JANUARI 3
JUMATANO JUMA LA 2 LA NOEL
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
TENZI angalia pia AU
AU
6
Ua lake Yuda, ua azizi,
Limechipuka kwenye mizizi,
Mizizi ambayo ni teketeke,
Waridi la kwenye Shina la Yese,
Kama walivyoimba manabii:
Limechipuka kwenye mizizi,
Majira ya baridi hilo ua
Tafanya usiku upambazuke.
Waridi rembo na lenye neema,
Ambalo Isaya analiimba,
Ni wewe Mama Bikira Maria
Na Kristo ni ua unalochipua;
Kwa amri kamambe yake Mungu;
Maria ulimzaa Mwokozi
Ulimzaa Mpenzi wa sisi
Ambaye akafa atukomboe.
Maria wewe u mama mpenzi,
Sisi tunakuomba mama kwa dhati,
Twasihi kwa mioyo yetu yote:
Jalia huyo mwanao mchanga
Madhambi yetu atuondolee,
Kwa upendo wake atuongoze
Tuweze kwishi naye huko juu
Pia tumtumikie milele.
Karne ya 15
AU
7
Kutoka lichomozeako jua
Hadi lizamiako magharibi,
Kwa Kristo Mfalme heshima twatoa,
Alozaliwa leo na Bikira.
Mwumba Mtukufu ulijishusha
Uwe mtwana kwa ajili yetu,
Mwili hadhi ukaurudishia
Sisi viumbe tupate kuishi.
Tumbo la uzazi safi likaa
Lililojaa neema za mbingu;
Wala Bikira hakuweza sema
Mgeni wake katokea wapi.
Kutoka juu Mungu alikuja
Kuuhifadhi utukufu wake
Kifuani mwa asiye na dhambi,
Bikira aliyejaa utii.
Bikira imani alionesha
Kwa neno lililotoka kwa Mungu,
Na hapo ndipo akapata mimba
Bila kuwa na hatia yo yote.
Kishapo Mtoto akamzaa,
Alivyojulishwa na Gabrieli;
Huyo ndo Mtoto alotangazwa
Na mtangulizi kabla yake.
Alilala fofofo majanini
Ndani ya chombo cha kulishia ng'ombe;
Alinyonya maziwa ya mamake,
Yeye ambaye huwalisha wote.
Utukufu kwa Mungu! yasikika,
Hao malaika juu waimba;
Mchungaji, Bwana wa watu wote
Aabudiwa kwanza na wachunga.
Karne ya 5
AU
8
Kristo kwa ajili ya watu
Damu yako ndo ilitiririka,
Wewe u nuru iliyoangaza
Kabla haijawa asubuhi,
Wewe Bwana hakika ndiwe Mungu
Nawe milele ni Mwana wa Mungu,
Tena Wewe pamoja naye Baba
Nyie ni Mungu mmoja milele;
Ewe uliye mng'ao azizi
Utokanao na Nuru ya Baba,
U nyota iletayo tumaini
Ambayo daima yametameta,
Zisikilize basi twakuomba
Sala zenye kukumiminikia,
Kutoka huku chini duniani
Watumishi wako wanazosali.
Ee Bwana ukumbuke ya kuwa
Ni kwa sababu ya upendo wako
Wewe ulikiacha kule juu
Kile kiti chako cha enzi kuu
Chini ukaja upate kutwaa
Hali dhaifu ya kibinadamu,
Na ndipo mimba ukachukuliwa,
Na Mama aliye safi Bikira.
Kwa hiyo usikubali ardhi
Iwe peke yake yashangilia,
Bali hata bahari na uwingu
Pamoja vichange zao sauti,
Kusudi na uimbwe wimbo mpya
Wa kuishangilia asubuhi
Ile ya siku alipozaliwa
Yeye aliye Bwana wa uzima.
Ewe aliyekuzaa bikira
Ni wewe wa kuzipokea sifa,
Haya, hivi sasa tunakusifu,
Na milele uwe unasifiwa;
Baba naye pia apewe sifa
Kama hizo utolewazo Mwana,
Hizo pia na zimwendee Roho,
Ninyi msifiwe milele yote.
AU
9
Njooni, wamini wote,
Kwa furaha na kwa shangwe,
Njooni Betlehemu
Njooni mpate mwona
Mfalme alozaliwa,
Mfalme wa Malaika.
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Ni Mungu sawa na Mungu,
Ni Nuru kutoka Nuru,
Lile tumbo la uzazi
La bikira hachukii;
Yeye ni Mungu halisi
Ana baba, hakuumbwa.
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Imbeni, nyi malaika,
Imbeni kwa shangwe kuu,
Imbeni, wakazi wote
Wa huko mbinguni juu;.
'Utukufu kwako Mungu
Uliye mbinguni juu.'
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Bwana tunakusalimu,
Uliyezaliwa leo
Asubuhi ya furaha,
Utukuzwe Bwana Yesu,
Neno wake Baba Mungu
Sasa u katika mwili.
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Karne ya 18
AU
10
Tumempata sisi
Tumepewa mtoto,
Analeta uhuru
Kristo Mwokozi,
Yeye ni Mshauri
Ni Baba wa milele,
Mungu aliye mtu,
Mfalme wa Amani.
Mamake ni Maria
Bikira na mpole,
Hiyo kazi ya Roho,
Roho yule wa Bwana;
Huyo alitamkwa
Kale tangu milele:
Huyu ndiye ni Neno
Wake Baba Mwenyezi.
Ndaniye tachanua
Upendo na ukweli,
Navyo tatenda kazi
Kwa nguvu zake Neno.
Matawi yaso kitu
Maua yatapata;
Furaha ilolala
Yaanza kuamka.
Na apatiwe sifa
Baba alo milele,
Pia na Neno wake
Mwanae wa pekee,
Pamoja nao pia
Roho Mtakatifu
Ni Utatu kamili
Na ni Mungu mmoja.
AU
11
Alozawa na upendo wa Baba
Kabla ya ulimwengu kuumbwa,
Yeye ndiye Alfa na Omega,
Yeye ni chanzo, yeye ni kikomo
Cha vilivyo na vilivyokuwapo
Na vitavyoonekana badaye:
Kwa milele na milele.
Ilibarikiwa milele siku
Bikira - aliyejaa neema,
Mwenye mimba kwa uwezo wa Roho-
Alipomzaa Mwokozi wetu,
Naye Mkombozi wa ulimwengu
Alipoonesha kwanza usowe:
Kwa milele na milele.
Atukuzwe Mungu Baba Mwenyezi,
Atukuzwe Mungu Mwana Mwokozi,
Atukuzwe Roho Mtakatifu,
Umungu mmoja, Nafsi tatu.
Viumbe vyote na vimtukuze
Mwenyezi Mungu kwa nyakati zote:
Kwa milele na milele.
Aurelio C. Prudensio
348-yapata 413
AU
12
Kristo huyu hapa,
Mwenyewe Emanueli,
Yeye ndiye mtukufu
Na ni mpole ajabu:
Hekima nayo neema,
Hekima nao ukweli
Vipo ila mefichama
Katika huyu Mtoto.
Vile Mungu alitaka
Yesu ndipo kaumbika,
Kristo ndiye Mwanga
Aliyetoka kwa Mwanga,
Amekuja waokoa
Waana wake Adamu
Ambao wanangojea
Katika giza - usiku.
Sifa kwa Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Utukufu wao hao
Wa mbinguni wanaimba,
Na walio duniani
Kwa sauti ilo kuu
Sawia wanausifu
Utatu wauabudu.
Stanbrook Abbey Hymnal
ANT. I: Ee Bwana, niepushe na mauti, miguu yangu isijikwae.
Zab.116:1-9 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Ni lazima sisi sote kupitia katika taabu nyingi ili tuingie katika Ufalme wa Mungu(Mate.14:22)
Nampenda Mungu, kwa maana anisikia,*
maana amesikiliza kilio cha ombi langu.
Yeye hunisikiliza*
kila ninapomlilia.
Hatari ya kifo ilinizunguka,/
vitisho vya kaburi vilinivamia;*
nilijawa mahangaiko na majonzi.
Kisha nikamlilia Mungu:*
"Ee Mungu, tafadhali unisalimishe!”
Mungu amejaa wema na haki;*
Mungu wetu ni mwenye huruma.
Mungu huwalinda wanyofu;*
nilikuwa nimekandamizwa, naye akaniokoa.
Uwe na utulivu mkuu, ee roho yangu,*
kwa maana Mungu amenitendea vyema.
Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;*
akanilinda nisije nikaanguka.
Basi, nitatembea mbele yake Mungu,*
katika nchi ya watu walio hai.
Asifiwe Mungu, Mungu wa Israeli!*
Asifiwe sasa na milele!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Ee Bwana, niepushe na mauti, miguu yangu isijikwae.
ANT. II: Msaada wangu utatoka kwa Bwana, aliyeumba mbingu na dunia.
Zab.121 Mungu kinga yetu
Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena(Ufu.7:16)
Ninatazama huko juu milimani;*
msaada wangu watoka wapi?
Msaada wangu watoka kwa Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.
Hatakuacha uanguke;*
mlinzi wako hasinzii.
Mlinzi wa Israeli*
hasinzii wala halali.
Mungu anakulinda na kukukinga;*
yuko pamoja nawe kukulinda.
Mchana jua halitakuumiza,*
wala mwezi wakati wa usiku.
Mungu anakukinga na majanga yote;*
anayalinda salama maisha yako.
Anakulinda ujapo na uendapo,*
sasa na hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Msaada wangu utatoka kwa Bwana, aliyeumba mbingu na dunia.
ANT. III: Njia zako ni za kweli na za haki, Ee Mfalme wa milele.
WIMBO: Ufu.15:3-4 Utenzi Wa sifa
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!
Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!
Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako? *
Wewe peke yako ni Mtakatifu.
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Njia zako ni za kweli na za haki, Ee Mfalme wa milele.
SOMO: 1Yoh.1:5b,7
Mungu ni mwanga; na hamna giza lo lote ndani yake. Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye
alivyo katika mwanga, basi, tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae,
inatutakasa dhambi zote.
KIITIKIZANO
K. Neno akatwaa mwili, aleluya, aleluya.
W. Neno akatwaa mwili, aleluya, aleluya.
K. Na akakaa kwetu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Neno akatwaa mwili, aleluya, aleluya.
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Tushangilie na kufurahi katika Bwana, kwa kuwa wokovu wa milele umeonekana duniani, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Tushangilie na kufurahi katika Bwana, kwa kuwa wokovu wa milele
umeonekana duniani, aleluya.
MAOMBI
Kwa kuzaliwa kwake Kristo, taifa takatifu la Mungu lilichanua maua. Tumwombe na kumshukuru Mwokozi wetu.
W. Kuzaliwa kwako kuiletee dunia furaha.
Kristo, uzima wetu, ulifika kuwa kichwa cha Kanisa:
- uukuze mwili wako na kuujenga katika upendo. (W.)
Tunakuabudu, ewe Kristo, Mungu na mtu:
- utushirikishe maisha yako na Baba. (W.)
Kwa kuwa kwako mtu, ulipata kuwa mshenga wetu:
- uwaunganishe zaidi nawe watumishi wa Kanisa, na uyafanye maisha yao yote yawe ya kueneza neema. (W.)
Kuzaliwa na kuwa kwako binadamu kunaonesha mpango mpya wa wokovu:
- uwajalie watu wote wamtambue Mungu anayeishi kati yao. (W.)
Nguvu ya mauti ilivunjwa ulipopata kuwa mtu:
- uwafungulie minyororo yote ya dhambi waamini marehemu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tuseme kwa pamoja yale maneno aliyotupatia Bwana
yawe kielelezo cha sala zote: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Mwenyezi, ubinadamu wa Mwanao, aliyezaliwa na Bikira, ulikuwa mwanzo wa ulimwengu mpya
usiotiwa doa na hali yetu ya dhambi. Utufanye upya katika Kristo, na utuondolee mawaa yote ya
dhambi. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na
Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.