JANUARI 7 au JUMATATU BAADA YA EPIFANIA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.
Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie -
Ulio mwetu mioyoni -
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.
Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Fumbo, lililofichwa kwa nyakati na kwa vizazi vilivyotangulia,
sasa limefumbuliwa.
Adhuhuri
Ant.: Kristo alifika, akawahubiria amani ninyi mliokuwa mbali, na ninyi
mliokuwa karibu.
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Nimekuteua wewe uwe nuru kwa mataifa yote, na uwe nguvu yangu
ya kuokoa hata miisho ya dunia.
Zab.119:41-48 VI Kutegemea sheria ya Mungu
Unifadhili upendo wako mkuu, Ee Mungu*
uniokoe kama ulivyoahidi.
Hapo nitaweza kuwajibu hao wanaonitukana,*
maana mimi nina imani na neno lako.
Unijalie kusema ukweli daima,*
maana tumaini langu liko katika hukumu zako.
Nitatii sheria yako daima,*
milele na milele.
Nitaishi katika uhuru kamili,*
maana nayatia maanani mafundisho yako.
Nitawatangazia wafalme maagizo yako,*
wala sitaona aibu.
Furaha yangu ni kuzitii amri zako,*
kwa sababu ninazipenda.
Naziheshimu na kuzipenda amri zako;*
nitazitafakari kanuni zako.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.40:1-13,16-17 Utenzi wa sifa
Hukutaka sadaka wala dhabihu, lakini umenitayarishia mwili (Ebr.10:5)
I
Nilimngojea Mungu kwa uvumilivu,*
akanielekea, na kunisikiliza kilio changu.
Aliniondoa katika shimo la hatari,*
katika matope ya dimbwi,
akaniweka salama juu ya mwamba,*
na kuuimarisha mwenendo wangu.
Alinifundisha wimbo mpya,*
wimbo wa sifa kwa Mungu wetu.
Wengi wataona na kuogopa,*
kisha watamtumainia Mungu.
Heri mtu anayemtumainia Mungu;/
mtu asiyejiunga na watu wenye majivuno,*
waliopotoka kwa kuabudu miungu ya uwongo.
Ee Mungu, Mungu wangu,*
umetufanyia mambo mengi ya ajabu,
na mipango yako juu yetu haihesabiki;*
hakuna yeyote aliye kama wewe.
Kama ningeweza kusimulia hayo yote,*
idadi yake ingenishinda.
Sadaka na dhabihu hutaki;/
wala hutaki sadaka za kuteketezwa,*
ila umenipa masikio nikusikie.
Ndiyo maana nilisema;/
"Niko tayari, Ee Mungu wangu, kutimiza mapenzi yako,*
kama nilivyoandikiwa katika kitabu cha sheria.
Naufurahia mwongozo wako,*
na kuuzingatia kwa moyo wote."
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II Sala ya kuomba msaada
Mbele ya jumuiya kubwa ya watu,/
nimesimulia habari njema ya ukombozi.*
Wajua, Ee Mungu, kuwa sikunyamaza hata kidogo.
Sikuificha habari hii moyoni mwangu,*
ya kwamba umeniokoa.
Nimetangaza daima uaminifu wako na msaada wako./
Sikuifichia jumuiya kubwa ya watu,*
uaminifu na upendo wako mkuu.
Ee Mungu, usinikatalie huruma yako:/
Upendo wako mkuu na uaminifu wako,*
viniweke salama salimini.
Maafa yasiyohesabika yanizunguka,*
maovu yangu yanikaba hata siwezi kuona;
ni mengi kuliko nywele kichwani mwangu,*
nami nimevunjika moyo.
Ee Mungu, upende kuniokoa;*
Ee Mungu, uje sasa kunisaidia.
Lakini wanaokutafuta wewe,*
wafurahi na kushangilia.
Wale wapendao wokovu utokao kwako,*
waseme daima: “Mkuu ni Mungu!”
Mimi ni maskini na fukara, Ee Bwana;*
lakini wewe hukunisahau.
Wewe ni mwokozi wangu na msaada wangu;*
uje, Ee Mungu wangu, usikawie!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Fumbo, lililofichwa kwa nyakati na kwa vizazi vilivyotangulia,
sasa limefumbuliwa.
Adhuhuri
Ant.: Kristo alifika, akawahubiria amani ninyi mliokuwa mbali, na ninyi
mliokuwa karibu.
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Nimekuteua wewe uwe nuru kwa mataifa yote, na uwe nguvu yangu
ya kuokoa hata miisho ya dunia.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Kum.4:7
Liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA, Mungu wetu, alivyo, kila
tumwitapo?
K. Alitokea duniani.
W. Na akaishi kati ya watu.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Isa.12:5-6
Mwimbieni BWANA; kwa kuwa ametenda makuu; Na yajulikane haya katika dunia yote. Paza sauti, piga
kelele, mwenyeji wa Sion; Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
K. Mataifa yote yamemwona Mtakatifu wako.
W. Wafalme wote wameuona utukufu wako.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Tob.14:6-7
Watu wasio Wayahudi wataiacha miungu yao, na watakuja Yerusalemu, na watakaa humo. Na wafalme wote
wa dunia watafurahi katika Yerusalemu, wakimwabudu Mfalme wa Israeli.
K. Mataifa yote, mtukuzeni Mungu wetu.
W. Msifuni kwa shangwe.
SALA:
Tuombe: Bwana, mng'aro wa utukufu wako uangaze mioyo yetu, na utuongoze tunapopita katika vivuli vya dunia
hii, mpaka tutakapofikia makao yetu ya mwanga wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.