SHEREHE YA BIKIRA MARIA MAMA WA MUNGU
1 Januari

ANTIFONA YA KUINGIA: Sedulius
Salamu, Mama mtakatifu wa Mungu, uliyemzaa Mfalme mwenye kutawala mbingu na dunia milele na milele.

Au:

Isa.9:2,6; Lk 1:33

Nuru itatuangazia leo, maana kwa ajili yetu Bwana amezaliwa; naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu, Mungu, Mfalme wa amani, Baba wa milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.

Utukufu husemwa

KOLEKTA:
Ee Mungu, umemwandalia mwanadamu thawabu za wokovu wa milele kwa njia ya kuzaa kwake Bikira Maria mtakatifu. Tunakuomba utujalie tuweze kutambua kwamba anatuombea sisi, yeye ambaye kwa njia yake tulistahili kumpokea Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, aliye Mkuu wa uzima. Anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Hes.6:22-27
Bwana alinena na Musa, na kumwambia, Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Hivi ndivyo mtakavyowabarikia wana wa Israeli; mtawaambia; Bwana akubarikie, na kukulinda; Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani. Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.67:1-2,4,6-7(K)1
1. Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulike duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote.

(K) Mungu na atufadhili na kutubariki.

2. Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)

3. Nchi imetoa mazao yake;
Mungu, Mungu wetu, ametubariki.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)

SOMO 2: Gal.4:4-7
Ndugu zangu: ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.

SHANGILIO: Kol.3:15,16
Aleluya, aleluya!
Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,
mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana aliyemweka kuwa mrithi wa yote,
tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.
Aleluya!

INJILI: Lk 2:16-21
Siku ile: Wachungaji walienda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa. Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu wapendwa, mwanzoni mwa mwaka mpya yafaa kujiweka chini ya ulinzi wa Bikira Maria ambaye ni mama yetu anayeelewa shida na matatizo yetu ya kila siku. Ee Mungu Mwenyezi,

1. Kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Kristo, uwasaidie viongozi wa Kanisa kutetea haki, imani na amani hapa duniani.

2. Kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Kristo: Uwaoneshe viongozi wa serikali njia za kujenga na kuimarisha amani na uelewano kati ya mataifa.

3. Kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Kristo: Uwasaidie wote wanaochochea magomvi, fitina na vita kuacha ubaya wao.

4. Uwafariji na kuwatuliza wale wanaoteseka kwa sababu ya vita, dhuluma na ubaya wa wenzao.

5. Uwapatanishe wale wote waliofarakana na kugombana kwa sababu ya ubinafsi.

6. Utusaidie kujenga na kuimarisha amani ndani yetu, katika familia zetu, katika vijiji na katika taifa letu.

7. Uwaweke marehemu wetu mahali pa amani mbinguni.

Ee Mungu uliye na uwezo, utujalie tunayoomba kwa jina la Kristo aliyemsikiliza mama yake huko Kana akawasaidia watu wa arusini. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu, ndiwe unayeanzisha mambo yote yaliyo mema kwa wema wako na kuyakamilisha. Utujalie, ili, sisi tunaosherehekea sikukuu ya Mama mtakatifu wa Mungu, tuufurahie utimilifu wa neema yako kama vile tunavyofurahia kuonja mwanzo wake. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI BIKIRA MARIA I
Umama wa Bikira Maria mwenye heri.

K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, na kukusifu, kukuhimidi na kukutangaza Wewe, katika adhimisho la sikukuu (katika adhimisho kwa heshima) ya Maria mwenye heri Bikira daima.
Yeye alimchukua mimba Mwanao pekee hapo Roho Mtakatifu alipomfunika kwa kivuli chake, na, pasipo kupoteza utukufu wa ubikira wake, aliuzalia ulimwengu mwanga wa milele, Yesu Kristo Bwana wetu. Kwa njia yake Malaika husifu adhama yako, Enzi hukuabudu, na Mamlaka hukupigia magoti wakitetemeka. Mbingu na Nguvu za mbinguni, na Maserafi wenye heri, wakuadhimisha pamoja kwa shangwe.
Tunakusihi, utujalie tujiunge nao kwa wimbo wa sifa, tukisema kwa sauti ya unyenyekevu:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Heb.13:8
Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tumepokea kwa furaha sakramenti za mbinguni. Tunakuomba utujalie sakramenti hizo zitupatie uzima wa milele, sisi tunaoona fahari kumwungama Maria Bikira daima kuwa Mama wa Mwanao na Mama wa Kanisa. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.