Generic placeholder image

JANUARI 9 au JUMATANO BAADA YA EPIFANIA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

TENZI angalia pia AU

AU
13
Betlehemu mji ulo bora,
Mji ulo sawa nawe hakuna:
Ndiwe peke uliyetuzalia
Bwana wa kutoka mbinguni juu.

Nyota ilotangaza kuzaliwa
Ilikuwa nzuri kuliko jua;
Ilitangazia nchi Mungu wao
Aloonekana katika mwili.

Wakiongozwa kwa mng'aro huo
Wafalme wa mashariki watokea;
Wasujudu na zawadi kutoa:
Ubani, dhahabu na manemane.

Zawadi takatifu zenye fumbo;
Ubani Mungu wamdhihirisha,
Dhahabu Mfalme yamtangaza,
Manemane yabashiri kaburi.

Sifa milele ziwe kwako Yesu,
Ulojionesha kwa Mataifa
Katika utukufu wako Bwana,
Pia ziwe kwa Roho na kwa Baba.
Aurelio C. Prudensio 348-yapata 413

AU
14
Nyimbo za sifa na shukrani
Bwana Yesu tunakutolea;
Kwa njia ya nyota uwinguni
Mamajusi walikutambua;
Tawi la mfalme Daudi
Betlehemu ulizaliwa;

Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

Ulidhihirishwa Yordani;
U kuhani, nabii, mfalme;
Na katika arusi ya Kana
Umungu wako ulionesha,
Ukageuza kwa yako nguvu
Maji yakawa divai tamu;

Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

Tujalie ne'ma tukuone
E Bwana, katika neno lako;
Tuwezeshe kukuiga wewe,
Na tuwe safi kama mwenyewe,
Ili utapotokea tena
Tuwe watukufu kama wewe,

Na tukusifu Mbarikiwa,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!
C. Wordsworth 1807-1885

Tenzi nam. 10, 11, 12 zafaa pia
10
Tumempata sisi
Tumepewa mtoto,
Analeta uhuru
Kristo Mwokozi,
Yeye ni Mshauri
Ni Baba wa milele,
Mungu aliye mtu,
Mfalme wa Amani.

Mamake ni Maria
Bikira na mpole,
Hiyo kazi ya Roho,
Roho yule wa Bwana;
Huyo alitamkwa
Kale tangu milele:
Huyu ndiye ni Neno
Wake Baba Mwenyezi.

Ndaniye tachanua
Upendo na ukweli,
Navyo tatenda kazi
Kwa nguvu zake Neno.
Matawi yaso kitu
Maua yatapata;
Furaha ilolala
Yaanza kuamka.

Na apatiwe sifa
Baba alo milele,
Pia na Neno wake
Mwanae wa pekee,
Pamoja nao pia
Roho Mtakatifu
Ni Utatu kamili
Na ni Mungu mmoja.

AU
11
Alozawa na upendo wa Baba
Kabla ya ulimwengu kuumbwa,
Yeye ndiye Alfa na Omega,
Yeye ni chanzo, yeye ni kikomo
Cha vilivyo na vilivyokuwapo
Na vitavyoonekana badaye:
Kwa milele na milele.

Ilibarikiwa milele siku
Bikira - aliyejaa neema,
Mwenye mimba kwa uwezo wa Roho-
Alipomzaa Mwokozi wetu,
Naye Mkombozi wa ulimwengu
Alipoonesha kwanza usowe:
Kwa milele na milele.

Atukuzwe Mungu Baba Mwenyezi,
Atukuzwe Mungu Mwana Mwokozi,
Atukuzwe Roho Mtakatifu,
Umungu mmoja, Nafsi tatu.
Viumbe vyote na vimtukuze
Mwenyezi Mungu kwa nyakati zote:
Kwa milele na milele.
Aurelio C. Prudensio
348-yapata 413

AU
12
Kristo huyu hapa,
Mwenyewe Emanueli,
Yeye ndiye mtukufu
Na ni mpole ajabu:
Hekima nayo neema,
Hekima nao ukweli
Vipo ila mefichama
Katika huyu Mtoto.

Vile Mungu alitaka
Yesu ndipo kaumbika,
Kristo ndiye Mwanga
Aliyetoka kwa Mwanga,
Amekuja waokoa
Waana wake Adamu
Ambao wanangojea
Katika giza - usiku.

Sifa kwa Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Utukufu wao hao
Wa mbinguni wanaimba,
Na walio duniani
Kwa sauti ilo kuu
Sawia wanausifu
Utatu wauabudu.
Stanbrook Abbey Hymnal

ANT. I: Tunangojea kwa matumaini, baraka za ujio mtukufu wa Mwokozi wetu.

Zab.62 Mungu mlinzi wangu
Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu (Rom.15:13)

Kimya kimya namngojea tu Mungu;*
kwake watoka wokovu wangu.

Yeye peke yake ndiye mwamba wa wokovu wangu,*
yeye ni ngome yangu, sitashindwa.

Hata lini mtamshambulia mtu/
aliye kama kiambaza kilichoinama,*
kama ukuta unaoanza kubomoka?

Naam, toka mahali pake pa heshima,*
mnakusudia tu kumwangusha.

Furaha yenu ni kusema uwongo./
Kwa maneno mnabariki,*
lakini moyoni mnalaani.

Kimya kimya namgojea tu Mungu;*
kwake naliweka tumaini langu.

Yeye peke yake ndiye mwamba wa wokovu wangu,*
yeye ni ngome yangu, sitashindwa.

Wokovu na fahari yangu vyatoka kwa Mungu;*
Mungu ni mwamba wa usalama na kimbilio langu.

Enyi watu, mtumainieni Mungu daima;*
mwelezeni shida zenu; Mungu ni kimbilio letu.

Binadamu wote ni kama pumzi tu;*
wote, wakubwa kwa wadogo, hawafai kitu.

Tena, ukiwapima uzito hawafikii kilo,*
wote pamoja ni wepesi kuliko pumzi.

Msitegemee ujambazi,/
msijisifie mali ya wizi;*
kama mali zikiongezeka msizitegemee.

Mungu ametamka mara moja,/
nami nimesikia tena na tena:*
kwamba enzi ni mali yake Mungu;

wewe, Ee Bwana, ndiwe mwenye upendo mkuu.*
Wewe wamlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Tunangojea kwa matumaini, baraka za ujio mtukufu wa Mwokozi wetu.

ANT. II: Mungu na atubariki; na atuangaze kwa nuru ya uso wake.

Zab.67 Wimbo wa shukrani
Jueni, basi, kwamba wokovu utokao kwa Mungu umepelekwa kwa watu wa mataifa (Mate.28:28)

Utuonee huruma, Ee Mungu, utubariki;*
utuelekezee uso wako kwa wema;

dunia yote itambue mwongozo wako,*
mataifa yote yajue nguvu yako ya kuokoa.

Watu wote wakutukuze, Ee Mungu;*
mataifa yote yakusifu.

Mataifa yote yafurahi na kushangilia;/
maana wawahukumu watu kwa haki,*
na kuyaongoza mataifa ya dunia.

Watu wote wakutukuze, Ee Mungu;*
mataifa yote yakusifu.

Nchi imetoa mazao yake;*
Mungu, Mungu wetu, ametubariki.

Mungu ametujalia baraka zake,*
watu wote duniani wamche.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Mungu na atubariki; na atuangaze kwa nuru ya uso wake.

ANT. III: Katika yeye vitu vyote viliumbwa, naye huvidumisha vyote.

WIMBO: Kol.1:12-20 Kristo ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, ni mzaliwa wa kwanza kutoka wafu.

Mshukuruni Baba*
aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu

katika mambo yale/
Mungu aliyowawekea watu wake*
katika Utawala wa mwanga.

Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza,/
akatuleta salama*
katika Utawala wa Mwanae mpenzi,

ambaye kwa njia yake tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Kristo ni mfano kamili unaoonekana*
wa Mungu asiyeonekana.

Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza,*
mkuu kuliko viumbe vyote.

Maana kwa njia yake/
Mungu aliumba kila kitu*
duniani na mbinguni,

vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:/
wenye enzi, watawala,*
wakuu na wenye mamlaka.

Vyote viliumbwa kwa njia yake*
na kwa ajili yake.

Kristo alikuwako kabla ya viumbe vyote/
na kwa kuungana naye,*
kila kitu hudumu mahali pake.

Yeye ni kichwa cha mwili wake,/
yaani kanisa;*
yeye nichanzo cha uhai wa huo mwili.

Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza*
aliyefufuliwa katika wafu,

ili yeye peke yake/
awe na nafasi ya kwanza*
katika vitu vyote.

Maana Mungu mwenyewe aliamua
kwamba Mwana anao ukamilifu wote*
wa kimungu ndani yake.

Basi, kwa njia yake,/
Mungu aliamua*
kuupatanisha ulimwengu wote naye.

Kwa damu ya Kristo msalabani*
Mungu alifanya amani,

na hivyo akavipatanisha naye*
vitu vyote duniani na mbinguni.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Katika yeye vitu vyote viliumbwa, naye huvidumisha vyote.

SOMO: Kol.1:13-15
Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika Utawala wa Mwanae mpenzi, ambaye kwa njia yake tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Kristo ni mfano kamili unaoonekana wa Mungu asiyeonekana. Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza, mkuu kuliko viumbe vyote.

KIITIKIZANO
K. Mataifa yote yatabarikiwa katika yeye. (W. Warudie)
K. Mataifa yote yatamtukuza.
W. Yatabarikiwa katika yeye.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mataifa...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Herode akawauliza Mamajusi, 'Mmeona ishara gani kuhusu huyo mfalme mpya aliyezaliwa?' Tuliona nyota angavu, ambayo nuru yake yaijaza dunia nzima.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana.
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Herode akawauliza Mamajusi, 'Mmeona ishara gani kuhusu huyo mfalme mpya aliyezaliwa?' Tuliona nyota angavu, ambayo nuru yake yaijaza dunia nzima.

MAOMBI
Kwa matumaini, tunasali kwa Neno wa Mungu, aliyekuja kuzamisha dhambi zetu katika bahari ya upendo wake.
W. Bwana, utuhurumie.

Kuhani Mkuu wa milele, katika wewe tumewezeshwa kumwabudu Mungu ipasavyo;
- Kwa njia ya Kanisa lako uwajalie watu wote kushiriki katika ibada hiyo. (W.)

Ulikuja kwetu kuwa mganga wa roho na mwili;
- uwapatie nguvu wagonjwa na kuwarudishia afya njema. (W.)

Umejaa huruma na uwezo wa kukomboa;
- uwawezeshe watu wote kugundua furaha kuu ipatikanayo kwa kutubu. (W.)

Mfalme Mwenye Nguvu, ulivunja minyororo iliyotufunga;
- uwape nguvu na faraja wale walio gerezani. (W.)

Bwana wa uzima na mauti, ulifungua mlango wa mbingu,
- uwapokee marehemu katika utukufu wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu uliye Baba, nuru ya wanadamu wote, uifanye mioyo yetu ing'are kwa utukufu wa nuru ile ambayo zamani uliwaangazia baba zetu katika imani, na uwajalie watu wako furaha ya amani ya kudumu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.