Generic placeholder image

JANUARI 8 au JUMANNE BAADA YA EPIFANIA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

TENZI angalia pia AU

AU
13
Betlehemu mji ulo bora,
Mji ulo sawa nawe hakuna:
Ndiwe peke uliyetuzalia
Bwana wa kutoka mbinguni juu.

Nyota ilotangaza kuzaliwa
Ilikuwa nzuri kuliko jua;
Ilitangazia nchi Mungu wao
Aloonekana katika mwili.

Wakiongozwa kwa mng'aro huo
Wafalme wa mashariki watokea;
Wasujudu na zawadi kutoa:
Ubani, dhahabu na manemane.

Zawadi takatifu zenye fumbo;
Ubani Mungu wamdhihirisha,
Dhahabu Mfalme yamtangaza,
Manemane yabashiri kaburi.

Sifa milele ziwe kwako Yesu,
Ulojionesha kwa Mataifa
Katika utukufu wako Bwana,
Pia ziwe kwa Roho na kwa Baba.
Aurelio C. Prudensio 348-yapata 413

AU
14
Nyimbo za sifa na shukrani
Bwana Yesu tunakutolea;
Kwa njia ya nyota uwinguni
Mamajusi walikutambua;
Tawi la mfalme Daudi
Betlehemu ulizaliwa;

Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

Ulidhihirishwa Yordani;
U kuhani, nabii, mfalme;
Na katika arusi ya Kana
Umungu wako ulionesha,
Ukageuza kwa yako nguvu
Maji yakawa divai tamu;

Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

Tujalie ne'ma tukuone
E Bwana, katika neno lako;
Tuwezeshe kukuiga wewe,
Na tuwe safi kama mwenyewe,
Ili utapotokea tena
Tuwe watukufu kama wewe,

Na tukusifu Mbarikiwa,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!
C. Wordsworth 1807-1885

Tenzi nam. 10, 11, 12 zafaa pia
10
Tumempata sisi
Tumepewa mtoto,
Analeta uhuru
Kristo Mwokozi,
Yeye ni Mshauri
Ni Baba wa milele,
Mungu aliye mtu,
Mfalme wa Amani.

Mamake ni Maria
Bikira na mpole,
Hiyo kazi ya Roho,
Roho yule wa Bwana;
Huyo alitamkwa
Kale tangu milele:
Huyu ndiye ni Neno
Wake Baba Mwenyezi.

Ndaniye tachanua
Upendo na ukweli,
Navyo tatenda kazi
Kwa nguvu zake Neno.
Matawi yaso kitu
Maua yatapata;
Furaha ilolala
Yaanza kuamka.

Na apatiwe sifa
Baba alo milele,
Pia na Neno wake
Mwanae wa pekee,
Pamoja nao pia
Roho Mtakatifu
Ni Utatu kamili
Na ni Mungu mmoja.

AU
11
Alozawa na upendo wa Baba
Kabla ya ulimwengu kuumbwa,
Yeye ndiye Alfa na Omega,
Yeye ni chanzo, yeye ni kikomo
Cha vilivyo na vilivyokuwapo
Na vitavyoonekana badaye:
Kwa milele na milele.

Ilibarikiwa milele siku
Bikira - aliyejaa neema,
Mwenye mimba kwa uwezo wa Roho-
Alipomzaa Mwokozi wetu,
Naye Mkombozi wa ulimwengu
Alipoonesha kwanza usowe:
Kwa milele na milele.

Atukuzwe Mungu Baba Mwenyezi,
Atukuzwe Mungu Mwana Mwokozi,
Atukuzwe Roho Mtakatifu,
Umungu mmoja, Nafsi tatu.
Viumbe vyote na vimtukuze
Mwenyezi Mungu kwa nyakati zote:
Kwa milele na milele.
Aurelio C. Prudensio
348-yapata 413

AU
12
Kristo huyu hapa,
Mwenyewe Emanueli,
Yeye ndiye mtukufu
Na ni mpole ajabu:
Hekima nayo neema,
Hekima nao ukweli
Vipo ila mefichama
Katika huyu Mtoto.

Vile Mungu alitaka
Yesu ndipo kaumbika,
Kristo ndiye Mwanga
Aliyetoka kwa Mwanga,
Amekuja waokoa
Waana wake Adamu
Ambao wanangojea
Katika giza - usiku.

Sifa kwa Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Utukufu wao hao
Wa mbinguni wanaimba,
Na walio duniani
Kwa sauti ilo kuu
Sawia wanausifu
Utatu wauabudu.
Stanbrook Abbey Hymnal

ANT. I: Hamwezi kutumikia Mungu na mali.

Zab.49 Upumbavu wa kutegemea mali
Itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni (Mt.19:23)

I
Enyi watu wote, sikilizeni jambo hili!*
Tegeni masikio, nyote mnaoishi duniani;

wote, wakubwa kwa wadogo,*
matajiri na fukara.

Maneno yangu yatakuwa mazito mazito;*
mimi nitasema maneno ya hekima.

Nitategea sikio nisikilize mithali,*
na kufafanua maana yake kwa muziki wa kinubi.

Mimi siogopi wakati wa hatari,*
wakati nizungukwapo na adui;

watu waovu wategemeao mali zao,*
na kujisifia wingi wa utajiri wao.

Hakika binadamu hawezi kujikomboa mwenyewe;*
hawezi kumlipa Mungu gharama ya maisha yake,

maana fidia ya maisha ni kubwa mno.*
Hawezi kutoa kitu chochote kinachotosha,

kimwezeshe aendelee kuishi,*
asipate kuonja kaburi.

Wote wajua kwamba hata wenye hekima hufa,/
wapumbavu, hali kadhalika na watu wajinga.*
Wote huwaachia wengine mali zao.

Makaburi ni makao yao hata milele;/
ni makao yao vizazi hata vizazi;*
ingawa hapo awali walikuwa wamemiliki ardhi.

Binadamu hatadumu katika fahari yake;*
atakufa tu kama mnyama.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Hamwezi kutumikia Mungu na mali.

ANT. II: Jiwekeeni hazina yenu mbinguni, asema Bwana.

II
Hayo ndiyo yawapatayo wanaojiamini kipumbavu,*
ndio mwisho wa wale wanaojivunia mali zao.

Watakufa tu kama kondoo,*
kifo kitakuwa mchungaji wao.

Waadilifu wataona fahari juu ya waovu,/
miili yao itakapokuwa ikioza huko kuzimu,*
mbali na nyumba zilizokuwa zao wenyewe.

Lakini mimi, Mungu atanisalimisha;*
ataniokoa na nguvu za kuzimu.

Usihangaike ukiona mtu anatajirika,*
wala mali yake ikiongezeka, zaidi na zaidi.

Atakapokufa hatachukua chochote,*
mali haitashuka kuzimu pamoja naye.

Ajapojikuza katika maisha haya,*
na kusifiwa kwa sababu ya kufanikiwa,

atajiunga tu na wazee wake huko kuzimu,*
ambako giza linatawala milele.

Binadamu hatadumu katika fahari yake.*
atakufa tu kama mnyama.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Jiwekeeni hazina yenu mbinguni, asema Bwana.

ANT. III: Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kupokea utukufu na heshima.

WIMBO: Ufu.4:11;5:9,10,12 Wimbo wa waliookolewa
Wewe ni Bwana na Mungu wetu,*
unastahili utukufu na heshima na nguvu;

maana wewe uliumba vitu vyote,/
na kwa matakwa yako* kila kitu kimepewa uhai na uzima.

Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu*
na kuivunja mihuri yake,

kwa sababu wewe umechinjwa,/
na kwa damu yako umemnunulia Mungu*
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani/
wamtumikie Mungu wetu,*
nao watatawala duniani.

Mwanakondoo aliyechinjwa*
anastahili kupokea

uwezo, utajiri, hekima,*
nguvu, heshima, utukufu na sifa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kupokea utukufu na heshima.

SOMO: Ef.2:3b-5
Kidunia, sisi, kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu. Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika, hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu ninyi mmeokolewa.

KIITIKIZANO
K. Mataifa yote yatabarikiwa katika yeye. (W. Warudie)
K. Mataifa yote yatamtukuza.
W. Yatabarikiwa katika yeye.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mataifa...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Ulikuja kutupatia mwanga wa milele; Mamajusi wakutolea zawadi, Ee Kristo, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana.
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Ulikuja kutupatia mwanga wa milele; Mamajusi wakutolea zawadi, Ee Kristo, aleluya.

MAOMBI
Tuungane na Wakristo wote, tukimtukuza Baba na kumwomba ulinzi wake.
W. Baba wa mbinguni, uwasikilize wanao.

Baba, uwasaidie wale wanaomtafuta Mungu wasiyemjua;
- na uwawezeshe kugundua mwanga wa Kristo. (W.)

Uwahurumie wale ambao wanakuabudu wewe, Mungu pekee;
- uwaoneshe kuwa daima u karibu nao. (W.)

Uwakumbuke wanao wote ko kote duniani;
- uwaangalie kusudi kamwe wasijitenge mbali nawe. (W.)

Uwatume malaika wako kuwalinda watu wote;
- na uwaokoe na kifo cha ghafla. (W.)

Uwajalie marehemu wauone utukufu wako;
- uwape raha ya milele katika makao yako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu, Baba yetu, Mwanao wa Pekee alipojidhihirisha kwa mwili na damu, tulipata kumtambua kuwa ni mwenzetu. Tunaomba atugeuze mioyo yetu ili tufanane naye, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.