, akamwuliza, “Ni kitu gani hiki ulichonitendea? Mbona hukunijulisha kwamba Sarai ni mkeo?
318Mwanzo. 12:19>>
Kwa nini ulisema ni dada yako hata nikamchukua kuwa mke wangu? Basi, sasa mkeo ndiye huyo. Mchukue uende zako!”
319Mwanzo. 12:20>>
Kisha Farao aliwaamuru watu wake, nao wakamsindikiza Abramu njiani akiwa na mke wake na mali yake yote.
320Mwanzo. 13:1>>
Abramu akarudi kutoka Misri, akaingia upande wa Negebu. Alikuwa na mkewe na mali yake yote pamoja na Loti.
321Mwanzo. 13:2>>
Wakati huo, Abramu alikuwa ametajirika sana. Alikuwa na mifugo, fedha na dhahabu.
322Mwanzo. 13:3>>
Akaendelea kusafiri toka eneo la Negebu hadi Betheli. Alifika mahali alipokuwa amepiga kambi ya hema hapo awali, kati ya Betheli na Ai,
323Mwanzo. 13:4>>
ambapo alikuwa amejenga madhabahu. Hapo Abramu akamwomba Mwenyezi-Mungu kwa jina lake.
324Mwanzo. 13:5>>
Kadhalika, Loti, ambaye alifuatana na Abramu, alikuwa na kondoo, mifugo na hema.
325Mwanzo. 13:6>>
Idadi ya mifugo yao ilikuwa kubwa mno hata nchi ile haikuweza kuwatosha Abramu na Loti kuishi pamoja.
326Mwanzo. 13:7>>
Basi, kukazuka ugomvi kati ya wachungaji wa Abramu na wachungaji wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo.
327Mwanzo. 13:8>>
Basi, Abramu akamwambia Loti, “Kusiwe na mafarakano kati yetu wala kati ya wachungaji wako na wachungaji wangu, kwa sababu sisi ni jamaa moja.
328Mwanzo. 13:9>>
Tazama nchi hii yote mbele yako. Na tutengane. Ukienda kushoto, mimi nitakwenda kulia; ukienda kulia, mimi nitakwenda kushoto.”
329Mwanzo. 13:10>>
Loti akatazama, akaliona bonde la mto Yordani, akaona kuwa lina maji ya kutosha kila mahali, kama bustani ya Mwenyezi-Mungu na kama nchi ya Misri upande wa Soari. (Hii ilikuwa kabla Mwenyezi-Mungu hajaiangamiza miji ya Sodoma na Gomora).
330Mwanzo. 13:11>>
Kwa hiyo, Loti akajichagulia bonde lote la mto Yordani, akaelekea mashariki, na hivyo wakatengana.
331Mwanzo. 13:12>>
Abramu akabaki nchini Kanaani na Loti akakaa kati ya miji iliyokuwa bondeni, akahamishia kambi yake Sodoma.
332Mwanzo. 13:13>>
Watu wa Sodoma walikuwa waovu na watenda dhambi wakuu dhidi ya Mwenyezi-Mungu.
333Mwanzo. 13:14>>
Baada ya Loti kujitenga na Abramu, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Angalia toka hapo ulipo utazame pande zote: Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi.
334Mwanzo. 13:15>>
Nchi hii yote unayoiona nitakupa wewe na wazawa wako iwe yenu milele.
335Mwanzo. 13:16>>
Wazawa wako nitawafanya wawe wengi wasiohesabika, kama vile mavumbi ya nchi yasivyoweza kuhesabika!
336Mwanzo. 13:17>>
Basi, inuka uitembelee nchi hii katika mapana na marefu, kwani nitakupa wewe.”
337Mwanzo. 13:18>>
Kwa hiyo, Abramu akangoa hema, akaenda kukaa karibu na mialoni ya Mamre kule Hebroni; huko akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu.
338Mwanzo. 14:1>>
Wakati huo, mfalme Amrafeli wa Shinari, mfalme Arioko wa Elasari, mfalme Kedorlaomeri wa Elamu na mfalme Tidali wa Goiimu,
339Mwanzo. 14:2>>
walipigana vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, dhidi ya Birsha mfalme wa Gomora, Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboimu, na dhidi ya mfalme wa Bela (yaani Soari).
340Mwanzo. 14:3>>
Wafalme hao watano waliyaunganisha majeshi yao katika bonde la Sidimu (yaani Bahari ya Chumvi).
341Mwanzo. 14:4>>
Kwa muda wa miaka kumi na miwili walikuwa wakimtii mfalme Kedorlaomeri, lakini mnamo mwaka wa kumi na tatu, walimwasi.
342Mwanzo. 14:5>>
Mnamo mwaka wa kumi na nne, mfalme Kedorlaomeri na wale wafalme wenzake walikuja na kuwashinda watu wa Refaimu huko Ashtaroth-karnaimu, na Wazuzi huko Hamu, na Waemi huko Shawe-kiriathaimu,
343Mwanzo. 14:6>>
na Wahori huko mlimani kwao Seiri, wakawafukuza hadi Elparani, mpakani mwa jangwa.
344Mwanzo. 14:7>>
Kisha wakarudi nyuma mpaka Enmishpati (yaani Kadeshi), wakaivamia nchi yote ya Waamaleki, na kuwashinda Waamori waliokaa Hasason-tamari.
345Mwanzo. 14:8>>
Ndipo mfalme wa Sodoma, mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboimu na mfalme wa Bela
346Mwanzo. 14:9>>
(yaani Soari), wakaingia vitani katika bonde la Sidimu kupigana na Kedorlaomeri mfalme wa Elamu, Tidali mfalme wa Goiimu, Amrafeli mfalme wa Shinari na Arioko mfalme wa Elasari; wafalme wanne dhidi ya wafalme watano.
347Mwanzo. 14:10>>
Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami; kwa hiyo wafalme wa Sodoma na Gomora walipokuwa wakiikimbia vita, wakatumbukia humo, lakini wengine wakatorokea mlimani.
348Mwanzo. 14:11>>
Basi, wale walioshinda, wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora, kadhalika na mazao yao, wakaenda zao.
349Mwanzo. 14:12>>
Walimteka hata Loti, mwana wa nduguye Abramu aliyekuwa anakaa Sodoma, pamoja na mali yake, wakaenda zao.
350Mwanzo. 14:13>>
Mtu mmoja aliyeponyoka, akaenda kumwarifu yule Mwebrania Abramu ambaye alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mwamori Mamre. Mamre alikuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri. Wote walikuwa wamefanya agano na Abramu.
351Mwanzo. 14:14>>
Abramu alipopata habari kwamba mpwa wake amechukuliwa mateka, akatoka na watu wake stadi 318 waliozaliwa katika nyumba yake, akawafuatia adui mpaka Dani.
352Mwanzo. 14:15>>
Huko, akaligawa jeshi lake katika makundi. Usiku, akawashambulia adui zake, akawashinda na kuwafukuza hadi Hoba, kaskazini mwa Damasko.
353Mwanzo. 14:16>>
Basi, Abramu akaikomboa mali yote iliyotekwa na adui, na kumkomboa Loti mpwa wake, mali yake, pamoja na wanawake na watu wengine.
354Mwanzo. 14:17>>
Abramu aliporudi baada ya kumshinda mfalme Kedorlaomeri na wenzake, mfalme wa Sodoma alitoka kwenda kumlaki katika bonde la Shawe, (yaani Bonde la Mfalme).
355Mwanzo. 14:18>>
Naye Melkisedeki, mfalme wa mji wa Salemu, ambaye alikuwa kuhani wa Mungu Mkuu, akaleta mkate na divai,
356Mwanzo. 14:19>>
akambariki Abramu akisema, “Abramu na abarikiwe na Mungu Mkuu, Muumba mbingu na dunia!
357Mwanzo. 14:20>>
Na atukuzwe Mungu Mkuu, aliyewatia adui zako mikononi mwako!” Naye Abramu akampa Melkisedeki mchango wake sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo.
358Mwanzo. 14:21>>
Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu, lakini jichukulie mali yote wewe mwenyewe.”
359Mwanzo. 14:22>>
Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu, aliyeumba mbingu na dunia,
360Mwanzo. 14:23>>
kwamba sitachukua uzi au kamba ya kiatu, wala chochote kilicho chako, usije ukajivuna na kusema kwamba umenitajirisha.
361Mwanzo. 14:24>>
Basi, sitachukua chochote isipokuwa tu vile vitu vijana wangu walivyokula na sehemu ya wale waliokuwa pamoja nami, Aneri, Eshkoli na Mamre ambao wana haki nayo.”
362Mwanzo. 15:1>>
Baada ya mambo hayo, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Abramu katika maono, “Abramu! Usiogope! Mimi ni ngao yako. Tuzo lako litakuwa kubwa!”
363Mwanzo. 15:2>>
Lakini Abramu akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, utanipa nini hali naendelea kuishi bila mtoto, na mrithi wangu ni Eliezeri wa Damasko?
364Mwanzo. 15:3>>
Tazama! Hujanijalia mtoto; mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye atakayekuwa mrithi wangu!”
365Mwanzo. 15:4>>
Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Huyu hatakuwa mrithi wako! Mwanao halisi ndiye atakayekuwa mrithi wako.”
366Mwanzo. 15:5>>
Hapo Mwenyezi-Mungu akamleta Abramu nje na kumwambia, “Tazama mbinguni! Zihesabu nyota, kama kweli utaweza kuzihesabu! Hivyo ndivyo wazawa wako watakavyokuwa wengi!”
367Mwanzo. 15:6>>
Abramu akamwamini Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akamkubali Abramu kuwa mwadilifu.
368Mwanzo. 15:7>>
Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu niliyekuleta toka Uri, mji wa Wakaldayo, ili nikupe nchi hii uimiliki.”
369Mwanzo. 15:8>>
Lakini Abramu akamwambia, “Ee Mwenyezi-Mungu, nitajuaje kwamba nitaimiliki nchi hii?”
370Mwanzo. 15:9>>
Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Niletee ndama wa miaka mitatu, mwanambuzi jike wa miaka mitatu, kondoo dume wa miaka mitatu, na hua na kinda la njiwa.”
371Mwanzo. 15:10>>
Abramu akamletea hao wote, akamkata kila mnyama vipande viwili, akavipanga katika safu mbili, vikielekeana; lakini ndege hakuwakata vipande viwili.
372Mwanzo. 15:11>>
Na tai walipoijia hiyo mizoga, Abramu akawa anawafukuza.
373Mwanzo. 15:12>>
Jua lilipokuwa likitua, Abramu alishikwa na usingizi mzito; hofu na giza nene vikamfunika.
374Mwanzo. 15:13>>
Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Ujue hakika ya kwamba wazawa wako watakaa kama wageni katika nchi isiyo yao, watakuwa watumwa na watateswa kwa muda wa miaka 400.
375Mwanzo. 15:14>>
Hata hivyo, nitaliadhibu taifa watakalolitumikia, na hatimaye watatoka wakiwa na mali nyingi.
376Mwanzo. 15:15>>
Lakini wewe mwenyewe utaishi maisha marefu na kufariki kwa amani. 16Wazawa wako watarudi hapa katika kizazi cha nne, kwa sababu uovu wa Waamori haujakamilika bado.”
377Mwanzo. 15:17>>
Jua lilipokwisha tua na giza kuingia, tanuri ifukayo moshi na mwenge uwakao moto vikapita katikati ya vile vipande vya nyama.
378Mwanzo. 15:18>>
Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu akafanya agano na Abramu akisema, “Wazawa wako ninawapa nchi hii, toka mto wa Misri hadi ule mto mkubwa wa Eufrate,
379Mwanzo. 15:19>>
yaani nchi za Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni,
380Mwanzo. 15:20>>
Wahiti, Waperizi, Warefai,
381Mwanzo. 15:21>>
Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.”
382Mwanzo. 16:1>>
Basi, Sarai, mkewe Abramu, alikuwa bado hajamzalia mumewe mtoto. Lakini alikuwa na mjakazi aliyeitwa Hagari, kutoka Misri.
383Mwanzo. 16:2>>
Basi, Sarai akamwambia Abramu, “Unajua kuwa Mwenyezi-Mungu hajanijalia kupata watoto. Mchukue Hagari mjakazi wangu; huenda nikapata watoto kwake.” Abramu akakubali shauri la Sarai.
384Mwanzo. 16:3>>
Kisha, Sarai akampa Abramu Hagari, mjakazi wake ambaye alikuwa Mmisri, awe mke wake. Haya yalitokea baada ya Abramu kukaa katika nchi ya Kanaani kwa muda wa miaka kumi.
385Mwanzo. 16:4>>
Abramu akamchukua Hagari, naye Hagari akapata mimba. Lakini mara tu alipoona amepata mimba, Hagari akaanza kumdharau bimkubwa wake.
386Mwanzo. 16:5>>
Sarai akamwambia Abramu, “Wewe utawajibika kwa ubaya ninaotendewa. Mimi nilikupa mjakazi wangu, lakini alipopata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake! Mwenyezi-Mungu na ahukumu kati yako na mimi!”
387Mwanzo. 16:6>>
Lakini Abramu akamwambia Sarai, “Mjakazi wako yuko chini ya mamlaka yako; mfanyie upendavyo.” Basi, Sarai akamtesa Hagari mpaka akatoroka.
388Mwanzo. 16:7>>
Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamkuta Hagari penye chemchemi ya maji jangwani, chemchemi iliyoko njiani kuelekea Shuri.
389Mwanzo. 16:8>>
Malaika akamwuliza, “Hagari, mjakazi wa Sarai! Unatoka wapi na unakwenda wapi?” Hagari akamjibu, “Namkimbia bimkubwa wangu Sarai.”
390Mwanzo. 16:9>>
Yule malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa bimkubwa wako Sarai na umtii.”
391Mwanzo. 16:10>>
Zaidi ya hayo, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Hagari, “Nitawazidisha wazawa wako hata wasiweze kuhesabika kwa wingi wao.”
392Mwanzo. 16:11>>
Kisha huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Wewe ni mjamzito na utajifungua mtoto wa kiume; utamwita Ishmaeli, maana Mwenyezi-Mungu amesikia mateso yako.
393Mwanzo. 16:12>>
Ishmaeli ataishi kama pundamwitu; atakuwa adui wa kila mtu na kila mtu atakuwa adui yake. Ataishi akiwa adui wa jamaa yake.”
394Mwanzo. 16:13>>
Basi, Hagari akampa jina Mwenyezi-Mungu aliyezungumza naye huko, “Wewe ni Mungu Aonaye” kwa maana alifikiri, “Kweli hapa nimemwona yeye anionaye!”
395Mwanzo. 16:14>>
Ndiyo maana kile kisima chaitwa Beer-lahai-roi. Kisima hiki kipo kati ya Kadeshi na Beredi.
396Mwanzo. 16:15>>
Hagari akamzalia Abramu mtoto wa kiume. Abramu akamwita mtoto huyo Ishmaeli.
397Mwanzo. 16:16>>
Abramu alikuwa na umri wa miaka 86 wakati Hagari alipomzaa Ishmaeli.
398Mwanzo. 17:1>>
Wakati Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa, Mwenyezi-Mungu alimtokea, akamwambia, “Mimi ni Mungu mwenye nguvu. Fuata mwongozo wangu na kuishi bila lawama.
399Mwanzo. 17:2>>
Nami nitafanya agano nawe na kuwazidisha wazawa wako.”
400Mwanzo. 17:3>>
Hapo Abramu akasujudu. Naye Mungu akamwambia,
401Mwanzo. 17:4>>
“Ninafanya agano hili nawe: Utakuwa baba wa mataifa mengi.
402Mwanzo. 17:5>>
Tangu sasa, hutaitwa tena Abramu, bali utaitwa Abrahamu, maana nimekufanya kuwa baba wa mataifa mengi.
403Mwanzo. 17:6>>
Nitakufanya uwe na wazawa wengi sana; kwako nitazusha mataifa mengi na wafalme.
404Mwanzo. 17:7>>
Nitalithibitisha agano langu nawe, wazawa wako na vizazi vyao vyote milele; tena nitakuwa Mungu wako na Mungu wa wazawa wako milele.
405Mwanzo. 17:8>>
Nitakupa wewe na wazawa wako nchi hii ambamo unaishi kama mgeni; yaani nchi yote ya Kanaani iwe mali yenu milele; nami nitakuwa Mungu wao.”
406Mwanzo. 17:9>>
Kisha Mungu akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wako, wewe utalishika agano langu, wewe binafsi, wazawa wako na vizazi vyao vyote.
407Mwanzo. 17:10>>
Hili ndilo agano utakaloshika kati yangu na wewe na wazawa wako: Kila mwanamume miongoni mwenu lazima atahiriwe.
408Mwanzo. 17:11>>
Mtatahiriwa kwa kukata magovi yenu, na hii itakuwa ndiyo alama ya agano kati yangu nanyi.
409Mwanzo. 17:12>>
Kila mtoto wa kiume wa siku nane miongoni mwenu ni lazima atahiriwe. Kila mwanamume katika vizazi vyenu, awe mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwenu au aliyenunuliwa kwa fedha zenu kutoka kwa mgeni asiye mzawa wako;
410Mwanzo. 17:13>>
naam, kila mmoja wao aliyezaliwa katika nyumba yako na hata aliyenunuliwa kwa fedha zako ni lazima atahiriwe. Hiyo ni alama ya agano langu katika miili yenu, agano la milele.
411Mwanzo. 17:14>>
Mwanamume yeyote asiyetahiriwa atatengwa na watu, kwani atakuwa amevunja agano langu.”
412Mwanzo. 17:15>>
Kisha Mungu akamwambia Abrahamu, “Kuhusu mkeo, hutamwita tena jina lake Sarai, bali jina lake litakuwa Sara.
413Mwanzo. 17:16>>
Nitambariki, naye atakuzalia mtoto wa kiume. Naam, nitambariki Sara, naye atakuwa mama wa mataifa mengi na wafalme wa mataifa watatoka kwake.”
414Mwanzo. 17:17>>
Hapo Abrahamu akasujudu, akacheka moyoni mwake akiwaza, “Ati, itawezekana kweli mtoto kuzaliwa kwa mzee wa miaka 100? Na je, Sara ambaye umri wake ni miaka tisini, ataweza kupata mtoto?”
415Mwanzo. 17:18>>
Basi, Abrahamu akamwambia Mungu, “Laiti ungekubali ahadi yako hiyo imhusu Ishmaeli.”
416Mwanzo. 17:19>>
Mungu akamjibu, “La! Ila mkeo Sara atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita Isaka Nitaliimarisha agano langu kwake na wazawa wake, kuwa agano la milele.
417Mwanzo. 17:20>>
“Na, kuhusu Ishmaeli, nimesikia ombi lako. Nitambariki, nitamjalia watoto wengi na kuwazidisha sana. Ishmaeli atakuwa baba wa watawala kumi na wawili, nami nitamfanya kuwa baba wa taifa kubwa.
418Mwanzo. 17:21>>
Lakini agano langu litathibitika kwa Isaka ambaye Sara atakuzalia mwakani wakati kama huu.”
419Mwanzo. 17:22>>
Basi, Mungu alipomaliza kuongea, akamwacha Abrahamu.
420Mwanzo. 17:23>>
Kisha, siku hiyohiyo, Abrahamu akamtahiri mwanawe Ishmaeli na kuwatahiri watumwa wote wa kiume waliozaliwa nyumbani mwake na walionunuliwa kwa fedha zake, kama Mungu alivyomwamuru.
421Mwanzo. 17:24>>
Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 99 alipotahiriwa.
422Mwanzo. 17:25>>
Na Ishmaeli mwanawe alikuwa na umri wa miaka 13 alipotahiriwa.
423Mwanzo. 17:26>>
Abrahamu na mwanawe Ishmaeli
424Mwanzo. 17:27>>
pamoja na wanaume wote wa nyumba yake, watumwa wote waliozaliwa nyumbani mwake na walionunuliwa kwa fedha zake walitahiriwa siku hiyohiyo.
425Mwanzo. 18:1>>
Mwenyezi-Mungu alimtokea Abrahamu penye mialoni ya Mamre. Abrahamu alikuwa ameketi penye mlango wa hema lake wakati wa joto la mchana,
426Mwanzo. 18:2>>
na alipoinua macho yake, akaona watu watatu wamesimama mbali kidogo mbele yake. Mara alipowaona, akapiga mbio kutoka mlangoni mwa hema lake, akaenda kuwalaki. Alipowafikia aliinama kwa heshima na kusema,
427Mwanzo. 18:3>>
“Bwana zangu, kama mnanipenda tafadhali msinipite mimi mtumishi wenu ila mshinde kwangu.
428Mwanzo. 18:4>>
Mtaletewa maji kidogo ili mnawe miguu na kupumzika chini ya mti.
429Mwanzo. 18:5>>
Wakati mnapopumzika, nitaandaa chakula kidogo, mle, ili mpate nguvu za kuendelea na safari yenu; maana mmenijia mimi mtumishi wenu.” Nao wakasema, “Sawa! Fanya kama ulivyosema.”
430Mwanzo. 18:6>>
Abrahamu akarudi haraka hemani akamwambia Sara, “Tayarisha haraka vipimo vitatu vya unga bora, uukande, uoke mikate.”
431Mwanzo. 18:7>>
Kisha akatoka haraka akaenda kwenye kundi la ngômbe, akachagua ndama mmoja mzuri na mnono, akamkabidhi mtumishi ambaye aliharakisha kumchinja na kumpika.
432Mwanzo. 18:8>>
Halafu Abrahamu akachukua siagi, maziwa na ile nyama iliyotayarishwa, akawaandalia wageni hao chakula; naye akasimama karibu nao kuwahudumia walipokuwa wakila chini ya mti.
433Mwanzo. 18:9>>
Wale wageni wakamwuliza, “Mkeo Sara yuko wapi?” Abrahamu akawajibu, “Yumo hemani.”
434Mwanzo. 18:10>>
Mmoja wao akasema, “Hakika nitakurudia wakati kama huu mwakani, na mkeo Sara atakuwa na mtoto wa kiume.” Sara alikuwa huko nyuma mlangoni mwa hema, akisikiliza.
435Mwanzo. 18:11>>
Abrahamu na Sara walikuwa wakongwe, naye Sara mambo ya kawaida ya wanawake yalikuwa yamekoma kitambo.
436Mwanzo. 18:12>>
Kwa hiyo, Sara alicheka kimoyomoyo akisema, “Mimi ni mzee, na mume wangu hali kadhalika. Je, nikiwa mzee hivi, nitaweza kufurahi na kupata watoto?”
437Mwanzo. 18:13>>
Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kujiuliza kama kweli itawezekana apate mtoto akiwa mzee?
438Mwanzo. 18:14>>
Je, kuna jambo lolote lisilowezekana kwa Mwenyezi-Mungu? Nitakurudia wakati uliopangwa, wakati kama huu mwakani, na Sara atakuwa na mtoto wa kiume.”
439Mwanzo. 18:15>>
Lakini Sara, akiwa na hofu, akakana akisema, “Sikucheka!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sivyo! Kucheka, ulicheka.”
440Mwanzo. 18:16>>
Ndipo wale watu wakaondoka, wakafika mahali walipoweza kuona mji wa Sodoma; naye Abrahamu akawasindikiza.
441Mwanzo. 18:17>>
Basi, Mwenyezi-Mungu akawaza: Je, nimfiche Abrahamu jambo ambalo nimepanga kutenda?
442Mwanzo. 18:18>>
Yeye atakuwa baba wa taifa kubwa na kwake mataifa yote ya ulimwengu yatabarikiwa!
443Mwanzo. 18:19>>
Nimemchagua yeye na wazawa wake. Yeye atawafunza wazawa wake kushika njia yangu: Wawe waadilifu na wenye kutenda mambo ya haki, nami nipate kuwatimizia ahadi zangu.
444Mwanzo. 18:20>>
Basi, Mwenyezi-Mungu akasema, “Kuna malalamiko mengi dhidi ya watu wa Sodoma na Gomora, na dhambi yao ni kubwa mno.
445Mwanzo. 18:21>>
Hivyo nitashuka kwenda huko nijionee mwenyewe kama kweli wamefanya kadiri ya kilio kilichonifikia. Nataka kujua.”
446Mwanzo. 18:22>>
Kutoka hapo, wale watu wakashika njia kuelekea Sodoma, lakini Mwenyezi-Mungu akawa amebaki, amesimama pamoja na Abrahamu.
447Mwanzo. 18:23>>
Basi, Abrahamu akamkaribia Mwenyezi-Mungu, akamwuliza, “Je, kweli utawaangamiza watu wema pamoja na waovu?
448Mwanzo. 18:24>>
Huenda ikawa mna watu wema hamsini humo mjini. Je, utauangamiza mji mzima badala ya kuuacha kwa sababu ya hao wema hamsini waliomo humo?
449Mwanzo. 18:25>>
Sidhani kama utafanya hivyo! Kuwaua watu wema pamoja na waovu; wema kutendewa sawa na waovu! La, hasha! Hakimu wa dunia yote hataacha kutenda yaliyo sawa!”
450Mwanzo. 18:26>>
Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nikikuta watu wema hamsini kule mjini Sodoma, basi nitauacha mji wote salama kwa ajili yao.”
451Mwanzo. 18:27>>
Abrahamu akasema, “Nimethubutu kuzungumza na Bwana, mimi niliye mavumbi na majivu tu.
452Mwanzo. 18:28>>
Huenda wakapatikana watu wema arubaini na watano badala ya hamsini. Je, utauangamiza mji mzima kwa sababu wamepungua watu watano?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sitauangamiza mji ikiwa kuna watu wema arubaini na watano.”
453Mwanzo. 18:29>>
Abrahamu akaongeza kusema, “Pengine watu arubaini watapatikana humo.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa ajili ya watu wema arubaini, sitafanya hivyo.”
454Mwanzo. 18:30>>
Abrahamu akaongeza kusema, “Ee Bwana, naomba usinikasirikie, nami nitasema tena. Huenda wakapatikana watu wema thelathini.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sitafanya hivyo nikiwakuta hao thelathini.”
455Mwanzo. 18:31>>
Abrahamu akasema, “Nimethubutu kuzungumza na Bwana. Labda watapatikana watu wema ishirini.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.”
456Mwanzo. 18:32>>
Hatimaye, Abrahamu akasema, “Ee Bwana, nakuomba usikasirike, ila nitasema tena mara moja tu. Je, wakipatikana watu wema kumi, itakuwaje?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa ajili ya hao watu wema kumi, sitauangamiza mji huo.”
457Mwanzo. 18:33>>
Mwenyezi-Mungu alipomaliza kuzungumza na Abrahamu, alikwenda zake; naye Abrahamu akarudi nyumbani kwake.
458Mwanzo. 19:1>>
Wale malaika wawili wakawasili mjini Sodoma jioni. Loti ambaye alikuwa ameketi penye lango la mji wa Sodoma, alipowaona, aliinuka kuwalaki, akainama kwa heshima,
459Mwanzo. 19:2>>
akasema, “Bwana zangu, karibuni nyumbani kwangu mimi mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala kwangu usiku wa leo. Asubuhi na mapema mtaweza kuendelea na safari yenu.” Lakini, wao wakasema, “La! Sisi tutalala huku mtaani.”
460Mwanzo. 19:3>>
Loti akawasihi sana, mwishowe wakakubali, wakageuka na kuingia nyumbani kwake. Loti akawaandalia karamu, akaoka mikate isiyotiwa chachu, wakala.
461Mwanzo. 19:4>>
Lakini kabla ya kulala usiku, wanaume wote wa mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, bila kubaki hata mmoja, wakaizingira nyumba ya Loti.
462Mwanzo. 19:5>>
Wakamwita Loti na kumwuliza, “Wako wapi wale wanaume waliokuja kwako? Watoe nje. Tunataka kulala nao.”
463Mwanzo. 19:6>>
Loti akatoka nje, akafunga mlango nyuma yake,
464Mwanzo. 19:7>>
akawaambia, “Ndugu zangu, nawasihi msitende uovu huo.
465Mwanzo. 19:8>>
Tazama, ninao binti wawili ambao bado hawajalala na mwanamume. Mniruhusu niwapeni hao wasichana muwatendee kama mpendavyo. Lakini msiwatende lolote wanaume hawa kwa sababu ni wageni wangu.”
466Mwanzo. 19:9>>
Lakini wao wakasema, “Tupishe! Wewe ulikuja huku ukiwa mgeni na sasa wajifanya hakimu! Basi, tutakutenda mabaya zaidi ya hao wageni wako.” Hapo wakamsukuma Loti nyuma hata karibu wauvunje mlango wake.
467Mwanzo. 19:10>>
Lakini wale wageni wakanyosha mikono yao, wakamvuta Loti ndani ya nyumba na kuufunga mlango.
468Mwanzo. 19:11>>
Kisha wakawapiga kwa kuwapofusha macho wanaume wote waliokuwapo mlangoni, wakubwa kwa wadogo, hata wakataabika kuutafuta ule mlango, wasiupate.
469Mwanzo. 19:12>>
Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Je, una mtu mwingine hapa, pengine wana, mabinti, wachumba wa binti zako au watu wengine wa jamaa yako wanaoishi mjini humu? Watoe mahali hapa haraka,
470Mwanzo. 19:13>>
kwa maana kilio kilichomfikia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wakazi wa hapa ni kikubwa mno, naye ametutuma tuje kuwaangamiza.”
471Mwanzo. 19:14>>
Basi, Loti akawaendea wachumba wa binti zake, akawaambia, “Haraka! Tokeni mahali hapa, maana Mwenyezi-Mungu atauangamiza mji huu.” Lakini wao wakamwona kama mtu mcheshi tu.
472Mwanzo. 19:15>>
Kulipokucha, malaika wakamhimiza Loti wakisema, “Amka, mchukue mkeo na hawa binti zako wawili msije mkaangamia wakati mji huu unapoadhibiwa.”
473Mwanzo. 19:16>>
Loti akawa anasitasita. Lakini kwa vile Mwenyezi-Mungu alivyomhurumia Loti, wale malaika wakamshika yeye, mkewe na binti zake wawili, wakamtoa nje ya mji.
474Mwanzo. 19:17>>
Walipowatoa nje ya mji, malaika mmoja wao akawaambia, “Kimbieni kwa usalama wenu. Msiangalie nyuma wala kusimama popote bondeni. Kimbilieni milimani, msije mkaangamia.”
475Mwanzo. 19:18>>
Loti akawaambia, “La, bwana zangu!
476Mwanzo. 19:19>>
Ni kweli kwamba mimi mtumishi wenu nimepata fadhili mbele yenu, nanyi mmenionea huruma sana kwa kuyaokoa maisha yangu; lakini milimani ni mbali mno. Maangamizi haya yatanikuta kabla sijafika huko, nami nitakufa.
477Mwanzo. 19:20>>
Tazameni, kule kuna mji mdogo ambao naweza kuukimbilia kwani uko karibu. Basi, mniruhusu nikimbilie huko. Ule ni mji mdogo tu, na huko nitasalimika.”
478Mwanzo. 19:21>>
Naye akamjibu, “Sawa, nimekubali ombi lako. Sitauangamiza mji ulioutaja.
479Mwanzo. 19:22>>
Harakisha! Kimbilia huko, nami sitafanya lolote mpaka utakapowasili huko.” Hivyo mji huo ukaitwa Soari.
480Mwanzo. 19:23>>
Jua lilikuwa limekwisha chomoza wakati Loti alipowasili mjini Soari.
481Mwanzo. 19:24>>
Ndipo Mwenyezi-Mungu akateremsha moto mkali wa kiberiti kutoka mbinguni juu ya Sodoma na Gomora,
482Mwanzo. 19:25>>
akaiangamiza miji hiyo, bonde lote, wakazi wake wote na mimea yote katika nchi hiyo.
483Mwanzo. 19:26>>
Lakini mkewe Loti aliyekuwa nyuma ya Loti, akatazama nyuma, akageuka nguzo ya chumvi.
484Mwanzo. 19:27>>
Asubuhi na mapema, Abrahamu alikwenda mahali alipokuwa amesimama mbele ya Mwenyezi-Mungu.
485Mwanzo. 19:28>>
Akiwa hapo, akatazama chini pande za Sodoma na Gomora na eneo lote la bondeni, akashangaa kuona moshi ukipanda, moshi kama wa tanuri kubwa.
486Mwanzo. 19:29>>
Mungu alipoiangamiza miji ya bondeni alimokuwa anakaa Loti, alimkumbuka Abrahamu kwa kumtoa Loti katika miji hiyo, ili Loti asije akaangamia pamoja nayo.
487Mwanzo. 19:30>>
Loti aliogopa kuishi mjini Soari, kwa hiyo akauhama mji huo, yeye pamoja na binti zake wawili, wakaenda kuishi pangoni, milimani.
488Mwanzo. 19:31>>
Wakiwa huko, binti mkubwa akamwambia dada yake, “Baba yetu ni mzee, na hakuna mwanamume nchini wa kutuoa tupate watoto.
489Mwanzo. 19:32>>
Basi, tumlevye baba kwa divai, ili tupate kulala naye na kudumisha uzawa kwa kupata watoto kwake.”
490Mwanzo. 19:33>>
Usiku huo wakamlevya baba yao kwa divai, na yule binti wa kwanza akaenda akalala naye. Lakini baba yake hakujua wakati bintiye alipolala naye, wala alipoondoka.
491Mwanzo. 19:34>>
Kesho yake, yule binti wa kwanza akamwambia yule mdogo, “Jana usiku mimi nililala na baba; leo pia tumlevye kwa divai, kisha wewe utalala naye, na hivyo sote tutadumisha uzao kwa kupata watoto.”
492Mwanzo. 19:35>>
Basi, usiku huo pia wakamlevya baba yao kwa divai, kisha yule binti mdogo akaenda akalala naye. Lakini baba yake hakujua wakati bintiye alipolala naye, wala alipoondoka.
493Mwanzo. 19:36>>
Hivyo, binti wote wawili wa Loti wakapata mimba kutokana na baba yao.
494Mwanzo. 19:37>>
Yule binti wa kwanza akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Moabu. Huyo ndiye baba wa Wamoabu hadi leo.
495Mwanzo. 19:38>>
Yule mdogo pia akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Ben-ami. Huyo ndiye baba wa Waamoni hadi leo.
496Mwanzo. 20:1>>
Toka Mamre, Abrahamu alisafiri kuelekea eneo la Negebu, akafanya makao yake kati ya Kadeshi na Shuri, kisha akaenda kukaa kwa muda huko Gerari.
497Mwanzo. 20:2>>
Akiwa huko, Abrahamu alisema kuwa mkewe Sara ni dada yake. Kwa hiyo, mfalme Abimeleki wa Gerari akamchukua Sara.
498Mwanzo. 20:3>>
Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto usiku, akamwambia, “Wewe utakufa kwa sababu ya mwanamke uliyemchukua, kwani ana mumewe.”
499Mwanzo. 20:4>>
Abimeleki ambaye bado hakuwa amelala na Sara, akajibu, “Bwana, utawaua watu wasio na hatia.
500Mwanzo. 20:5>>
Abrahamu mwenyewe ndiye aliyesema kuwa huyu ni dada yake. Tena hata Sara mwenyewe alisema kuwa Abrahamu ni kaka yake! Mimi nimefanya nilivyofanya kwa moyo mnyofu na sina hatia.”
501Mwanzo. 20:6>>
Basi, Mungu akamwambia katika hiyo ndoto, “Sawa. Najua kwamba umefanya hivyo kwa moyo mnyofu, na mimi ndiye niliyekuzuia kutenda dhambi dhidi yangu; ndiyo maana sikukuruhusu umguse huyo mwanamke.
502Mwanzo. 20:7>>
Sasa mrudishe huyo mwanamke kwa mume wake. Abrahamu ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini usipomrudisha, ujue kwa hakika kwamba wewe utakufa pamoja na watu wako wote.”
503Mwanzo. 20:8>>
Basi, Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumishi wake wote na kuwaeleza mambo aliyoyaona katika ndoto; nao wakaogopa sana.
504Mwanzo. 20:9>>
Ndipo Abimeleki akamwita Abrahamu, akamwuliza, “Umetutendea nini? Nimekukosea nini hata ukaniletea balaa hili mimi na ufalme wangu? Umenitendea mambo yasiyostahili kutendwa.”
505Mwanzo. 20:10>>
Tena Abimeleki akazidi kumwuliza, “Ni kitu gani kimekusukuma kufanya hivyo?”
506Mwanzo. 20:11>>
Abrahamu akamjibu, “Nilifanya hivyo kwa kuwa hakuna amchaye Mungu mahali hapa, na kwamba mngeniua ili mumchukue mke wangu.
507Mwanzo. 20:12>>
Zaidi ya hayo, kwa kweli, yeye ni dada yangu: Baba yake na baba yangu ni mmoja, lakini mama tofauti; ndiyo maana akawa mke wangu.
508Mwanzo. 20:13>>
Wakati Mungu aliponifanya niiache nyumba ya baba yangu na kwenda ugenini, nilimwambia mke wangu, ‘Popote tutakapokwenda tafadhali useme kwamba mimi ni kaka yako!’”
509Mwanzo. 20:14>>
Abimeleki akamrudishia Abrahamu mke wake Sara, akampa na kondoo, ngômbe na watumwa wa kiume na kike.
510Mwanzo. 20:15>>
Tena Abimeleki akamwambia Abrahamu, “Tazama, nchi hii yote ni yangu! Basi, chagua popote upendapo, ukae.”
511Mwanzo. 20:16>>
Kisha, akamwambia Sara, “Tazama, mimi nimempa ndugu yako vipande 1,000 vya fedha ili kuwaonesha wote walio pamoja nawe kwamba huna hatia; umethibitishwa huna lawama.”
512Mwanzo. 20:17>>
Kisha Abrahamu akamwomba Mungu, naye akamponya Abimeleki, mkewe na mjakazi wake, hata wakaweza kupata tena watoto.
513Mwanzo. 20:18>>
Hapo kwanza Mwenyezi-Mungu alikuwa amewazuia wanawake wote wa nyumba ya Abimeleki kupata watoto kwa sababu ya Sara, mke wa Abrahamu.
514Mwanzo. 21:1>>
Mwenyezi-Mungu alimkumbuka Sara, akamtendea kama alivyoahidi.
515Mwanzo. 21:2>>
Basi, Abrahamu akiwa mzee, Sara akapata mimba, akamzalia mtoto wa kiume, wakati uleule Mungu alioutaja.
516Mwanzo. 21:3>>
Abrahamu akampa huyo mwanawe ambaye Sara alimzalia jina Isaka.
517Mwanzo. 21:4>>
Isaka alipotimiza umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri kama alivyoamriwa na Mungu.
518Mwanzo. 21:5>>
Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 100 wakati mwanawe Isaka alipozaliwa.
519Mwanzo. 21:6>>
Naye Sara akasema, “Mungu amenipatia kicheko; yeyote atakayesikia habari hizi, atacheka pamoja nami.”
520Mwanzo. 21:7>>
Kisha akaongeza, “Ni nani angeweza kumwambia Abrahamu kwamba mimi Sara nitanyonyesha watoto? Tena nimemzalia mtoto wa kiume katika uzee wake!”
521Mwanzo. 21:8>>
Isaka akaendelea kukua, na siku alipoachishwa kunyonya, Abrahamu akafanya sherehe kubwa.
522Mwanzo. 21:9>>
Baadaye Sara alimwona Ishmaeli, mtoto wa Abrahamu aliyezaliwa na Hagari, Mmisri, akicheza na Isaka mwanawe.
523Mwanzo. 21:10>>
Basi, Sara akamwambia Abrahamu, “Mfukuzie mbali mjakazi huyu na mwanawe. Haiwezekani kabisa mtoto wa mjakazi kurithi pamoja na mwanangu Isaka.”
524Mwanzo. 21:11>>
Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa kuwa Ishmaeli pia alikuwa mtoto wake.
525Mwanzo. 21:12>>
Lakini Mungu akamwambia Abrahamu, “Usihuzunike kwa sababu ya mtoto huyu, wala huyo mtumwa wako wa kike. Lolote akuambialo Sara lifanye; kwa kweli wazawa wako watatokana na Isaka.
526Mwanzo. 21:13>>
Na kuhusu huyo mwana wa mjakazi wako, nitamfanya awe baba wa taifa kubwa kwa kuwa yeye pia ni mtoto wako.”
527Mwanzo. 21:14>>
Hivyo, asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari na kumtwika begani; akamfukuza pamoja na mwanawe. Hagari akaondoka, akawa anatangatanga nyikani Beer-sheba.
528Mwanzo. 21:15>>
Ikawa maji yalipomwishia katika kile kiriba, Hagari akamlaza mwanawe chini ya mti.
529Mwanzo. 21:16>>
Naye akaenda kando, akaketi umbali wa kama mita 100 hivi, akisema moyoni mwake, “Heri nisimwone mwanangu akifa.” Na alipokuwa ameketi hapo, mtoto akalia kwa sauti.
530Mwanzo. 21:17>>
Mungu akamsikia mtoto huyo akilia, na malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni, akamwambia, “Una shida gani Hagari? Usiogope; Mungu amesikia sauti ya mtoto huko alipo.
531Mwanzo. 21:18>>
Simama umwinue mtoto na kumshika vizuri mikononi mwako, kwani nitamfanya awe baba wa taifa kubwa.”
532Mwanzo. 21:19>>
Mungu akamfumbua Hagari macho, naye akaona kisima cha maji. Akaenda akajaza kiriba maji, akamnywesha mtoto wake.
533Mwanzo. 21:20>>
Mungu akawa pamoja na huyo mtoto, naye akaendelea kukua. Alikaa nyikani na akawa mpiga upinde hodari sana.
534Mwanzo. 21:21>>
Alikuwa akikaa katika nyika za Parani, na mama yake akamwoza mke kutoka nchi ya Misri.
535Mwanzo. 21:22>>
Wakati huo, Abimeleki pamoja na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, alimwendea Abrahamu, akamwambia, “Mungu yuko pamoja nawe katika kila kitu unachofanya.
536Mwanzo. 21:23>>
Kwa hiyo niapie kwa jina la Mungu kwamba hutanifanyia hila mimi au watoto wangu au wazawa wangu. Kadiri mimi nilivyokuwa mwaminifu kwako, vivyo hivyo nawe uwe mwaminifu kwangu na kwa nchi hii unamokaa.”
537Mwanzo. 21:24>>
Abrahamu akasema, “Naapa.”
538Mwanzo. 21:25>>
Wakati huo Abrahamu alikuwa amemlalamikia Abimeleki juu ya kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyanganya.
539Mwanzo. 21:26>>
Abimeleki akamwambia, “Mimi sijui nani aliyefanya hivyo; mpaka leo hii wewe hukuniambia; wala mimi sijapata kusikia habari hizi hadi leo.”
540Mwanzo. 21:27>>
Basi, Abrahamu akachukua kondoo na ngômbe akampa Abimeleki nao wawili wakafanya agano baina yao.
541Mwanzo. 21:28>>
Abrahamu akatenga wanakondoo wa kike saba.
542Mwanzo. 21:29>>
Abimeleki akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini unawatenga hao wanakondoo wa kike saba?”
543Mwanzo. 21:30>>
Abrahamu akamjibu, “Hawa wanakondoo wa kike saba ninakupa kwa mkono wangu mwenyewe kama shahidi wangu kwamba mimi ndimi niliyechimba kisima hiki.”
544Mwanzo. 21:31>>
Kwa hiyo kisima hicho kikaitwa Beer-sheba, maana wote wawili walikula kiapo mahali hapo.
545Mwanzo. 21:32>>
Hivyo, wakafanya agano huko Beer-sheba. Abimeleki na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, akaondoka na kurudi katika nchi ya Wafilisti.
546Mwanzo. 21:33>>
Abrahamu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akamwabudu Mungu, Mungu wa milele.
547Mwanzo. 21:34>>
Abrahamu alikaa katika nchi ya Wafilisti muda mrefu.
548Mwanzo. 22:1>>
Baada ya muda fulani, Mungu alimjaribu Abrahamu. Mungu alimwita, “Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam nasikiliza.”
549Mwanzo. 22:2>>
Mungu akamwambia, “Mchukue mwanao, Isaka, mwanao wa pekee umpendaye, uende mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuonesha.”
550Mwanzo. 22:3>>
Basi, kesho yake, Abrahamu akaamka asubuhi na mapema, akatandika punda wake, akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Akatayarisha kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kisha akaanza safari kuelekea mahali alipoambiwa na Mungu.
551Mwanzo. 22:4>>
Mnamo siku ya tatu, Abrahamu aliinua macho akapaona mahali hapo kwa mbali.
552Mwanzo. 22:5>>
Akawaambia wale watumishi wake, “Ngojeni hapa na huyu punda. Mimi na mwanangu tutakwenda mpaka kule, tukamwabudu Mungu, kisha tutawarudiani.”
553Mwanzo. 22:6>>
Basi, Abrahamu akazitwaa zile kuni, akamtwika Isaka mwanawe; yeye mwenyewe akachukua moto na kisu mkononi; wakaondoka pamoja.
554Mwanzo. 22:7>>
Isaka akamwuliza baba yake, “Baba, moto na kuni tunazo; lakini mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa yuko wapi?”
555Mwanzo. 22:8>>
Abrahamu akamjibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atatujalia mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa.” Basi, wakaendelea na safari yao.
556Mwanzo. 22:9>>
Walipofika mahali ambapo Mungu alimwagiza, Abrahamu akajenga madhabahu na kupanga kuni juu yake. Kisha akamfunga Isaka mwanawe na kumlaza juu ya kuni juu ya madhabahu.
557Mwanzo. 22:10>>
Abrahamu akaunyosha mkono wake, akatwaa kisu tayari kumchinja mwanawe.
558Mwanzo. 22:11>>
Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita kutoka mbinguni, “Abrahamu! Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam, nasikiliza!”
559Mwanzo. 22:12>>
Malaika akamwambia, “Usimdhuru mtoto wala usimfanye lolote! Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwani hukuninyima hata mwanao wa pekee.”
560Mwanzo. 22:13>>
Ndipo Abrahamu akatazama, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake kichakani. Basi, akaenda, akamchukua huyo kondoo, akamtoa sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.
561Mwanzo. 22:14>>
Kwa hiyo, Abrahamu akapaita mahali hapo, “Mwenyezi-Mungu hujalia.” Kama isemwavyo hata leo, “Katika mlima wa Mwenyezi-Mungu, watu hujaliwa.”
562Mwanzo. 22:15>>
Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita Abrahamu mara ya pili kutoka mbinguni,
563Mwanzo. 22:16>>
akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimeapa kwa nafsi yangu kwamba kwa kuwa umefanya hivi, wala hukuninyima mwanao wa pekee,
564Mwanzo. 22:17>>
hakika nitakubariki, na wazawa wako nitawazidisha kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ufuoni mwa bahari. Wazawa wako wataimiliki miji ya adui zao.
565Mwanzo. 22:18>>
Kutokana na wazawa wako mataifa yote duniani yatabarikiwa kwa sababu wewe umeitii amri yangu.”
566Mwanzo. 22:19>>
Basi, Abrahamu akawarudia wale watumishi wake, nao kwa pamoja wakaondoka, wakarudi Beer-sheba; Abrahamu akakaa huko Beer-sheba.
567Mwanzo. 22:20>>
Baada ya matukio hayo Abrahamu alipata habari kwamba Milka pia amemzalia Nahori, nduguye, watoto wa kiume:
568Mwanzo. 22:21>>
Usi mzaliwa wa kwanza, Buzi ndugu yake, Kemueli baba yake Aramu,
569Mwanzo. 22:22>>
Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.
570Mwanzo. 22:23>>
Bethueli alimzaa Rebeka. Milka alimzalia Nahori, ndugu yake Abrahamu, watoto hao wanane.
571Mwanzo. 22:24>>
Zaidi ya hayo, Reuma, suria wa Nahori, pia alimzalia watoto: Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.
572Mwanzo. 23:1>>
Sara aliishi miaka 127. Hiyo ndiyo iliyokuwa miaka ya maisha yake Sara.
573Mwanzo. 23:2>>
Alifia huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Abrahamu akaomboleza na kumfanyia matanga Sara mkewe.
574Mwanzo. 23:3>>
Abrahamu akaiacha maiti ya mkewe, akatoka kwenda kuzungumza na Wahiti, akawaambia,
575Mwanzo. 23:4>>
“Mimi ninaishi kama mgeni miongoni mwenu. Nipatieni sehemu ya ardhi ya kaburi, ili nipate kumzika marehemu mke wangu.”
576Mwanzo. 23:5>>
Wahiti wakamjibu,
577Mwanzo. 23:6>>
“Ee bwana wetu, tusikilize; wewe ni kiongozi maarufu miongoni mwetu. Mzike marehemu mkeo katika kaburi lolote utakalojichagulia; hakuna yeyote miongoni mwetu atakayekunyima kaburi lake, wala kukuzuia kumzika marehemu mkeo.”
578Mwanzo. 23:7>>
Hapo Abrahamu akasimama na kuinama kwa heshima mbele ya wananchi Wahiti,
579Mwanzo. 23:8>>
akawaambia, “Ikiwa mnaniruhusu nimzike marehemu mke wangu, tafadhali mwombeni Efroni mwana wa Sohari, kwa niaba yangu,
580Mwanzo. 23:9>>
aniuzie lile pango lake la Makpela lililo mpakani mwa shamba lake. Msihini aniuzie nilifanye makaburi yangu; anipatie kwa bei ya haki papa hapa mbele yenu.”
581Mwanzo. 23:10>>
Efroni mwenyewe alikuwa miongoni mwa Wahiti hao waliokuwa wamekutanika penye lango la mji. Basi, Efroni Mhiti, akamjibu Abrahamu, mbele ya Wahiti wote hapo langoni,
582Mwanzo. 23:11>>
“La, bwana; tafadhali unisikilize. Ninakupa shamba lote na pango lililomo humo; tena ninakupa mbele ya wananchi wenzangu. Mzike humo marehemu mkeo.”
583Mwanzo. 23:12>>
Abrahamu akainama tena kwa heshima mbele ya wananchi,
584Mwanzo. 23:13>>
akamwambia Efroni, wananchi wote wakisikia, “Nakuomba, tafadhali unisikilize. Nitakulipa bei kamili ya shamba lako, na ninakuomba upokee malipo haya, ili nipate kumzika humo marehemu mke wangu.”
585Mwanzo. 23:14>>
Efroni akamjibu Abrahamu, “Bwana, nisikilize;
586Mwanzo. 23:15>>
shamba lenye thamani ya shekeli 400 tu za fedha ni nini kati yako na mimi? Mzike marehemu mke wako.”
587Mwanzo. 23:16>>
Abrahamu akakubaliana na Efroni, akampimia kiasi cha fedha alichotaja mbele ya Wahiti wote, fedha shekeli 400, kadiri ya vipimo vya wafanyabiashara wa wakati huo.
588Mwanzo. 23:17>>
Basi, shamba la Efroni lililoko huko Makpela, mashariki ya Mamre, pango na miti yote iliyokuwamo pamoja na eneo zima, likawa lake
589Mwanzo. 23:18>>
Abrahamu mbele ya Wahiti wote waliokutanika penye lango la mji.
590Mwanzo. 23:19>>
Baada ya hayo, Abrahamu akamzika Sara mkewe katika pango hilo lililokuwamo katika shamba la Makpela, mashariki ya Mamre (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani.
591Mwanzo. 23:20>>
Shamba na pango lililokuwamo humo lilithibitishwa na Wahiti liwe mali yake Abrahamu apate kuzika humo wafu wake.
592Mwanzo. 24:1>>
Sasa Abrahamu alikuwa mzee wa miaka mingi, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa amembariki katika kila hali.
593Mwanzo. 24:2>>
Siku moja Abrahamu akamwambia mtumishi wake aliyekuwa mzee kuliko wengine na msimamizi wa mali yake yote, “Weka mkono wako mapajani mwangu,
594Mwanzo. 24:3>>
nami nitakuapisha kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu na dunia, kwamba hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ninaoishi nao.
595Mwanzo. 24:4>>
Niapie kwamba utakwenda mpaka katika nchi yangu, kwa jamaa zangu, umtafutie mwanangu Isaka mke.”
596Mwanzo. 24:5>>
Mtumishi akamwambia, “Huenda mwanamke huyo atakataa kufuatana nami kuja huku, ikiwa hivyo, je, ni lazima nimrudishe mwanao nchini ulikotoka?”
597Mwanzo. 24:6>>
Abrahamu akamwambia, “La! Angalia sana usimrudishe mwanangu huko.
598Mwanzo. 24:7>>
Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani kwa baba yangu na kutoka katika nchi nilimozaliwa, na ambaye alisema nami, aliniapia kwamba atawapa wazawa wangu nchi hii. Yeye atamtuma malaika wake mbele yako ili umletee mwanangu mke kutoka huko.
599Mwanzo. 24:8>>
Iwapo mwanamke huyo hatapenda kufuatana nawe hadi huku, basi kiapo changu hakitakufunga, lakini kwa vyovyote vile usimrudishe mwanangu huko.”
600Mwanzo. 24:9>>
Basi, mtumishi huyo akaweka mkono wake mapajani mwa Abrahamu, bwana wake, akaapa kuhusu jambo hilo.
601Mwanzo. 24:10>>
Kisha, huyo mtumishi akachukua ngamia kumi wa bwana wake akaondoka akiwa na zawadi nzuri za kila aina. Akasafiri kwenda katika mji alimokaa Nahori, nchini Mesopotamia.
602Mwanzo. 24:11>>
Alipowasili, aliwapigisha magoti ngamia wake kando ya kisima kilichokuwa nje ya mji. Ilikuwa jioni wakati ambapo wanawake huenda kisimani kuteka maji.
603Mwanzo. 24:12>>
Naye akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba unijalie nifaulu leo na umfadhili Abrahamu bwana wangu.
604Mwanzo. 24:13>>
Niko hapa kando ya kisima ambapo binti za wenyeji wa mji huja kuteka maji.
605Mwanzo. 24:14>>
Basi, msichana nitakayemwambia atue mtungi wake wa maji anipatie maji ninywe, naye akanipa mimi pamoja na kuwanywesha ngamia wangu, na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka. Jambo hilo litanionesha kwamba umemfadhili bwana wangu.”
606Mwanzo. 24:15>>
Kabla hajamaliza kuomba, mara Rebeka, binti Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu yake Abrahamu, akafika amebeba mtungi wake begani.
607Mwanzo. 24:16>>
Msichana huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, na bikira ambaye hakuwa amelala na mwanamume yeyote. Basi, akateremka kisimani, akaujaza mtungi wake maji na kupanda.
608Mwanzo. 24:17>>
Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye, akamwambia, “Tafadhali, nipatie maji ya kunywa kutoka mtungi wako.”
609Mwanzo. 24:18>>
Msichana akamjibu, “Haya kunywa bwana wangu.” Na papo hapo akautua mtungi wake, akiushikilia ili amnyweshe.
610Mwanzo. 24:19>>
Alipokwisha kumpatia maji, akamwambia, “Nitawatekea maji ngamia wako pia, wanywe mpaka watosheke.”
611Mwanzo. 24:20>>
Basi, akafanya haraka, akawamiminia ngamia maji ya mtungi wake katika hori, akakimbia kisimani kuteka maji mengine na kuwanywesha ngamia wake wote.
612Mwanzo. 24:21>>
Yule mtu akawa anamtazama kwa makini bila kusema lolote, apate kufahamu kama Mwenyezi-Mungu ameifanikisha safari yake au sivyo.
613Mwanzo. 24:22>>
Ngamia walipotosheka kunywa maji, yule mtu akampa huyo msichana pete ya dhahabu yenye uzito upatao gramu sita, na bangili mbili za dhahabu za gramu kumi kila moja.
614Mwanzo. 24:23>>
Akamwuliza, “Niambie tafadhali: Wewe ni binti nani? Je, kuna nafasi ya kulala nyumbani kwenu?”
615Mwanzo. 24:24>>
Rebeka akajibu, “Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori.
616Mwanzo. 24:25>>
Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha na mahali pa kulala wageni.”
617Mwanzo. 24:26>>
Ndipo yule mtu akainamisha kichwa chake, akamwabudu Mwenyezi-Mungu
618Mwanzo. 24:27>>
akisema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hajasahau fadhili zake na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mwenyezi-Mungu ameniongoza mimi mwenyewe moja kwa moja hadi kwa jamaa ya bwana wangu!”
619Mwanzo. 24:28>>
Kisha yule msichana akakimbia kwenda kuwapa habari jamaa za mama yake.
620Mwanzo. 24:29>>
Rebeka alikuwa na kaka yake aitwaye Labani. Labani akatoka mbio kukutana na yule mtu kisimani.
621Mwanzo. 24:30>>
Labani alikuwa ameiona ile pete na bangili mikononi mwa dada yake, na kusikia mambo Rebeka aliyoambiwa na huyo mtu. Labani alimkuta yule mtu amesimama karibu na ngamia wake kando ya kisima.
622Mwanzo. 24:31>>
Labani akamwambia, “Karibu kwetu wewe uliyebarikiwa na Mwenyezi-Mungu. Mbona unasimama nje? Mimi mwenyewe nimekwisha tayarisha nyumba na mahali kwa ajili ya hawa ngamia wako!”
623Mwanzo. 24:32>>
Basi, mtumishi huyo wa Abrahamu akaingia nyumbani. Labani akawafungua ngamia na kuwapatia majani ngamia wake, akampa yeye na watu wake maji ya kunawa miguu.
624Mwanzo. 24:33>>
Basi, wakamwandalia chakula, lakini yeye akasema, “Sitakula mpaka nimesema ninachotaka kusema.” Labani akamwambia, “Haya, tuambie.”
625Mwanzo. 24:34>>
Yule mtu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu.
626Mwanzo. 24:35>>
Mwenyezi-Mungu amembariki sana bwana wangu, naye amekuwa mtu maarufu. Amempa makundi ya kondoo na mifugo mingi, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda!
627Mwanzo. 24:36>>
Sara, mke wa bwana wangu katika uzee wake, alimzalia bwana wangu mtoto; na bwana wangu amempa huyo mtoto mali yake yote.
628Mwanzo. 24:37>>
Bwana wangu aliniapisha mimi akisema, ‘Hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ambao ninaishi katika nchi yao.
629Mwanzo. 24:38>>
Bali utakwenda mpaka nchi yangu, kwa jamaa zangu, ili umtafutie mwanangu Isaka mke.’
630Mwanzo. 24:39>>
Nami nikamwambia bwana wangu, ‘Huenda mwanamke huyo akakataa kufuatana nami kuja huku.’
631Mwanzo. 24:40>>
Lakini yeye akasema, ‘Mwenyezi-Mungu aniongozaye maishani mwangu, atamtuma malaika wake aende pamoja nawe na kukufanikisha katika safari yako; nawe utamtwalia mwanangu mke kutoka kwa jamaa yangu na nyumba ya baba yangu.
632Mwanzo. 24:41>>
Kama utakapofika kwa jamaa zangu hawatakupa huyo msichana, basi, hutafungwa na kiapo changu.’
633Mwanzo. 24:42>>
“Leo nilipofika kisimani nimeomba, ‘Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba nifaulu leo katika safari yangu na umfadhili Abrahamu bwana wangu.
634Mwanzo. 24:43>>
Niko hapa kando ya kisima. Msichana atakayekuja kuteka maji ambaye nitamwomba anipatie maji kidogo ya kunywa kutoka mtungi wake,
635Mwanzo. 24:44>>
naye akanipa na kuwatekea maji ngamia wangu, basi huyo na awe ndiye uliyemchagua kuwa mke wa mwana wa bwana wangu.’
636Mwanzo. 24:45>>
“Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, mara Rebeka alifika na mtungi wake wa maji begani, akateremka kisimani na kuteka maji. Nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ya kunywa.’
637Mwanzo. 24:46>>
Naye akautua mtungi wake haraka kutoka begani mwake, akasema, ‘Haya, kunywa bwana wangu. Nitawatekea maji ngamia wako pia.’ Basi mimi nikanywa na ngamia wangu pia akawapa maji.
638Mwanzo. 24:47>>
Ndipo nilipomwuliza, ‘Je, wewe ni binti wa nani?’ Akaniambia, ‘Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori.’ Ndipo nilipompa pete na kumvisha bangili mikononi.
639Mwanzo. 24:48>>
Kisha nikainama na kumwabudu Mwenyezi-Mungu; nikamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye ameniongoza moja kwa moja kwa binti wa ukoo wa bwana wangu kwa ajili ya mwanawe.
640Mwanzo. 24:49>>
Sasa, basi, niambieni kama mko tayari kumtendea bwana wangu kwa uaminifu na haki; kama sivyo, basi semeni, nami nitajua cha kufanya.”
641Mwanzo. 24:50>>
Baada ya kusikia hayo, Labani na Bethueli wakamjibu, “Jambo hili limetoka kwa Mwenyezi-Mungu, sisi hatuwezi kuamua lolote.
642Mwanzo. 24:51>>
Rebeka huyu hapa; mchukue uende. Na awe mke wa mwana wa bwana wako kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.”
643Mwanzo. 24:52>>
Mtumishi wa Abrahamu aliposikia maneno hayo, alimsujudia Mwenyezi-Mungu.
644Mwanzo. 24:53>>
Kisha akatoa vito vya fedha na dhahabu na nguo, akampa Rebeka. Pia aliwapa ndugu na mama yake Rebeka mapambo ya thamani kubwa.
645Mwanzo. 24:54>>
Mtumishi wa Abrahamu na watu aliokuja nao wakala, wakanywa na kulala huko. Walipoamka asubuhi, mtumishi yule akasema, “Naomba kurudi kwa bwana wangu.”
646Mwanzo. 24:55>>
Lakini ndugu na mama yake Rebeka wakasema, “Mwache msichana akae nasi muda mfupi, kama siku kumi hivi; kisha anaweza kwenda.”
647Mwanzo. 24:56>>
Lakini yeye akasema, “Tafadhali, msinicheleweshe, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha fanikisha safari yangu; naomba mniruhusu kurudi kwa bwana wangu.”
648Mwanzo. 24:57>>
Nao wakasema, “Basi, tumwite msichana mwenyewe, tumwulize.”
649Mwanzo. 24:58>>
Wakamwita Rebeka na kumwuliza, “Je, utakwenda na mtu huyu?” Naye akajibu, “Nitakwenda.”
650Mwanzo. 24:59>>
Basi, wakamwacha Rebeka na yaya wake aende na mtumishi wa Abrahamu na watu wake. Yaya wake Rebeka pia aliandamana naye.
651Mwanzo. 24:60>>
Basi, wakambariki Rebeka wakisema, “Ewe dada yetu! Uwe mama wa maelfu kwa maelfu; wazawa wako waimiliki miji ya adui zao.”
652Mwanzo. 24:61>>
Kisha, Rebeka na wajakazi wake wakapanda ngamia na kumfuata huyo mtumishi wa Abrahamu; nao wote wakaondoka.
653Mwanzo. 24:62>>
Wakati huo, Isaka alikuwa ameondoka Beer-lahai-roi, akawa anakaa huko pande za Negebu.
654Mwanzo. 24:63>>
Siku moja jioni, Isaka alikwenda mashambani kutafakari. Basi, akatazama akaona ngamia wanakuja.
655Mwanzo. 24:64>>
Naye Rebeka alipotazama na kumwona Isaka, alishuka chini
656Mwanzo. 24:65>>
na kumwuliza mtumishi wa Abrahamu, “Ni nani yule mtu anayetembea kule shambani, anakuja kutulaki?” Yule mtumishi akasema, “Ni bwana wangu.” Basi, Rebeka akatwaa shela yake, akajifunika uso.
657Mwanzo. 24:66>>
Yule mtumishi akamsimulia Isaka yote aliyokuwa ameyafanya.
658Mwanzo. 24:67>>
Basi, Isaka akamchukua Rebeka ndani ya hema iliyokuwa ya Sara mama yake, akawa mke wake. Isaka akampenda Rebeka na kupata faraja baada ya kifo cha mama yake.
659Mwanzo. 25:1>>
Abrahamu alioa mke mwingine, jina lake Ketura.
660Mwanzo. 25:2>>
Ketura alimzalia Abrahamu: Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua.
661Mwanzo. 25:3>>
Yokshani alimzaa Sheba na Dedani; wazawa wa Dedani walikuwa Waashuru, Waletushi na Waleumi.
662Mwanzo. 25:4>>
Watoto wa Midiani walikuwa Efa, Eferi, Henoki, Abida na Eldaa. Wote hao walikuwa wazawa wa Ketura.
663Mwanzo. 25:5>>
Abrahamu alimrithisha Isaka mali yake yote.
664Mwanzo. 25:6>>
Lakini watoto wa kiume wa masuria wake akawapa zawadi, na wakati alipokuwa bado hai, aliwapeleka katika nchi ya mashariki, mbali na Isaka mwanawe.
665Mwanzo. 25:7>>
Abrahamu aliishi miaka 175.
666Mwanzo. 25:8>>
Alifariki baada ya kuishi maisha marefu na ya fanaka, akajiunga na wazee wake waliomtangulia.
667Mwanzo. 25:9>>
Isaka na Ishmaeli, wanawe Abrahamu, wakamzika baba yao katika pango la Makpela, mashariki ya Mamre kwenye shamba lililokuwa la Efroni, mwana wa Sohari, Mhiti.
668Mwanzo. 25:10>>
Abrahamu alikuwa amenunua shamba hilo kwa Wahiti. Huko ndiko alikozikwa Abrahamu na mkewe Sara.
669Mwanzo. 25:11>>
Baada ya kifo cha Abrahamu, Mungu alimbariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akawa anaishi karibu na kisima cha Beer-lahai-roi.
670Mwanzo. 25:12>>
Hawa ndio wazawa wa Ishmaeli mwanawe Abrahamu ambaye Hagari Mmisri, aliyekuwa mjakazi wa Sara, alimzalia Abrahamu.
671Mwanzo. 25:13>>
Hii ni orodha yao kufuatana na kuzaliwa kwao: Nebayothi, mzaliwa wa kwanza, Kedari, Adbeeli, Mibsamu,
672Mwanzo. 25:14>>
Mishma, Duma, Masa,
673Mwanzo. 25:15>>
Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi na Kedema.
674Mwanzo. 25:16>>
Hao ndio watoto wa kiume wa Ishmaeli, waliokuwa asili ya makabila kumi na mawili; makazi na vijiji vyao vilijulikana kwa majina yao.
675Mwanzo. 25:17>>
Ishmaeli alikuwa na umri wa miaka 137 alipofariki, akajiunga na wazee wake waliotangulia.
676Mwanzo. 25:18>>
Wazawa wa Ishmaeli walikaa katika eneo lililo kati ya Hawila na Shuri, mashariki ya Misri, kuelekea Ashuru. Walikaa kwa utengano na wazawa wengine wa Abrahamu.
677Mwanzo. 25:19>>
Hawa ndio wazawa wa Isaka mwana wa Abrahamu.
678Mwanzo. 25:20>>
Isaka alipokuwa na umri wa miaka arubaini alimwoa Rebeka, binti Bethueli, Mwaramu wa Padan-aramu. Rebeka alikuwa dada yake Labani.
679Mwanzo. 25:21>>
Rebeka alikuwa tasa, kwa hiyo Isaka akamwomba Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu akakubali ombi lake, Rebeka akapata mimba.
680Mwanzo. 25:22>>
Mimba hiyo ilikuwa ya mapacha. Watoto hao wakashindana tumboni mwake Rebeka, naye akasema, “Kama hivi ndivyo mambo yalivyo, ya nini kuishi?” Basi, akaenda kumwuliza Mwenyezi-Mungu.
681Mwanzo. 25:23>>
Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako; makabila mawili yatakayozaliwa nawe, yatafarakana. Moja litakuwa lenye nguvu kuliko lingine; mkubwa atamtumikia mdogo.”
682Mwanzo. 25:24>>
Siku zake za kujifungua zilipotimia, Rebeka alijifungua mapacha.
683Mwanzo. 25:25>>
Wa kwanza alikuwa mwekundu, mwenye nywele mwili wote; hivyo wakamwita Esau.
684Mwanzo. 25:26>>
Wa pili alizaliwa akiwa amemshika Esau kisigino, hivyo wakampa jina Yakobo. Isaka alikuwa na umri wa miaka sitini wakati Esau na Yakobo walipozaliwa.
685Mwanzo. 25:27>>
Watoto hao wakakua; Esau akawa mwindaji hodari, mpenda maisha ya mbugani, na Yakobo akawa mtu mtulivu, mpenda maisha ya nyumbani.
686Mwanzo. 25:28>>
Basi, Isaka akampenda Esau kwa sababu alipenda kula mawindo yake, lakini Rebeka akampenda Yakobo.
687Mwanzo. 25:29>>
Siku moja, Yakobo alipokuwa anapika dengu, Esau alirudi nyumbani kutoka mawindoni ana njaa sana.
688Mwanzo. 25:30>>
Kwa hiyo akamwambia Yakobo, “Nafa njaa; tafadhali, nigawie chakula hicho chekundu nile.” (Ndiyo maana walimpanga jina Edomu yaani mwekundu).
689Mwanzo. 25:31>>
Yakobo akajibu, “Kwanza niuzie haki yako ya mzaliwa wa kwanza.”
690Mwanzo. 25:32>>
Esau akasema, “Sawa! Niko karibu kufa; haki yangu ya mzaliwa wa kwanza itanifaa nini?”
691Mwanzo. 25:33>>
Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Basi, Esau akamwapia na kumwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
692Mwanzo. 25:34>>
Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na dengu kiasi. Esau akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo ndivyo Esau alivyoidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
693Mwanzo. 26:1>>
Baadaye palitokea njaa nchini humo, njaa tofauti na ile ya hapo awali wakati wa uhai wa Abrahamu. Isaka akaenda Gerari kwa Abimeleki mfalme wa Wafilisti.
694Mwanzo. 26:2>>
Mwenyezi-Mungu akamtokea Isaka na kumwambia, “Usiende Misri, bali kaa katika nchi nitakayokuambia.
695Mwanzo. 26:3>>
Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa nawe na kukubariki. Nitatimiza ahadi niliyompa baba yako Abrahamu, kwani nitakupa wewe na wazawa wako nchi hizi zote.
696Mwanzo. 26:4>>
Nitawazidisha wazawa wako wawe kama nyota za mbinguni na kuwapa nchi hizi zote. Kutokana na wazawa wako, mataifa yote duniani yatabarikiwa,
697Mwanzo. 26:5>>
kwa sababu Abrahamu alinitii mimi, akazingatia maagizo yangu, amri zangu, masharti yangu na sheria zangu.”
698Mwanzo. 26:6>>
Basi, Isaka akakaa huko Gerari.
699Mwanzo. 26:7>>
Watu wa huko walipomwuliza habari za mkewe, yeye alijibu, “Huyu ni dada yangu.” Aliogopa kusema kwamba ni mke wake kwa kuogopa kwamba wakazi wa nchi wangemuua kwa sababu ya Rebeka, maana Rebeka alikuwa mzuri sana.
700Mwanzo. 26:8>>
Baada ya kukaa huko kwa muda mrefu, Abimeleki mfalme wa Wafilisti alichungulia dirishani akamwona Isaka akimkumbatia mkewe Rebeka.
701Mwanzo. 26:9>>
Abimeleki akamwita Isaka na kumwambia, “Kumbe huyo ni mke wako! Mbona ulisema ni dada yako?” Isaka akajibu, “Kwa kuwa niliogopa kwamba ningeuawa kwa sababu yake.”
702Mwanzo. 26:10>>
Abimeleki akamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilotutendea? Mmoja wa watu wangu angaliweza kulala na mkeo bila wasiwasi, nawe ungekuwa umetutia hatiani.”
703Mwanzo. 26:11>>
Ndipo Abimeleki akawaonya watu wote akisema, “Yeyote atakayemgusa mtu huyu au mke wake, atauawa.”
704Mwanzo. 26:12>>
Mwaka huo Isaka alipanda mbegu katika nchi ile, akavuna mara mia zaidi, maana Mwenyezi-Mungu alimbariki,
705Mwanzo. 26:13>>
naye akatajirika. Alizidi kupata mali hadi akawa tajiri sana.
706Mwanzo. 26:14>>
Alikuwa na makundi ya kondoo, ngômbe na watumwa wengi, hata Wafilisti wakamwonea wivu.
707Mwanzo. 26:15>>
Wafilisti walikuwa wamevifukia visima vyote vya maji ambavyo watumishi wa Abrahamu, baba yake, walikuwa wamechimba wakati alipokuwa bado hai.
708Mwanzo. 26:16>>
Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwani wewe umetuzidi nguvu.”
709Mwanzo. 26:17>>
Basi, Isaka akaondoka huko, akapiga kambi yake katika bonde la Gerari, akakaa huko.
710Mwanzo. 26:18>>
Isaka akavichimbua vile visima vilivyokuwa vimechimbwa wakati Abrahamu baba yake alipokuwa hai, visima ambavyo Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kifo cha Abrahamu. Akavipa majina yaleyale aliyovipa baba yake.
711Mwanzo. 26:19>>
Lakini watumishi wa Isaka walipochimba katika lile bonde na kupata kisima cha maji yanayobubujika,
712Mwanzo. 26:20>>
wachungaji wa hapo Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu.” Hivyo Isaka akakiita kisima hicho Eseki, kwa sababu waligombana naye.
713Mwanzo. 26:21>>
Halafu wakachimba kisima kingine, nacho pia wakakigombania; hivyo Isaka akakiita kisima hicho Sitna.
714Mwanzo. 26:22>>
Kisha Isaka akaenda mahali pengine na kuchimba kisima kingine. Lakini hicho hawakukigombania; hivyo Isaka akakiita Rehobothi akisema, “Sasa Mwenyezi-Mungu ametuachia nafasi, nasi tutastawi katika nchi hii.”
715Mwanzo. 26:23>>
Kutoka huko, Isaka alikwenda Beer-sheba.
716Mwanzo. 26:24>>
Usiku huohuo Mwenyezi-Mungu alimtokea na kumwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako Abrahamu. Usiogope kwa kuwa niko pamoja nawe; nitakubariki na kuwazidisha wazawa wako kwa ajili ya Abrahamu, mtumishi wangu.”
717Mwanzo. 26:25>>
Kwa hiyo, Isaka akajenga huko madhabahu, akamwabudu Mwenyezi-Mungu. Akapiga kambi huko; na watumishi wake wakachimba kisima.
718Mwanzo. 26:26>>
Abimeleki alitoka Gerari akiwa pamoja na Ahuzathi, mshauri wake, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, akamwendea Isaka.
719Mwanzo. 26:27>>
Isaka akawauliza, “Kwa nini mmekuja kwangu hali mnanichukia na mlinifukuza kwenu?”
720Mwanzo. 26:28>>
Wao wakamjibu, “Tumeona wazi kwamba Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nawe. Kwa hiyo, tunafikiri inafaa tule kiapo pamoja nawe na kufanya agano,
721Mwanzo. 26:29>>
kwamba hutatudhuru, nasi kadhalika hatutakudhuru. Tulikutendea mema, tukakuacha uende zako kwa amani, bila kukutendea baya lolote lile. Na sasa wewe ni mbarikiwa wa Mwenyezi-Mungu.”
722Mwanzo. 26:30>>
Basi, Isaka akawafanyia karamu, nao wakala na kunywa.
723Mwanzo. 26:31>>
Kesho yake wakaamka asubuhi na mapema na kula kiapo. Kisha Isaka akawasindikiza na kuagana nao kwa amani.
724Mwanzo. 26:32>>
Siku ileile watumishi wa Isaka walimjia na kumpasha habari za kile kisima walichokuwa wamechimba, wakasema, “Tumepata maji!”
725Mwanzo. 26:33>>
Basi, Isaka akakiita kisima hicho Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba hata leo.
726Mwanzo. 26:34>>
Esau alipokuwa na umri wa miaka arubaini, alioa wake wawili Wahiti: Yudithi bintiye Beeri, na Basemathi bintiye Eloni.
727Mwanzo. 26:35>>
Wanawake hao waliyafanya maisha ya Isaka na Rebeka kuwa machungu.
728Mwanzo. 27:1>>
Isaka alikuwa amezeeka na macho yake yalikuwa hayaoni. Basi, alimwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu!” Naye akaitika “Naam baba, nasikiliza!”
729Mwanzo. 27:2>>
Isaka akasema, “Tazama, mimi ni mzee, wala siku ya kufa kwangu siijui.
730Mwanzo. 27:3>>
Basi, chukua silaha zako, yaani podo na upinde wako, uende porini ukaniwindie mnyama.
731Mwanzo. 27:4>>
Halafu unitengenezee chakula kitamu, kile nipendacho, uniletee ili nile, nipate kukubariki kabla ya kufa kwangu.”
732Mwanzo. 27:5>>
Kumbe, wakati huo Isaka alipokuwa akiongea na Esau mwanawe, Rebeka alikuwa anasikiliza. Kwa hiyo, Esau alipokwenda porini kuwinda,
733Mwanzo. 27:6>>
Rebeka alimwambia mwanawe Yakobo, “Nimemsikia baba yako akimwambia kaka yako Esau,
734Mwanzo. 27:7>>
amwindie mnyama na kumtengenezea chakula kitamu, ili ale, apate kumbariki mbele ya Mwenyezi-Mungu kabla ya kufa kwake.
735Mwanzo. 27:8>>
Sasa mwanangu, sikiliza maneno yangu na utii ninayokuagiza.
736Mwanzo. 27:9>>
Nenda kwenye kundi la mbuzi uniletee wanambuzi wawili wazuri, nimtengenezee baba yako chakula kitamu, kile apendacho.
737Mwanzo. 27:10>>
Kisha utampelekea baba yako ale, apate kukubariki kabla hajafa.”
738Mwanzo. 27:11>>
Lakini Yakobo akamwambia mama yake Rebeka, “Kumbuka kaka yangu Esau amejaa nywele mwilini, hali mimi sina.
739Mwanzo. 27:12>>
Labda baba atataka kunipapasa, nami nitaonekana kama ninamdhihaki, kwa hiyo nitajiletea laana badala ya baraka.”
740Mwanzo. 27:13>>
Mama yake akamwambia, “Laana yako na inipate mimi, mwanangu; wewe fanya ninavyokuagiza: Nenda ukaniletee hao wanambuzi.”
741Mwanzo. 27:14>>
Basi, Yakobo akaenda, akachukua wanambuzi wawili, akamletea mama yake; naye akatayarisha chakula kitamu, kile apendacho Isaka baba yake.
742Mwanzo. 27:15>>
Kisha Rebeka akatwaa mavazi bora ya Esau, mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo, mwanawe mdogo.
743Mwanzo. 27:16>>
Akamvika pia ngozi za wale wanambuzi mikononi na kwenye sehemu laini shingoni mwake.
744Mwanzo. 27:17>>
Kisha akampa kile chakula kitamu na mkate aliokuwa ametayarisha.
745Mwanzo. 27:18>>
Basi, Yakobo akaingia ndani kwa baba yake, akamwita, “Baba!” Naye akaitika, “Naam! Ni nani wewe mwanangu?”
746Mwanzo. 27:19>>
Yakobo akamjibu baba yake, “Ni mimi Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniagiza. Tafadhali baba, kaa kitako ule mawindo yangu ili upate kunibariki.”
747Mwanzo. 27:20>>
Lakini Isaka akamwuliza, “Imekuwaje umepata mawindo upesi hivyo, mwanangu?” Yakobo akamjibu, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.”
748Mwanzo. 27:21>>
Ndipo Isaka akamwambia Yakobo, “Basi, mwanangu, karibia nipate kukupapasa ili nijue kweli kama wewe ndiwe mwanangu Esau au la.”
749Mwanzo. 27:22>>
Yakobo akamkaribia baba yake Isaka, naye akampapasa na kusema, “Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.”
750Mwanzo. 27:23>>
Hakumtambua kwa sababu mikono yake ilikuwa yenye nywele nyingi kama ya Esau kaka yake; kwa hiyo akambariki.
751Mwanzo. 27:24>>
Akamwuliza tena, “Kweli wewe ndiwe mwanangu Esau?” Naye akamjibu, “Ndiyo.”
752Mwanzo. 27:25>>
Basi, baba yake akasema, “Niletee hiyo nyama nile mawindo yako mwanangu, nikubariki.” Hapo Yakobo akampelekea chakula, naye akala; akampelekea divai pia, akanywa.
753Mwanzo. 27:26>>
Ndipo baba yake Isaka, akamwambia, “Sogea karibu, mwanangu, unibusu.”
754Mwanzo. 27:27>>
Basi, Yakobo akamkaribia baba yake na kumbusu, na baba yake aliposikia harufu ya mavazi yake, akambariki akisema, “Tazama, harufu nzuri ya mwanangu ni kama harufu ya shamba alilobariki Mwenyezi-Mungu!
755Mwanzo. 27:28>>
Mungu akumiminie umande wa mbinguni; akupe ardhi yenye rutuba, nafaka na divai kwa wingi.
756Mwanzo. 27:29>>
Jamii za watu zikutumikie, na mataifa yakuinamie kwa heshima. Uwe mtawala wa ndugu zako, watoto wa kiume wa mama yako wakuinamie kwa heshima. Kila akulaaniye na alaaniwe, kila akubarikiye na abarikiwe!”
757Mwanzo. 27:30>>
Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, naye Yakobo alipokuwa ndio tu ametoka mbele ya baba yake Isaka, Esau kaka yake Yakobo, akarudi kutoka mawindoni.
758Mwanzo. 27:31>>
Esau pia akatengeneza chakula kitamu, akampelekea baba yake, akamwambia, “Haya baba, inuka ule mawindo yangu mimi mwanao, ili upate kunibariki!”
759Mwanzo. 27:32>>
Isaka akauliza, “Wewe ni nani?” Naye akamjibu, “Ni mimi mwanao Esau, mzaliwa wako wa kwanza.”
760Mwanzo. 27:33>>
Hapo Isaka akatetemeka mno, akasema, “Ni nani basi yule aliyewinda na kuniletea mawindo, nami nimekwisha kula kabla hujaja? Tena nimekwisha mbariki; naam, amekwisha barikiwa!”
761Mwanzo. 27:34>>
Esau alipoyasikia maneno ya baba yake, akaangua kilio cha uchungu. Kisha akamwambia baba yake, “Ee baba yangu, nibariki na mimi, tafadhali!”
762Mwanzo. 27:35>>
Lakini Isaka akasema, “Ndugu yako alikuja kwa hila, naye amechukua baraka yako.”
763Mwanzo. 27:36>>
Esau akasema, “Ndio maana anaitwa Yakobo! Amechukua nafasi yangu mara mbili. Kwanza alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua baraka Zangu.” Kisha akamwuliza baba yake, “Je, hukunibakizia baraka yoyote?”
764Mwanzo. 27:37>>
Isaka akamjibu, “Nimekwisha mfanya Yakobo kuwa mtawala wako, na kumpa ndugu zake wote kuwa watumishi wake. Nimempatia nafaka na divai. Nikufanyie nini sasa, wewe mwanangu?”
765Mwanzo. 27:38>>
Esau akamwambia baba yake, “Baba, kwani una baraka moja tu? Nibariki hata mimi, ee baba!” Hapo Esau akalia kwa sauti kubwa.
766Mwanzo. 27:39>>
Ndipo Isaka, baba yake, akamwambia, “Makao yako yatakuwa mbali na ardhi yenye rutuba, na mbali na umande wa mbinguni.
767Mwanzo. 27:40>>
Utaishi kwa upanga wako, na utamtumikia ndugu yako; lakini utakapoasi utaivunja kongwa yake shingoni mwako.”
768Mwanzo. 27:41>>
Basi, Esau akamchukia Yakobo kwa sababu ya baraka aliyokuwa amepewa na baba yake. Esau akawaza, “Siku za matanga ya baba zitakapokwisha, ndipo nitakapomuua ndugu yangu Yakobo.”
769Mwanzo. 27:42>>
Lakini Rebeka alipojua nia ya mwanawe mkubwa, akamwita mwanawe mdogo Yakobo, akamwambia, “Jihadhari, ndugu yako Esau anajifariji kwa kupanga kukuua.
770Mwanzo. 27:43>>
Kwa hiyo, mwanangu, sikiliza maneno yangu. Ondoka ukimbilie kwa kaka yangu Labani kule Harani.
771Mwanzo. 27:44>>
Kaa naye kwa muda, mpaka ghadhabu ya nduguyo itakapopoa.
772Mwanzo. 27:45>>
Ghadhabu yake itakapopoa, naye atakapokuwa amesahau uliyomtendea, nitatuma mtu akurudishe. Kwa nini nifiwe na nyinyi wote wawili siku moja?”
773Mwanzo. 27:46>>
Rebeka akamwambia Isaka, “Sina raha kabisa maishani kwa sababu ya hawa wanawake wa Esau Wahiti. Ikiwa Yakobo ataoa mmojawapo wa wanawake hawa Wahiti, maisha yangu yana faida gani?”
774Mwanzo. 28:1>>
Hivyo Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akisema, “Usioe mwanamke yeyote Mkanaani.
775Mwanzo. 28:2>>
Nenda Padan-aramu, nyumbani kwa babu yako Bethueli, ukaoe mmojawapo wa binti za mjomba wako Labani.
776Mwanzo. 28:3>>
Mungu mwenye nguvu na akubariki upate wazawa wengi na kuongezeka, ili uwe jamii kubwa ya watu.
777Mwanzo. 28:4>>
Akubariki wewe pamoja na wazawa wako kama alivyombariki Abrahamu, upate kuimiliki nchi ambamo unakaa kama mgeni; nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu!”
778Mwanzo. 28:5>>
Basi, Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mwaramu, kaka yake Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.
779Mwanzo. 28:6>>
Esau alitambua kwamba Isaka alikuwa amembariki Yakobo na kumtuma aende kuoa huko Padan-aramu, na ya kuwa alipombariki, alimkataza asioe mwanamke Mkanaani.
780Mwanzo. 28:7>>
Alitambua pia kuwa Yakobo alimtii mama yake na baba yake, akaenda Padan-aramu.
781Mwanzo. 28:8>>
Basi, Esau akafahamu kwamba baba yake hapendezwi na wanawake wa Kanaani.
782Mwanzo. 28:9>>
Hivyo, mbali na wale wake zake wengine, Esau akaenda kwa Ishmaeli, mwana wa Abrahamu, akamwoa Mahalathi binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi.
783Mwanzo. 28:10>>
Yakobo aliondoka Beer-sheba, akaelekea Harani.
784Mwanzo. 28:11>>
Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Alichukua jiwe moja la mahali hapo, akaliweka chini ya kichwa chake, akalala.
785Mwanzo. 28:12>>
Aliota ndoto, na katika ndoto hiyo, aliona ngazi iliyosimamishwa duniani na ncha yake inafika mbinguni. Malaika wa Mungu walikuwa wakipanda na kushuka katika ngazi hiyo.
786Mwanzo. 28:13>>
Mwenyezi-Mungu alisimama juu ya ngazi hiyo, akamwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu baba yako, na Mungu wa Isaka. Nchi unayoilalia nitakupa wewe na wazawa wako.
787Mwanzo. 28:14>>
Wazawa wako watakuwa wengi kama mavumbi ya dunia, na milki yao itaenea kila mahali: Magharibi, Mashariki, Kaskazini na Kusini. Kwako jamii zote duniani zitabarikiwa.
788Mwanzo. 28:15>>
Mimi nipo pamoja nawe; nitakulinda popote uendapo na kukurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapotimiza ahadi niliyokupa.”
789Mwanzo. 28:16>>
Ndipo Yakobo akaamka usingizini, akasema, “Hakika, Mwenyezi-Mungu yupo mahali hapa, nami sikujua!”
790Mwanzo. 28:17>>
Yakobo akaogopa na kusema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ni nyumba ya Mungu na lango la mbinguni.”
791Mwanzo. 28:18>>
Yakobo akaamka asubuhi na mapema, akachukua lile jiwe alilokuwa ameliweka chini ya kichwa chake, akalisimika kama nguzo na kuliweka wakfu kwa kulimiminia mafuta.
792Mwanzo. 28:19>>
Akapaita mahali hapo Betheli; lakini jina la awali la mji huo lilikuwa Luzu.
793Mwanzo. 28:20>>
Kisha Yakobo akaweka nadhiri akisema, “Iwapo, ee Mungu, utakuwa pamoja nami na kunilinda katika safari yangu, ukinipa chakula na mavazi
794Mwanzo. 28:21>>
ili nirudi nyumbani kwa baba yangu salama, basi, wewe Mwenyezi-Mungu utakuwa ndiwe Mungu wangu.
795Mwanzo. 28:22>>
Nalo jiwe hili nililosimika hapa kama nguzo, litakuwa nyumba yako Mungu, nami nitakupa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote utakavyonipa.”
796Mwanzo. 29:1>>
Yakobo aliendelea na safari yake, akafika katika nchi za watu wa mashariki.
797Mwanzo. 29:2>>
Siku moja akaona kisima mbugani, na kando yake makundi matatu ya kondoo wamepumzika. Kondoo walikuwa wananyweshwa kutoka kisima hicho kilichokuwa kimefunikwa kwa jiwe kubwa.
798Mwanzo. 29:3>>
Kwa kawaida, makundi yote ya kondoo yalipokusanyika, wachungaji walivingirisha hilo jiwe kwa pamoja toka kisimani na kuwanywesha kondoo. Halafu walikifunika tena kisima kwa jiwe hilo.
799Mwanzo. 29:4>>
Yakobo akawauliza wachungaji, “Ndugu zangu, mmetoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka Harani.”
800Mwanzo. 29:5>>
Naye akawauliza, “Je, mnamfahamu Labani mwana wa Nahori?” Wakamjibu, “Tunamfahamu.”
801Mwanzo. 29:6>>
Akaendelea kuwauliza, “Je, hajambo?” Nao wakamjibu, “Hajambo; hata binti yake Raheli, yule kule anakuja na kondoo wake!”
802Mwanzo. 29:7>>
Hapo Yakobo akawaambia, “Naona bado ni mchana, na si wakati wa kuwakusanya kondoo pamoja. Basi, wanywesheni kondoo maji, mwende mkawachunge.”
803Mwanzo. 29:8>>
Lakini wao wakamwambia, “Hatuwezi kufanya hivyo mpaka makundi yote yawe yamekusanyika pamoja, na jiwe limevingirishwa kisimani, ndipo tuwanyweshe kondoo.”
804Mwanzo. 29:9>>
Yakobo alipokuwa bado anazungumza na hao wachungaji, Raheli akafika na kondoo wa baba yake, kwani ndiye aliyekuwa akiwachunga.
805Mwanzo. 29:10>>
Yakobo alipomwona Raheli, bintiye Labani, kaka ya mama yake, na alipowaona kondoo wa Labani, mjomba wake, akaenda na kulivingirisha lile jiwe kwenye mdomo wa kisima, akalinywesha maji kundi la Labani, mjomba wake.
806Mwanzo. 29:11>>
Kisha Yakobo akambusu Raheli na kulia kwa sauti.
807Mwanzo. 29:12>>
Halafu Yakobo akamjulisha Raheli kuwa yeye ni wa jamaa ya baba yake, na kwamba ni mwana wa Rebeka. Raheli akapiga mbio nyumbani akamwarifu baba yake.
808Mwanzo. 29:13>>
Labani aliposikia habari za Yakobo, mpwa wake, alikwenda mbio kumlaki, akamkumbatia, akambusu, akamkaribisha nyumbani kwake. Yakobo akamsimulia Labani mambo yote yaliyotokea.
809Mwanzo. 29:14>>
Naye Labani akasema, “Hakika, wewe ni jamaa yangu, damu moja nami!” Yakobo akakaa naye kwa muda wa mwezi mmoja.
810Mwanzo. 29:15>>
Siku moja Labani alimwambia Yakobo, “Wewe ni jamaa yangu lakini hiyo haimaanishi kwamba utanitumikia bure. Niambie unataka ujira kiasi gani!”
811Mwanzo. 29:16>>
Sasa, Labani alikuwa na binti wawili: Mkubwa aliitwa Lea, na mdogo aliitwa Raheli.
812Mwanzo. 29:17>>
Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo na wa kupendeza.
813Mwanzo. 29:18>>
Yakobo alimpenda Raheli; kwa hiyo akamwambia Labani, “Nitakutumikia miaka saba ili unioze Raheli, binti yako mdogo.”
814Mwanzo. 29:19>>
Labani akamwambia, “Afadhali nimwoze Raheli kwako wewe kuliko kumwoza mtu mwingine yeyote. Endelea kuishi nami.”
815Mwanzo. 29:20>>
Basi, Yakobo akamtumikia Labani miaka saba kwa ajili ya Raheli, lakini kwake muda huo ulikuwa kama siku chache, kwa vile alivyompenda Raheli.
816Mwanzo. 29:21>>
Kisha Yakobo akamwambia Labani, “Muda wangu umetimia, kwa hiyo nipe mke wangu.”
817Mwanzo. 29:22>>
Basi, Labani akaandaa karamu na kuwaalika watu wote wa huko.
818Mwanzo. 29:23>>
Lakini jioni, Labani akamchukua Lea, binti yake mkubwa, na kumpeleka kwa Yakobo. Yakobo akalala naye.
819Mwanzo. 29:24>>
(Labani akamtoa Zilpa, mjakazi wake, awe mtumishi wa Lea.)
820Mwanzo. 29:25>>
Asubuhi, Yakobo akagundua ya kuwa ni Lea! Basi, akamwuliza Labani, “Umenitendea jambo gani? Je, si nilikutumikia kwa ajili ya Raheli? Mbona basi, umenidanganya?”
821Mwanzo. 29:26>>
Labani akamjibu, “Nchini mwetu hatufanyi hivyo; si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya mkubwa.
822Mwanzo. 29:27>>
Mtimizie Lea siku zake saba, nasi tutakupa Raheli kwa utumishi wa miaka saba mingine.”
823Mwanzo. 29:28>>
Yakobo akakubali. Na Yakobo alipomtimizia Lea siku zake saba, Labani akampa Raheli, binti yake mdogo awe mke wake.
824Mwanzo. 29:29>>
(Labani akamtoa Bilha, mjakazi wake, awe mtumishi wa Raheli).
825Mwanzo. 29:30>>
Basi, Yakobo akalala na Raheli pia. Lakini Yakobo akampenda Raheli kuliko Lea; akamtumikia Labani miaka mingine saba.
826Mwanzo. 29:31>>
Mwenyezi-Mungu alipoona kwamba Lea anachukiwa, akamjalia watoto; lakini Raheli alikuwa tasa.
827Mwanzo. 29:32>>
Lea akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Reubeni, akisema, “Mwenyezi-Mungu ameyaona mateso yangu; bila shaka sasa mume wangu atanipenda.”
828Mwanzo. 29:33>>
Lea akapata mimba tena, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Simeoni, akisema, “Mwenyezi-Mungu amenipa mtoto mwingine wa kiume kwa sababu amesikia jinsi ninavyochukiwa.”
829Mwanzo. 29:34>>
Akapata mimba mara nyingine, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Lawi, akisema, “Wakati huu mume wangu atajiunga nami, kwani nimemzalia watoto watatu wa kiume.”
830Mwanzo. 29:35>>
Lea akapata mimba tena, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Yuda, akisema, “Safari hii nitamsifu Mwenyezi-Mungu.” Kisha Lea akaacha kuzaa.
831Mwanzo. 30:1>>
Raheli alipoona kwamba hajamzalia Yakobo watoto, alimwonea wivu Lea, dada yake, akamwambia Yakobo, “Nipatie watoto, la sivyo, nitakufa.”
832Mwanzo. 30:2>>
Yakobo akamkasirikia Raheli sana na kumwambia, “Je, mimi nimekuwa badala ya Mungu aliyekuzuia kupata watoto?”
833Mwanzo. 30:3>>
Raheli akamjibu, “Mjakazi wangu Bilha yupo. Lala naye ili azae watoto badala yangu, nami pia nipate watoto kutokana naye.”
834Mwanzo. 30:4>>
Kwa hiyo Raheli akampa Yakobo mtumishi wake, Bilha, awe mkewe, naye akalala naye.
835Mwanzo. 30:5>>
Bilha akapata mimba na kumzalia Yakobo mtoto wa kiume.
836Mwanzo. 30:6>>
Raheli akasema, “Mungu amenitendea sawa, amekisikia kilio changu na kunipa mtoto wa kiume.” Akamwita mtoto huyo Dani.
837Mwanzo. 30:7>>
Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena na kumzalia Yakobo mtoto wa pili wa kiume.
838Mwanzo. 30:8>>
Hapo Raheli akasema, “Nimepigana miereka mikali na dada yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Naftali.
839Mwanzo. 30:9>>
Lea alipoona ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, na kumpa Yakobo ili awe mkewe.
840Mwanzo. 30:10>>
Zilpa akamzalia Yakobo mtoto wa kiume.
841Mwanzo. 30:11>>
Lea akasema, “Bahati njema.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Gadi.
842Mwanzo. 30:12>>
Zilpa, mtumishi wa Lea, alimzalia Yakobo mtoto wa pili wa kiume.
843Mwanzo. 30:13>>
Lea akasema, “Bahati njema! Sasa wanawake wataniita heri.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Asheri.
844Mwanzo. 30:14>>
Ikawa wakati wa mavuno ya ngano, Reubeni alikwenda shambani na huko akapata tunguja, akamletea mama yake Lea. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali, nipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
845Mwanzo. 30:15>>
Lakini Lea akamsemea kwa ukali, “Je, unadhani ni jambo dogo kuninyanganya mume wangu, na sasa unataka kuchukua tunguja za mwanangu?” Raheli akamjibu, “Ikiwa utanipa tunguja za mwanao, Yakobo atalala kwako leo.”
846Mwanzo. 30:16>>
Basi, jioni Yakobo alipokuwa anarudi toka shambani, Lea alitoka kwenda kumlaki, akamwambia, “Leo huna budi kulala nami, kwani nimekuajiri kwa tunguja za mwanangu.” Hivyo Yakobo akalala kwa Lea usiku huo.
847Mwanzo. 30:17>>
Mungu akasikiliza ombi la Lea, naye akapata mimba na kumzalia Yakobo mtoto wa tano wa kiume.
848Mwanzo. 30:18>>
Lea akasema, “Mungu amenipa ujira wangu kwa sababu nilimpa mume wangu mjakazi wangu.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Isakari.
849Mwanzo. 30:19>>
Lea akapata mimba tena na kumzalia Yakobo mtoto wa sita wa kiume.
850Mwanzo. 30:20>>
Akasema, “Mungu amenipa zawadi bora. Sasa mume wangu ataniheshimu kwa maana nimemzalia watoto sita wa kiume.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Zebuluni.
851Mwanzo. 30:21>>
Baadaye akazaa mtoto wa kike, akamwita Dina.
852Mwanzo. 30:22>>
Kisha Mungu akamkumbuka Raheli, akalikubali ombi lake na kumjalia kupata watoto.
853Mwanzo. 30:23>>
Raheli akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume, akasema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.”
854Mwanzo. 30:24>>
Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Yosefu akisema, “Mwenyezi-Mungu na aniongezee mtoto mwingine wa kiume.”
855Mwanzo. 30:25>>
Baada ya Raheli kumzaa Yosefu, Yakobo akamwambia Labani, “Niruhusu nirudi nyumbani, katika nchi yangu.
856Mwanzo. 30:26>>
Nipe wake zangu na watoto wangu ambao nimejipatia kutokana na utumishi wangu kwako, niondoke nao. Unajua kwamba nimekutumikia vema.”
857Mwanzo. 30:27>>
Lakini Labani akamwambia, “Hebu niruhusu nami niseme. Nimetambua kwa kuagua kwamba Mwenyezi-Mungu amenibariki kwa sababu yako.
858Mwanzo. 30:28>>
Taja ujira wako, nami nitakulipa.”
859Mwanzo. 30:29>>
Yakobo akamwambia, “Wewe mwenyewe unajua jinsi nilivyokutumikia, na jinsi nilivyowatunza wanyama wako.
860Mwanzo. 30:30>>
Kwa kuwa kabla sijaja ulikuwa na mali chache tu lakini tangu nifike, mali yako imeongezeka kwa wingi sana, na Mwenyezi-Mungu amekubariki kila nilikokwenda. Lakini sasa, nitaitunza lini jamaa yangu mwenyewe?”
861Mwanzo. 30:31>>
Labani akamwuliza, “Nikupatie nini?” Yakobo akamjibu, “Hutanipatia chochote. Nitaendelea kuwatunza wanyama wako ikiwa utanifanyia jambo hili:
862Mwanzo. 30:32>>
Niruhusu nipite kati ya wanyama wako wote leo, nitenge katika kundi kila kondoo mwenye madoadoa na mabakamabaka, kila kondoo mweusi, na mbuzi walio na madoadoa na mabakamabaka. Huo ndio utakaokuwa ujira wangu.
863Mwanzo. 30:33>>
Hivyo, siku zijazo, uaminifu wangu utaonekana waziwazi utakapokuja kuuangalia ujira wangu. Mbuzi yeyote asiye na madoadoa au mabakamabaka, au kondoo yeyote asiye mweusi akionekana katika kundi langu, huyo atakuwa ameibiwa.”
864Mwanzo. 30:34>>
Labani akasema, “Vema! Na iwe kama ulivyosema.”
865Mwanzo. 30:35>>
Lakini siku hiyohiyo Labani akaenda akawatenga mabeberu wote wenye milia na madoadoa, mbuzi wote majike waliokuwa na madoadoa na mabakamabaka, kila mnyama aliyekuwa na weupe mwilini mwake, na kila kondoo mweusi, akawaweka chini ya ulinzi wa wanawe.
866Mwanzo. 30:36>>
Labani akajitenga na Yakobo umbali wa mwendo wa siku tatu; naye Yakobo akabaki akichunga wanyama wa Labani waliosalia.
867Mwanzo. 30:37>>
Basi, Yakobo akatwaa fito mbichi za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni, akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo.
868Mwanzo. 30:38>>
Akazisimamisha fito hizo alizozibambua mbele ya wanyama katika mabirika ya kunyweshea maji, mahali ambapo wanyama walikuja kunywa maji. Na kwa kuwa wanyama walichukua mimba walipokuja kunywa maji,
869Mwanzo. 30:39>>
wakapata mimba mbele ya hizo fito; wakazaa wanyama wenye milia, mabakamabaka na madoadoa.
870Mwanzo. 30:40>>
Yakobo akawatenga hao wanakondoo, kisha akawaelekeza kwenye wanyama wenye milia na weusi katika kundi la Labani. Kwa njia hii, Yakobo akajipatia kundi lake mwenyewe, wala hakulichanganya na lile la Labani.
871Mwanzo. 30:41>>
Ikawa kila yalipofika majira ya wanyama wenye afya kuchukua mimba, Yakobo aliziweka zile fito mbele yao katika mabirika ya kunyweshea maji, ili wachukue mimba penye fito hizo.
872Mwanzo. 30:42>>
Lakini hakuziweka fito hizo mbele ya wanyama dhaifu walipochukua mimba. Punde si punde, wanyama dhaifu wakawa wa Labani, na wenye afya wakawa wa Yakobo.
873Mwanzo. 30:43>>
Basi, Yakobo akatajirika sana, akawa na makundi makubwa ya wanyama, watumishi wa kike na wa kiume, ngamia na punda.
874Mwanzo. 31:1>>
Basi, ikasikika kwamba watoto wa kiume wa Labani walinungunika na kusema, “Yakobo amenyakua kila kitu cha baba yetu; ndivyo alivyopata kuwa tajiri.”
875Mwanzo. 31:2>>
Yakobo alijua pia kuwa Labani hakumjali yeye kama hapo awali.
876Mwanzo. 31:3>>
Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya wazee wako na kwa jamaa yako, nami nitakuwa pamoja nawe.”
877Mwanzo. 31:4>>
Basi Yakobo akataka Raheli na Lea waitwe; nao wakamwendea mbugani alikokuwa anachunga wanyama.
878Mwanzo. 31:5>>
Yakobo akawaambia, “Naona kuwa baba yenu hanijali tena kama hapo awali. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami.
879Mwanzo. 31:6>>
Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote.
880Mwanzo. 31:7>>
Hata hivyo yeye amenidanganya na kuubadilisha ujira wangu mara kumi. Lakini Mungu hakumruhusu kunidhuru.
881Mwanzo. 31:8>>
Kila mara baba yenu aliposema, ‘Wanyama wenye madoadoa ndio watakaokuwa ujira wako,’ basi kundi lote lilizaa wanyama wenye madoadoa. Na kila aliposema, ‘Wanyama wenye milia ndio watakaokuwa ujira wako,’ basi, kundi lote lilizaa wanyama wenye milia.
882Mwanzo. 31:9>>
Ndivyo Mungu alivyochukua wanyama wa baba yenu, akanipa mimi.
883Mwanzo. 31:10>>
“Wakati wa majira ya wanyama kupata mimba niliota ndoto, na katika ndoto hiyo niliona mabeberu wote waliopanda majike walikuwa wenye milia, madoadoa na mabakamabaka.
884Mwanzo. 31:11>>
Malaika wa Mungu akaongea nami katika ndoto hiyo, akaniita, ‘Yakobo,’ nami nikaitika, ‘Naam!’
885Mwanzo. 31:12>>
Naye akaniambia, ‘Tazama mabeberu wote wanaowapanda majike wana milia, madoadoa na mabaka mabaka. Jambo hili limekuwa hivyo kwa sababu nimeona alivyokutendea Labani.
886Mwanzo. 31:13>>
Mimi ndimi yule Mungu aliyekutokea kule Betheli, mahali pale ulipoweka lile jiwe wakfu kwa kulimiminia mafuta na ambapo uliniwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii urudi katika nchi yako.’”
887Mwanzo. 31:14>>
Raheli na Lea wakamjibu Yakobo, “Sisi hatuna tena sehemu au urithi wowote katika nyumba ya baba yetu!
888Mwanzo. 31:15>>
Aidha yeye anatuona sisi kama wageni, kwa maana ametuuza; na mali ileile tuliyonunuliwa nayo ndiyo anayotumia.
889Mwanzo. 31:16>>
Mali yote ambayo Mungu ameichukua kutoka kwa baba yetu ni yetu sisi na watoto wetu. Kwa hiyo, fanya hayo aliyokuagiza Mungu!”
890Mwanzo. 31:17>>
Basi, Yakobo akajitayarisha kusafiri, akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia.
891Mwanzo. 31:18>>
Alichukua wanyama wake wote pamoja na mali yote aliyochuma huko Padan-aramu, akaanza safari ya kurudi nchini Kanaani kwa baba yake Isaka.
892Mwanzo. 31:19>>
Wakati huo Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya wanyama wake. Hivyo Raheli alipata nafasi ya kuiba vinyago vya miungu ya baba yake.
893Mwanzo. 31:20>>
Yakobo alimdanganya Labani, Mwaramu, kwa kuondoka bila kumjulisha.
894Mwanzo. 31:21>>
Basi, Yakobo akachukua mali yake yote, akatoroka. Baada ya kuvuka mto Eufrate, alielekea Gileadi, nchi ya milima.
895Mwanzo. 31:22>>
Siku tatu baadaye, Labani alijulishwa kwamba Yakobo amemtoroka.
896Mwanzo. 31:23>>
Basi, Labani akawachukua ndugu zake, akamfuata Yakobo kwa muda wa siku saba, akamkuta milimani, nchini Gileadi.
897Mwanzo. 31:24>>
Lakini usiku, Mungu akamtokea Labani, Mwaramu, katika ndoto, akamwambia, “Jihadhari! Usimwambie Yakobo neno lolote lile, jema au baya.”
898Mwanzo. 31:25>>
Basi, Labani akamfikia Yakobo. Wakati huo Yakobo alikuwa amepiga kambi yake milimani. Labani naye, pamoja na ndugu zake, akapiga kambi yake kwenye milima ya Gileadi.
899Mwanzo. 31:26>>
Ndipo Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini? Mbona umenidanganya, ukawachukua binti zangu kama mateka vitani?
900Mwanzo. 31:27>>
Kwa nini ulitoroka kisiri, ukanihadaa, wala hukuniarifu ili nipate kukuaga kwa shangwe, nyimbo, matari na vinubi?
901Mwanzo. 31:28>>
Mbona hukunipa fursa ya kuwabusu kwaheri binti zangu na wajukuu zangu? Kweli umetenda kipumbavu!
902Mwanzo. 31:29>>
Nina uwezo wa kukudhuru; lakini Mungu wa baba yako alinitokea usiku wa kuamkia leo, akanitahadharisha akisema, ‘Jihadhari! Usimwambie Yakobo neno lolote lile, jema au baya’.
903Mwanzo. 31:30>>
Najua ulitoroka kwa sababu ya hamu kubwa ya kurudi nyumbani kwa baba yako. Lakini kwa nini uliiba vinyago vya miungu yangu?”
904Mwanzo. 31:31>>
Yakobo akamjibu, “Niliogopa kwa sababu nilidhani ungelininyanganya binti zako.
905Mwanzo. 31:32>>
Lakini utakayempata na vinyago vya miungu yako asiishi! Mbele ya hawa ndugu zetu, onesha chochote kilicho chako, ukichukue.” Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiba vinyago vya miungu ya Labani.
906Mwanzo. 31:33>>
Basi, Labani akatafuta vinyago hivyo vya miungu yake katika hema la Yakobo, la Lea na la wale wajakazi wawili; lakini hakuvipata. Akatoka katika hema la Lea na kuingia hema la Raheli.
907Mwanzo. 31:34>>
Raheli alikuwa amevichukua hivyo vinyago, akavificha chini ya matandiko ya ngamia na kuketi juu yake. Labani akavitafuta katika hema lote; lakini hakuvipata.
908Mwanzo. 31:35>>
Ndipo Raheli akamwambia baba yake, “Samahani baba, usiudhike, kwani siwezi kusimama mbele yako kwa sababu nimo katika siku zangu.” Basi, Labani akavitafuta vinyago vya miungu yake, lakini hakuvipata.
909Mwanzo. 31:36>>
Ndipo Yakobo akakasirika, akamshutumu Labani akisema, “Kosa langu ni nini?
910Mwanzo. 31:37>>
Je, umepata nini kilicho chako hata baada ya kuipekua mizigo yangu yote? Kiweke mbele ya ndugu zangu na ndugu zako, ili wao waamue kati yetu sisi wawili!
911Mwanzo. 31:38>>
Nimekaa nawe kwa muda wa miaka ishirini; na muda huo wote kondoo wako, wala mbuzi wako hawajapata kuharibu mimba, wala sijawahi kula kondoo dume wa kundi lako.
912Mwanzo. 31:39>>
Mimi sikukuletea hata mara moja mnyama wako aliyeuawa na mnyama wa porini, bali nilifidia hasara hiyo mimi mwenyewe. Wewe ulinitaka nilipe bila kujali kama aliibiwa mchana au usiku!
913Mwanzo. 31:40>>
Hivyo, mchana nilistahimili jua kali na usiku baridi ilinipiga hata nisiweze kupata usingizi hata kidogo.
914Mwanzo. 31:41>>
Kwa miaka ishirini hii yote nimeishi nyumbani kwako. Nilikutumikia miaka kumi na minne kwa ajili ya binti zako wawili, na miaka sita nikawachunga wanyama wako. Lakini wewe, ukabadilisha ujira wangu mara kumi.
915Mwanzo. 31:42>>
Kama Mungu wa babu yangu Abrahamu, Mungu ambaye alimfanya baba yangu Isaka kutetemeka, asingelikuwa upande wangu, hakika ungeliniacha niondoke mikono mitupu. Lakini Mungu aliyaona mateso yangu na kazi niliyofanya kwa mikono yangu, akakukemea usiku wa kuamkia leo.”
916Mwanzo. 31:43>>
Hapo Labani akamjibu Yakobo, “Binti hawa ni binti zangu, watoto hawa ni watoto wangu, wanyama hawa ni wanyama wangu, na yote unayoyaona hapa ni yangu. Lakini mimi ninaweza kufanya nini leo juu ya hawa binti zangu na watoto wao waliowazaa?
917Mwanzo. 31:44>>
Basi, tufanye agano mimi nawe, liwe ushahidi kati yako nami.”
918Mwanzo. 31:45>>
Basi, Yakobo akachukua jiwe, akalisimika kama nguzo ya ukumbusho.
919Mwanzo. 31:46>>
Tena Yakobo akawaambia ndugu zake, “Kusanyeni mawe.” Nao wakakusanya mawe na kufanya rundo. Kisha wakala chakula karibu na rundo hilo la mawe.
920Mwanzo. 31:47>>
Labani akaliita rundo hilo Yegar-sahadutha, lakini Yakobo akaliita Galeedi.
921Mwanzo. 31:48>>
Labani akasema, “Rundo hili ni ushahidi kati yako na mimi leo.” Kwa hiyo Labani akaliita Galeedi,
922Mwanzo. 31:49>>
na ile nguzo akaiita Mizpa akisema, “Mwenyezi-Mungu na atulinde tuwapo mbali bila kuonana.
923Mwanzo. 31:50>>
Kama ukiwatesa binti zangu, au ukioa wanawake wengine zaidi ya hawa, basi ujue kwamba hakuna aliye shahidi kati yetu ila Mungu mwenyewe.”
924Mwanzo. 31:51>>
Halafu Labani akamwambia Yakobo, “Tazama rundo hili la mawe na nguzo ambayo nimeisimika kati yako nami.
925Mwanzo. 31:52>>
Rundo hili ni ushahidi na nguzo hii ni ushahidi kwamba mimi sitavuka rundo hili kuja kwako kukudhuru, na wala wewe hutavuka rundo hili na nguzo hii kuja kwangu kunidhuru.
926Mwanzo. 31:53>>
Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Nahori, ataamua kati yetu.” Basi, Yakobo akaapa kwa Mungu ambaye alimfanya baba yake Isaka, kutetemeka.
927Mwanzo. 31:54>>
Kisha akatoa tambiko huko mlimani na kuwaalika ndugu zake wale chakula. Baada ya kula, wakabaki huko usiku kucha.
928Mwanzo. 31:55>>
Asubuhi na mapema Labani akaamka, akawabusu wajukuu na binti zake, akawabariki. Kisha akaondoka, akarudi nyumbani.
929Mwanzo. 32:1>>
Yakobo aliendelea na safari yake. Basi, malaika wa Mungu wakakutana naye.
930Mwanzo. 32:2>>
Yakobo alipowaona, akasema, “Hili ni jeshi la Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali hapo Mahanaimu.
931Mwanzo. 32:3>>
Yakobo aliwatuma wajumbe wamtangulie kwenda kwa nduguye Esau, huko Seiri, katika nchi ya Edomu.
932Mwanzo. 32:4>>
Aliwapa maagizo haya, “Mtamwambia bwana wangu Esau hivi: Mtumishi wako Yakobo asema hivi, ‘Nimekaa ugenini kwa Labani mpaka sasa.
933Mwanzo. 32:5>>
Nina ngômbe, punda, makundi ya kondoo na watumishi wa kiume na wa kike. Ninakutumia ujumbe huu, bwana wangu, ili nipate fadhili mbele yako.’”
934Mwanzo. 32:6>>
Hao wajumbe walikwenda, kisha wakarudi na kumwambia Yakobo, “Tumefika kwa ndugu yako Esau, naye yuko njiani kuja kukulaki, akiwa na watu 400.”
935Mwanzo. 32:7>>
Basi, Yakobo akaogopa sana na kufadhaika. Akawagawa katika makundi mawili watu waliokuwa pamoja naye, kondoo, mifugo mingine na ngamia,
936Mwanzo. 32:8>>
akifikiri, “Kama Esau akija na kuliangamiza kundi moja, basi, kundi litakalosalia litaponyoka.”
937Mwanzo. 32:9>>
Kisha Yakobo akamwomba Mungu akisema, “Ee Mungu wa babu yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaka! Ewe Mwenyezi-Mungu uliyeniambia nirudi katika nchi yangu kwa jamaa yangu, ukaniahidi kunitendea mema,
938Mwanzo. 32:10>>
sistahili hata kidogo fadhili ulizonipa kwa uaminifu mimi mtumishi wako. Nilipovuka mto Yordani, sikuwa na kitu ila fimbo; lakini sasa ninayo makundi haya mawili.
939Mwanzo. 32:11>>
Nakuomba uniokoe sasa kutoka kwa ndugu yangu Esau, maana nina hofu kuwa atatushambulia na kutuua sote, akina mama pamoja na watoto.
940Mwanzo. 32:12>>
Wewe uliniahidi kunitendea mema na kuwafanya wazawa wangu wawe wengi kama mchanga wa bahari ambao hauhesabiki kwa wingi wake.”
941Mwanzo. 32:13>>
Basi, Yakobo akalala hapo usiku huo. Kisha akatenga sehemu ya mali yake, iwe zawadi kwa ndugu yake Esau:
942Mwanzo. 32:14>>
Mbuzi majike 200 na mabeberu 20, kondoo majike 200 na madume 20,
943Mwanzo. 32:15>>
ngamia 30 wanyonyeshao pamoja na ndama wao, ngômbe majike 40 na mafahali kumi, na punda majike 20 na madume kumi.
944Mwanzo. 32:16>>
Akawakabidhi watumishi wake, kila mmoja kundi lake, akawaambia, “Nitangulieni mkiacha nafasi kati ya kundi na kundi katika msafara wenu.”
945Mwanzo. 32:17>>
Akamwagiza yule aliyetangulia, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni mtumishi wa nani? Unakwenda wapi? Na wanyama hawa ni wa nani?’
946Mwanzo. 32:18>>
Wewe utamjibu, ‘Hii ni mali ya mtumishi wako Yakobo, nayo ni zawadi yako wewe bwana wangu Esau. Tena Yakobo mwenyewe yuko nyuma anafuata.’”
947Mwanzo. 32:19>>
Akatoa agizo hilohilo kwa mtumishi wa kundi la pili na la tatu na wengine wote, akisema, “Mtamwambia Esau maneno hayohayo mtakapokutana naye.
948Mwanzo. 32:20>>
Zaidi ya yote, mtamwambia, ‘Mtumishi wako Yakobo yuko nyuma, anafuata.’” Yakobo alifanya hivyo akifikiri, “Pengine nitamtuliza kwa zawadi hizi ninazomtangulizia, na baadaye naweza kuonana naye ana kwa ana; huenda atanipokea.”
949Mwanzo. 32:21>>
Basi, akatanguliza zawadi zake, lakini yeye mwenyewe akalala kambini usiku huo.
950Mwanzo. 32:22>>
Usiku huohuo Yakobo akaamka, akawachukua wake zake wawili, wajakazi wake wawili na watoto wake kumi na mmoja, akapita kivuko cha Yaboki.
951Mwanzo. 32:23>>
Baada ya kuwavusha ngambo ya kijito wale waliokuwa nao na mali yake yote,
952Mwanzo. 32:24>>
Yakobo alibaki peke yake. Mtu mmoja akaja, akapigana naye mwereka mpaka alfajiri.
953Mwanzo. 32:25>>
Mtu huyo alipoona kwamba hawezi kumshinda Yakobo, alimgusa Yakobo nyonga ya kiuno, naye akateguka alipokuwa anapigana naye mwereka.
954Mwanzo. 32:26>>
Kisha yule mtu akamwambia Yakobo, “Niache niende zangu, kwani kunapambazuka.” Lakini Yakobo akamwambia, “Sikuachi kamwe, mpaka umenibariki!”
955Mwanzo. 32:27>>
Naye akamwuliza, “Jina lako nani?” Yeye akamjibu, “Yakobo.”
956Mwanzo. 32:28>>
Yule mtu akamwambia, “Hutaitwa Yakobo tena, bali Israeli, kwa kuwa umeshindana na Mungu na wanadamu, ukashinda.”
957Mwanzo. 32:29>>
Ndipo Yakobo akamwambia, “Tafadhali, nakuomba uniambie jina lako.” Lakini yeye akamwambia, “Ya nini kuniuliza jina langu?” Kisha akambariki Yakobo.
958Mwanzo. 32:30>>
Yakobo akapaita mahali hapo Penueli, akisema, “Nimemwona Mungu uso kwa uso, nami sikufa.”
959Mwanzo. 32:31>>
Jua lilikuwa limekwisha chomoza wakati Yakobo alipoondoka Penueli; akawa anachechemea kwa sababu ya kiuno chake.
960Mwanzo. 32:32>>
Ndiyo maana mpaka leo Waisraeli hawali msuli wa nyonga, kwa maana yule mtu alimgusa Yakobo panapo nyonga katika msuli wa kiuno chake.
961Mwanzo. 33:1>>
Basi, Yakobo alitazama, akamwona Esau akija pamoja na watu 400. Hapo, akawagawa watoto wake kati ya Lea, Raheli na wale wajakazi wawili.
962Mwanzo. 33:2>>
Akawaweka wajakazi na watoto wao mbele, kisha Lea na watoto wake, na nyuma kabisa wakafuata Raheli na mwanawe Yosefu.
963Mwanzo. 33:3>>
Kisha yeye mwenyewe akawatangulia, akaenda akiinama mpaka chini kwa heshima mara saba, mpaka alipofika karibu na ndugu yake.
964Mwanzo. 33:4>>
Basi, Esau akaenda mbio kumlaki Yakobo, akamkumbatia na kumbusu shingoni, na wote wawili wakalia.
965Mwanzo. 33:5>>
Esau alipotazama na kuwaona wale kina mama na watoto, akauliza, “Ni kina nani hawa ulio nao?” Yakobo akamjibu, “Hawa ni watoto ambao Mungu, kwa neema yake, amenijalia mimi mtumishi wako.”
966Mwanzo. 33:6>>
Kisha wale wajakazi wakakaribia pamoja na watoto wao, wakainama kwa heshima.
967Mwanzo. 33:7>>
Hali kadhalika Lea akaja pamoja na watoto wake, akainama kwa heshima. Hatimaye, Raheli na Yosefu wakaja, wakainama kwa heshima.
968Mwanzo. 33:8>>
Ndipo Esau akauliza, “Nini maana ya kundi hili nililokutana nalo njiani?” Yakobo akamjibu, “Nilitumaini kupata fadhili kwako ee bwana wangu.”
969Mwanzo. 33:9>>
Lakini Esau akasema, “Nina mali ya kutosha ndugu yangu. Mali yako na iwe yako mwenyewe.”
970Mwanzo. 33:10>>
Yakobo akamwambia, “La! Kama kweli umekubali kunipokea, basi, nakusihi uipokee zawadi yangu. Hakika, kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa vile ulivyonipokea kwa wema mkubwa.
971Mwanzo. 33:11>>
Basi, nakuomba uikubali zawadi niliyokuletea, kwa sababu hata mimi pia Mungu amenineemesha, nami ninayo mali nyingi.” Ndivyo Yakobo alivyomshawishi Esau, naye akaipokea zawadi yake.
972Mwanzo. 33:12>>
Esau akasema, “Haya! Tuendelee na safari yetu; mimi nitakutangulia.”
973Mwanzo. 33:13>>
Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu, wewe unajua kwamba watoto hawa ni wachanga, na kwamba mifugo hii inanyonyesha, nami sina budi kuitunza; kama wanyama hawa watapelekwa mbio kwa siku moja, wote watakufa.
974Mwanzo. 33:14>>
Basi, nakuomba utangulie, nami nitafuata polepole kadiri ya mwendo wa wanyama na watoto, mpaka nitakapokufikia huko Seiri.”
975Mwanzo. 33:15>>
Hapo Esau akasema, “Heri nikuachie baadhi ya watu wangu.” Lakini Yakobo akasema, “Kuna haja gani ya kufanya hivyo? Yanitosha kwamba mimi nimepata fadhili yako, ewe bwana wangu.”
976Mwanzo. 33:16>>
Basi, siku hiyo Esau akaanza safari ya kurudi Seiri.
977Mwanzo. 33:17>>
Lakini Yakobo akasafiri kwenda Sukothi, na huko akajijengea nyumba na vibanda kwa ajili ya wanyama wake. Kwa sababu hiyo, mahali hapo pakaitwa Sukothi.
978Mwanzo. 33:18>>
Kutoka Padan-aramu, Yakobo alifika salama mjini Shekemu, katika nchi ya Kanaani, akapiga kambi yake karibu na mji huo.
979Mwanzo. 33:19>>
Sehemu hiyo ya ardhi ambako alipiga kambi aliinunua kutoka kwa wazawa wa Hamori, baba yake Shekemu, kwa vipande 100 vya fedha.
980Mwanzo. 33:20>>
Huko, akajenga madhabahu na kupaita Mungu ni Mungu wa Israeli.
981Mwanzo. 34:1>>
Siku moja, Dina, binti yake Yakobo na Lea, alikwenda kuwatembelea wanawake wa nchi hiyo.
982Mwanzo. 34:2>>
Basi, Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, aliyekuwa mkuu wa nchi hiyo, alipomwona Dina, akamshika, akalala naye kwa nguvu.
983Mwanzo. 34:3>>
Lakini Shekemu akavutiwa sana na huyo msichana, akampenda hata akaanza kumbembeleza.
984Mwanzo. 34:4>>
Kwa hiyo, Shekemu akazungumza na Hamori baba yake, akamwambia, “Tafadhali, niombee huyo msichana nimwoe.”
985Mwanzo. 34:5>>
Yakobo akapata habari kwamba Dina, bintiye, alikuwa amenajisiwa na Shekemu; lakini kwa kuwa wanawe walikuwa malishoni, alinyamaza mpaka waliporudi.
986Mwanzo. 34:6>>
Hamori, baba yake Shekemu, akaenda kwa Yakobo ili azungumze naye,
987Mwanzo. 34:7>>
na wakati huohuo watoto wa kiume wa Yakobo wakawa wanarudi nyumbani kutoka malishoni. Waliposikia hayo, vijana hao wakaona uchungu mwingi na kukasirika sana, kwa vile Shekemu alikuwa amewafanyia watu wa Israeli ovu hilo la kulala na binti ya Yakobo, maana jambo hilo lilikuwa mwiko.
988Mwanzo. 34:8>>
Lakini Hamori akawaambia, “Mwanangu Shekemu anampenda sana binti yenu. Basi, tafadhali mumruhusu amwoe.
989Mwanzo. 34:9>>
Acheni tuoane: Nyinyi mtatuoza binti zenu, nasi tutawaoza binti zetu.
990Mwanzo. 34:10>>
Kwa hiyo mtaishi pamoja nasi; mtakuwa huru katika nchi hii. Mtaishi humu, mfanye biashara na kujipatia mali.”
991Mwanzo. 34:11>>
Hali kadhalika, Shekemu akawaambia baba na ndugu zake Dina, “Tafadhali, mniwie radhi, nami nitawapeni chochote mtakachosema.
992Mwanzo. 34:12>>
Niambieni kiasi chochote cha mahari na zawadi, hata kikiwa kikubwa namna gani, nami nitatoa, mradi tu mnioze msichana huyu.”
993Mwanzo. 34:13>>
Basi, watoto wa kiume wa Yakobo wakamjibu Shekemu na baba yake Hamori kwa hila, kwa kuwa Shekemu alikuwa amekwisha mnajisi dada yao Dina.
994Mwanzo. 34:14>>
Waliwaambia, “Hatuwezi kumwoza dada yetu kwa mtu asiyetahiriwa. Kufanya hivyo ni aibu kwetu.
995Mwanzo. 34:15>>
Tutakubaliana nanyi tu kwa sharti hili: Kwamba mtakuwa kama sisi kwa kumtahiri kila mwanamume miongoni mwenu.
996Mwanzo. 34:16>>
Hapo ndipo tutakapowaoza binti zetu na kuwaoa binti zenu; tutaishi pamoja nanyi na kuwa jamaa moja.
997Mwanzo. 34:17>>
Lakini msipokubaliana nasi na kutahiriwa, basi, sisi tutamchukua binti yetu na kwenda zetu.”
998Mwanzo. 34:18>>
Pendekezo lao likawapendeza Hamori na mwanawe Shekemu.
999Mwanzo. 34:19>>
Kijana huyo hakusita hata kidogo kutekeleza sharti hilo, kwa vile alivyompenda binti wa Yakobo. Isitoshe, Shekemu ndiye aliyeheshimika kuliko wote nyumbani kwao.
1000Mwanzo. 34:20>>
Basi, Hamori na mwanawe, Shekemu, wakaenda kwenye lango la mji, mahali pa mikutano, wakaongea na watu wao wakisema,
1001Mwanzo. 34:21>>
“Watu hawa ni marafiki zetu. Tuwakaribishe waishi nchini mwetu na kufanya biashara, kwa sababu tunayo nchi ya kututosha sisi na wao pia; kisha tutaoa binti zao na kuwaoza binti zetu.
1002Mwanzo. 34:22>>
Lakini wao watakubali kuishi nasi na tutakuwa jamaa moja kwa sharti hili: Kwamba tutamtahiri kila mwanamume miongoni mwetu kama wao walivyotahiriwa.
1003Mwanzo. 34:23>>
Je, hamwoni kwamba mifugo yao na mali yao yote itakuwa mali yetu? Haya, tukubaliane nao ili wakae pamoja nasi.”
1004Mwanzo. 34:24>>
Wanaume wote waliokusanyika penye lango la mji huo wakakubaliana na Hamori na mwanawe Shekemu. Kisha, wanaume wote wakatahiriwa.
1005Mwanzo. 34:25>>
Siku tatu baadaye, waliotahiriwa wakiwa bado wana maumivu makali, watoto wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, kaka zake Dina, walizitwaa panga zao, wakauvamia mji ghafla na kuwaua wanaume wote.
1006Mwanzo. 34:26>>
Waliwaua kwa upanga Hamori na mwanawe Shekemu, wakamtoa Dina katika nyumba ya Shekemu, wakaenda zao.
1007Mwanzo. 34:27>>
Baada ya mauaji hayo, watoto wengine wa kiume wa Yakobo waliingia mjini na kuuteka nyara mji huo, kwa sababu dada yao alikuwa amenajisiwa.
1008Mwanzo. 34:28>>
Walichukua kondoo na mbuzi, ngômbe, punda na chochote kilichokuwa mjini au shambani.
1009Mwanzo. 34:29>>
Waliteka nyara mali yote, watoto na wanawake wote na chochote kilichokuwa majumbani.
1010Mwanzo. 34:30>>
Basi, Yakobo akamwambia Simeoni na Lawi, “Nyinyi mmeniletea taabu kwa kunifanya nichukiwe na wakazi wa nchi hii ya Wakanaani na Waperizi. Mimi sina watu wengi, na kama wakikusanyika kunishambulia wataniangamiza mimi pamoja na jamaa yangu.”
1011Mwanzo. 34:31>>
Hao ndugu wawili wakajibu, “Ana haki gani ya kumtendea dada yetu kama malaya?”
1012Mwanzo. 35:1>>
Siku moja, Mungu alimwambia Yakobo, “Anza safari, uende kuishi Betheli na kunijengea humo mahali pa kunitambikia mimi Mungu niliyekutokea wakati ulipomkimbia kaka yako Esau.”
1013Mwanzo. 35:2>>
Basi, Yakobo akawaambia jamaa yake na wote aliokuwa nao, “Tupilieni mbali sanamu za miungu ya kigeni mlizo nazo, mjitakase na kubadili mavazi yenu.
1014Mwanzo. 35:3>>
Kisha, tutakwenda Betheli ili nimjengee mahali pa kumtambikia Mungu aliyenisaidia siku ya taabu, Mungu ambaye amekuwa nami popote nilipokwenda.”
1015Mwanzo. 35:4>>
Basi, wakampa Yakobo sanamu zote za miungu ya kigeni walizokuwa nazo pamoja na vipuli walivyokuwa wamevaa masikioni; naye akavifukia chini ya mwaloni uliokuwa karibu na Shekemu.
1016Mwanzo. 35:5>>
Yakobo na wanawe walipokuwa wanasafiri, Mungu aliwatia hofu wenyeji wa miji yote ya jirani hata hawakuthubutu kuwafuatia.
1017Mwanzo. 35:6>>
Basi, Yakobo akawasili Luzu yaani Betheli katika nchi ya Kanaani, pamoja na watu wote aliokuwa nao.
1018Mwanzo. 35:7>>
Akajenga hapo madhabahu na kupaita El-betheli kwani hapo ndipo mahali Mungu alipojionesha kwake wakati alipokuwa akimkimbia kaka yake.
1019Mwanzo. 35:8>>
Debora, mlezi wa Rebeka, alifariki, akazikwa chini ya mwaloni upande wa kusini wa Betheli. Kwa hiyo Yakobo akauita mji huo Alon-bakuthi.
1020Mwanzo. 35:9>>
Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki.
1021Mwanzo. 35:10>>
Mungu alimwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa hivyo tena, bali sasa jina lako litakuwa Israeli.” Kwa hiyo Yakobo akaitwa Israeli.
1022Mwanzo. 35:11>>
Tena Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu mwenye nguvu. Ujaliwe wazawa wengi; kwako wewe kutatokea taifa, mataifa na wafalme.
1023Mwanzo. 35:12>>
Nchi niliyowapa Abrahamu na Isaka, nitakupa wewe na wazawa wako.”
1024Mwanzo. 35:13>>
Basi, baada ya kuongea na Yakobo, Mungu akamwacha na kupanda juu.
1025Mwanzo. 35:14>>
Yakobo akasimika nguzo ya jiwe la ukumbusho mahali hapo Mungu alipozungumza naye, akaiweka wakfu kwa kuimiminia tambiko ya kinywaji na mafuta.
1026Mwanzo. 35:15>>
Basi, Yakobo akapaita mahali hapo alipozungumza na Mungu Betheli.
1027Mwanzo. 35:16>>
Yakobo na jamaa yake yote waliendelea na safari yao kutoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efratha, Raheli akashikwa na uchungu mkali wa kuzaa.
1028Mwanzo. 35:17>>
Naye alipokuwa katika uchungu huo, mkunga akamwambia, “Usiogope, umepata mtoto mwingine wa kiume.”
1029Mwanzo. 35:18>>
Raheli huku akikata roho, akampa huyo mtoto jina Ben-oni. Lakini baba yake akamwita mtoto huyo Benyamini.
1030Mwanzo. 35:19>>
Basi, Raheli akafariki na kuzikwa kando ya njia iendayo Efratha (yaani Bethlehemu).
1031Mwanzo. 35:20>>
Yakobo akasimika nguzo ya kumbukumbu juu ya kaburi la Raheli ambayo ipo mpaka leo.
1032Mwanzo. 35:21>>
Israeli akaendelea na safari yake na kupiga kambi yake baada ya kuupita mnara wa Ederi.
1033Mwanzo. 35:22>>
Wakati Israeli alipokuwa anakaa nchini humo, mwanawe Reubeni, alilala na Bilha, suria wa baba yake; naye Israeli akasikia habari hizo. Yakobo alikuwa na watoto wa kiume kumi na wawili.
1034Mwanzo. 35:23>>
Wana wa Lea walikuwa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zebuluni.
1035Mwanzo. 35:24>>
Watoto wa kiume wa Raheli walikuwa Yosefu na Benyamini.
1036Mwanzo. 35:25>>
Watoto wa kiume waliozaliwa na Bilha, mjakazi wa Raheli, walikuwa Dani na Naftali.
1037Mwanzo. 35:26>>
Na watoto wa kiume waliozaliwa na Zilpa, mjakazi wa Lea, walikuwa Gadi na Asheri. Hao ndio watoto wa kiume wa Yakobo, aliowazaa alipokuwa kule Padan-aramu.
1038Mwanzo. 35:27>>
Yakobo aliondoka akaenda Mamre kwa baba yake Isaka, huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, mahali ambapo Abrahamu na Isaka walikaa kama wageni.
1039Mwanzo. 35:28>>
Isaka alikuwa na miaka 180
1040Mwanzo. 35:29>>
akafariki akiwa mzee wa miaka mingi. Watoto wake, Esau na Yakobo wakamzika.
1041Mwanzo. 36:1>>
Wafuatao ni wazawa wa Esau (yaani Edomu).
1042Mwanzo. 36:2>>
Esau alioa wake Wakanaani: Ada binti Eloni Mhiti, Oholibama binti Ana, binti Sibeoni, Mhivi,
1043Mwanzo. 36:3>>
na Basemathi, binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi.
1044Mwanzo. 36:4>>
Ada alimzalia Esau Elifazi, naye Basemathi akamzalia Reueli.
1045Mwanzo. 36:5>>
Oholibama alimzalia Yeushi, Yalamu na Kora. Hao ndio watoto wa kiume wa Esau ambao wake zake walimzalia alipokaa katika nchi ya Kanaani.
1046Mwanzo. 36:6>>
Kisha, Esau akawachukua wake zake, watoto wake wa kiume na wa kike, watu wote wa nyumbani mwake, ngômbe wake, wanyama wake wengine wote na mali yake yote ambayo alikuwa ameipata katika nchi ya Kanaani, akahamia mahali pengine, mbali na nduguye Yakobo.
1047Mwanzo. 36:7>>
Alifanya hivyo kwa sababu mali zao zilikuwa nyingi hata wasiweze kuishi pamoja. Nchi waliyokaa kama wageni haikuweza kuwatosha kwa sababu ya wingi wa mifugo yao.
1048Mwanzo. 36:8>>
Kwa hiyo, Esau akaenda kukaa katika nchi ya milima ya Seiri. Jina lingine la Esau ni Edomu.
1049Mwanzo. 36:9>>
Wafuatao ni wazawa wa Esau, baba ya Waedomu katika nchi ya milima ya Seiri.
1050Mwanzo. 36:10>>
Watoto wa kiume wa Esau walikuwa Elifazi aliyezaliwa na Ada mkewe, na Reueli aliyezaliwa na Basemathi mke wake mwingine.
1051Mwanzo. 36:11>>
Watoto wa kiume wa Elifazi walikuwa Temani, Omari, Sefo, Gatamu na Kenazi.
1052Mwanzo. 36:12>>
Elifazi alikuwa na suria jina lake Timna. Huyu alimzalia mwana, jina lake Amaleki.
1053Mwanzo. 36:13>>
Basemathi, mkewe Esau, alimzaa Reueli. Watoto wa kiume wa Reueli walikuwa Nahathi, Zera, Shama na Miza.
1054Mwanzo. 36:14>>
Oholibama, binti Ana, binti Sibeoni, alimzalia Esau mumewe watoto wa kiume watatu: Yeushi, Yalamu na Kora.
1055Mwanzo. 36:15>>
Wafuatao ni wakuu wa makabila yaliyotokana na Esau. Elifazi, aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Esau aliwazaa Temani, Omari, Sefo, Kenazi,
1056Mwanzo. 36:16>>
Kora, Gatamu na Amaleki, kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake. Hao wote ni watoto wa kiume wa Elifazi katika nchi ya Edomu, waliotokana na Ada, mkewe Esau.
1057Mwanzo. 36:17>>
Reueli, mwanawe Esau, aliwazaa Nahathi, Zera, Shama na Miza, kila mmoja wao akawa mkuu wa kabila lake. Hao wote ni watoto wa kiume wa Reueli katika nchi ya Edomu, waliotokana na Basemathi, mkewe Esau.
1058Mwanzo. 36:18>>
Watoto wa kiume wa Oholibama, mkewe Esau, walikuwa Yeushi, Yalamu na Kora, kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake. Hao wote ni watoto wa kiume wa Oholibama, binti Ana, mkewe Esau.
1059Mwanzo. 36:19>>
Basi, hao ndio wazawa wa Esau yaani Edomu, kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake.
1060Mwanzo. 36:20>>
Wafuatao ni wazawa wa Seiri, Mhori, na ndio wenyeji wa nchi hiyo: Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana,
1061Mwanzo. 36:21>>
Dishoni, Eseri na Dishani; kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake miongoni mwa Wahori wa uzawa wa Seiri, katika nchi ya Edomu.
1062Mwanzo. 36:22>>
Watoto wa kiume wa Lotani walikuwa Hori na Hemani; na dada yake Lotani aliitwa Timna.
1063Mwanzo. 36:23>>
Watoto wa kiume wa Shobali walikuwa Alvani, Manahathi, Ebali, Shefo na Onamu.
1064Mwanzo. 36:24>>
Watoto wa kiume wa Sibeoni walikuwa Aya na Ana. Ana ndiye aliyeziona chemchemi za maji ya moto jangwani, alipokuwa anawachunga punda wa baba yake Sibeoni.
1065Mwanzo. 36:25>>
Watoto wa Ana walikuwa Dishoni na dada yake mmoja aitwaye Oholibama.
1066Mwanzo. 36:26>>
Watoto wa kiume wa Dishoni walikuwa Hemdani, Eshbani, Ithrani na Kerani.
1067Mwanzo. 36:27>>
Watoto wa kiume wa Eseri walikuwa Bilhani Zaawani na Akani.
1068Mwanzo. 36:28>>
Watoto wa kiume wa Dishani walikuwa Usi na Arani.
1069Mwanzo. 36:29>>
Basi, hao ndio wakuu wa Wahori: Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana,
1070Mwanzo. 36:30>>
Dishoni, Eseri na Dishani; kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake katika nchi ya Seiri.
1071Mwanzo. 36:31>>
Wafuatao ni wafalme waliotawala nchi ya Edomu, kabla mfalme yeyote hajawatawala Waisraeli:
1072Mwanzo. 36:32>>
Bela mwana wa Beori alitawala nchi ya Edomu akiwa na makao yake makuu katika mji wa Dinhaba.
1073Mwanzo. 36:33>>
Bela alipofariki, Yobabu mwana wa Zera kutoka Bosra alitawala badala yake.
1074Mwanzo. 36:34>>
Yobabu alipofariki, Hushamu wa nchi ya Watemani, alitawala badala yake.
1075Mwanzo. 36:35>>
Hushamu alipofariki, Hadadi mwana wa Bedadi alitawala badala yake, makao yake makuu yakiwa katika mji wa Avithi. Huyu ndiye aliyewapiga na kuwashinda Wamidiani katika nchi ya Moabu.
1076Mwanzo. 36:36>>
Hadadi alipofariki, Samla kutoka Masreka, alitawala badala yake.
1077Mwanzo. 36:37>>
Samla alipofariki, Shauli kutoka Rehobothi, ulio karibu na mto Eufrate, alitawala badala yake.
1078Mwanzo. 36:38>>
Shauli alipofariki, Baal-hanani, mwana wa Akbori, alitawala badala yake.
1079Mwanzo. 36:39>>
Baal-hanani, mwana wa Akbori alipofariki, Hadadi alitawala badala yake, na jina la mji wake likiwa Pau. Mkewe Akbori alikuwa Mehetabeli, binti Matredi na mjukuu wa Mezahabu.
1080Mwanzo. 36:40>>
Wakuu wa makabila yaliyotokana na Esau, kadiri ya makabila yao na makazi yao walikuwa: Timna, Alva, Yethethi,
1081Mwanzo. 36:41>>
Oholibama, Ela, Pinoni,
1082Mwanzo. 36:42>>
Kenazi, Temani, Mibsari,
1083Mwanzo. 36:43>>
Magdieli na Iramu. Hao ndio wakuu wa makabila yaliyotokana na Edomu, yaani Esau, baba yake Edomu; wametajwa kulingana na makazi yao katika sehemu za nchi walizomiliki.
1084Mwanzo. 37:1>>
Yakobo aliendelea kukaa katika nchi ya Kanaani, alimoishi baba yake kama mgeni.
1085Mwanzo. 37:2>>
Hizi ndizo habari za ukoo wa Yakobo. Yosefu, akiwa kijana wa umri wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake, wana wa Bilha na Zilpa, wake za baba yake. Yosefu akawa anamjulisha baba yake juu ya tabia mbaya za ndugu zake.
1086Mwanzo. 37:3>>
Israeli alimpenda Yosefu kuliko watoto wake wote kwa sababu alikuwa amezaliwa wakati wa uzee wake. Alimshonea Yosefu kanzu ndefu.
1087Mwanzo. 37:4>>
Lakini ndugu zake walipoona kwamba baba yao alimpenda Yosefu kuliko wao, wakamchukia hata hawakuzungumza naye kwa amani.
1088Mwanzo. 37:5>>
Usiku mmoja, Yosefu aliota ndoto, lakini alipowasimulia ndugu zake, wao wakazidi kumchukia.
1089Mwanzo. 37:6>>
Aliwaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota:
1090Mwanzo. 37:7>>
Niliota kuwa sote tulikuwa shambani tukifunga miganda na ghafla mganda wangu ukainuka na kusimama wima. Miganda yenu ikakusanyika kuuzunguka na kuuinamia mganda wangu.”
1091Mwanzo. 37:8>>
Ndugu zake wakamwuliza, “Je, unataka kutuambia kwamba utatutawala? Au utakuwa na mamlaka juu yetu?” Basi, wakazidi kumchukia kwa sababu ya ndoto na maneno yake.
1092Mwanzo. 37:9>>
Kisha Yosefu akaota ndoto nyingine, akawasimulia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine; nimeona jua, mwezi na nyota kumi na moja vinaniinamia.”
1093Mwanzo. 37:10>>
Lakini alipomsimulia baba yake na ndugu zake ndoto hiyo, baba yake alimkemea akisema, “Ni ndoto gani hiyo uliyoota? Je, itatulazimu mimi, mama yako na ndugu zako kuja kuinama chini kwa heshima mbele yako?”
1094Mwanzo. 37:11>>
Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akawa analifikiria jambo hilo.
1095Mwanzo. 37:12>>
Siku moja, ndugu zake Yosefu walikwenda kuchunga wanyama wa baba yao karibu na Shekemu.
1096Mwanzo. 37:13>>
Basi, Israeli akamwambia Yosefu, “Unajua ndugu zako wanachunga wanyama kule Shekemu. Kwa hiyo nataka nikutume kwao.” Yosefu akajibu, “Niko tayari.”
1097Mwanzo. 37:14>>
Baba yake akamwambia, “Nenda ukawaangalie ndugu zako na wanyama kama wako salama, kisha uniletee habari.” Basi, Yakobo akamtuma Yosefu kutoka bonde la Hebroni. Yosefu alipokaribia Shekemu
1098Mwanzo. 37:15>>
mtu mmoja akamkuta akitangatanga mbugani, akamwuliza, “Unatafuta nini?”
1099Mwanzo. 37:16>>
Yosefu akamjibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Tafadhali, niambie mahali wanakochunga wanyama.”
1100Mwanzo. 37:17>>
Yule mtu akamwambia, “Bila shaka wamekwisha ondoka, kwa sababu niliwasikia wakisema kwamba wanakwenda Dothani.” Basi, Yosefu akawafuata ndugu zake, akawakuta huko Dothani.
1101Mwanzo. 37:18>>
Ndugu zake walipomwona akiwa mbali na kabla hajafika karibu, wakafanya mpango wa kumuua.
1102Mwanzo. 37:19>>
Waliambiana, “Tazameni! Yule mwota ndoto anakuja.
1103Mwanzo. 37:20>>
Haya, tumuue na kumtupa ndani ya shimo mojawapo. Baadaye tutasema kwamba ameuawa na mnyama wa porini. Halafu tutaona hizo ndoto zake zitakuwaje.”
1104Mwanzo. 37:21>>
Lakini Reubeni aliposikia maneno hayo, akataka kumwokoa mikononi mwao; basi akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, tusimuue.
1105Mwanzo. 37:22>>
Msimwage damu. Ila mtumbukizeni katika shimo hili hapa mbugani, lakini msimdhuru.” Alisema hivyo kusudi aweze kumwokoa Yosefu mikononi mwao, na baadaye amrudishe kwa baba yake.
1106Mwanzo. 37:23>>
Yosefu alipowafikia ndugu zake, wao wakamvua kanzu yake.
1107Mwanzo. 37:24>>
Kisha wakamshika na kumtupa shimoni. Lakini shimo hilo halikuwa na maji.
1108Mwanzo. 37:25>>
Walipoketi kula, wakaona msafara wa Waishmaeli wakisafiri kutoka Gileadi kwenda Misri. Ngamia wao walikuwa wamebeba ubani, zeri na manemane.
1109Mwanzo. 37:26>>
Hapo Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutapata faida gani tukimuua ndugu yetu na kuficha mauaji yake?
1110Mwanzo. 37:27>>
Afadhali tumwuze kwa hawa Waishmaeli, lakini tusiguse maisha yake, kwani yeye ni ndugu yetu; yeye ni damu moja nasi.” Ndugu zake wakakubaliana naye.
1111Mwanzo. 37:28>>
Wafanyabiashara Wamidiani walipofika mahali hapo, hao ndugu wakamtoa Yosefu katika shimo, wakamwuza kwa Waishmaeli kwa bei ya vipande ishirini vya fedha; nao wakamchukua Yosefu hadi Misri.
1112Mwanzo. 37:29>>
Basi, Reubeni aliporudi kwenye lile shimo, na asimwone Yosefu tena, akazirarua nguo zake kwa huzuni,
1113Mwanzo. 37:30>>
akawaendea ndugu zake, akawaambia, “Kijana hayupo nami niende wapi?”
1114Mwanzo. 37:31>>
Basi, wakachinja mbuzi, wakaichukua kanzu ya Yosefu na kuichovya katika damu ya huyo mbuzi.
1115Mwanzo. 37:32>>
Kisha wakampelekea baba yao ile kanzu, wakamwambia, “Tumeiokota kanzu hii. Hebu iangalie kama ni ya mwanao, au siyo.”
1116Mwanzo. 37:33>>
Baba yao akaitambua hiyo kanzu, akasema, “Ndiyo hasa! Bila shaka mnyama wa porini amemshambulia na kumla. Hakika Yosefu ameraruliwa vipandevipande.”
1117Mwanzo. 37:34>>
Hapo Yakobo akayararua mavazi yake kwa huzuni, akavaa vazi la gunia kiunoni. Akamlilia mwanawe kwa muda wa siku nyingi.
1118Mwanzo. 37:35>>
Watoto wake wa kiume na wa kike wakamjia ili kumfariji, lakini akakataa kufarijiwa, akisema, “Niacheni; nitaendelea kuomboleza kwa ajili ya mwanangu, mpaka nitakaposhuka kuzimu alipo.” Ndivyo baba yake alivyomlilia.
1119Mwanzo. 37:36>>
Wakati huo, kule Misri, wale Wamidiani walimwuza Yosefu kwa mtu aitwaye Potifa, mmoja wa maofisa wa Farao, ambaye alikuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi.
1120Mwanzo. 38:1>>
Wakati huo, Yuda alitengana na ndugu zake, akaenda kukaa na mtu mmoja Mwadulami, jina lake Hira.
1121Mwanzo. 38:2>>
Akiwa huko, Yuda akamwona binti Shua, Mkanaani, akamwoa.
1122Mwanzo. 38:3>>
Binti Shua akapata mimba akazaa mtoto wa kiume, Yuda akamwita Eri.
1123Mwanzo. 38:4>>
Akapata mimba nyingine, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Onani.
1124Mwanzo. 38:5>>
Kisha akapata mtoto mwingine wa kiume, akamwita Shela. Wakati Shela alipozaliwa, Yuda alikuwa Kezibu.
1125Mwanzo. 38:6>>
Baadaye Yuda alimwoza mtoto wake wa kwanza Eri, kwa mwanamke aitwaye Tamari.
1126Mwanzo. 38:7>>
Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; hivyo Mwenyezi-Mungu akamuua.
1127Mwanzo. 38:8>>
Basi, Yuda akamwambia Onani, “Mchukue mke wa ndugu yako marehemu, kwani ndivyo inavyokupasa kufanya, upate kumzalia nduguyo watoto.”
1128Mwanzo. 38:9>>
Lakini Onani alijua kwamba hao watoto wasingekuwa wake. Kwa hiyo, alipolala na mke wa nduguye, alimwaga chini mbegu ya uzazi, asije akampatia nduguye watoto.
1129Mwanzo. 38:10>>
Tendo hilo likamwudhi Mwenyezi-Mungu, akamuua Onani pia.
1130Mwanzo. 38:11>>
Ndipo Yuda akamwambia Tamari, mke wa mwanawe, “Rudi nyumbani kwa baba yako, ubaki mjane hadi mwanangu Shela atakapokua.” Yuda alihofu Shela naye asije akafa kama ndugu zake. Basi, Tamari akarudi nyumbani kwa baba yake.
1131Mwanzo. 38:12>>
Kisha binti Shua, mkewe Yuda, akafariki. Yuda alipomaliza kufanya matanga akaondoka na rafiki yake Hira, Mwadulami, wakaenda Timna kwa wakata-manyoya ya kondoo wake.
1132Mwanzo. 38:13>>
Tamari aliposikia kwamba baba mkwe wake alikuwa njiani kwenda Timna kukata manyoya ya kondoo wake,
1133Mwanzo. 38:14>>
alivua mavazi yake ya ujane na kujifunika shela kisha akaketi penye lango la kuingilia Enaimu, kijiji kilichokuwa njiani kwenda Timna. Alifanya hivyo kwa vile aliona kwamba Shela alikwisha kuwa mtu mzima, lakini yeye Tamari hakuozwa awe mkewe.
1134Mwanzo. 38:15>>
Basi, Yuda alipomkuta Tamari hapo, alimdhania kuwa mwanamke malaya, kwani alikuwa amejifunika uso.
1135Mwanzo. 38:16>>
Hapo, bila kujua kwamba huyo alikuwa mke wa mwanawe, akamwendea pale kando ya njia, akamwambia, “Napenda kulala nawe.” Tamari akamwuliza, “Utanipa nini nikikubali?”
1136Mwanzo. 38:17>>
Yuda akamjibu, “Nitakupa mwanambuzi kutoka kundi langu.” Tamari akamwambia, “Weka rehani kuthibitisha utaniletea huyo mwanambuzi.”
1137Mwanzo. 38:18>>
Yuda akamwuliza, “Unataka nikupe nini kama rehani?” Naye akamjibu, “Nipe hiyo pete na kamba yake pamoja na hiyo fimbo unayoshika.” Basi, Yuda akampa vitu hivyo vyote, akalala naye. Tamari akapata mimba yake.
1138Mwanzo. 38:19>>
Basi, Tamari akarudi nyumbani akavua ile shela aliyojifunika, akavaa tena mavazi yake ya ujane.
1139Mwanzo. 38:20>>
Wakati Yuda alipomtuma yule rafiki yake, Mwadulami, ampelekee yule mwanamke mwanambuzi ili arudishiwe rehani aliyomwachia, Hira hakumpata.
1140Mwanzo. 38:21>>
Hira akawauliza wenyeji wa Enaimu, “Yuko wapi yule mwanamke kahaba aliyekuwa kando ya njia karibu na hapa?” Wakamjibu, “Hapa hapajawa na mwanamke kahaba.”
1141Mwanzo. 38:22>>
Basi, huyo rafiki akarudi kwa Yuda, akamwambia, “Sikumpata! Tena wenyeji wa huko wameniambia kwamba hapajawa na mwanamke kahaba yeyote huko.”
1142Mwanzo. 38:23>>
Yuda akasema, “Acha avichukue vitu hivyo, la sivyo atatufanya tuchekwe. Wewe mwenyewe umeona kwamba nilimpelekea mwanambuzi, lakini wewe hukumpata.”
1143Mwanzo. 38:24>>
Baada ya miezi mitatu, Yuda akapata habari, “Tamari, mke wa mwanao amekuwa kahaba, tena amepata mimba kwa kufanya ukahaba.” Basi, Yuda akaamuru, “Mtoeni nje achomwe moto!”
1144Mwanzo. 38:25>>
Walipokuwa wakimtoa nje, Tamari akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake, akisema, “Mwenye vitu hivi ndiye aliyenipa mimba. Kwa hiyo, nakuomba umtambue mwenye pete hii na kamba yake, na fimbo hii.”
1145Mwanzo. 38:26>>
Yuda alivitambua vitu hivyo, akasema, “Tamari ni mwadilifu kuliko mimi. Ni kweli, maana sikumwoza kwa mwanangu Shela.” Tokea siku hiyo Yuda hakulala tena na Tamari.
1146Mwanzo. 38:27>>
Wakati wa kujifungua kwake Tamari ulipofika, ikafahamika kuwa alikuwa na mimba ya mapacha.
1147Mwanzo. 38:28>>
Basi, alipopata uchungu wa kuzaa pacha mmojawapo alitoa mkono nje, naye mkunga akaufunga kwa uzi mwekundu, akisema, “Huyu ndiye aliyezaliwa kwanza.”
1148Mwanzo. 38:29>>
Lakini huyo mtoto alipourudisha mkono wake ndani, ndugu yake akazaliwa wa kwanza. Mkunga akasema, “Mbona wewe umepita kwa nguvu?” Kwa hiyo akaitwa Peresi.
1149Mwanzo. 38:30>>
Baadaye ndugu yake akazaliwa akiwa na ule uzi mwekundu mkononi, naye akaitwa Zera.
1150Mwanzo. 39:1>>
Basi, Yosefu alipochukuliwa mpaka Misri, Mmisri mmoja aitwaye Potifa ambaye alikuwa ofisa wa Farao na mkuu wa kikosi chake cha ulinzi, akamnunua kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri.
1151Mwanzo. 39:2>>
Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, akamfanikisha sana. Yosefu akawa anakaa katika nyumba ya bwana wake, Mmisri.
1152Mwanzo. 39:3>>
Huyo bwana wake akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, na kwamba ndiye aliyeyafanikisha mambo yote aliyofanya Yosefu.
1153Mwanzo. 39:4>>
Basi, Yosefu akapendeka sana mbele ya Potifa, hata akawa ndiye mtumishi wake binafsi; alimfanya msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake yote.
1154Mwanzo. 39:5>>
Tokea wakati Potifa alipomfanya Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake, Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya huyo Mmisri kwa ajili ya Yosefu. Baraka za Mwenyezi-Mungu zikawa juu ya kila alichokuwa nacho, nyumbani na shambani.
1155Mwanzo. 39:6>>
Kwa sababu hiyo Potifa alimpa Yosefu mamlaka juu ya mambo yake yote, naye Potifa akaacha kushughulika na chochote isipokuwa tu chakula chake mwenyewe. Yosefu alikuwa kijana mzuri na wa kupendeza.
1156Mwanzo. 39:7>>
Basi, baada ya muda fulani, mke wa Potifa akamtamani Yosefu na kumwambia, “Lala na mimi”.
1157Mwanzo. 39:8>>
Lakini Yosefu akakataa na kumwambia huyo bwana wake, “Kamwe! Bwana wangu amenipa mamlaka juu ya kila kitu hapa nyumbani na, kwa vile niko, hajishughulishi na kitu chochote tena.
1158Mwanzo. 39:9>>
Hapa nyumbani yeye hana madaraka kuliko mimi. Yeye hakunikataza kushika chochote isipokuwa wewe tu kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu mbaya kama huo, na kumkosea Mungu.”
1159Mwanzo. 39:10>>
Huyo mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, lakini Yosefu hakumsikiliza wala kukubali kulala naye kamwe.
1160Mwanzo. 39:11>>
Siku moja, Yosefu aliingia nyumbani kufanya kazi yake kama kawaida, na wafanyakazi wengine hawakuwamo nyumbani.
1161Mwanzo. 39:12>>
Basi, mke wa Potifa alimshika joho lake na kumwambia, “Lala na mimi!” Lakini Yosefu akamwachia vazi lake mikononi mwake, akakimbilia nje.
1162Mwanzo. 39:13>>
Hapo, yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu ameliacha vazi lake mikononi mwake na kukimbilia nje,
1163Mwanzo. 39:14>>
akawaita watumishi wa nyumbani mwake na kuwaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania tuliyeletewa anatuaibisha. Alikuja kwangu akitaka kunishika kwa nguvu, lakini nikapiga kelele.
1164Mwanzo. 39:15>>
Aliposikia napiga kelele, aliliacha vazi lake, akakimbilia nje!”
1165Mwanzo. 39:16>>
Basi, yule mwanamke akaliweka vazi hilo mpaka mumewe aliporudi nyumbani.
1166Mwanzo. 39:17>>
Akamsimulia kisa kile akisema, “Huyu mtumishi Mwebrania uliyemleta kwetu alinijia ili kuniaibisha.
1167Mwanzo. 39:18>>
Lakini mara tu nilipopiga kelele, aliliacha vazi lake na kukimbilia nje.”
1168Mwanzo. 39:19>>
Basi, bwana wake Yosefu alipoyasikia maneno ya mkewe, kwamba ndivyo mtumishi wake alivyomtendea, akawaka hasira,
1169Mwanzo. 39:20>>
akamchukua Yosefu na kumtia gerezani, mahali walipofungwa wahalifu wa mfalme.
1170Mwanzo. 39:21>>
Lakini hata humo gerezani Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu akimfadhili hata kumfanya apendeke mbele ya mkuu wa gereza.
1171Mwanzo. 39:22>>
Hivyo mkuu wa gereza alimweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa wote humo gerezani; kila kitu kilichofanyika humo kilifanywa kwa mamlaka yake.
1172Mwanzo. 39:23>>
Huyo mkuu wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote alichokabidhiwa Yosefu kwa maana Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu na kufanikisha kila kitu alichofanya.
1173Mwanzo. 40:1>>
Wakati fulani baada ya mambo hayo, maofisa wawili wa mfalme wa Misri walimkosea mfalme. Maofisa hao walikuwa mtunza vinywaji mkuu na mwoka mikate mkuu wa mfalme.
1174Mwanzo. 40:2>>
Farao aliwakasirikia hao maofisa wake wawili,
1175Mwanzo. 40:3>>
akawafungia ndani ya ngome ya mkuu wa kikosi cha ulinzi, katika gereza, mahali alipofungwa Yosefu.
1176Mwanzo. 40:4>>
Mkuu wa kikosi cha ulinzi akamteua Yosefu awatumikie. Nao wakawa kifungoni kwa muda fulani.
1177Mwanzo. 40:5>>
Basi, usiku mmoja, yule mtunza vinywaji mkuu na yule mwoka mikate mkuu wa mfalme wa Misri, waliota ndoto humo gerezani, kila mmoja na ndoto yake tofauti.
1178Mwanzo. 40:6>>
Yosefu alipokwenda kwao asubuhi na kuwaona, wote wawili walikuwa wenye wasiwasi.
1179Mwanzo. 40:7>>
Basi, Yosefu akawauliza maofisa hao wa Farao waliokuwa kifungoni pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, “Mbona leo mna nyuso za huzuni?”
1180Mwanzo. 40:8>>
Wakamjibu, “Tuna huzuni kwa kuwa tumeota ndoto na hakuna awezaye kututafsiria ndoto zetu.” Yosefu akawaambia, “Je, kutafsiri ndoto si kazi ya Mungu? Basi, niambieni ndoto zenu.”
1181Mwanzo. 40:9>>
Mtunza vinywaji mkuu wa mfalme akamsimulia Yosefu ndoto yake, akisema, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu,
1182Mwanzo. 40:10>>
nao ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua majani, maua yake yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu mbivu.
1183Mwanzo. 40:11>>
Mkononi mwangu nilikuwa na kikombe cha Farao, basi, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe hicho, nikampa Farao.”
1184Mwanzo. 40:12>>
Yosefu akamwambia huyo mtumishi, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Yale matawi matatu ni siku tatu.
1185Mwanzo. 40:13>>
Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani na kukurudisha tena katika cheo chako. Utaweza tena kumpa Farao kikombe mkononi kama ulivyokuwa unafanya hapo awali.
1186Mwanzo. 40:14>>
Lakini tafadhali usinisahau wakati mambo yatakapokwendea vema; unifanyie fadhili na kunitaja mbele ya Farao, nipate kutoka humu gerezani.
1187Mwanzo. 40:15>>
Maana mimi nilitoroshwa kutoka nchi ya Waebrania, na hapa Misri sijafanya chochote kinachostahili nitiwe gerezani.”
1188Mwanzo. 40:16>>
Yule mwoka mikate mkuu alipoona kwamba tafsiri ile ni nzuri, akamwambia Yosefu, “Hata mimi niliota ndoto! Katika ndoto yangu nilikuwa nimechukua kichwani nyungo tatu za mikate.
1189Mwanzo. 40:17>>
Katika ungo wa juu, kulikuwa na vyakula mbalimbali vilivyookwa kwa ajili ya Farao. Lakini, ndege walikuwa wakivila kutoka ungo huo kichwani pangu!”
1190Mwanzo. 40:18>>
Yosefu akamwambia, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Zile nyungo tatu ni siku tatu.
1191Mwanzo. 40:19>>
Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani, atakiinua kichwa chako akutundike mtini, nao ndege wataula mwili wako.”
1192Mwanzo. 40:20>>
Mnamo siku ya tatu, ambayo ilikuwa siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake, Farao aliwaandalia karamu watumishi wake wote. Akawatoa gerezani mtunza vinywaji wake mkuu na mwoka mikate mkuu, akawaweka mbele ya maofisa wake.
1193Mwanzo. 40:21>>
Kisha akamrudishia cheo chake mtunza vinywaji, apate kumpatia Farao kikombe.
1194Mwanzo. 40:22>>
Lakini yule mwoka mkate mkuu akamtundika mtini, kama Yosefu alivyokuwa amewatafsiria ndoto zao.
1195Mwanzo. 40:23>>
Hata hivyo, yule mtunza vinywaji mkuu akamsahau Yosefu, badala ya kumkumbuka.
1196Mwanzo. 41:1>>
Baada ya miaka miwili mizima, Farao aliota ndoto: Alijikuta amesimama kando ya mto Nili,
1197Mwanzo. 41:2>>
akaona ngômbe saba wazuri na wanono wakitoka mtoni na kula nyasi.
1198Mwanzo. 41:3>>
Halafu, baada ya hao, ngômbe wengine saba waliokonda sana wakatoka katika mto Nili, wakaja na kusimama karibu na wale ngômbe wazuri na wanono, kando ya mto.
1199Mwanzo. 41:4>>
Hao ngômbe waliokonda sana wakawala wale wengine saba wazuri na wanono. Hapo Farao akaamka usingizini.
1200Mwanzo. 41:5>>
Alipolala tena, akaota mara ya pili. Aliona masuke saba makubwa na mazuri yanachipuka katika bua moja.
1201Mwanzo. 41:6>>
Halafu, baada ya hayo, masuke mengine saba membamba na yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani yakatokeza.
1202Mwanzo. 41:7>>
Hayo masuke saba membamba yakayameza yale masuke saba makubwa yaliyojaa nafaka. Basi, Farao alipoamka akagundua kuwa ilikuwa ndoto.
1203Mwanzo. 41:8>>
Kulipokuwa asubuhi, Farao akiwa na wasiwasi sana, aliwaita wachawi wote wa Misri, na wenye hekima, akawaambia ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumtafsiria ndoto hizo.
1204Mwanzo. 41:9>>
Ndipo, yule mtunza vinywaji mkuu akamwambia Farao, “Leo nayakumbuka makosa yangu!
1205Mwanzo. 41:10>>
Wakati ule ulipotukasirikia sisi watumishi wako, mimi na mwoka mikate mkuu, ulitufungia ndani ya ngome ya mkuu wa kikosi cha ulinzi.
1206Mwanzo. 41:11>>
Usiku mmoja tuliota ndoto, kila mmoja ndoto yake tofauti.
1207Mwanzo. 41:12>>
Basi, kijana mmoja Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi, alikuwa pamoja nasi kifungoni. Tulipomsimulia ndoto zetu, yeye aliweza kututafsiria kila mmoja wetu kulingana na ndoto yake.
1208Mwanzo. 41:13>>
Alivyotafsiri ndivyo ilivyotokea: Mimi nikarudishwa kazini kwangu, na yule mwoka mikate mkuu akatundikwa mtini.”
1209Mwanzo. 41:14>>
Basi, Farao akaamuru Yosefu aitwe; naye akatolewa gerezani haraka. Baada ya kunyoa na kubadili nguo zake, Yosefu akaja mbele ya Farao.
1210Mwanzo. 41:15>>
Farao akamwambia Yosefu, “Mimi nimeota ndoto, lakini hakuna mtu aliyeweza kunitafsiria. Nimesikia sifa zako kwamba wewe ukiambiwa ndoto unaweza kuitafsiri.”
1211Mwanzo. 41:16>>
Yosefu akamjibu Farao, “Sina uwezo huo; lakini Mungu atakupa jibu lifaalo.”
1212Mwanzo. 41:17>>
Hapo Farao akamwambia Yosefu, “Niliota kwamba nimesimama kando ya mto Nili,
1213Mwanzo. 41:18>>
nikaona ngômbe saba wazuri na wanono wakitoka mtoni na kula nyasi.
1214Mwanzo. 41:19>>
Hao wakafuatwa na ngômbe wengine saba dhaifu, wembamba na wamekonda sana. Mimi sijapata kamwe kuona ngômbe wa hali hiyo katika nchi ya Misri.
1215Mwanzo. 41:20>>
Basi, wale ngômbe waliokonda sana wakawala wale ngômbe saba wanono.
1216Mwanzo. 41:21>>
Lakini hata baada ya kuwala wale wanono, mtu yeyote asingeweza kutambua kwamba wamewala wenzao, kwani bado walikuwa wamekondeana kama mwanzo. Hapo nikaamka usingizini.
1217Mwanzo. 41:22>>
Kisha nikaota ndoto nyingine: Niliona masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka yakichipua katika bua moja.
1218Mwanzo. 41:23>>
Halafu yakafuatwa na masuke mengine saba matupu, membamba na yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani.
1219Mwanzo. 41:24>>
Yale masuke saba membamba yakayameza yale masuke saba mazuri. Basi, mimi niliwaambia wachawi ndoto hizo lakini hakuna mtu aliyeweza kunifafanulia.”
1220Mwanzo. 41:25>>
Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto zako zote mbili tafsiri yake ni moja. Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni.
1221Mwanzo. 41:26>>
ngômbe wale saba wazuri ni miaka saba, na yale masuke saba mazuri pia ni miaka saba; ndoto hiyo tafsiri yake ni moja.
1222Mwanzo. 41:27>>
Wale ngômbe saba waliokonda sana, ambao waliwafuata wale wanono, na yale masuke matupu saba, yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani, maana yake ni miaka saba ya njaa.
1223Mwanzo. 41:28>>
Kama nilivyokueleza, ee Farao, Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni.
1224Mwanzo. 41:29>>
Kutakuwa na miaka saba ya shibe katika nchi nzima ya Misri.
1225Mwanzo. 41:30>>
Lakini baadaye itafuata miaka saba ya njaa, hata hiyo shibe isahaulike kabisa. Njaa hiyo itaiangamiza nchi hii.
1226Mwanzo. 41:31>>
Shibe hiyo itasahaulika kabisa kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno.
1227Mwanzo. 41:32>>
Ndoto yako ilirudiwa mara mbili kwa mifano inayofanana kukuonesha kwamba Mungu ameamua, naye atatekeleza jambo hilo karibuni.
1228Mwanzo. 41:33>>
“Kwa hiyo yafaa sasa, ee Farao, umteue mtu mwenye ujuzi na hekima, umpe jukumu la kuiangalia nchi yote ya Misri.
1229Mwanzo. 41:34>>
Tena, ee Farao, uwateue wasimamizi kadhaa hapa nchini, uwaagize wakusanye sehemu ya tano ya mavuno yote ya Misri katika kipindi hiki cha miaka saba ya shibe.
1230Mwanzo. 41:35>>
Uwaagize wasimamizi hao wakusanye chakula chote katika miaka saba ijayo ya mavuno kwa wingi. Nafaka hiyo na iwekwe chini ya mamlaka yako, ee Farao, iwe akiba ya chakula kwa miji yote, nao waitunze nafaka hiyo.
1231Mwanzo. 41:36>>
Chakula hicho kitakuwa akiba ya kinga kwa nchi ya Misri isije ikaangamia kutokana na njaa ya miaka saba itakayofuata.”
1232Mwanzo. 41:37>>
Shauri alilotoa Yosefu lilionekana kuwa jema mbele ya Farao na watumishi wake wote.
1233Mwanzo. 41:38>>
Kwa hiyo Farao akawauliza watumishi wake, “Huyu mtu ana roho ya Mungu! Je, tunaweza kumpata mtu mwingine kama huyu?”
1234Mwanzo. 41:39>>
Kisha akamwambia Yosefu, “Kwa kuwa Mungu amekufunulia haya yote, hakuna mtu mwingine mwenye busara na hekima kama wewe.
1235Mwanzo. 41:40>>
Wewe ndiwe utakayeisimamia nchi yangu, na watu wangu wote watakuwa chini ya amri yako. Mimi tu ndiye mkuu kuliko wewe kwa kuwa nakalia kiti cha kifalme.
1236Mwanzo. 41:41>>
Basi, sasa nakuteua rasmi kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri!”
1237Mwanzo. 41:42>>
Ndipo, Farao akaivua pete yake ya mhuri kidoleni mwake na kumvisha Yosefu, akamvalisha na mavazi ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni.
1238Mwanzo. 41:43>>
Farao akampandisha katika gari lake la pili la farasi na walinzi wakatangulia mbele ya Yosefu wakipaza sauti na kusema, “Pigeni magoti!” Ndivyo Farao alivyompa Yosefu madaraka makubwa juu ya nchi yote ya Misri.
1239Mwanzo. 41:44>>
Zaidi ya hayo, Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ndimi Farao! Nasema: Mtu yeyote katika nchi nzima ya Misri asiinue mkono wala mguu wake bila kibali chako.”
1240Mwanzo. 41:45>>
Farao akampa Yosefu jina la Kimisri: Safenath-panea. Akamwoza Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni. Basi, Yosefu akaanza kuitembelea nchi nzima ya Misri.
1241Mwanzo. 41:46>>
Yosefu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kumtumikia Farao, mfalme wa Misri. Alitoka nyumbani kwa Farao na kuitembelea nchi yote ya Misri.
1242Mwanzo. 41:47>>
Ikawa, katika miaka ile saba ya shibe, mashamba ya Misri yakatoa mazao kwa wingi sana.
1243Mwanzo. 41:48>>
Yosefu akakusanya chakula chote wakati huo wa miaka saba ya shibe na kukiweka akiba katika miji ya Misri. Katika kila mji akaweka akiba ya chakula kutoka mashamba yaliyo karibu na mji huo.
1244Mwanzo. 41:49>>
Yosefu akaweka akiba ya nafaka kwa wingi mno ikawa nyingi kama mchanga wa bahari, hata isiweze kupimika.
1245Mwanzo. 41:50>>
Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Yosefu alikuwa amekwisha pata wana wawili kwa mkewe, Asenathi, binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni.
1246Mwanzo. 41:51>>
Yosefu alimwita mwanawe wa kwanza Manase, akisema, “Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote na jamaa ya baba yangu.”
1247Mwanzo. 41:52>>
Mwanawe wa pili akamwita Efraimu, akisema, “Mungu amenipa watoto katika nchi ya mateso yangu.”
1248Mwanzo. 41:53>>
Miaka ile saba ya shibe nchini Misri ikapita.
1249Mwanzo. 41:54>>
Ikaanza miaka saba ya njaa kama alivyokuwa amesema Yosefu hapo awali. Nchi nyingine zote zikawa na njaa, lakini nchi yote ya Misri ilikuwa na chakula.
1250Mwanzo. 41:55>>
Wakati wananchi wa Misri walipoanza kuona njaa, walimlilia Farao awape chakula. Naye Farao akawaambia Wamisri wote, “Nendeni kwa Yosefu; atakalowaambia fanyeni.”
1251Mwanzo. 41:56>>
Njaa ikazidi kuwa kali na kuenea katika nchi yote. Kwa hiyo Yosefu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri chakula.
1252Mwanzo. 41:57>>
Zaidi ya hayo, watu toka kila mahali duniani walikuja Misri kwa Yosefu kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa kali duniani kote.
1253Mwanzo. 42:1>>
Yakobo alipopata habari kwamba kulikuwa na nafaka huko Misri, aliwaambia wanawe, “Mbona mnaketi mkitazamana tu?
1254Mwanzo. 42:2>>
Nimesikia kwamba Misri kuna nafaka. Nendeni huko mkanunue nafaka tusije tukafa njaa.”
1255Mwanzo. 42:3>>
Hivyo ndugu kumi wa Yosefu wakaenda Misri kununua nafaka.
1256Mwanzo. 42:4>>
Lakini Yakobo hakumwacha Benyamini, nduguye Yosefu, aende pamoja nao maana aliogopa kwamba angeweza kupata madhara.
1257Mwanzo. 42:5>>
Basi, wana wa Israeli wakafika Misri wakiwa miongoni mwa wanunuzi wengine, kwani hata katika nchi ya Kanaani kulikuwa na njaa.
1258Mwanzo. 42:6>>
Wakati huo Yosefu alikuwa ndiye mkuu huko Misri. Yeye ndiye aliyehusika na kuwauzia wananchi nafaka. Basi, kaka zake wakaja na kumwinamia Yosefu kwa heshima.
1259Mwanzo. 42:7>>
Yosefu alipowaona kaka zake akawatambua, lakini akajifanya kana kwamba hawafahamu, akasema nao kwa ukali. Akawauliza, “Mmetoka wapi nyinyi?” Wakamjibu, “Tumetoka nchini Kanaani, tumekuja kununua chakula.”
1260Mwanzo. 42:8>>
Ingawa Yosefu aliwatambua kaka zake, wao hawakumtambua.
1261Mwanzo. 42:9>>
Akakumbuka ndoto zake za zamani juu ya kaka zake, akawaambia, “Nyinyi ni wapelelezi. Mmekuja kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.”
1262Mwanzo. 42:10>>
Wao wakamjibu, “Sivyo, bwana wetu. Sisi watumishi wako tumekuja kununua chakula.
1263Mwanzo. 42:11>>
Sisi ni ndugu, wana wa baba mmoja. Sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi.”
1264Mwanzo. 42:12>>
Lakini Yosefu akasisitiza, “Sivyo! Mmekuja hapa ili kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.”
1265Mwanzo. 42:13>>
Wakamwambia, “Sisi, watumishi wako, tuko ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja, mwenyeji wa nchi ya Kanaani. Mdogo wetu amebaki na baba nyumbani, na ndugu yetu mwingine ni marehemu.”
1266Mwanzo. 42:14>>
Lakini Yosefu akawaambia, “Ni kama nilivyosema: Nyinyi ni wapelelezi tu.
1267Mwanzo. 42:15>>
Hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Naapa kwa jina la Farao, kwamba hamtatoka hapa mpaka mdogo wenu atakapokuja.
1268Mwanzo. 42:16>>
Mtumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu mdogo, wakati wengine wenu wanamngoja gerezani. Hapo ndipo maneno yenu yatakapojulikana ukweli wake. La sivyo, naapa kwa jina la Farao kwamba nyinyi ni wapelelezi.”
1269Mwanzo. 42:17>>
Kisha akawatia wote gerezani kwa muda wa siku tatu.
1270Mwanzo. 42:18>>
Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Kwa kuwa mimi ni mcha Mungu, fanyeni hivi ili mpate kuishi:
1271Mwanzo. 42:19>>
Kama kweli nyinyi ni watu waaminifu, mmoja wenu na abaki kifungoni, na wengine wawapelekee nafaka jamaa zenu wenye njaa.
1272Mwanzo. 42:20>>
Kisha mleteni kwangu ndugu yenu mdogo. Hii itathibitisha ukweli wa maneno yenu, nanyi hamtauawa.” Basi, wakakubali kufanya hivyo.
1273Mwanzo. 42:21>>
Kisha wakasemezana wao kwa wao, “Kweli sisi tulimkosea ndugu yetu. Ingawa tulimwona akisononeka rohoni mwake, sisi hatukumjali hata alipotusihi. Ndiyo maana taabu hii yote inatupata.”
1274Mwanzo. 42:22>>
Reubeni akawaambia, “Je, mimi sikuwaambieni tusimdhuru kijana? Lakini nyinyi hamkunisikiliza! Sasa tunaadhibiwa kwa ajili ya damu yake.”
1275Mwanzo. 42:23>>
Wao hawakujua kuwa Yosefu alielewa yote hayo waliyosema, maana alipoongea nao ilikuwa kwa njia ya mkalimani.
1276Mwanzo. 42:24>>
Yosefu akaenda kando, akaangua kilio. Alipotulia, akarudi kuzungumza nao. Kisha akamkamata Simeoni na kumtia pingu mbele ya macho yao.
1277Mwanzo. 42:25>>
Yosefu akatoa amri mifuko yao ijazwe nafaka, kila mmoja wao arudishiwe fedha yake katika gunia lake, na wapewe chakula cha njiani. Wakafanyiwa mambo hayo yote.
1278Mwanzo. 42:26>>
Wakawatwisha punda wao mizigo yao ya nafaka, wakaondoka.
1279Mwanzo. 42:27>>
Ikawa walipofika mahali pa kulala wageni huko njiani, mmoja wao akafungua gunia lake ili apate kumlisha punda wake, akashangaa kukuta fedha yake mdomoni mwa gunia lake.
1280Mwanzo. 42:28>>
Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Hii hapa mdomoni mwa gunia langu!” Waliposikia hayo, wakafa moyo. Wakatazamana huku wanatetemeka na kuulizana, “Ni jambo gani hili alilotutendea Mungu?”
1281Mwanzo. 42:29>>
Walipowasili nchini Kanaani kwa baba yao Yakobo, walimsimulia yote yaliyowapata, wakamwambia,
1282Mwanzo. 42:30>>
“Mkuu wa nchi ile alisema nasi kwa ukali, na kutushuku kwamba sisi ni wapelelezi nchini mwake.
1283Mwanzo. 42:31>>
Lakini sisi tulimweleza kuwa sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi.
1284Mwanzo. 42:32>>
Tulimweleza kuwa sisi tuko ndugu kumi na wawili wa baba mmoja, na kwamba mmoja wetu ni marehemu na yule mdogo yuko nyumbani nchini Kanaani pamoja na baba yetu.
1285Mwanzo. 42:33>>
Ndipo mkuu wa nchi hiyo akatuambia, ‘Hivi ndivyo nitakavyotambua kama kweli nyinyi ni watu waaminifu: Mwacheni kwangu ndugu yenu mmoja, nanyi wengine mpeleke nafaka nyumbani kwa jamaa zenu wenye njaa.
1286Mwanzo. 42:34>>
Kisha mleteni kwangu huyo ndugu yenu mdogo, na hapo nitajua kuwa nyinyi si wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Mkifanya hivyo nitamwacha huru ndugu yenu, nanyi mtaruhusiwa kufanya biashara katika nchi hii.’”
1287Mwanzo. 42:35>>
Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka magunia yao, walishangaa kuona kila mmoja wao amerudishiwa kifuko chake na fedha ndani ya gunia lake. Walipoona hayo, wote pamoja na baba yao, wakashikwa na hofu.
1288Mwanzo. 42:36>>
Baba yao Yakobo, akawaambia, “Mnanipokonya watoto wangu! Yosefu hayuko; Simeoni hayuko; sasa mnataka kumchukua na Benyamini. Yote hayo yamenipata!”
1289Mwanzo. 42:37>>
Hapo Reubeni akamwambia baba yake, “Nisipomrudisha Benyamini, waue wanangu wawili. Mwache Benyamini mikononi mwangu, nami nitamlinda na kumrudisha kwako.”
1290Mwanzo. 42:38>>
Lakini baba yake akamjibu, “Mwanangu hatakwenda nanyi; ndugu yake amekwisha fariki, naye peke yake ndiye aliyebaki. Mimi ni mzee mwenye mvi ikiwa kijana huyu atapatwa na madhara yoyote katika safari mtakayofanya basi, mtaniua kwa huzuni.”
1291Mwanzo. 43:1>>
Kisha njaa ilizidi kuwa kali katika nchi ya Kanaani.
1292Mwanzo. 43:2>>
Baada ya kile chakula walichokuwa wamenunua kutoka Misri kumalizika, Yakobo akawaambia wanawe, “Nendeni tena Misri, mkatununulie chakula kidogo.”
1293Mwanzo. 43:3>>
Lakini Yuda akamwambia baba yake, “Yule mtu alituonya vikali, akisema, ‘Sitawapokea msipokuja na ndugu yenu mdogo.’
1294Mwanzo. 43:4>>
Kama utakubali ndugu yetu kwenda pamoja nasi, basi, tutakwenda kukununulia chakula.
1295Mwanzo. 43:5>>
Lakini iwapo hutakubali aende nasi, basi, hatutakwenda huko, kwani yule mtu alituambia waziwazi, ‘Hamtaniona msipokuja na ndugu yenu mdogo.’”
1296Mwanzo. 43:6>>
Israeli akasema, “Kwa nini mkanitia taabuni kwa kumwambia huyo mtu kwamba mnaye ndugu mwingine?”
1297Mwanzo. 43:7>>
Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa makini sana kuhusu mambo yetu na jamaa yetu akisema, ‘Je, baba yenu angali hai? Je, mnaye ndugu mwingine?’ Hivyo tulimjibu kulingana na maswali yake. Tungaliwezaje kujua kwamba atatuambia, ‘Mleteni ndugu yenu?’”
1298Mwanzo. 43:8>>
Yuda akamwambia Israeli, baba yake, “Niruhusu mimi niende naye ili tuondoke mara moja, tuende tukanunue chakula, tusije tukafa njaa pamoja nawe na watoto wetu.
1299Mwanzo. 43:9>>
Mimi mwenyewe nitakuwa mdhamini wake. Wewe utanidai mimi. Nisipomrudisha ukamwona kwa macho yako mwenyewe, lawama na iwe juu yangu milele.
1300Mwanzo. 43:10>>
Kama tusingalikawia, tungalikuwa tumekwisha kwenda na kurudi mara mbili.”
1301Mwanzo. 43:11>>
Hapo Israeli, baba yao, akawaambia, “Haya! Kwa vile ni lazima iwe hivyo basi, fanyeni hivi: Chukueni katika mifuko yenu baadhi ya mazao bora ya nchi yetu, mkampelekee zawadi huyo mkuu. Mchukulieni mafuta kidogo ya mkwaju, asali kidogo, ubani, manemane, kungu na lozi.
1302Mwanzo. 43:12>>
Chukueni fedha mara mbili ya ile inayohitajika, kwa sababu ni lazima mrudishe fedha ile iliyowekwa midomoni mwa magunia yenu; pengine ilirudishwa kwa makosa.
1303Mwanzo. 43:13>>
Mchukueni pia ndugu yenu mwende kwa huyo mtu.
1304Mwanzo. 43:14>>
Mungu Mwenye Nguvu na awajalieni kupata huruma mbele ya mtu huyo, awaachieni yule ndugu yenu mwingine na Benyamini warudi pamoja nanyi. Kwa upande wangu, ikinipasa kufiwa na wanangu basi!”
1305Mwanzo. 43:15>>
Hapo, wakachukua zile zawadi, na fedha mara mbili ya zile za awali, wakaenda Misri pamoja na ndugu yao Benyamini. Walipowasili, wakaenda na kusimama mbele ya Yosefu.
1306Mwanzo. 43:16>>
Yosefu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wapeleke watu hawa nyumbani, umchinje mnyama mmoja na kumtengeneza vizuri, maana watu hawa watakula nami chakula cha mchana.”
1307Mwanzo. 43:17>>
Msimamizi huyo akafanya kama alivyoagizwa: Akawapeleka wale wageni nyumbani kwa Yosefu.
1308Mwanzo. 43:18>>
Walipoona wamepelekwa nyumbani kwa Yosefu, wakashikwa na hofu, wakasema wao kwa wao, “Tumeletwa huku kwa sababu ya ile fedha tuliyorudishiwa katika magunia yetu tulipokuja safari ya kwanza ili apate kisingizio cha kutushambulia ghafla na kutunyanganya punda wetu na kutufanya watumwa wake.”
1309Mwanzo. 43:19>>
Kwa hiyo wakamwendea yule msimamizi wa nyumba ya Yosefu wakaongea naye wakiwa mlangoni,
1310Mwanzo. 43:20>>
wakamwambia, “Samahani, bwana! Sisi tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula.
1311Mwanzo. 43:21>>
Tulipofika mahali pa kulala wageni huko njiani, tulifungua magunia yetu, tukashangaa kukuta fedha ya kila mmoja wetu mdomoni mwa gunia lake bila kuguswa. Sasa tumeirudisha fedha hiyo.
1312Mwanzo. 43:22>>
Tumeleta na fedha nyingine kununulia chakula. Hatujui ni nani aliyeweka fedha yetu katika magunia yetu.”
1313Mwanzo. 43:23>>
Yule msimamizi akawajibu, “Msiwe na wasiwasi, wala msiogope. Bila shaka Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, ndiye aliyewarudishieni fedha katika magunia yenu. Mimi nilipokea fedha yenu.” Kisha akawaletea Simeoni, ndugu yao.
1314Mwanzo. 43:24>>
Huyo msimamizi alipowakaribisha nyumbani kwa Yosefu, akawapa maji ya kunawa miguu yao, na punda wao akawalisha.
1315Mwanzo. 43:25>>
Nao wakatayarisha zawadi zao za kumpa Yosefu, kwa sababu walisikia kuwa watakula pamoja naye.
1316Mwanzo. 43:26>>
Yosefu, aliporudi nyumbani, wakamletea zile zawadi walizokuwa nazo, wakamwinamia kwa heshima.
1317Mwanzo. 43:27>>
Yosefu akawauliza habari zao na kusema, “Mlinisimulia habari za mzee, baba yenu. Je, hajambo? Angali hai?”
1318Mwanzo. 43:28>>
Wakamjibu, “Mtumishi wako, baba yetu, hajambo na angali hai.” Kisha wakainama kwa heshima.
1319Mwanzo. 43:29>>
Yosefu alipoinua macho yake na kumwona Benyamini, nduguye, mtoto wa mama yake, akasema, “Huyu ndiye ndugu yenu mdogo mliyeniambia habari zake? Mungu na akufadhili, mwanangu!”
1320Mwanzo. 43:30>>
Ghafla, Yosefu akatoka mahali hapo, kwani machozi yalikuwa yanamlengalenga kwa shauku kubwa juu ya ndugu yake, akaingia chumbani mwake na kuangua kilio.
1321Mwanzo. 43:31>>
Baada ya kunawa uso wake, alitoka huku akijikaza, akaamuru chakula kiletwe.
1322Mwanzo. 43:32>>
Yosefu aliandaliwa chakula chake peke yake, na ndugu zake wakaandaliwa peke yao, hali kadhalika na Wamisri waliokula pamoja naye, wakaandaliwa peke yao, kwani ni chukizo kwa Wamisri kula chakula pamoja na Waebrania.
1323Mwanzo. 43:33>>
Ndugu zake Yosefu waliketi mbele yake kulingana na umri wao, kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho, wakawa wanaangaliana kwa mshangao.
1324Mwanzo. 43:34>>
Chakula kilikuwa kikichukuliwa kutoka mezani pa Yosefu na kupelekwa kwao, lakini Benyamini alipewa mara tano zaidi ya kiasi walichopewa ndugu zake. Basi, wakanywa na kufurahi pamoja naye.
1325Mwanzo. 44:1>>
Kisha Yosefu alimwagiza msimamizi wa nyumba yake akisema, “Yajaze magunia ya watu hawa nafaka kiasi watakachoweza kuchukua. Halafu, weka fedha ya kila mmoja wao mdomoni mwa gunia lake.
1326Mwanzo. 44:2>>
Katika gunia la yule mdogo kabisa, kiweke kile kikombe changu cha fedha, pamoja na fedha yake.” Huyo msimamizi akafanya kama alivyoamriwa na Yosefu.
1327Mwanzo. 44:3>>
Kulipopambazuka wakaruhusiwa kuondoka pamoja na punda wao.
1328Mwanzo. 44:4>>
Walipokuwa wamesafiri mwendo mfupi tu kutoka mjini, Yosefu alimwambia msimamizi wa nyumba yake, “Haraka! Wafuate wale watu, na utakapowakuta, uwaulize, ‘Kwa nini mmelipa mema mliyotendewa kwa maovu? Kwa nini mmeiba kikombe cha bwana wangu ambacho
1329Mwanzo. 44:5>>
yeye hunywa nacho na kukitumia kupiga ramli? Mmekosa sana kwa kufanya hivyo!’”
1330Mwanzo. 44:6>>
Yule msimamizi alipowakuta akawaambia maneno haya.
1331Mwanzo. 44:7>>
Lakini wao wakamwuliza, “Bwana, una maana gani kutuambia maneno kama hayo? Sisi watumishi wako kamwe hatuwezi kufanya jambo kama hilo!
1332Mwanzo. 44:8>>
Kumbuka, bwana, fedha tuliyokuta katika midomo ya magunia yetu tuliirudisha kutoka katika nchi ya Kanaani. Itawezekanaje tena tuibe fedha au dhahabu nyumbani mwa bwana wako?
1333Mwanzo. 44:9>>
Basi, kama akipatikana mmoja wetu ana kikombe hicho, na auawe, na sisi wengine wote tutakuwa watumwa wako.”
1334Mwanzo. 44:10>>
Huyo msimamizi akasema, “Sawa; na iwe kama mlivyosema. Yeyote atakayepatikana na kikombe hicho, atakuwa mtumwa wangu, lakini wengine wote hamtakuwa na lawama.”
1335Mwanzo. 44:11>>
Basi, kila mmoja akashusha gunia lake chini haraka na kulifungua.
1336Mwanzo. 44:12>>
Yule msimamizi akayapekua magunia yote, akianzia la mkubwa wao na kumalizia na la mdogo kabisa. Kikombe kikapatikana katika gunia la Benyamini.
1337Mwanzo. 44:13>>
Hapo wakayararua mavazi yao kwa huzuni. Kila mmoja wao akambebesha punda wake mzigo wake, wakarudi mjini.
1338Mwanzo. 44:14>>
Yuda na nduguze wakafika nyumbani kwa Yosefu naye Yosefu alikuwapo bado nyumbani. Basi, wakamwinamia kwa heshima,
1339Mwanzo. 44:15>>
naye Yosefu akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivyo? Je hamjui kwamba mtu kama mimi ninao uwezo wa kubashiri?”
1340Mwanzo. 44:16>>
Yuda akamjibu, “Tukuambie nini bwana? Tuseme nini kuonesha kwamba hatuna hatia? Mungu ameyafichua makosa yetu, sisi watumishi wako. Sasa sote tu watumwa wako, sisi pamoja na yule aliyepatikana na kikombe chako.”
1341Mwanzo. 44:17>>
Lakini Yosefu akasema, “La! Mimi siwezi kufanya hivyo! Yule tu aliyepatikana na kikombe changu ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nyinyi wengine wote rudini kwa amani kwa baba yenu.”
1342Mwanzo. 44:18>>
Ndipo Yuda akamkaribia Yosefu na kumwambia, “Bwana, nakuomba uniruhusu mimi mtumishi wako, nijitetee mbele yako kwa maneno machache; ninakusihi usinikasirikie, kwani wewe ni kama Farao mwenyewe.
1343Mwanzo. 44:19>>
Bwana, wewe ulituuliza kama tuna baba au ndugu,
1344Mwanzo. 44:20>>
nasi tukakueleza kwamba tunaye baba, naye ni mzee, na kwamba tunaye ndugu mwingine mdogo aliyezaliwa wakati wa uzee wa baba yetu. Kaka yake huyo kijana amekwisha fariki, na huyo mdogo ndiye peke yake aliyebaki wa mama yake; na mzee wetu anampenda sana kijana huyo.
1345Mwanzo. 44:21>>
Bwana, ulituagiza sisi watumishi wako kumleta huyo mdogo wetu upate kumwona.
1346Mwanzo. 44:22>>
Tukakueleza kwamba huyo kijana hawezi kuachana na baba yake, kwa sababu akifanya hivyo baba yake atakufa.
1347Mwanzo. 44:23>>
Lakini wewe bwana ukatuambia kwamba kama hatutakuja na ndugu yetu mdogo, hutatupokea tena.
1348Mwanzo. 44:24>>
“Tuliporudi nyumbani kwa mtumishi wako, baba yetu, tulimwarifu ulivyotuagiza, bwana.
1349Mwanzo. 44:25>>
Naye alipotuambia tuje tena huku kununua chakula,
1350Mwanzo. 44:26>>
tulimwambia, ‘Hatuwezi kwenda, isipokuwa tu kama ndugu yetu mdogo atakwenda pamoja nasi; kama hatakwenda pamoja nasi hatuwezi kupokelewa na yule mtu.’
1351Mwanzo. 44:27>>
Basi, baba yetu, mtumishi wako, akatuambia, ‘Mnajua kwamba mke wangu Raheli alinizalia wana wawili:
1352Mwanzo. 44:28>>
Mmoja alitoweka, nami nikasema, bila shaka ameraruliwa vipandevipande na mnyama wa porini, maana sijapata kumwona tena.
1353Mwanzo. 44:29>>
Kama mtamchukua huyu pia kutoka kwangu, akipatwa na madhara basi, mtanishusha kuzimu nikiwa mzee mwenye huzuni.’
1354Mwanzo. 44:30>>
Kwa hiyo basi, bwana, nikimrudia baba yangu mtumishi wako bila kijana huyu, na hali uhai wa baba unategemea uhai wa kijana huyu,
1355Mwanzo. 44:31>>
akiona kwamba kijana hayupo pamoja nasi, atakufa! Hivyo sisi watumishi wako, tutamuua baba yetu kwa huzuni.
1356Mwanzo. 44:32>>
Zaidi ya hayo, mimi binafsi nilijitoa kuwa mdhamini wa huyu kijana kwa baba yangu, nikisema, ‘Nisipomrudisha Benyamini kwako, lawama na iwe juu yangu milele.’
1357Mwanzo. 44:33>>
Sasa, ee bwana, nakusihi, mimi mtumishi wako, nibaki, niwe mtumwa wako badala ya kijana huyu. Mwache yeye arudi nyumbani pamoja na ndugu zake.
1358Mwanzo. 44:34>>
Nitawezaje kumrudia baba yangu bila kijana huyu? Siwezi kustahimili kuyaona madhara yatakayompata baba yangu.”
1359Mwanzo. 45:1>>
Hapo Yosefu akashindwa kujizuia mbele ya wote walioandamana naye, akawaamuru watoke nje. Hivyo Yosefu alikuwa peke yake alipojitambulisha kwa ndugu zake.
1360Mwanzo. 45:2>>
Lakini alilia kwa sauti kubwa hata Wamisri wakamsikia, hali kadhalika na watu wa jamaa ya Farao nao wakamsikia.
1361Mwanzo. 45:3>>
Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu. Je, baba yangu angali hai?” Lakini ndugu zake wakapigwa na bumbuazi mbele yake, hata wakashindwa kumjibu.
1362Mwanzo. 45:4>>
Yosefu akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, sogeeni karibu nami.” Walipomkaribia, akawaambia, “Mimi ndiye ndugu yenu Yosefu, mliyemwuza Misri.
1363Mwanzo. 45:5>>
Lakini sasa msifadhaike wala kujilaumu kwa kuniuza. Mungu ndiye aliyenileta huku niwatangulie, ili niyaokoe maisha ya watu.
1364Mwanzo. 45:6>>
Huu ni mwaka wa pili tu wa njaa nchini, na bado kuna miaka mitano zaidi ambapo watu hawataweza kulima wala kuvuna mavuno.
1365Mwanzo. 45:7>>
Mungu alinileta huku niwatangulie, ili kusalimisha maisha yenu mbaki hai nchini na kuwakomboa kwa ukombozi mkubwa.
1366Mwanzo. 45:8>>
Kwa hiyo, si nyinyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Ndiye aliyenifanya kama baba kwa Farao, msimamizi wa nyumba yake yote na mtawala wa nchi yote ya Misri.
1367Mwanzo. 45:9>>
Basi, fanyeni haraka, mwende kwa baba na kumwambia, ‘Yosefu, mwana wako, anasema: Mungu amenifanya kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri. Basi, usikawie kuja kwangu.
1368Mwanzo. 45:10>>
Utakaa karibu nami katika eneo la Gosheni: Wewe, wana wako na wajukuu wako, mifugo yako na mali yako yote.
1369Mwanzo. 45:11>>
Utakapokuwa Gosheni, mimi nitakutunza wewe, jamaa yako pamoja na mifugo yako ili msije mkafa njaa, kwani bado miaka mitano zaidi ya njaa.’”
1370Mwanzo. 45:12>>
Kisha Yosefu akasema, “Nyinyi wenyewe mmeona kwa macho yenu na hata ndugu yangu Benyamini ameona kwa macho yake kwamba ni mimi mwenyewe Yosefu ninayezungumza nanyi.
1371Mwanzo. 45:13>>
Ni lazima kumwambia baba yangu juu ya fahari yangu huku Misri na yote mliyoyaona. Basi, fanyeni haraka, mkamlete baba yangu huku.”
1372Mwanzo. 45:14>>
Kisha Yosefu akamkumbatia Benyamini, nduguye, akalia; Benyamini naye akalia, huku wamekumbatiana.
1373Mwanzo. 45:15>>
Akiwa bado analia, Yosefu akawakumbatia ndugu zake na kuwabusu. Hapo ndipo ndugu zake walipoweza kuzungumza naye.
1374Mwanzo. 45:16>>
Habari hizo zilipofika ikulu ya mfalme, kwamba ndugu za Yosefu wamekuja, zikamfurahisha sana Farao na watumishi wake.
1375Mwanzo. 45:17>>
Kwa hiyo, Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako wawapakie punda wao mizigo, warudi nchini Kanaani,
1376Mwanzo. 45:18>>
wamlete hapa baba yao na jamaa zao wote. Mimi nitawapa sehemu nzuri kabisa ya nchi ya Misri, ambako wataweza kufurahia matunda yote ya nchi hii.
1377Mwanzo. 45:19>>
Waambie pia wachukue kutoka hapa magari ya kukokotwa ya kuwaleta watoto wao wachanga na wake zao na wala wasikose kumleta baba yao.
1378Mwanzo. 45:20>>
Waambie wasijali juu ya mali zao maana sehemu nzuri kuliko zote katika nchi ya Misri itakuwa yao.”
1379Mwanzo. 45:21>>
Basi, wana wa Israeli wakafanya kama walivyoagizwa. Yosefu akawapa magari kulingana na maagizo ya Farao na chakula cha njiani.
1380Mwanzo. 45:22>>
Aliwapa kila mmoja wao mavazi ya kubadili, lakini akampa Benyamini vipande 300 vya fedha na mavazi matano ya kubadili.
1381Mwanzo. 45:23>>
Tena alimpelekea baba yake zawadi hizi kwa ajili ya safari yake: Punda kumi waliobeba bidhaa bora za Misri, punda jike kumi waliobeba nafaka, mikate na vyakula vingine.
1382Mwanzo. 45:24>>
Basi, Yosefu akaagana na ndugu zake. Walipokuwa wanaondoka aliwaonya akisema, “Msigombane njiani!”
1383Mwanzo. 45:25>>
Basi, wakatoka Misri na kurudi nyumbani kwa baba yao Yakobo, nchini Kanaani.
1384Mwanzo. 45:26>>
Wakamwambia baba yao, “Yosefu yu hai! Yeye ndiye mtawala wa nchi yote ya Misri!” Hapo baba yao akapigwa na bumbuazi, kwani hakuweza kuyasadiki maneno yao.
1385Mwanzo. 45:27>>
Lakini, walipomsimulia yote waliyoagizwa na Yosefu na alipoyaona magari aliyopelekewa na Yosefu kumchukua, moyo wake ukajaa furaha kupita kiasi.
1386Mwanzo. 45:28>>
Israeli akasema, “Sasa nimeridhika; mwanangu Yosefu yu hai! Nitakwenda nimwone kabla sijafa.”
1387Mwanzo. 46:1>>
Basi, Israeli akaanza safari yake pamoja na mali yake yote. Alipofika Beer-sheba, akamtolea tambiko Mungu wa Isaka, baba yake.
1388Mwanzo. 46:2>>
Mungu akaongea na Israeli katika maono usiku, akamwita, “Yakobo! Yakobo!” Yakobo akaitika, “Naam nasikiliza.”
1389Mwanzo. 46:3>>
Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu, Mungu wa baba yako. Usiogope kwenda Misri; utakapokuwa huko, nitakufanya uwe taifa kubwa.
1390Mwanzo. 46:4>>
Mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nawe huko Misri na kukurudisha huku. Utakapofariki, mkono wa Yosefu ndio utakaoyafumba macho yako.”
1391Mwanzo. 46:5>>
Basi, Yakobo akaondoka Beer-sheba. Wanawe wakamchukua yeye, watoto wao wachanga pamoja na wake zao katika magari ambayo Farao alipeleka kumchukua.
1392Mwanzo. 46:6>>
Walichukua pia mifugo na mali yao yote waliyokuwa wamechuma katika nchi ya Kanaani, wakaenda Misri. Yakobo aliwachukua wazawa wake wote:
1393Mwanzo. 46:7>>
Wanawe, wajukuu wake wa kiume na wa kike, wote akawaleta Misri.
1394Mwanzo. 46:8>>
Wazawa wa Israeli ambao walikwenda Misri pamoja naye walikuwa Reubeni, mzaliwa wake wa kwanza,
1395Mwanzo. 46:9>>
pamoja na wana wa Reubeni: Henoki, Palu, Hesroni na Karmi.
1396Mwanzo. 46:10>>
Simeoni na wanawe: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli, aliyezaliwa na mwanamke Mkanaani.
1397Mwanzo. 46:11>>
Lawi na wanawe: Gershoni, Kohathi na Merari.
1398Mwanzo. 46:12>>
Yuda na wanawe: Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera. (Lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani). Wana wa Peresi walikuwa Hesroni na Hamuli.
1399Mwanzo. 46:13>>
Isakari na wanawe: Tola, Puva, Yashubu na Shimroni.
1400Mwanzo. 46:14>>
Zebuluni na wanawe: Seredi, Eloni na Yaleeli.
1401Mwanzo. 46:15>>
Hao ndio wana ambao Lea alimzalia Yakobo kule Padan-aramu, pamoja na Dina binti yake. Jumla ya wanawe, binti zake na wajukuu wake walikuwa watu thelathini na watatu.
1402Mwanzo. 46:16>>
Gadi na wanawe: Sifioni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli.
1403Mwanzo. 46:17>>
Asheri na wanawe: Imna, Ishva, Ishvi, Beria na Sera, dada yao. Beria na wanawe: Heberi na Malkieli.
1404Mwanzo. 46:18>>
Hawa kumi na sita ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Zilpa, mjakazi ambaye Labani alimpa Lea, binti yake.
1405Mwanzo. 46:19>>
Raheli alimzalia Yakobo wana wawili: Yosefu na Benyamini.
1406Mwanzo. 46:20>>
Huko Misri, Asenathi, binti Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yosefu wana wawili: Manase na Efraimu.
1407Mwanzo. 46:21>>
Wana wa Benyamini walikuwa Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi.
1408Mwanzo. 46:22>>
Watu hao kumi na wanne ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Raheli, mkewe.
1409Mwanzo. 46:23>>
Dani na Hushimu, mwanawe.
1410Mwanzo. 46:24>>
Naftali na wanawe: Yaseeli, Guni, Yeseri na Shilemu.
1411Mwanzo. 46:25>>
Hao saba ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Bilha, mjakazi ambaye Labani alimpa binti yake Raheli.
1412Mwanzo. 46:26>>
Jumla ya wazawa wa Yakobo aliokwenda nao Misri, bila kuwahesabu wake za wanawe, ilikuwa watu sitini na sita.
1413Mwanzo. 46:27>>
Huko nchini Misri Yosefu alikuwa amepata wana wawili. Kwa hiyo watu wote wa jamaa ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini.
1414Mwanzo. 46:28>>
Yakobo akamtanguliza Yuda kwa Yosefu kumwomba waonane huko Gosheni; nao wakafika katika eneo la Gosheni.
1415Mwanzo. 46:29>>
Yosefu akapanda gari lake la farasi, akaenda kumlaki Israeli, baba yake, huko Gosheni. Alipomfikia baba yake, alimkumbatia na kulia kwa kitambo kirefu.
1416Mwanzo. 46:30>>
Israeli akamwambia Yosefu, “Hata nikifa sasa si kitu kwa kuwa nimeuona uso wako na kujua kwamba wewe u hai!”
1417Mwanzo. 46:31>>
Yosefu akawaambia ndugu zake na jamaa yote ya baba yake, “Nakwenda kumwarifu Farao kwamba ndugu zangu na jamaa yote ya baba yangu waliokuwa katika nchi ya Kanaani wamekuja kwangu.
1418Mwanzo. 46:32>>
Nitamweleza kwamba nyinyi ni wachungaji kwani mmekuwa mkichunga mifugo, na kwamba mmewasili pamoja na mbuzi, kondoo, ngômbe na mali yenu yote.
1419Mwanzo. 46:33>>
Basi, Farao akiwaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’
1420Mwanzo. 46:34>>
Semeni: ‘Bwana, sisi watumishi wako, ni wafugaji wa mifugo tangu utoto wetu mpaka leo, kwani ndivyo walivyokuwa babu zetu’; semeni hivyo ili mruhusiwe kukaa katika eneo la Gosheni.” Yosefu alisema hivyo kwa sababu kwa Wamisri wachungaji wote wa kondoo ni chukizo.
1421Mwanzo. 47:1>>
Basi, Yosefu akaenda kwa Farao, akamwambia, “Baba yangu na ndugu zangu pamoja na kondoo, ngômbe na mali yao yote, wamefika kutoka nchi ya Kanaani. Sasa wako katika eneo la Gosheni.”
1422Mwanzo. 47:2>>
Yosefu alikuwa amewachukua ndugu zake watano, akawajulisha kwa Farao.
1423Mwanzo. 47:3>>
Farao akawauliza, “Kazi yenu ni nini?” Wakamjibu, “Bwana, sisi watumishi wako ni wachungaji, kama walivyokuwa babu zetu.”
1424Mwanzo. 47:4>>
Kisha wakamwambia Farao, “Sisi watumishi wako tumekuja kukaa kama wageni humu nchini kwa kuwa njaa ni kali huko Kanaani na hakuna tena malisho kwa mifugo yetu. Hivyo, bwana, tunakuomba, sisi watumishi wako, uturuhusu kukaa katika eneo la Gosheni.”
1425Mwanzo. 47:5>>
Farao akamwambia Yosefu, “Baba yako na ndugu zako wamekujia wewe.
1426Mwanzo. 47:6>>
Nchi yote ya Misri iko chini yako; wape baba yako na ndugu zako sehemu bora ya nchi hii. Waache wakae katika eneo la Gosheni. Na iwapo unawafahamu watu stadi miongoni mwao, wateue wawe waangalizi wa mifugo yangu.”
1427Mwanzo. 47:7>>
Kisha, Yosefu akamleta baba yake Yakobo kumwamkia Farao; naye Yakobo akampa Farao baraka zake.
1428Mwanzo. 47:8>>
Farao akamwuliza Yakobo, “Umri wako ni miaka mingapi?”
1429Mwanzo. 47:9>>
Yakobo akamjibu, “Umri niliojaliwa kama msafiri ni miaka 130. Miaka hiyo imekuwa michache na iliyojaa mateso, tena haijafikia idadi ya miaka waliyoishi wazee wangu kama wasafiri.”
1430Mwanzo. 47:10>>
Kisha Yakobo akambariki Farao, akaondoka.
1431Mwanzo. 47:11>>
Basi, Yosefu akawapa baba yake na ndugu zake eneo la Ramesesi lililo bora kabisa katika nchi ya Misri, liwe makao yao, nao wakalimiliki kama alivyoagiza Farao.
1432Mwanzo. 47:12>>
Yosefu akawa anawapatia chakula baba yake, ndugu zake na jamaa yote ya baba yake kulingana na idadi ya watu waliowategemea.
1433Mwanzo. 47:13>>
Baadaye chakula kiliadimika kabisa nchini kote. Njaa ilikuwa kali sana hata ikawafanya watu wote katika nchi ya Misri na ya Kanaani kudhoofika.
1434Mwanzo. 47:14>>
Yosefu akakusanya fedha yote ya nchi ya Misri na Kanaani kutokana na nafaka waliyonunua, akaipeleka fedha hiyo ikulu kwa Farao.
1435Mwanzo. 47:15>>
Baada ya watu wote wa nchi ya Misri na Kanaani kutumia fedha yao yote Wamisri wote walimjia Yosefu na kumwambia, “Tupe chakula! Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Tazama, sasa fedha yetu imekwisha!”
1436Mwanzo. 47:16>>
Yosefu akawaambia, “Kama fedha yenu imekwisha, basi nipeni mifugo yenu, nami nitawapa nafaka.”
1437Mwanzo. 47:17>>
Ndipo wakamletea Yosefu mifugo yao: Farasi, ngômbe, kondoo, mbuzi na punda, naye akawapa chakula. Mwaka huo Yosefu akawa anawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote.
1438Mwanzo. 47:18>>
Mwaka uliofuata wakamjia tena na kumwambia, “Bwana, ukweli ni kwamba fedha yetu yote imekwisha, na wanyama wetu wamekuwa mali yako. Sasa, bwana, sisi watumishi wako hatuna chochote tunachoweza kukupa isipokuwa miili yetu na mashamba yetu.
1439Mwanzo. 47:19>>
Ya nini sisi tufe mbele ya macho yako na mashamba yetu yaharibike? Utununue sisi pamoja na mashamba yetu, tuwe watumwa wa Farao, mradi tu utupe chakula. Tupe nafaka, tusije tukafa; utupe na mbegu kwa ajili ya mashamba yetu.”
1440Mwanzo. 47:20>>
Hivyo Yosefu akainunua nchi yote ya Misri iwe mali ya Farao. Kila Mmisri alilazimika kuuza shamba lake, kwa jinsi njaa ilivyokuwa kali. Nchi yote ikawa mali ya Farao,
1441Mwanzo. 47:21>>
na Yosefu akawafanya watu kuwa watumwa, kutoka pembe moja hadi pembe nyingine ya nchi ya Misri.
1442Mwanzo. 47:22>>
Ardhi ambayo Yosefu hakuinunua ni ile iliyomilikiwa na makuhani. Hao hawakulazimika kuiuza ardhi yao kwani waliishi kwa posho maalumu waliyopewa na Farao.
1443Mwanzo. 47:23>>
Kisha Yosefu akawaambia watu, “Tazameni, nimekwisha wanunua nyinyi nyote na mashamba yenu kuwa mali ya Farao. Mtapewa mbegu nanyi mtapanda mashamba yenu.
1444Mwanzo. 47:24>>
Wakati wa mavuno, sehemu moja ya tano mtampa Farao. Sehemu nne zitakazobaki zitakuwa mbegu na chakula kwa ajili yenu na jamaa zenu na watoto wenu.”
1445Mwanzo. 47:25>>
Wakamjibu, “Bwana, umeyaokoa maisha yetu! Kwa vile umetuonesha wema wako, sisi tutakuwa watumwa wa Farao.”
1446Mwanzo. 47:26>>
Ndivyo Yosefu alivyotangaza sheria moja ambayo iko mpaka leo nchini Misri: Kila raia lazima atoe sehemu moja ya tano ya mavuno yake kwa Farao. Ardhi ya makuhani tu ndiyo haikununuliwa na kufanywa mali ya Farao.
1447Mwanzo. 47:27>>
Basi, watu wa Israeli wakakaa katika eneo la Gosheni nchini Misri. Wakiwa huko, wakachuma mali nyingi, wakazaana na kuongezeka sana.
1448Mwanzo. 47:28>>
Yakobo alikaa katika nchi ya Misri kwa muda wa miaka kumi na saba, hadi alipofikia umri wa miaka 147.
1449Mwanzo. 47:29>>
Wakati wa kufa kwake ulipokaribia, Yakobo akamwita mwanawe Yosefu, akamwambia, “Sasa, kama kweli unanipenda, weka mkono wako mapajani mwangu, uniahidi kwamba utanitendea kwa heshima na haki. Usinizike huku Misri,
1450Mwanzo. 47:30>>
ila unilaze pamoja na babu zangu. Nichukue kutoka Misri, ukanizike katika makaburi yao.” Yosefu akamjibu, “Nitafanya kama ulivyosema.”
1451Mwanzo. 47:31>>
Yakobo akamwambia, “Niapie!” Yosefu akamwapia. Kisha Israeli akainamia upande wa kichwa cha kitanda chake.
1452Mwanzo. 48:1>>
Baada ya hayo, Yosefu alipewa habari kwamba baba yake ni mgonjwa. Hivyo, akawachukua wanawe wawili, Manase na Efraimu, akaenda nao kwa baba yake.
1453Mwanzo. 48:2>>
Yakobo alipofahamishwa kwamba mwanawe Yosefu amefika kumwona, akajitahidi kuinuka, akaketi kitandani.
1454Mwanzo. 48:3>>
Yakobo akamwambia Yosefu, “Mungu mwenye nguvu alinitokea nilipokuwa kule Luzu katika nchi ya Kanaani, akanibariki.
1455Mwanzo. 48:4>>
Aliniambia, ‘Tazama, nitakufanya uwe na wazawa na uongezeke; nitakufanya uwe babu wa jamii kubwa za watu. Ardhi hii nitawapa wazawa wako, waimiliki milele.’”
1456Mwanzo. 48:5>>
Yakobo akaendelea kusema, “Wanao wawili uliowapata hapa Misri kabla sijafika, ni wanangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu kama walivyo Reubeni na Simeoni.
1457Mwanzo. 48:6>>
Lakini, watoto utakaopata baadaye watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao.
1458Mwanzo. 48:7>>
Naamua hivyo kwa sababu ya mama yako, Raheli. Nilipokuwa narudi kutoka Padani yeye alifariki katika nchi ya Kanaani, tukiwa karibu kufika Efratha, akaniachia huzuni. Basi, nikamzika papo hapo, kando ya njia iendayo Efratha, yaani Bethlehemu.”
1459Mwanzo. 48:8>>
Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akamwuliza, “Ni akina nani hawa?”
1460Mwanzo. 48:9>>
Yosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wanangu alionijalia Mungu nikiwa huku.” Israeli akasema, “Tafadhali, walete karibu nipate kuwabariki.”
1461Mwanzo. 48:10>>
Macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee. Basi, Yosefu akawasogeza wanawe karibu na baba yake, naye akawabusu na kuwakumbatia.
1462Mwanzo. 48:11>>
Kisha Israeli akamwambia Yosefu, “Sikutazamia kuuona uso wako tena; lakini, kumbe, Mungu amenijalia hata kuwaona watoto wako!”
1463Mwanzo. 48:12>>
Hapo Yosefu akawaondoa wanawe kwenye magoti ya baba yake, kisha akainama kwa heshima.
1464Mwanzo. 48:13>>
Yosefu akawainua wanawe wawili, Efraimu katika mkono wake wa kulia, akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa baba yake, na Manase katika mkono wake wa kushoto, akimwelekeza kwenye mkono wa kulia wa baba yake, akawasogeza kwa babu yao.
1465Mwanzo. 48:14>>
Lakini Israeli akaipishanisha mikono yake: Mkono wake wa kulia akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, aliyekuwa mzaliwa wa kwanza.
1466Mwanzo. 48:15>>
Kisha Israeli akambariki Yosefu, akisema, “Mungu ambaye babu zangu Abrahamu na Isaka walimtii maishani mwao, Mungu ambaye ameniongoza maishani mwangu hadi leo,
1467Mwanzo. 48:16>>
na malaika ambaye aliniokoa katika mabaya yote, na awabariki vijana hawa! Jina langu na majina ya wazee wangu, Abrahamu na Isaka, yadumishwe katika vijana hawa; nao waongezeke kwa wingi duniani.”
1468Mwanzo. 48:17>>
Yosefu alipoona kwamba baba yake ameuweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa cha Efraimu hakupendezwa. Basi, akaushika mkono wa baba yake, akitaka kuuondoa juu ya kichwa cha Efraimu auweke juu ya kichwa cha Manase.
1469Mwanzo. 48:18>>
Akamwambia baba yake, “Sivyo, baba! Huyu hapa ndiye mzaliwa wa kwanza. Tafadhali, uweke mkono wako wa kulia juu ya kichwa chake.”
1470Mwanzo. 48:19>>
Lakini baba yake akakataa, akisema, “Najua, mwanangu, najua. Wana wa Manase pia watakuwa taifa kubwa na mashuhuri. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, na wazawa wake watakuwa mataifa mengi.”
1471Mwanzo. 48:20>>
Basi, Israeli akawabariki siku hiyo, akisema, “Waisraeli watayatumia majina yenu kubarikia, watasema, ‘Mungu akutendee mema kama Efraimu na Manase!’” Ndivyo Israeli alivyomweka Efraimu mbele ya Manase.
1472Mwanzo. 48:21>>
Kisha Israeli akamwambia Yosefu, “Kama uonavyo, mimi niko karibu kufa. Hata hivyo, Mungu atakuwa pamoja nanyi, na kuwarudisheni katika nchi ya babu zenu.
1473Mwanzo. 48:22>>
Zaidi ya hayo, nimekupa wewe, wala si ndugu zako, eneo moja milimani, nililowanyanganya Waamori kwa upanga na upinde wangu.”
1474Mwanzo. 49:1>>
Yakobo akawaita wanawe, akasema, “Kusanyikeni pamoja niwaambieni mambo yatakayowapata siku zijazo.
1475Mwanzo. 49:2>>
“Kusanyikeni msikie, enyi wana wa Yakobo, nisikilizeni mimi Israeli, baba yenu.
1476Mwanzo. 49:3>>
“Wewe Reubeni ni mzaliwa wangu wa kwanza, nguvu yangu na tunda la ujana wangu. Wewe wawapita ndugu zako kwa ukuu na nguvu.
1477Mwanzo. 49:4>>
“Wewe ni kama maji ya mafuriko. Lakini hutakuwa wa kwanza tena, maana ulipanda kitandani mwangu mimi baba yako, wewe ulikitia najisi; naam wewe ulikipanda!
1478Mwanzo. 49:5>>
Simeoni na Lawi ni ndugu: Silaha zao wanatumia kufanya ukatili,
1479Mwanzo. 49:6>>
lakini mimi sitashiriki njama zao; ee roho yangu, usishiriki mikutano yao, maana, katika hasira yao, walimuua mtu, kwa utundu wao walikata mshipa wa ngômbe.
1480Mwanzo. 49:7>>
“Nalaani hasira yao maana ni kali mno, na ghadhabu yao isiyo na huruma. Nitawatawanya katika nchi ya Yakobo, nitawasambaza katika nchi ya Israeli.
1481Mwanzo. 49:8>>
“Wewe Yuda, ndugu zako watakusifu. Adui zako utawakaba shingo; na ndugu zako watainama mbele yako.
1482Mwanzo. 49:9>>
“Wewe Yuda, mwanangu, ni kama mwanasimba ambaye amepata mawindo yake akapanda juu. Kama simba hujinyosha na kulala chini; simba mwenye nguvu, nani athubutuye kumwamsha?
1483Mwanzo. 49:10>>
“Fimbo ya kifalme haitatoka kwa Yuda, wala bakora ya utawala miguuni pake, mpaka atakapofika yule ambaye ni yake; ambaye mataifa yatamtii.
1484Mwanzo. 49:11>>
“Atafunga punda wake katika mzabibu na mwanapunda wake kwenye mzabibu bora. Hufua nguo zake katika divai, na mavazi yake katika divai nyekundu.
1485Mwanzo. 49:12>>
“Macho yake ni mekundu kwa divai, meno yake ni meupe kwa maziwa.
1486Mwanzo. 49:13>>
Zebuluni ataishi sehemu za pwani, pwani yake itakuwa mahali pa kuegesha meli. Nchi yake itapakana na Sidoni.
1487Mwanzo. 49:14>>
Isakari ni kama punda mwenye nguvu, ajilazaye kati ya mizigo yake.
1488Mwanzo. 49:15>>
“Aliona kuwa mahali pa kupumzikia ni pema, na kwamba nchi ni ya kupendeza, akauinamisha mgongo wake kubeba mzigo, akawa mtumwa kufanya kazi za shuruti.
1489Mwanzo. 49:16>>
Dani atakuwa mwamuzi wa watu wake, kama mojawapo ya makabila ya Israeli.
1490Mwanzo. 49:17>>
“Atakuwa kama nyoka njiani, nyoka mwenye sumu kando ya njia, aumaye visigino vya farasi, naye mpandafarasi huanguka chali.
1491Mwanzo. 49:18>>
“Ee Mwenyezi-Mungu, nangojea uniokoe!
1492Mwanzo. 49:19>>
Gadi atashambuliwa na wanyanganyi, lakini yeye atawafuata nyuma na kuwashambulia.
1493Mwanzo. 49:20>>
“Ardhi ya Asheri itatoa mavuno kwa wingi, naye atatoa chakula kimfaacho mfalme.
1494Mwanzo. 49:21>>
Naftali ni kama paa aliye huru, azaaye watoto walio wazuri.
1495Mwanzo. 49:22>>
Yosefu ni kama mti uzaao, mti uzaao kando ya chemchemi, matawi yake hutanda ukutani.
1496Mwanzo. 49:23>>
“Wapiga mishale walimshambulia vikali, wakamtupia mishale na kumsumbua sana.
1497Mwanzo. 49:24>>
“Lakini upinde wake bado imara, na mikono yake imepewa nguvu, kwa uwezo wa Mwenye Nguvu wa Yakobo, kwa jina la Mchungaji, Mwamba wa Israeli;
1498Mwanzo. 49:25>>
“kwa Mungu wa baba yako atakayekusaidia, kwa Mungu mwenye nguvu atakayekubariki; upate baraka za mvua toka juu mbinguni, baraka za maji ya vilindi vilivyo chini, baraka za uzazi wa akina mama na mifugo.
1499Mwanzo. 49:26>>
Baraka za baba yako zishinde baraka za milima ya milele, ziwe bora kuliko vilima vya kale. Baraka hizo na ziwe juu ya kichwa cha Yosefu, juu ya paji lake yeye aliyekuwa ametengwa na ndugu zake.
1500Mwanzo. 49:27>>
Benyamini ni mbwamwitu mkali; asubuhi hula mawindo yake, na jioni hugawa nyara.”
1501Mwanzo. 49:28>>
Hayo ndiyo makabila kumi na mawili ya Israeli, na hayo ndiyo maneno aliyowaambia baba yao alipowabariki, kila mmoja wao kama alivyostahili.
1502Mwanzo. 49:29>>
Kisha Israeli akawaagiza wanawe hivi, “Mimi karibu nife na kujiunga na watu wangu. Nizikeni pamoja na wazee wangu katika pango lililoko shambani mwa Efroni Mhiti,
1503Mwanzo. 49:30>>
kule Makpela, mashariki ya Mamre, nchini Kanaani. Abrahamu alinunua pango na shamba hilo kwa Efroni, Mhiti, liwe lake la kuzikia.
1504Mwanzo. 49:31>>
Huko ndiko walikozikwa Abrahamu na mkewe Sara; huko ndiko walikozikwa Isaka na mkewe Rebeka; na huko ndiko nilikomzika Lea.
1505Mwanzo. 49:32>>
Shamba hilo na pango lake lilinunuliwa kwa Wahiti.”
1506Mwanzo. 49:33>>
Yakobo alipomaliza kuwausia wanawe, aliirudisha miguu yake kitandani, akatoa roho akajiunga na wazee wake.
1507Mwanzo. 50:2>>
Kisha, akawaagiza waganga wake wampake Israeli, baba yake, dawa ili asioze, nao wakafanya hivyo.
1508Mwanzo. 50:3>>
Kama kawaida, siku arubaini zilihitajika kwa kazi hiyo. Wamisri nao wakaomboleza kifo cha Yakobo kwa muda wa siku sabini.
1509Mwanzo. 50:4>>
Baada ya matanga kumalizika, Yosefu akawaambia watu wa jamaa ya Farao, “Ikiwa nimekubalika mbele yenu, tafadhali zungumzeni na Farao kwa niaba yangu kwamba baba yangu aliniapisha, akisema,
1510Mwanzo. 50:5>>
‘Mimi karibu nitafariki. Yakupasa kunizika katika kaburi nililojichongea katika nchi ya Kanaani.’ Kwa hiyo namwomba aniruhusu niende kumzika baba yangu, kisha nitarudi.”
1511Mwanzo. 50:6>>
Farao akajibu, “Nenda ukamzike baba yako kama alivyokuapisha.”
1512Mwanzo. 50:7>>
Basi, Yosefu akaondoka kwenda kumzika baba yake akifuatana na watumishi wote wa Farao, wazee wa nyumba ya Farao, pamoja na wazee wa nchi nzima ya Misri.
1513Mwanzo. 50:8>>
Hali kadhalika, Yosefu alifuatana na jamaa yake yote, ndugu zake na jamaa yote ya baba yake Yakobo. Katika eneo la Gosheni walibaki watoto wao tu pamoja na kondoo, mbuzi na ngômbe wao.
1514Mwanzo. 50:9>>
Pia waliandamana naye wapandafarasi na magari; lilikuwa kundi kubwa sana.
1515Mwanzo. 50:10>>
Walipofika katika uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, ngambo ya mto Yordani, waliomboleza kwa huzuni kubwa, naye Yosefu akamfanyia baba yake marehemu matanga ya siku saba.
1516Mwanzo. 50:11>>
Wakanaani wenyeji wa nchi hiyo, walipoyaona maombolezo yaliyofanywa kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, wakasema, “Maombolezo haya ya Wamisri, kweli ni makubwa!” Kwa hiyo, mahali pale pakaitwa Abel-misri, napo pako ngambo ya mto Yordani.
1517Mwanzo. 50:12>>
Wana wa Yakobo walimfanyia baba yao kama alivyowaagiza:
1518Mwanzo. 50:13>>
Walimchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika katika pango lililokuwa katika shamba kule Makpela, mashariki ya Mamre. Pango pamoja na shamba hilo Abrahamu alikuwa amelinunua kwa Efroni Mhiti, ili pawe mahali pake pa kuzikia.
1519Mwanzo. 50:14>>
Baada ya kumzika baba yake, Yosefu alirudi Misri pamoja na ndugu zake na watu wote waliokuwa wameandamana naye kwenda kumzika baba yake.
1520Mwanzo. 50:15>>
Baada ya kifo cha baba yao, ndugu zake Yosefu walisemezana, “Huenda Yosefu atatuchukia na kutulipiza mabaya yote tuliyomtendea.”
1521Mwanzo. 50:16>>
Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakisema, “Baba yako, kabla hajafariki, aliagiza hivi,
1522Mwanzo. 50:17>>
‘Mwambieni Yosefu kwa niaba yangu: Tafadhali uwasamehe ndugu zako makosa yao mabaya na maovu yote waliyokutendea.’ Sasa basi, tafadhali usamehe uovu tuliokutendea sisi watumishi wa Mungu wa baba yako.” Yosefu alipopata ujumbe huu, alilia.
1523Mwanzo. 50:18>>
Kisha ndugu zake wakamjia, wakainama mpaka chini mbele yake, wakasema, “Tazama, sisi tu watumishi wako.”
1524Mwanzo. 50:19>>
Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope, je, mimi ni badala ya Mungu?
1525Mwanzo. 50:20>>
Nyinyi mlitaka kunitendea vibaya, lakini Mungu alikusudia mema ili watu wengi wapate kuwa hai kama mwonavyo leo.
1526Mwanzo. 50:21>>
Haya, msiogope. Mimi nitawapeni chakula pamoja na watoto wenu.” Basi akawafariji na kusema nao vizuri.
1527Mwanzo. 50:22>>
Yosefu akaendelea kukaa katika nchi ya Misri pamoja na jamaa yote ya baba yake. Aliishi kwa muda wa miaka 110.
1528Mwanzo. 50:23>>
Yosefu alijaliwa kuwaona watoto na wajukuu wa mwanawe Efraimu, na pia kuwapokea kama wanawe watoto wa Makiri mwana wa Manase.
1529Mwanzo. 50:24>>
Baadaye Yosefu aliwaambia ndugu zake, “Mimi sasa ninakaribia kufa. Lakini Mungu hakika atawajia kuwasaidia. Atawatoa katika nchi hii na kuwapelekeni katika nchi aliyowaapia Abrahamu, Isaka na Yakobo.”
1530Mwanzo. 50:25>>
Kisha Yosefu akawaapiza wana wa Israeli, akisema, “Mungu atakapowajia kuwasaidia, hakikisheni kwamba mmeichukua mifupa yangu kutoka huku.”
1531Mwanzo. 50:26>>
Basi, Yosefu akafariki kule Misri, akiwa na umri wa miaka 110. Nao wakaupaka mwili wake dawa usioze, wakauweka katika jeneza kule Misri.