Generic placeholder image

MARIA MAMA WA MUNGU
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

TENZI angalia pia AU

AU
40
Ee Nyota ya bahari,
Mlango wetu wa mbingu,
Mama wa Muumba wetu,
Isikie sala yetu.

Salamu ulipokea
Ile alokupa Mungu,
Mwokozi ukamzaa
Ni hakika - siyo ndoto.

Tufungulie vifungo
'Tika upofu wa dhambi,
Macho yetu uyaponye
Tufwate nuru ya Mungu.

Ulomchukua mimba
Ndiye mwenye kutuponya:
Sema wewe mama yetu
Atakusikiliza tu.

Bikira mpole sana,
Hifadhi upendo wetu,
Uthabiti na furaha,
Tuepushe na maovu.

Hatari za maishani
Utwongoze tuzipite,
Tufikishe bandarini,
Tutulie naye Yesu.

Umwimbie Baba Yetu
Na Mwana Mwokozi wetu
Na yeye Roho kwa shangwe
Sifa daima milele.

AU
41
Bikira, na papo hapo ni Mama
Binti yake Mwana wako mwenyewe,
U juu kuliko wengine wote -
Ila hapana wa chini zaidi;
Wewe ndio utimilifu wote
Ulopangwa kwa amri ya Mungu
Ulimwengu wetu uloanguka
Katika wewe lipokuwa bora!

Akisha tayarishiwa mahali,
Yeye aliyeumba vitu vyote
Kakaa kati ya viumbe vyake,
Kifuani pako ndo akalala;
Hapo akalisha upendo wake-
Kwa joto ambalo liliukuza
Mzizi ule ulostawisha
Amani yetu sisi ya milele.

Na si peke yako usikiaye
Sisi tunaposifu lako jina;
Mara nyingi huwa karibu sana
Sauti zetu zinapokatika;
Viumbe vyote kaumbwa vizuri
Kwa umbo na kwa sura yako nzuri,
Huruma, nguvu, upole na wema,
Na neema umejaliwa mama.

Bibi, tushindwapo kuona mbele,
Katika kutarajia ya mbingu,
Endelea bado kutuombea
Sisi kwa huyo Mwanao daima,
Ambaye anastahili sifa,
Nguvu na enzi na wote uweza,
Pamoja na Roho Mtakatifu,
Na pamoja na Baba mtukufu.
Dante Alighieri 1265-1321

AU
42
Maria mwenye taji ya nuru,
Wewe ni hekalu lake Bwana,
La amani na utakatifu,
Ndiwe nyumba akaamo Neno.

Fumbo la maisha bila dhambi
Kati ya watu walopotoka;
Kivuli wewe huna, wang'aa,
Sababu una neema tele.

Bikira Mama wa Mungu wetu,
Utuinue tuangukapo,
Umekuwa mama yetu sote,
Kasema Yesu Msalabani.

Baba, Mwana pamoja na Roho,
Mbingu masifu zawaimbia;
Anawatukuzeni Maria,
Siku zote na hata milele.
Stanbrook Abbey Hymnal

AU
43
Salaamu, Malkia wa mbingu,
Salamu ewe nyota ya bahari,
Kiongozi bora wa wale wote
Wanaotangatanga hapa chini;
Ututunze sisi tuliotupwa
Katika mawimbi yake maisha:
Tukinge na hatari na balaa.
Mama ya Kristo, nyota ya bahari,
Uwaombee waliopotea,
Niombee na mimi, niombee.

Ewe mwali mtulivu na safi,
Ewe Bikira usiye na doa,
Sisi wenye dhambi twatoa dua
Kwa kupitia kwako wewe mama;
Umkumbushe mwana wako kwamba
Kalipa fidia ya dhambi zetu,
Ametulipia madeni yetu.
Bikira safi, nyota ya bahari,
Uwaombee wenye dhambi wote,
Niombee na mimi, niombee.

Wasafiri katika bonde hili,
Bonde la machozi, twakulilia
Ewe mtetezi mbarikiwa;
Na uzitazame huzuni zetu,
Yatulize Mama mashaka yetu,
Katika taabu utufariji,
Utuliwaze kwa matumaini.
U kimbilio, nyota ya bahari,
Uwaombee wote waliao,
Niombee na mimi, niombee.
Yohane Lingard 1771-1851

AU
44
Mungu aloumba mbingu na nchi
Na bahari yenye mabadiliko,
Mtukufu akauvaa mwili:
Akawa ni mtu kati ya watu.

Bikira Maria mwanga kajazwa,
Kateuliwa 'toka wanadamu,
Akamzaa Mwana wake Baba
Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Yeye ambaye kote kote yuko,
Ambaye hawezi kulazimishwa,
Aliweka Umungu wake hapa,
Ili awe nasi wakati wetu.

Sifa kwa Baba, Bwana wa nyakati,
Na sifa kwa wanae wa pekee,
Pamoja na Roho Mtakatifu,
Utatu katika Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal

AU
45
Malkia mwenye taji
Ya ubikira kamili
Katika paji la uso,
Paji lako ling'aalo
Mungu aliyekuumba,
Kutoka yako maziwa,
Alinyonya na kushiba,
Kwa ajili yetu sisi.

Ne'ma aloikataa
Yule mkosefu Eva,
Tena inajitokeza
Mwanao napomzaa;
Mlango bora wa mbingu,
Ulofunguliwa wazi,
Wakaribisha watoto
Wa machozi yake Eva.

Mlango unaofaa
Kwa umati wa kifalme,
Mwenge utoao mwanga
Unaoangaza hivyo,
Watu walokombolewa
Wanaliheshimu sana
Tumbo lako la uzazi
Lililowapa uhai!

Ewe Yesu ulozawa
Na yule mama Bikira
Usifiwe sikuzote,
Sikuzote utukuzwe;
Pia sifa kwake yeye
Baba yetu wa milele,
Na kwa yule Roho wake,
Uzima atutiaye.
Venansio Fortunato 530-609

ANT. I: Loo, mabadilishano ya ajabu! Mwumba wa ubinadamu alitwaa mwili wa kibinadamu, akazaliwa na Bikira. Alipata kuwa mtu bila ya baba wa kibinadamu, na ametupatia sisi hali yake ya kimungu.

Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Nilifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu.“

Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!

Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!

Humo ndimo makabila yanafika,/.
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.

Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.

Uombeeni Yerusalemu amani;*
“Wote wakupendao wafanikiwe!

Ukumbini mwako kuwe na amani,*
majumbani mwako kuweko usalama!“

Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
Ee Yerusalemu, nakutakia amani!

Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
ninakuombea upate fanaka!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Loo, mabadilishano ya ajabu! Mwumba wa ubinadamu alitwaa mwili wa kibinadamu, akazaliwa na Bikira. Alipata kuwa mtu bila ya baba wa kibinadamu, na ametupatia sisi hali yake ya kimungu.

ANT. II: Ulizaliwa na Bikira kwa namna ya ajabu, ambayo hakuna mtu anayeweza kuieleza; hivyo maandiko yalitimia: kama vile mvua inyeshavyo kwa utulivu juu ya nchi, ndivyo ulivyoshuka kwetu kuwaokoa watu wote. Tunakusifu; wewe ni Mungu wetu.

Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.

Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.

Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu.*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?

Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!

Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.

Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ulizaliwa na Bikira kwa namna ya ajabu, ambayo hakuna mtu anayeweza kuieleza; hivyo maandiko yalitimia: kama vile mvua inyeshavyo kwa utulivu juu ya nchi, ndivyo ulivyoshuka kwetu kuwaokoa watu wote. Tunakusifu; wewe ni Mungu wetu.

ANT. III: Musa aliona kichaka kilichokuwa kinaungua moto bila kuteketea. Hiyo ni ishara ya ubikira wako, ambao watu wote ni lazima wauheshimu; Mama wa Mungu, utuombee.

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo

ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Musa aliona kichaka kilichokuwa kinaungua moto bila kuteketea. Hiyo ni ishara ya ubikira wako, ambao watu wote ni lazima wauheshimu; Mama wa Mungu, utuombee.

SOMO: Gal.4:4-5
Lakini wakati ule maalum ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya Sheria, apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya Sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu.

KIITIKIZANO
K. Neno akatwaa mwili, aleluya, aleluya.
W. Neno akatwaa mwili, aleluya, aleluya.
K. Na akakaa kwetu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Neno akatwaa mwili, aleluya, aleluya.

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Heri tumbo la uzazi lililokuchukua, Kristo; yamebarikiwa maziwa uliyonyonya, maana wewe ni Bwana na Mwokozi wa dunia, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Heri tumbo la uzazi lililokuchukua, Kristo; yamebarikiwa maziwa uliyonyonya, maana wewe ni Bwana na Mwokozi wa dunia, aleluya.

MAOMBI
Atukuzwe Kristo, Emanueli, aliyezaliwa na Bikira Maria.
W. Mwana wa Bikira Maria, sikiliza sala zetu.

Ulimjalia Bikira Maria furaha ya kuwa mama;
- uwajalie wazazi wote furaha katika watoto wao. (W.)

Mfalme wa amani, utawala wako ni wa haki na amani;
- utuwezeshe kutafuta yale ambayo yatakuza uelewano kati ya watu. (W.)

Ulifika kuwafanya wanadamu wawe taifa takatifu;
- uyaunganishe mataifa yote katika umoja wa Roho Mtakatifu. (W.)

Ulizaliwa katika familia ya kibinadamu;
- uyafanye maisha katika familia yaimarike kwa upendo. (W.)

Ulikuja kwetu, ukaishi maisha ya unyonge;
- uwajalie marehemu uzima na utukufu katika ufalme wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu, Baba yetu, kwa kuwa umewapa wanadamu mwokozi kwa njia ya Maria mwenye heri, bikira na mama, utujalie tuweze kuhisi nguvu ya maombezi yake wakati anapotuombea kwa Yesu Kristo, Mwanao, chanzo cha uzima, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.