Generic placeholder image

JANUARI 4
ALHAMISI JUMA LA 2 LA NOEL
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yosefu na Maria, mama wa Yesu, waliyastaajabia yaliyokuwa yanasemwa juu yake.

Adhuhuri
Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Macho yangu yameuona wokovu uliouandaa machoni pa watu wote.

Zab.119:81-88 XI Sala wakati wa kudhulumiwa
Niko hoi kwa kukungojea uniokoe;*
naweka tumaini langu katika neno lako.

Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi.*
Nauliza:“Utakuja lini kunifariji?”

Nimekunjamana kama kiriba katika moshi,*
hata hivyo sijasahau amri zako.

Nitasubiri mpaka lini?*
Utawaadhibu lini wenye kunidhulumu?

Wenye kiburi, wasiojali sheria yako,*
wamenichimbia mashimo kunitega.

Amri zako zote ni za kuaminika;/
watu waongo wananidhulumu,*
tafadhali unisaidie!

Karibu wangefaulu kuniangamiza,*
lakini mimi sijavunja amri zako.

Unisalimishe kadiri ya upendo wako mkuu,*
nipate kuzingatia maagizo yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.61 Kuomba ulinzi
Sala ya mwadilifu atamaniye mambo ya mbinguni (Mt. Hilari)

Usikie kilio changu, Ee Mungu;*
usikilize sala yangu.

Ninakulilia ugenini humu;*
nikiwa nimevunjika moyo.

Unipeleke kwenye mwamba wa usalama,/
maana wewe ndiwe kimbilio langu,*
kinga yangu imara dhidi ya adui.

Uniruhusu nikae hemani mwako milele*
nipate usalama chini ya mabawa yako.

Ee Mungu, umezipokea nadhiri zangu,*
umenijalia mema uliyowaahidia wakuchao.

Umjalie mfalme maisha marefu,*
miaka yake iwe ya vizazi vingi.

Atawale milele mbele yako, Ee Mungu;*
mapendo na uaminifu wako vimlinde.

Hapo nitakuimbia nyimbo za sifa,*
nikizitekeleza kila siku nadhiri zangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.64 Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
Zaburi hii hasa yatualika kuyafikiria mateso ya Bwana (Mt. Augustino)

Usikie, Ee Mungu, usikilize lalamiko langu;*
unilinde maisha yangu na vitisho vya adui.

Unikinge na njama za waovu,*
na ghasia za watu wabaya.

Wananoa ndimi zao kama upanga,*
wanafyatua maneno ya ukatili kama mishale.

Toka mafichoni wanamshambulia mtu mnyofu,*
wanamshambulia ghafula bila kuogopa.

Wanashirikiana katika nia yao mbaya;/
wanapatana mahali pa kuficha mitego yao.*
Wakifikiri: “Hakuna atakayeweza kuiona!”

Hufanya njama zao na kusema:/
"Sasa tumekamilisha mpango.*
Nani atagundua hila zetu?”

Mipango ya siri imefichika moyoni mwa mtu!/
Lakini Mungu atawapiga mishale,*
na kuwajeruhi ghafula.

Atawaangamiza kwa sababu ya maneno yao;*
kila atakayewaona atatikisa kichwa.

Hapo watu wote wataogopa;/
watatangaza aliyotenda Mungu,*
na kufikiri juu ya matendo yake.

Waadilifu watafurahia aliyotenda Mungu,/
watakimbilia usalama kwake.*
Watu wote wema wataona fahari.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yosefu na Maria, mama wa Yesu, waliyastaajabia yaliyokuwa yanasemwa juu yake.

Adhuhuri
Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Macho yangu yameuona wokovu uliouandaa machoni pa watu wote.

MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Yer.31:7-8
Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee BWANA, uwaokoe watu wako mabaki ya Israeli. Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya katika miisho ya dunia.

K. Bwana ameikumbuka rehema yake, aleluya.
W. Amekuwa mwaminifu kwa nyumba ya Israeli, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Yer.31:11-12
BWANA amemweka huru Yakobo, amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye. Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sion, wataukimbilia wema wa BWANA.

K. Miisho yote ya dunia inastaajabu, aleluya.
W. Imeuona uwezo wa kuokoa wa Mungu wetu, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Zek.8:7-8
Tazama, nitawaokoa watu wangu toka nchi ya mashariki, na toka nchi ya magharibi; nami nitawaleta, nao watakaa katikati ya Yerusalemu; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, katika kweli na katika haki.

K. Rehema na uaminifu vimekutana, aleluya.
W. Haki na amani vimekumbatiana, aleluya.

SALA:
Tuombe: Mungu mwenyezi, nuru ya nyota mpya uwinguni ilitangaza upendo wako wa kuokoa. Nuru ya wokovu wako iangaze mioyo yetu, na iiweke daima tayari kupokea neema yako iletayo uzima. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.