Generic placeholder image

JANUARI 9 au JUMATANO BAADA YA EPIFANIA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Fumbo, lililofichwa kwa nyakati na kwa vizazi vilivyotangulia, sasa limefumbuliwa.

Adhuhuri
Ant.: Kristo alifika, akawahubiria amani ninyi mliokuwa mbali, na ninyi mliokuwa karibu.

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Nimekuteua wewe uwe nuru kwa mataifa yote, na uwe nguvu yangu ya kuokoa hata miisho ya dunia.

Zab.119:57-64 VIII Heshima kwa sheria ya Mungu
Ee Mungu, ndiwe uliye pekee muhimu kwangu;*
naahidi kushika maagizo yako.

Nakusihi kwa moyo wangu wote;*
unionee huruma kama ulivyoahidi!

Nimeufikiria mwenendo wangu,*
na ninaahidi kuyafuata maagizo yako.

Bila kukawia nafanya haraka*
kuzishika amri zako.

Ingawa mitego ya wakosefu inanisonga,*
lakini sisahau sheria yako.

Usiku wa manane naamka kukusifu,*
kwa sababu ya hukumu zako adilifu.

Mimi ni rafiki ya wote wakuchao,*
wa wote wanaozitii amri zako.

Dunia imejaa upendo wako mkuu, Ee Mungu;*
unifundishe kanuni zako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.55:1-14,16-23 Sala ya mtu anayedhulumiwa
Yesu akaanza kufadhaika sana na kuhangaika (Mt.14:33)

I
Ee Mungu, sikiliza sala yangu;*
usilipe kisogo ombi langu.

Unisikilize na kunikubalia;*
nimechoshwa na mahangaiko yangu.

Nina hofu kubwa kwa vitisho vya adui zangu,*
na kwa kudhulumiwa na watu waovu.

Watu waovu wananitaabisha,*
na kwa hasira wananifanyia uhasama.

Moyo wangu umejaa hofu,*
vitisho vya kifo vimenisonga.

Natetemeka kwa hofu kubwa,*
nimevamiwa na vitisho vikubwa.

Laiti ningekuwa na mabawa kama njiwa!*
Ningeruka mbali na kupata pumziko;

naam, ningesafiri mbali sana,*
na kupata makao jangwani.

Ningekimbilia mahali pa usalama,*
mbali na upepo mkali na dhoruba.

Ee Bwana, vuruga lugha yao;*
maana naona ukatili na ugomvi mjini,

vikiuzunguka usiku na mchana,*
na kuujaza maafa na jinai.

Uharibifu umeenea pote mjini,*
uhasama na ukandamizaji kila mahali.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

II
Kama adui yangu angenitukana,*
ningeweza kustahimili hayo;

kama mpinzani wangu angenidharau,*
ningeweza kujificha mbali naye.

Kumbe, lakini, ni wewe mwenzangu;*
ni wewe rafiki yangu na msiri wangu!

Sisi tulizoea kuzungumza kirafiki;*
pamoja tulifanya ibada nyumbani mwa Mungu.

Lakini mimi namlilia Mungu,*
naye Mungu ataniokoa.

Jioni, asubuhi na adhuhuri,/
nalalama na kulia kwa huzuni,*
naye ataisikia sauti yangu.

Ataniokoa na kunisalimisha*
katika vita ninavyovikabili, dhidi ya maadui wengi.

Mungu atawalaye tangu milele,/
atatega sikio na kuwashinda;*
maana hawashiki sheria wala kumcha Mungu.

Mwenzangu amewashambulia rafiki zake,*
amevunja mapatano yake.

Maneno yake laini kuliko siagi,*
lakini moyo wake watamani vita.

Maneno yake mororo kama mafuta,*
lakini yanakata kama upanga mkali.

Mwachie Mungu mzigo wako,/
naye atakutegemeza;*
kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.

Lakini wauaji na wabaya,*
Mungu atawaporomosha shimoni mwa maangamizi,

kabla ya kufikia nusu ya maisha yao.*
Lakini mimi nitakutumainia wewe, Ee Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Fumbo, lililofichwa kwa nyakati na kwa vizazi vilivyotangulia, sasa limefumbuliwa.

Adhuhuri
Ant.: Kristo alifika, akawahubiria amani ninyi mliokuwa mbali, na ninyi mliokuwa karibu.

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Nimekuteua wewe uwe nuru kwa mataifa yote, na uwe nguvu yangu ya kuokoa hata miisho ya dunia.

MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: 1Tim.1:15
Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi.

K. Alitokea duniani.
W. Na akaishi kati ya watu.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Ufu.21:23-24
Mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuangazia, maana utukufu wa Mungu huuangazia, na taa yake ni yule Mwana-kondoo. Watu wa mataifa watatembea katika mwanga wake na wafalme wa dunia watauletea utajiri wao.

K. Mataifa yote yamemwona Mtakatifu wako.
W. Wafalme wote wameuona utukufu wako.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 1Joh.1:5
Habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga; na hamna giza lo lote ndani yake.

K. Mataifa yote, mtukuzeni Mungu wetu.
W. Msifuni kwa shangwe.

SALA:
Tuombe: Mungu uliye Baba, nuru ya wanadamu wote, uifanye mioyo yetu ing'are kwa utukufu wa nuru ile ambayo zamani uliwaangazia baba zetu katika imani, na uwajalie watu wako furaha ya amani ya kudumu. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.