Generic placeholder image

JANUARI 8 au JUMANNE BAADA YA EPIFANIA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo ametutokea: njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.) Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu

Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

TENZI angalia pia AU

AU
13
Betlehemu mji ulo bora,
Mji ulo sawa nawe hakuna:
Ndiwe peke uliyetuzalia
Bwana wa kutoka mbinguni juu.

Nyota ilotangaza kuzaliwa
Ilikuwa nzuri kuliko jua;
Ilitangazia nchi Mungu wao
Aloonekana katika mwili.

Wakiongozwa kwa mng'aro huo
Wafalme wa mashariki watokea;
Wasujudu na zawadi kutoa:
Ubani, dhahabu na manemane.

Zawadi takatifu zenye fumbo;
Ubani Mungu wamdhihirisha,
Dhahabu Mfalme yamtangaza,
Manemane yabashiri kaburi.

Sifa milele ziwe kwako Yesu,
Ulojionesha kwa Mataifa
Katika utukufu wako Bwana,
Pia ziwe kwa Roho na kwa Baba.
Aurelio C. Prudensio 348-yapata 413

AU
14
Nyimbo za sifa na shukrani
Bwana Yesu tunakutolea;
Kwa njia ya nyota uwinguni
Mamajusi walikutambua;
Tawi la mfalme Daudi
Betlehemu ulizaliwa;

Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

Ulidhihirishwa Yordani;
U kuhani, nabii, mfalme;
Na katika arusi ya Kana
Umungu wako ulionesha,
Ukageuza kwa yako nguvu
Maji yakawa divai tamu;

Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

Tujalie ne'ma tukuone
E Bwana, katika neno lako;
Tuwezeshe kukuiga wewe,
Na tuwe safi kama mwenyewe,
Ili utapotokea tena
Tuwe watukufu kama wewe,

Na tukusifu Mbarikiwa,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!
C. Wordsworth 1807-1885

Tenzi nam. 10, 11, 12 zafaa pia
10
Tumempata sisi
Tumepewa mtoto,
Analeta uhuru
Kristo Mwokozi,
Yeye ni Mshauri
Ni Baba wa milele,
Mungu aliye mtu,
Mfalme wa Amani.

Mamake ni Maria
Bikira na mpole,
Hiyo kazi ya Roho,
Roho yule wa Bwana;
Huyo alitamkwa
Kale tangu milele:
Huyu ndiye ni Neno
Wake Baba Mwenyezi.

Ndaniye tachanua
Upendo na ukweli,
Navyo tatenda kazi
Kwa nguvu zake Neno.
Matawi yaso kitu
Maua yatapata;
Furaha ilolala
Yaanza kuamka.

Na apatiwe sifa
Baba alo milele,
Pia na Neno wake
Mwanae wa pekee,
Pamoja nao pia
Roho Mtakatifu
Ni Utatu kamili
Na ni Mungu mmoja.

AU
11
Alozawa na upendo wa Baba
Kabla ya ulimwengu kuumbwa,
Yeye ndiye Alfa na Omega,
Yeye ni chanzo, yeye ni kikomo
Cha vilivyo na vilivyokuwapo
Na vitavyoonekana badaye:
Kwa milele na milele.

Ilibarikiwa milele siku
Bikira - aliyejaa neema,
Mwenye mimba kwa uwezo wa Roho-
Alipomzaa Mwokozi wetu,
Naye Mkombozi wa ulimwengu
Alipoonesha kwanza usowe:
Kwa milele na milele.

Atukuzwe Mungu Baba Mwenyezi,
Atukuzwe Mungu Mwana Mwokozi,
Atukuzwe Roho Mtakatifu,
Umungu mmoja, Nafsi tatu.
Viumbe vyote na vimtukuze
Mwenyezi Mungu kwa nyakati zote:
Kwa milele na milele.
Aurelio C. Prudensio
348-yapata 413

AU
12
Kristo huyu hapa,
Mwenyewe Emanueli,
Yeye ndiye mtukufu
Na ni mpole ajabu:
Hekima nayo neema,
Hekima nao ukweli
Vipo ila mefichama
Katika huyu Mtoto.

Vile Mungu alitaka
Yesu ndipo kaumbika,
Kristo ndiye Mwanga
Aliyetoka kwa Mwanga,
Amekuja waokoa
Waana wake Adamu
Ambao wanangojea
Katika giza - usiku.

Sifa kwa Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Utukufu wao hao
Wa mbinguni wanaimba,
Na walio duniani
Kwa sauti ilo kuu
Sawia wanausifu
Utatu wauabudu.
Stanbrook Abbey Hymnal

ANT. I: Ee Bwana, niletee nuru yako na kweli yako.

Zab.43 Sala ya mkimbizi yaendelea
Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani (Yoh.12:46)

Uwe upande wangu, Ee Mungu;*
unitetee haki zangu;

unikinge na watu wanaokuchukia,*
watu waongo na waovu.

Wewe Mungu wangu, uliye nguvu yangu,*
kwa nini umenitupilia mbali?

Mbona naendelea kuteseka,*
nikisumbuliwa na adui zangu?

Upeleke mwanga wako na ukweli wako,*
vipate kuniongoza na kunipeleka kwako;

mpaka kwenye mlima wako mtakatifu, kwenye makao yako.*
Hapo, Ee Mungu, nitakwenda madhabahuni pako;

nitakuja kwako, Ee Mungu, asili ya furaha yangu.*
Nitakusifu kwa kinubi, Ee Mungu, Mungu wangu.

Mbona ninahuzunika hivyo moyoni?*
Kwa nini nahangaika hivyo?

Nitamtumainia Mungu!*
Nitamsifu tena Mungu, mwokozi wangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, niletee nuru yako na kweli yako.

ANT. II: Bwana, uje kutusaidia siku zote za maisha yetu.

WIMBO: Isa.38:10-14,17-20 Kihoro cha mgonjwa mahututi; furaha ya aliyepona.

Nalisema, Katika usitawi wa siku zangu/
nitakwenda kuingia malango ya kuzimu;*
Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.

Nalisema, Sitamwona BWANA, yeye BWANA,*
katika nchi ya walio hai;

Sitamwona mwanadamu tena*
pamoja na hao wakaao duniani.

Kao langu limeondolewa kabisa,*
limechukuliwa kama hema ya mchungaji;

Nimekunja maisha yangu kama mfumaji;*
atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi;

Naliomboleza usiku kucha;/
kama simba ameivunja mifupa yangu yote;*
Tangu mchana hata usiku wananimaliza.

Kama mbayuwayu au korongo ndivyo nilivyolia;/
Naliomboleza kama hua;*
macho yangu yamedhoofu kwa kutazama juu;

Ee BWANA, nimeonewa,*
na uwe mdhamini wangu.

Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi*
kwa ajili ya amani yangu;

Lakini kwa kunipenda/
umeniokoa na shimo la uharibifu;*
Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako.

Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu;*
mauti haiwezi kukuadhimisha;

Wale washukao shimoni*
hawawezi kuitarajia kweli yako.

Aliye hai, naam, aliye hai, /
ndiye atakayekusifu, kama mimi leo;*
Baba atawajulisha watoto kweli yako.

BWANA yu tayari kunipa wokovu.*
Basi, kwa vinubi tutaziimba nyimbo zangu,

Siku zote za maisha yetu*
Nyumbani mwa BWANA.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana, uje kutusaidia siku zote za maisha yetu.

ANT. III: Ee Bwana, wastahili sifa zetu Sion.

Zab.65 Wimbo wa shukrani
Sion ieleweke kuwa ni mji wa Mungu (Origen)

Wastahili sifa, Ee Mungu, katika Sion;*
nasi tutakutimizia nadhiri zetu,

maana wewe wasikiliza sala zetu.*
Watu wote watakujia na kukiri dhambi zao:

dhambi zetu zinapotulemea,*
wewe watuondolea.

Heri uliowachagua wakae patakatifu pako,/
Sisi tutashiba kwa mema ya nyumba yako;*
kwa baraka za Hekalu lako takatifu.

Kwa matendo ya ajabu, Ee Mungu, mkombozi wetu,*
wewe watusikiliza na kutupatia ushindi.

Duniani kote na kupita bahari za mbali,*
watu wakutumainia wewe.

Wewe umejawa nguvu tele tele:*
kwa nguvu yako waisimika milima mahali pake,

watuliza mshindo wa bahari na wa mawimbi yake,*
wakomesha ghasia za watu.

Ulimwengu wote washangazwa na matendo yako./
Wasababisha furaha kila mahali,*
toka mashariki hata magharibi.

Wewe waitunza nchi kwa kuinyeshea mvua,/
waijalia rutuba na kuisitawisha;*
mito yake waijaza maji ya mbinguni,

waifanikisha nchi na kuipatia mavuno.*
Hivi ndivyo ufanyavyo:

Mashamba wayanyeshea mvua kwa wingi,*
na kuyalowanisha kwa maji;

ardhi wailainisha kwa manyunyu,*
na kuibariki mimea ichipue.

Wautunukia mwaka wote mema yako,*
kila ulipopitia pamejaa fanaka.

Mbuga za majani zimejaa mifugo,*
milima nayo imejawa furaha.

Malisho yamejaa kondoo,/
mabonde yamefunikwa kwa ngano.*
Kila kitu kinashangilia kwa furaha.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Ee Bwana, wastahili sifa zetu Sion.

SOMO: Isa.4:2-3
Siku hiyo chipukizi la BWANA litakuwa zuri, lenye utukufu, na matunda ya nchi yatakuwa mema sana, na kupendeza, kwa ajili ya Waisraeli wale waliookoka. Tena itakuwa ya kwamba yeye aliyebaki katika Sion, na yeye aliyeachwa ndani ya Yerusalemu, ataitwa mtakatifu; yaani, kila mmoja aliyeandikwa miongoni mwa hao walio hai ndani ya Yerusalemu.

KIITIKIZANO
K. Wafalme wote wa dunia watamwabudu. (W. Warudie)
K. Mataifa yote yatamtumikia.
W. Wafalme watamwabudu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wafalme wote...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Mamajusi walimtolea Bwana zawadi tatu: dhahabu, ubani na manemane. Walitoa zawadi hizo kwa Mwana wa Mungu, kwa Mfalme mkuu, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mamajusi walimtolea Bwana zawadi tatu: dhahabu, ubani na manemane. Walitoa zawadi hizo kwa Mwana wa Mungu, kwa Mfalme mkuu, aleluya.

MAOMBI
Kristo alikuja ili watu wapate kufanywa huru kutoka utumwa wao wa kutenda maovu, na hivi waweze kufurahia uhuru wa wana wa Mungu. Na tumwombe:
W. Kwa kuzaliwa kwako, utuokoe na uovu wote.

Bwana Yesu, ulikuja kutuletea uzima mpya;
- utufanye upya kwa fumbo la kuzaliwa kwako. (W.)

Kristo, Mungu na mtu, uyawezeshe maisha yako ya kimungu yapenye ubinadamu wetu;
- utufanye tuishi kama wana wa Mungu. (W.)

Nuru ya mataifa, mwalimu wa utakatifu;
- Neno lako na lituangazie njia ya maisha yetu. (W.)

Ulifanywa mtu kwa njia ya Mama Maria;
- daima ubaki mioyoni mwetu kwa njia ya imani yetu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tunapoungojea ujio wa utawala wa Mungu, tusali tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu, Baba yetu, Mwanao wa Pekee alipojidhihirisha kwa mwili na damu, tulipata kumtambua kuwa ni mwenzetu. Tunaomba atugeuze mioyo yetu ili tufanane naye, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.