Generic placeholder image

JANUARI 7 au JUMATATU BAADA YA EPIFANIA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo ametutokea: njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.) Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu

Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

TENZI angalia pia AU

AU
13
Betlehemu mji ulo bora,
Mji ulo sawa nawe hakuna:
Ndiwe peke uliyetuzalia
Bwana wa kutoka mbinguni juu.

Nyota ilotangaza kuzaliwa
Ilikuwa nzuri kuliko jua;
Ilitangazia nchi Mungu wao
Aloonekana katika mwili.

Wakiongozwa kwa mng'aro huo
Wafalme wa mashariki watokea;
Wasujudu na zawadi kutoa:
Ubani, dhahabu na manemane.

Zawadi takatifu zenye fumbo;
Ubani Mungu wamdhihirisha,
Dhahabu Mfalme yamtangaza,
Manemane yabashiri kaburi.

Sifa milele ziwe kwako Yesu,
Ulojionesha kwa Mataifa
Katika utukufu wako Bwana,
Pia ziwe kwa Roho na kwa Baba.
Aurelio C. Prudensio 348-yapata 413

AU
14
Nyimbo za sifa na shukrani
Bwana Yesu tunakutolea;
Kwa njia ya nyota uwinguni
Mamajusi walikutambua;
Tawi la mfalme Daudi
Betlehemu ulizaliwa;

Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

Ulidhihirishwa Yordani;
U kuhani, nabii, mfalme;
Na katika arusi ya Kana
Umungu wako ulionesha,
Ukageuza kwa yako nguvu
Maji yakawa divai tamu;

Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

Tujalie ne'ma tukuone
E Bwana, katika neno lako;
Tuwezeshe kukuiga wewe,
Na tuwe safi kama mwenyewe,
Ili utapotokea tena
Tuwe watukufu kama wewe,

Na tukusifu Mbarikiwa,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!
C. Wordsworth 1807-1885

Tenzi nam. 10, 11, 12 zafaa pia
10
Tumempata sisi
Tumepewa mtoto,
Analeta uhuru
Kristo Mwokozi,
Yeye ni Mshauri
Ni Baba wa milele,
Mungu aliye mtu,
Mfalme wa Amani.

Mamake ni Maria
Bikira na mpole,
Hiyo kazi ya Roho,
Roho yule wa Bwana;
Huyo alitamkwa
Kale tangu milele:
Huyu ndiye ni Neno
Wake Baba Mwenyezi.

Ndaniye tachanua
Upendo na ukweli,
Navyo tatenda kazi
Kwa nguvu zake Neno.
Matawi yaso kitu
Maua yatapata;
Furaha ilolala
Yaanza kuamka.

Na apatiwe sifa
Baba alo milele,
Pia na Neno wake
Mwanae wa pekee,
Pamoja nao pia
Roho Mtakatifu
Ni Utatu kamili
Na ni Mungu mmoja.

AU
11
Alozawa na upendo wa Baba
Kabla ya ulimwengu kuumbwa,
Yeye ndiye Alfa na Omega,
Yeye ni chanzo, yeye ni kikomo
Cha vilivyo na vilivyokuwapo
Na vitavyoonekana badaye:
Kwa milele na milele.

Ilibarikiwa milele siku
Bikira - aliyejaa neema,
Mwenye mimba kwa uwezo wa Roho-
Alipomzaa Mwokozi wetu,
Naye Mkombozi wa ulimwengu
Alipoonesha kwanza usowe:
Kwa milele na milele.

Atukuzwe Mungu Baba Mwenyezi,
Atukuzwe Mungu Mwana Mwokozi,
Atukuzwe Roho Mtakatifu,
Umungu mmoja, Nafsi tatu.
Viumbe vyote na vimtukuze
Mwenyezi Mungu kwa nyakati zote:
Kwa milele na milele.
Aurelio C. Prudensio
348-yapata 413

AU
12
Kristo huyu hapa,
Mwenyewe Emanueli,
Yeye ndiye mtukufu
Na ni mpole ajabu:
Hekima nayo neema,
Hekima nao ukweli
Vipo ila mefichama
Katika huyu Mtoto.

Vile Mungu alitaka
Yesu ndipo kaumbika,
Kristo ndiye Mwanga
Aliyetoka kwa Mwanga,
Amekuja waokoa
Waana wake Adamu
Ambao wanangojea
Katika giza - usiku.

Sifa kwa Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Utukufu wao hao
Wa mbinguni wanaimba,
Na walio duniani
Kwa sauti ilo kuu
Sawia wanausifu
Utatu wauabudu.
Stanbrook Abbey Hymnal

ANT. I: Lini nitaingia, ili niuone uso wa Mungu?

Zab.42 Sala ya mkimbizi
Kisha, ye yote aliye na kiu na aje; anayetaka maji ya uzima na apokee bila malipo yo yote (Ufu.22:17)

Kama paa atamanivyo maji ya chemchemi,*
ndivyo nami ninavyokutamani, Ee Mungu wangu!

Nina kiu ya Mungu,/
naam, ya Mungu aliye hai.*
Nitafika kwake lini nakumwona?

Machozi yamekuwa chakula changu mchana na usiku;*
kila siku wananiambia: "Yuko wapi basi, Mungu wako?"

Ninasongwa na huzuni nikikumbuka ya awali:*
jinsi nilivyoandamana na umati,

nikiongozana nao kwenda nyumbani kwa Mungu,/
tukipiga vigelegele na kuimba nyimbo za shukrani,*
kati ya umati wa watu wanaofanya sherehe.

Mbona ninahuzunika hivyo moyoni?*
Kwa nini nahangaika hivyo?

Nitamtumainia Mungu,*
nitamsifu tena Mungu, mwokozi wangu.

Nimesongwa na huzuni moyoni,*
kwa hiyo ninakukumbuka wewe, Ee Mungu,

kutoka katika nchi ya Yordan na Hermon,*
na kutoka mlima Mizar.

Ameniletea vilindi na maporomoko ya uchungu,*
mawimbi na mafuriko yake yameniangukia.

Mungu hunijalia upendo wake mkuu mchana;/
nami namwimbia wimbo wa sifa usiku,*
ombi kwake yeye anipaye uhai.

Namwambia Mungu, mwamba wangu:*
kwa nini umenisahau?

Mbona naendelea kuhuzunika,*
kwa sababu ya kukandamizwa na adui zangu?

Nimepondwa kwa matukano yao,/
wanaponiulizia kila siku;*
"Yuko wapi basi, Mungu wako?"

Mbona ninahuzunika hivyo moyoni?*
Kwa nini nahangaika hivyo?

Nitamtumainia Mungu,*
nitamsifu tena Mungu, mwokozi wangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Lini nitaingia, ili niuone uso wa Mungu?

ANT. II: Utuonyeshe, Ee Bwana, mwanga wa huruma yako.

WIMBO: YBS.36:1-5,10-13
Sala ya kuuombea mji mtakatifu Yerusalemu. Na, uzima wa milele ndio huu: kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma (Yoh.17:3)

Ee Bwana, Mungu wa watu wote, utuokoe;*
uangalie, uwatishe mataifa yote;

uuinue mkono wako juu ya watu wageni;*
na kuwaonesha nguvu zako zilizo kuu.

Kama vile ulivyojitakasa kati yetu mbele yao,*
Vivyo hivyo ujitukuze kati yao mbele yetu;

nao wakujue Wewe kama sisi tukujuavyo,*
ya kwamba hakuna Mungu ila Wewe peke yako.

Tuoneshe ishara tena,*
na kufanya mambo ya ajabu;

uutukuze mkono wako,*
naam, mkono wako wa kuume.

Uwakusanye kabila zote za Yakobo,/
na kuwafanya urithi wako*
kama siku za kale.

Ee BWANA, uwarehemu/
watu walioitwa kwa jina lako,*
na Israeli uliyemwita mzaliwa wa kwanza wako.

Uuonee huruma/
mji wa patakatifu pako, Yerusalemu,*
mahali pako pa raha;

uujaze Sion adhama yako,*
na patakatifu pako utukufu wako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Utuonyeshe, Ee Bwana, mwanga wa huruma yako.

ANT. III: Utukuzwe, Bwana, katika anga la mbingu.

Zab.19A Utukufu wa Mungu katika viumbe
Mwanga utokao juu umetufikia kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani (Lk.1:79)

Mbingu zadhihirisha utukufu wa Mungu;*
anga laitangaza kazi ya mikono yake.

Mchana waupasha habari mchana ufuatao,*
usiku waufahamisha usiku ufuatao.

Hamna msemo au maneno yanayotumika;*
wala hakuna sauti inayosikika;

hata hivyo, sauti yao yaenea nchini kote;*
ujumbe wao wasikika popote duniani.

Mungu ameliwekea jua makao yake angani;/
nalo latoka nje kama bwana arusi,*
kama shujaa aliye tayari kushindana.

Lachomoza toka upande mmoja,/
na kuzunguka hadi upande mwingine;*
wala hakuna kiwezacho kuliepa joto lake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Utukuzwe, Bwana, katika anga la mbingu.

SOMO: Isa.9:6
Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.

KIITIKIZANO
K. Wafalme wote wa dunia watamwabudu. (W. Warudie)
K. Mataifa yote yatamtumikia.
W. Wafalme watamwabudu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wafalme wote...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Mamajusi walitoka Mashariki, wakaenda Betlehemu kumwabudu Bwana; walifungua hazina zao, wakamtolea zawadi za thamani: dhahabu kwa ajili ya mfalme mkuu, ubani kwa ajili ya Mungu wa kweli, manemane kwa ajili ya mazishi yake, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mamajusi walitoka Mashariki, wakaenda Betlehemu kumwabudu Bwana; walifungua hazina zao, wakamtolea zawadi za thamani: dhahabu kwa ajili ya mfalme mkuu, ubani kwa ajili ya Mungu wa kweli, manemane kwa ajili ya mazishi yake, aleluya.

MAOMBI
Tunakutukuza, ewe Kristo. Kwa njia yako wokovu wa Mungu waenea duniani pote.
W. Utukufu kwako, Kristo Bwana.

Kristo, Mkombozi wetu, umewavutia watu wote kwako;
- bomoa kuta za chuki zinazowatenganisha wanadamu. (W.)

Ulikuja kuishi kati yetu:
- utusaidie tuweze kuzitambua jinsi zote zinazoonesha kwamba upo katika Kanisa, na katika maisha ya watu. (W.)

Katika wewe Mungu amedhihirika:
- tunaomba imani na matendo yetu vilingane na mafundisho yako. (W.)

Emanueli, Mungu pamoja na watu, uyafanye upya kabisa maisha yetu;
- utufanye tuwe watu wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tunapoungojea ujio wa utawala wa Mungu, tusali tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, mng'aro wa utukufu wako uangaze mioyo yetu, na utuongoze tunapopita katika vivuli vya dunia hii, mpaka tutakapofikia makao yetu ya mwanga wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.