JANUARI 7 au JUMATATU BAADA YA EPIFANIA
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
TENZI angalia pia AU
AU
13
Betlehemu mji ulo bora,
Mji ulo sawa nawe hakuna:
Ndiwe peke uliyetuzalia
Bwana wa kutoka mbinguni juu.
Nyota ilotangaza kuzaliwa
Ilikuwa nzuri kuliko jua;
Ilitangazia nchi Mungu wao
Aloonekana katika mwili.
Wakiongozwa kwa mng'aro huo
Wafalme wa mashariki watokea;
Wasujudu na zawadi kutoa:
Ubani, dhahabu na manemane.
Zawadi takatifu zenye fumbo;
Ubani Mungu wamdhihirisha,
Dhahabu Mfalme yamtangaza,
Manemane yabashiri kaburi.
Sifa milele ziwe kwako Yesu,
Ulojionesha kwa Mataifa
Katika utukufu wako Bwana,
Pia ziwe kwa Roho na kwa Baba.
Aurelio C. Prudensio 348-yapata 413
AU
14
Nyimbo za sifa na shukrani
Bwana Yesu tunakutolea;
Kwa njia ya nyota uwinguni
Mamajusi walikutambua;
Tawi la mfalme Daudi
Betlehemu ulizaliwa;
Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!
Ulidhihirishwa Yordani;
U kuhani, nabii, mfalme;
Na katika arusi ya Kana
Umungu wako ulionesha,
Ukageuza kwa yako nguvu
Maji yakawa divai tamu;
Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!
Tujalie ne'ma tukuone
E Bwana, katika neno lako;
Tuwezeshe kukuiga wewe,
Na tuwe safi kama mwenyewe,
Ili utapotokea tena
Tuwe watukufu kama wewe,
Na tukusifu Mbarikiwa,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!
C. Wordsworth 1807-1885
Tenzi nam. 10, 11, 12 zafaa pia
10
Tumempata sisi
Tumepewa mtoto,
Analeta uhuru
Kristo Mwokozi,
Yeye ni Mshauri
Ni Baba wa milele,
Mungu aliye mtu,
Mfalme wa Amani.
Mamake ni Maria
Bikira na mpole,
Hiyo kazi ya Roho,
Roho yule wa Bwana;
Huyo alitamkwa
Kale tangu milele:
Huyu ndiye ni Neno
Wake Baba Mwenyezi.
Ndaniye tachanua
Upendo na ukweli,
Navyo tatenda kazi
Kwa nguvu zake Neno.
Matawi yaso kitu
Maua yatapata;
Furaha ilolala
Yaanza kuamka.
Na apatiwe sifa
Baba alo milele,
Pia na Neno wake
Mwanae wa pekee,
Pamoja nao pia
Roho Mtakatifu
Ni Utatu kamili
Na ni Mungu mmoja.
AU
11
Alozawa na upendo wa Baba
Kabla ya ulimwengu kuumbwa,
Yeye ndiye Alfa na Omega,
Yeye ni chanzo, yeye ni kikomo
Cha vilivyo na vilivyokuwapo
Na vitavyoonekana badaye:
Kwa milele na milele.
Ilibarikiwa milele siku
Bikira - aliyejaa neema,
Mwenye mimba kwa uwezo wa Roho-
Alipomzaa Mwokozi wetu,
Naye Mkombozi wa ulimwengu
Alipoonesha kwanza usowe:
Kwa milele na milele.
Atukuzwe Mungu Baba Mwenyezi,
Atukuzwe Mungu Mwana Mwokozi,
Atukuzwe Roho Mtakatifu,
Umungu mmoja, Nafsi tatu.
Viumbe vyote na vimtukuze
Mwenyezi Mungu kwa nyakati zote:
Kwa milele na milele.
Aurelio C. Prudensio
348-yapata 413
AU
12
Kristo huyu hapa,
Mwenyewe Emanueli,
Yeye ndiye mtukufu
Na ni mpole ajabu:
Hekima nayo neema,
Hekima nao ukweli
Vipo ila mefichama
Katika huyu Mtoto.
Vile Mungu alitaka
Yesu ndipo kaumbika,
Kristo ndiye Mwanga
Aliyetoka kwa Mwanga,
Amekuja waokoa
Waana wake Adamu
Ambao wanangojea
Katika giza - usiku.
Sifa kwa Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Utukufu wao hao
Wa mbinguni wanaimba,
Na walio duniani
Kwa sauti ilo kuu
Sawia wanausifu
Utatu wauabudu.
Stanbrook Abbey Hymnal
ANT. I: U mzuri wa kupendeza kuliko wanadamu wote; neema imemiminwa
midomoni mwako.
Zab.45 Utenzi wa arusi ya kifalme
Tazameni, Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki (Mt.25:6)
I
Moyo wangu umejaa mawazo mema:/
namtungia mfalme shairi langu,*
ulimi wangu u tayari kama kalamu ya mwandishi mwepesi:
wewe u mzuri kuliko wanadamu wote,/
maneno yako ni fadhili tupu,*
naye Mungu amekubariki milele.
Ewe shujaa, weka upanga wako tayari;*
wewe ni mtukufu na mwenye fahari.
Songa mbele kwa ushindi, utetee haki na ukweli,*
mkono wako ukupatie ushindi mkubwa.
Mishale yako ni mikali,/
hupenya mioyo ya adui za mfalme;*
nayo mataifa huanguka chini yako.
Utawala wako ni kama wa Mungu, wadumu milele;*
wewe wawatawala watu wako kwa haki.
Wapenda uadilifu na kuchukia uovu./
Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuteua,*
na kukumiminia furaha kubwa zaidi kuliko wenzako.
Mavazi yako yanukia marashi na udi,/
wanamuziki wakuimbia katika majumba*
yaliyopambwa kwa pembe za ndovu.
Binti za wafalme ni baadhi ya wanaokulaki,/
naye malkia amesimama kulia kwako,*
amevaa mapambo ya dhahabu safi.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: U mzuri wa kupendeza kuliko wanadamu wote; neema imemiminwa midomoni mwako.
ANT. II: Tazameni, Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.
II
Nawe binti sikiliza! Nisikilize kwa makini:*
sahau sasa watu wako na jamaa zako.
Uzuri wako wamvutia mfalme;*
yeye ni bwana wako, lazima umtii.
Watu wa Turo watakuletea zawadi;*
matajiri watataka upendeleo wako.
Binti mfalme anaingia - mzuri kabisa!*
Vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.
Amevalia vazi la rangi nyingi,*
aongozwa kwa mfalme
akisindikizwa na wanawali wenzake,*
nao pia wanapelekwa kwa mfalme.
Kwa furaha na shangwe wanafika huko,*
na kuingia katika jumba la mfalme.
Ee mfalme, utapata watoto wengi/
watakaotawala badala ya wazee wako;*
utawafanya watawale duniani kote.
Sifa zako, nitazieneza kwa vizazi vyote daima,*
nayo mataifa yatakusifu daima na milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Tazameni, Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.
ANT. III: Mungu alikusudia kuvijumlisha vitu vyote katika
Kristo, utimilifu wa wakati utakapowadia.
WIMBO: Ef.1:3-10 Mungu Mwokozi
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!
Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.
Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake
katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.
Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani
kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.
Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu
Kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!
Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!
Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,
akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.
Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,
ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Mungu alikusudia kuvijumlisha vitu vyote katika
Kristo, utimilifu wa wakati utakapowadia.
SOMO: 2Pet.1:3-4
Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji ili tuishi maisha ya kumcha
Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe. Kwa namna hiyo
ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa
tamaa mbaya zilizoko duniani, na mpate kushiriki hali yake ya kimungu.
KIITIKIZANO
K. Mataifa yote yatabarikiwa katika yeye. (W. Warudie)
K. Mataifa yote yatamtukuza.
W. Yatabarikiwa katika yeye.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mataifa...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mamajusi walipoiona nyota walijawa na furaha kuu; waliingia ndani, wakamtolea Bwana dhahabu,
ubani na manemane.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana.
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Mamajusi walipoiona nyota walijawa na furaha kuu; waliingia ndani,
wakamtolea Bwana dhahabu, ubani na manemane.
MAOMBI
Atukuzwe Kristo Bwana, ambaye alikuja kukaa nasi, kuwapatia mwanga wale ambao wanaishi katika
giza na kivuli cha mauti.
W. Kristo, Jua lichomozalo, uwaangazie watu wote
mwanga wako, Kristo Bwana wetu, ulipokuja, Kanisa, yaani mwili wako, lilizaliwa:
- uliwezeshe kuongezeka daima na kujengeka katika upendo duniani. (W.)
Wazishika mikononi mwako mbingu na dunia:
- uyafanye mataifa yote yakutangaze wewe kuwa Bwana wao. (W.)
Kwa kuwa kwako mtu, ulipata kuwa Kuhani wetu Mkuu wa milele:
- uamshe katika mapadre wako wote neema ya kutangaza ukombozi wako. (W.)
Uliyezaliwa na mama aliye bikira;
- uwabariki watawa wanawake wote, na uwafanye wawe ishara ya kudumu ya Kanisa, ambalo ni bi arusi wako. (W.)
Kwa kuuchukua mwili wa kibinadamu unaokabiliwa na kifo, umekomesha nguvu ya mauti:
- uwajalie marehemu wote waungane nawe katika uzima wa milele. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana, mng'aro wa utukufu wako uangaze mioyo yetu, na utuongoze tunapopita katika vivuli vya dunia
hii, mpaka tutakapofikia makao yetu ya mwanga wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu
Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu,
Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.