MARIA MAMA WA MUNGU
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Na tuadhimishe Kukingiwa Dhambi ya Asili Bikira Maria. Tumwabudu Mwanae, ambaye ni Kristo Bwana.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
TENZI angalia pia AU
AU
40
Ee Nyota ya bahari,
Mlango wetu wa mbingu,
Mama wa Muumba wetu,
Isikie sala yetu.
Salamu ulipokea
Ile alokupa Mungu,
Mwokozi ukamzaa
Ni hakika - siyo ndoto.
Tufungulie vifungo
'Tika upofu wa dhambi,
Macho yetu uyaponye
Tufwate nuru ya Mungu.
Ulomchukua mimba
Ndiye mwenye kutuponya:
Sema wewe mama yetu
Atakusikiliza tu.
Bikira mpole sana,
Hifadhi upendo wetu,
Uthabiti na furaha,
Tuepushe na maovu.
Hatari za maishani
Utwongoze tuzipite,
Tufikishe bandarini,
Tutulie naye Yesu.
Umwimbie Baba Yetu
Na Mwana Mwokozi wetu
Na yeye Roho kwa shangwe
Sifa daima milele.
AU
41
Bikira, na papo hapo ni Mama
Binti yake Mwana wako mwenyewe,
U juu kuliko wengine wote -
Ila hapana wa chini zaidi;
Wewe ndio utimilifu wote
Ulopangwa kwa amri ya Mungu
Ulimwengu wetu uloanguka
Katika wewe lipokuwa bora!
Akisha tayarishiwa mahali,
Yeye aliyeumba vitu vyote
Kakaa kati ya viumbe vyake,
Kifuani pako ndo akalala;
Hapo akalisha upendo wake-
Kwa joto ambalo liliukuza
Mzizi ule ulostawisha
Amani yetu sisi ya milele.
Na si peke yako usikiaye
Sisi tunaposifu lako jina;
Mara nyingi huwa karibu sana
Sauti zetu zinapokatika;
Viumbe vyote kaumbwa vizuri
Kwa umbo na kwa sura yako nzuri,
Huruma, nguvu, upole na wema,
Na neema umejaliwa mama.
Bibi, tushindwapo kuona mbele,
Katika kutarajia ya mbingu,
Endelea bado kutuombea
Sisi kwa huyo Mwanao daima,
Ambaye anastahili sifa,
Nguvu na enzi na wote uweza,
Pamoja na Roho Mtakatifu,
Na pamoja na Baba mtukufu.
Dante Alighieri 1265-1321
AU
42
Maria mwenye taji ya nuru,
Wewe ni hekalu lake Bwana,
La amani na utakatifu,
Ndiwe nyumba akaamo Neno.
Fumbo la maisha bila dhambi
Kati ya watu walopotoka;
Kivuli wewe huna, wang'aa,
Sababu una neema tele.
Bikira Mama wa Mungu wetu,
Utuinue tuangukapo,
Umekuwa mama yetu sote,
Kasema Yesu Msalabani.
Baba, Mwana pamoja na Roho,
Mbingu masifu zawaimbia;
Anawatukuzeni Maria,
Siku zote na hata milele.
Stanbrook Abbey Hymnal
AU
43
Salaamu, Malkia wa mbingu,
Salamu ewe nyota ya bahari,
Kiongozi bora wa wale wote
Wanaotangatanga hapa chini;
Ututunze sisi tuliotupwa
Katika mawimbi yake maisha:
Tukinge na hatari na balaa.
Mama ya Kristo, nyota ya bahari,
Uwaombee waliopotea,
Niombee na mimi, niombee.
Ewe mwali mtulivu na safi,
Ewe Bikira usiye na doa,
Sisi wenye dhambi twatoa dua
Kwa kupitia kwako wewe mama;
Umkumbushe mwana wako kwamba
Kalipa fidia ya dhambi zetu,
Ametulipia madeni yetu.
Bikira safi, nyota ya bahari,
Uwaombee wenye dhambi wote,
Niombee na mimi, niombee.
Wasafiri katika bonde hili,
Bonde la machozi, twakulilia
Ewe mtetezi mbarikiwa;
Na uzitazame huzuni zetu,
Yatulize Mama mashaka yetu,
Katika taabu utufariji,
Utuliwaze kwa matumaini.
U kimbilio, nyota ya bahari,
Uwaombee wote waliao,
Niombee na mimi, niombee.
Yohane Lingard 1771-1851
AU
44
Mungu aloumba mbingu na nchi
Na bahari yenye mabadiliko,
Mtukufu akauvaa mwili:
Akawa ni mtu kati ya watu.
Bikira Maria mwanga kajazwa,
Kateuliwa 'toka wanadamu,
Akamzaa Mwana wake Baba
Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Yeye ambaye kote kote yuko,
Ambaye hawezi kulazimishwa,
Aliweka Umungu wake hapa,
Ili awe nasi wakati wetu.
Sifa kwa Baba, Bwana wa nyakati,
Na sifa kwa wanae wa pekee,
Pamoja na Roho Mtakatifu,
Utatu katika Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal
AU
45
Malkia mwenye taji
Ya ubikira kamili
Katika paji la uso,
Paji lako ling'aalo
Mungu aliyekuumba,
Kutoka yako maziwa,
Alinyonya na kushiba,
Kwa ajili yetu sisi.
Ne'ma aloikataa
Yule mkosefu Eva,
Tena inajitokeza
Mwanao napomzaa;
Mlango bora wa mbingu,
Ulofunguliwa wazi,
Wakaribisha watoto
Wa machozi yake Eva.
Mlango unaofaa
Kwa umati wa kifalme,
Mwenge utoao mwanga
Unaoangaza hivyo,
Watu walokombolewa
Wanaliheshimu sana
Tumbo lako la uzazi
Lililowapa uhai!
Ewe Yesu ulozawa
Na yule mama Bikira
Usifiwe sikuzote,
Sikuzote utukuzwe;
Pia sifa kwake yeye
Baba yetu wa milele,
Na kwa yule Roho wake,
Uzima atutiaye.
Venansio Fortunato 530-609
ANT. I: Chipukizi limechipuka kutoka shina la Yese; nyota imechomoza
kutoka kwa Yakobo. Bikira amemzaa Mwokozi; tunakutukuza, Mungu wetu.
Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.
Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.
Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.
Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.
Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.
Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.
Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.
Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;
maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.
Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Chipukizi limechipuka kutoka shina la Yese; nyota imechomoza
kutoka kwa Yakobo. Bikira amemzaa Mwokozi; tunakutukuza, Mungu wetu.
ANT. II: Maria alimzaa Mwokozi wetu; Yohane alimwona, akapaaza sauti:
huyu ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu, aondoaye dhambi za dunia, aleluya.
WIMBO: Dan:3.37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)
Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.
Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.
Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.
Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.
Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.
Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.
Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.
Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.
Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.
Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.
Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.
Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.
Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.
Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.
Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Ant. II: Maria alimzaa Mwokozi wetu; Yohane alimwona, akapaaza sauti:
huyu ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu, aondoaye dhambi za dunia, aleluya.
ANT. III: Maria alimzaa mfalme ambaye jina lake ni la milele; aliunganisha
furaha ya kuwa mama mzazi, na heshima ya kuwa bikira; hilo halikupata kutokea kabla, na wala halitatokea
tena, aleluya.
Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo,
mfalme wao (Hesychius)
Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!
Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.
Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.
Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.
Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.
Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,
ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;
wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.
kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Maria alimzaa mfalme ambaye jina lake ni la milele; aliunganisha
furaha ya kuwa mama mzazi, na heshima ya kuwa bikira; hilo halikupata kutokea kabla, na wala
halitatokea tena, aleluya.
SOMO: Mika5:3,4,5a
Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya
nduguze watawarudia wana wa Israeli. Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za BWANA,
kwa enzi ya jina la BWANA, Mungu wake. Na mtu huyu atakuwa amani yetu.
KIITIKIZANO
K. Bwana ametujulisha wokovu wetu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Ameonesha uwezo wake wa kuokoa.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana ametujulisha...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Leo fumbo la ajabu linatangazwa: jambo jipya limetokea; Mungu amepata kuwa mtu; amebaki Mungu
kama alivyokuwa kwanza, na amekuwa kile ambacho hakuwa kabla yake: na ingawa hali hizo mbili ni
tofauti, yeye ni nafsi moja.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Leo fumbo la ajabu linatangazwa: jambo jipya limetokea; Mungu
amepata kuwa mtu; amebaki Mungu kama alivyokuwa kwanza, na amekuwa kile ambacho hakuwa kabla yake:
na ingawa hali hizo mbili ni tofauti, yeye ni nafsi moja.
MAOMBI
Tumtukuze Kristo, aliyezaliwa na Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
W. Mwana wa Bikira Maria, utuhurumie.
Mwana wa Bikira Maria, mtoto wa ajabu, na mfalme wa amani,
- amani yako na idhihirike duniani. (W.)
Bwana Yesu, tunaomba imani uliyotujalia iimarike ndani yetu siku kwa siku,
- na ionekane katika fani zote za maisha yetu. (W.)
Ulitwaa hali yetu ya kibinadamu;
- utusaidie tukue katika maisha yako ya kimungu. (W.)
Ulipata kuwa raia wa dunia hii;
- utufanye tuwe raia wa ufalme wako wa mbinguni. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu, Baba yetu, kwa kuwa umewapa wanadamu mwokozi kwa njia ya Maria mwenye heri, bikira na
mama, utujalie tuweze kuhisi nguvu ya maombezi yake wakati anapotuombea kwa Yesu Kristo, Mwanao,
chanzo cha uzima, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.