Generic placeholder image

JANUARI 4
ALHAMISI JUMA LA 2 LA NOEL
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo amezaliwa kwa ajili yetu: njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.) Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;

Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

TENZI angalia pia AU

AU
6
Ua lake Yuda, ua azizi,
Limechipuka kwenye mizizi,
Mizizi ambayo ni teketeke, Waridi la kwenye Shina la Yese,
Kama walivyoimba manabii:
Limechipuka kwenye mizizi,
Majira ya baridi hilo ua
Tafanya usiku upambazuke.

Waridi rembo na lenye neema,
Ambalo Isaya analiimba,
Ni wewe Mama Bikira Maria
Na Kristo ni ua unalochipua;
Kwa amri kamambe yake Mungu;
Maria ulimzaa Mwokozi
Ulimzaa Mpenzi wa sisi
Ambaye akafa atukomboe.

Maria wewe u mama mpenzi,
Sisi tunakuomba mama kwa dhati,
Twasihi kwa mioyo yetu yote:
Jalia huyo mwanao mchanga
Madhambi yetu atuondolee,
Kwa upendo wake atuongoze
Tuweze kwishi naye huko juu
Pia tumtumikie milele.
Karne ya 15

AU
7
Kutoka lichomozeako jua
Hadi lizamiako magharibi,
Kwa Kristo Mfalme heshima twatoa,
Alozaliwa leo na Bikira.

Mwumba Mtukufu ulijishusha
Uwe mtwana kwa ajili yetu,
Mwili hadhi ukaurudishia
Sisi viumbe tupate kuishi.

Tumbo la uzazi safi likaa
Lililojaa neema za mbingu;
Wala Bikira hakuweza sema
Mgeni wake katokea wapi.

Kutoka juu Mungu alikuja
Kuuhifadhi utukufu wake
Kifuani mwa asiye na dhambi,
Bikira aliyejaa utii.

Bikira imani alionesha
Kwa neno lililotoka kwa Mungu,
Na hapo ndipo akapata mimba
Bila kuwa na hatia yo yote.

Kishapo Mtoto akamzaa,
Alivyojulishwa na Gabrieli;
Huyo ndo Mtoto alotangazwa
Na mtangulizi kabla yake.

Alilala fofofo majanini
Ndani ya chombo cha kulishia ng'ombe;
Alinyonya maziwa ya mamake,
Yeye ambaye huwalisha wote.

Utukufu kwa Mungu! yasikika,
Hao malaika juu waimba;
Mchungaji, Bwana wa watu wote
Aabudiwa kwanza na wachunga.
Karne ya 5

AU
8
Kristo kwa ajili ya watu
Damu yako ndo ilitiririka,
Wewe u nuru iliyoangaza
Kabla haijawa asubuhi,
Wewe Bwana hakika ndiwe Mungu
Nawe milele ni Mwana wa Mungu,
Tena Wewe pamoja naye Baba
Nyie ni Mungu mmoja milele;

Ewe uliye mng'ao azizi
Utokanao na Nuru ya Baba,
U nyota iletayo tumaini
Ambayo daima yametameta,
Zisikilize basi twakuomba
Sala zenye kukumiminikia,
Kutoka huku chini duniani
Watumishi wako wanazosali.

Ee Bwana ukumbuke ya kuwa
Ni kwa sababu ya upendo wako
Wewe ulikiacha kule juu
Kile kiti chako cha enzi kuu
Chini ukaja upate kutwaa
Hali dhaifu ya kibinadamu,
Na ndipo mimba ukachukuliwa,
Na Mama aliye safi Bikira.

Kwa hiyo usikubali ardhi
Iwe peke yake yashangilia,
Bali hata bahari na uwingu
Pamoja vichange zao sauti,
Kusudi na uimbwe wimbo mpya
Wa kuishangilia asubuhi
Ile ya siku alipozaliwa
Yeye aliye Bwana wa uzima.

Ewe aliyekuzaa bikira
Ni wewe wa kuzipokea sifa,
Haya, hivi sasa tunakusifu,
Na milele uwe unasifiwa;
Baba naye pia apewe sifa
Kama hizo utolewazo Mwana,
Hizo pia na zimwendee Roho,
Ninyi msifiwe milele yote.

AU
9
Njooni, wamini wote,
Kwa furaha na kwa shangwe,
Njooni Betlehemu
Njooni mpate mwona
Mfalme alozaliwa,
Mfalme wa Malaika.

W. Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.

Ni Mungu sawa na Mungu,
Ni Nuru kutoka Nuru,
Lile tumbo la uzazi
La bikira hachukii;
Yeye ni Mungu halisi
Ana baba, hakuumbwa.

W. Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.

Imbeni, nyi malaika,
Imbeni kwa shangwe kuu,
Imbeni, wakazi wote
Wa huko mbinguni juu;.
'Utukufu kwako Mungu
Uliye mbinguni juu.'

W. Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.

Bwana tunakusalimu,
Uliyezaliwa leo
Asubuhi ya furaha,
Utukuzwe Bwana Yesu,
Neno wake Baba Mungu
Sasa u katika mwili.

W. Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Karne ya 18

AU
10
Tumempata sisi
Tumepewa mtoto,
Analeta uhuru
Kristo Mwokozi,
Yeye ni Mshauri
Ni Baba wa milele,
Mungu aliye mtu,
Mfalme wa Amani.

Mamake ni Maria
Bikira na mpole,
Hiyo kazi ya Roho,
Roho yule wa Bwana;
Huyo alitamkwa
Kale tangu milele:
Huyu ndiye ni Neno
Wake Baba Mwenyezi.

Ndaniye tachanua
Upendo na ukweli,
Navyo tatenda kazi
Kwa nguvu zake Neno.
Matawi yaso kitu
Maua yatapata;
Furaha ilolala
Yaanza kuamka.

Na apatiwe sifa
Baba alo milele,
Pia na Neno wake
Mwanae wa pekee,
Pamoja nao pia
Roho Mtakatifu
Ni Utatu kamili
Na ni Mungu mmoja.

AU
11
Alozawa na upendo wa Baba
Kabla ya ulimwengu kuumbwa,
Yeye ndiye Alfa na Omega,
Yeye ni chanzo, yeye ni kikomo
Cha vilivyo na vilivyokuwapo
Na vitavyoonekana badaye:
Kwa milele na milele.

Ilibarikiwa milele siku
Bikira - aliyejaa neema,
Mwenye mimba kwa uwezo wa Roho-
Alipomzaa Mwokozi wetu,
Naye Mkombozi wa ulimwengu
Alipoonesha kwanza usowe:
Kwa milele na milele.

Atukuzwe Mungu Baba Mwenyezi,
Atukuzwe Mungu Mwana Mwokozi,
Atukuzwe Roho Mtakatifu,
Umungu mmoja, Nafsi tatu.
Viumbe vyote na vimtukuze
Mwenyezi Mungu kwa nyakati zote:
Kwa milele na milele.
Aurelio C. Prudensio
348-yapata 413

AU
12
Kristo huyu hapa,
Mwenyewe Emanueli,
Yeye ndiye mtukufu
Na ni mpole ajabu:
Hekima nayo neema,
Hekima nao ukweli
Vipo ila mefichama
Katika huyu Mtoto.

Vile Mungu alitaka
Yesu ndipo kaumbika,
Kristo ndiye Mwanga
Aliyetoka kwa Mwanga,
Amekuja waokoa
Waana wake Adamu
Ambao wanangojea
Katika giza - usiku.

Sifa kwa Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Utukufu wao hao
Wa mbinguni wanaimba,
Na walio duniani
Kwa sauti ilo kuu
Sawia wanausifu
Utatu wauabudu.
Stanbrook Abbey Hymnal

ANT. I: Ee Bwana, tunatangaza rehema zako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku.

Zab.92 Wimbo wa kumsifu Mungu
Matendo ya Mwana wa pekee wa Mungu yanasifiwa (Mt. Athanasius)

Ni vema kukushukuru, Ee Mungu,*
kuimba kwa heshima yako, Ee Mungu Mkuu.

Ni vema kutangaza upendo wako mkuu asubuhi,*
na uaminifu wako kila usiku,

kwa muziki wa zeze na kinanda,*
kwa sauti tamu ya kinubi.

Ee Mungu, matendo yako makuu yanifurahisha;*
nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda.

Matendo yako, Ee Mungu, ni makuu mno!*
Mawazo yako ni mazito mno!

Mtu mpumbavu hawezi kufahamu,*
wala mjinga hajui jambo hili:

kwamba waovu waweza kusitawi kama nyasi;*
watenda maovu waweza kupata fanaka,

lakini mwisho wao wote ni kuangamia milele;*
maana wewe, Ee Mungu, ni mkuu milele.

Maana tazama, Ee Mungu,/
adui zako hakika wataangamia;*
Wote watendao maovu, watatawanyika!

Wewe umenipa nguvu kama nyati;*
umenimiminia mafuta ya furaha.

Kwa macho nimeona adui zangu wameshindwa;*
nimesikia kilio chao watendao maovu.

Waadilifu husitawi kama mtende;*
hukua kama mwerezi wa Lebanon!

Kama mti uliopandwa katika nyumba ya Mungu,*
wanasitawi katika nyua za Mungu wetu.

Ingawa wamezeeka, wataendelea kuwa na nguvu;*
wapate kuutangaza uadilifu wa Mungu,

na kwamba hamna uovu wowote,*
kwake yeye aliye ngome yangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, tunatangaza rehema zako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku.

ANT. II: Utangazeni ukuu wa Mungu wetu.

WIMBO: Kum.32:1-12 Fadhili alizowatendea Mungu watu wake
Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya kwangu watoto wako, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake (Mt.23:37)

Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitanena;*
Na nchi isikie maneno ya kinywa changu.

Mafundisho yangu yatadondoka kama mvua,*
Maneno yangu yatatonatona kama umande;

Kama manyunyu juu ya majani mabichi;*
Kama matone ya mvua juu ya mimea.

Maana nitalitangaza Jina la BWANA;*
Mpeni ukuu Mungu wetu.

Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu;*
Maana, njia zake zote ni haki.

Mungu wa uaminifu, asiye na uovu,*
Yeye ndiye mwenye haki na adili.

Wametenda mambo ya uharibifu,/
Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao;*
Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka.

Je! mnamlipa BWANA hivi,*
Enyi watu wapumbavu na wajinga?

Je! yeye siye baba yako aliyekununua?*
Amekufanya, na kukuweka imara.

Kumbuka siku za kale,*
Tafakari miaka ya vizazi vingi;

Mwulize baba yako, naye atakuonesha;*
Wazee wako, nao watakuambia.

Yeye Aliye Juu alipowapa mataifa urithi wao,*
Alipowabagua wanadamu,

Aliweka mipaka ya watu*
Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli.

Maana, sehemu ya BWANA ni watu wake,*
Yakobo ni kura ya urithi wake.

Alimkuta katika nchi ya ukame,*
Na katika jangwa tupu litishalo;

Alimzunguka, akamtunza;*
Akamhifadhi kama mboni ya jicho;

Mfano wa tai ataharikishaye kiota chake;*
Na kupapatika juu ya makinda yake,

Alikunjua mbawa zake, akawatwaa,*
Akawachukua juu ya mbawa zake;

BWANA peke yake alimwongoza,*
Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Utangazeni ukuu wa Mungu wetu.

ANT. III: Bwana, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote!

Zab.8 Utukufu wa Mungu na cheo cha binadamu
Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa Kanisa, akiwa ndio mkuu wa vitu vyote (Ef.1:22)

Ee Mwenyezi, Bwana wetu,/
jina lako latukuka kote duniani!*
Utukufu wako wafika hata mbinguni;

wasifika na vinywa vya watoto wadogo na wachanga/
Wewe uko imara mbele ya wapinzani wako;*
wawakomesha maadui na waasi.

Nikiangalia anga,/
kazi ya vidole vyako mwenyewe,*
mwezi na nyota ulivyoviumba:

mtu ni nini, Ee Mungu, hata umfikirie?*
Mwanadamu ni nini hata umjali?

Hata hivyo, ulimfanya mdogo kidogo tu,/
kuliko wewe mwenyewe,*
na umemvika taji ya utukufu na heshima.

Ulimpa mamlaka juu ya kazi zako zote;*
uliviweka viumbe vyote chini ya miguu yake:

kondoo, ng'ombe na wanyama wa porini;*
ndege, samaki na viumbe vyote vya baharini.

Ee Mwenyezi, Bwana wetu:*
Jina lako latukuka duniani kote!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote!

SOMO: Isa.45:22-24
Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine. Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa.

KIITIKIZANO
K. Bwana ametujulisha wokovu wetu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Ameonesha uwezo wake wa kuokoa.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Kristo, Mungu wetu, ambaye ndani yake uko utimilifu wa umungu, aliuchukua udhaifu wetu wa kibinadamu, akazaliwa kama mtu mpya, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Kristo, Mungu wetu, ambaye ndani yake uko utimilifu wa umungu, aliuchukua udhaifu wetu wa kibinadamu, akazaliwa kama mtu mpya, aleluya.

MAOMBI
Neno wa Mungu alijionesha kwetu kwa njia ya mwili, akaonwa na malaika, na kuhubiriwa kati ya mataifa. Na tumtukuze:
W. Mwana wa pekee wa Mungu, tunakuabudu.

Mkombozi wa watu wote, kwa njia ya Bikira Maria ulifika kwetu kushiriki maisha yetu:
- kwa maombezi ya Mama huyo, utuwezeshe kuambatana nawe daima. (W.)

Umetudhihirishia kwamba Mungu ni mwaminifu:
- daima uwe mwanga wa maisha yetu. (W.)

Unatuwezesha kuuona upendo wa Baba kwetu:
- utuwezeshe kuwaonesha wengine mapendo ya Mungu. (W.)

Ulikuja kuishi kati yetu:
- utustahilishe kuwa rafiki zako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu mwenyezi, nuru ya nyota mpya uwinguni ilitangaza upendo wako wa kuokoa. Nuru ya wokovu wako iangaze mioyo yetu, na iiweke daima tayari kupokea neema yako iletayo uzima. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.