Generic placeholder image

JANUARI 3
JUMATANO JUMA LA 2 LA NOEL
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yosefu na Maria, mama wa Yesu, waliyastaajabia yaliyokuwa yanasemwa juu yake.

Adhuhuri
Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Macho yangu yameuona wokovu uliouandaa machoni pa watu wote.

Zab.119:65-72 IX Umuhimu wa sheria ya Mungu
Umenitendea vema mimi mtumishi wako,*
kama ulivyoahidi, Ee Mungu.

Unipe hekima na maarifa,*
maana nina imani na amri zako.

Kabla ya kuniadhibu nilikosa,*
lakini sasa nashika agizo lako.

Wewe ni mwema na mfadhili;*
unifundishe kanuni zako.

Wenye kiburi wanasema uwongo juu yangu,*
lakini nashika amri zako kwa moyo wote.

Watu hao hawana akili,*
lakini mimi nafurahia sheria yako.

Nimefaidika kutokana na taabu yangu,*
maana imenifanya nijifunze amri zako.

Sheria uliyoweka ni muhimu zaidi kwangu*
kuliko mali zote za dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.56:1-6,8-13 Kumtumainia Mungu
Kristo ameoneshwa akiteseka (Mt. Jeromu)

Ee Mungu, unionee huruma,/
maana watu wananivamia.*
Wakati wote adui zangu wanizingira.

Mchana kutwa adui zangu wanishambulia;*
ni wengi mno hao wanaonipiga vita.

Ee Mungu, hofu inaponishika,*
mimi nakutumainia wewe.

Namtumainia Mungu, wala siogopi./
Ninamsifu kwa ajili ya ahadi yake.*
Binadamu watanifanya nini?

Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu;*
mawazo yao yote ni ya kunidhuru.

Wanakutana kupanga na kunivizia;/
wanachunguza yote nifanyayo;*
wananiotea kwa shabaha ya kuniua.

Ee Mungu, uwalipe kwa kadiri ya uovu wao,*
uwaangushe hao waovu kwa hasira yako.

Wewe wakujua kutangatanga kwangu;/.
umeweka kumbukumbu ya machozi yangu.*
Je, yote si yamo kitabuni mwako?

Kila mara ninapokuomba msaada wako,/
adui zangu wanarudishwa nyuma.*
Najua kwa hakika: Mungu yuko upande wangu.

Sheria uliyoweka ni muhimu zaidi kwangu*
kuliko mali zote za dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.57 Kuomba msaada
Zaburi hii yaeleza mateso ya Bwana (Mt. Augustino)

Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,*
kwako ninakimbilia usalama.

Kivulini mwa mabawa yako, napata usalama,*
hata hapo dhoruba kali itakapopita.

Namlilia Mungu Mkuu,*
Mungu anijaliaye kila kitu.

Atanisikiliza kutoka mbinguni na kuniokoa;/
atawashinda hao wenye kunidhulumu.*
Mungu atanionesha mapendo na uaminifu wake.

Adui wanizunguka kama simba wala watu;/
meno yao ni kama mikuki na mishale,*
ndimi zao ni kama panga kali.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu,*
utukufu wako uenee duniani kote.

Adui wamenitegea wavu waninase,*
nami nasononeka kwa huzuni.

wamenichimbia shimo njiani,*
lakini wao wenyewe wametumbukia humo.

Niko imara, Ee Mungu, niko imara;*
nitaimba na kukushangilia!

Amka, ee nafsi yangu!/
Amkeni, enyi zeze na kinubi!*
Nitayaamsha mapambazuko!

Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa;*
nitakuimbia sifa kati ya watu.

Upendo wako mkuu waenea hata mbinguni,*
uaminifu wako wafika hata mawinguni.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu;/
utukufu wako uenee duniani kote.*
Kinanda na kinubi, amkeni, nitaiamsha alfajiri.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yosefu na Maria, mama wa Yesu, waliyastaajabia yaliyokuwa yanasemwa juu yake.

Adhuhuri
Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Macho yangu yameuona wokovu uliouandaa machoni pa watu wote.

MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Isa.2:3-4
Katika Sion itatoka sheria, na neno la BWANA katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi, nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.

K. Bwana ameikumbuka rehema yake, aleluya.
W. Amekuwa mwaminifu kwa nyumba ya Israeli, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Isa.9:2
Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.

K. Miisho yote ya dunia inastaajabu, aleluya.
W. Imeuona uwezo wa kuokoa wa Mungu wetu, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Isa.60:4-5
Wana wako watakuja kutoka mbali, Na binti zako watabebwa nyongani. Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia.

K. Rehema na uaminifu vimekutana, aleluya.
W. Haki na amani vimekumbatiana, aleluya.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, ubinadamu wa Mwanao, aliyezaliwa na Bikira, ulikuwa mwanzo wa ulimwengu mpya usiotiwa doa na hali yetu ya dhambi. Utufanye upya katika Kristo, na utuondolee mawaa yote ya dhambi. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.