KUTOLEWA BWANA HEKALUNI
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: 2Tim.1:12;4:8
Tumezitafakari fadhili zako, ee Mungu, katikati ya hekalu lako. Kama lilivyo jina lako, ee Mungu ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia; mkono wako wa kuume umejaa haki.

UTUKUFU husemwa:

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, tunakuomba kwa unyenyekevu, wewe uliye mtukufu, ili, kama vile Mwanao pekee alivyotolewa leo hekaluni akiwa mwanadamu kama sisi, vivyo hivyo utufanye sisi tuwekwe mbele yako tukiwa na mioyo safi. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Mal.3:1-4
Bwana Mungu asema hivi: Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.24:7-10 (K)8
1. Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Inukeni, enyi malango ya milele,
Mfalme wa utukufu apate kuingia.

(K) Ni nani Mfalme wa utukufu?
Ni Bwana, mwenye nguvu, hodari

2. Ni nani Mfalme wa utukufu?
Bwana mwenye nguvu, hodari,
Bwana hodari wa vita. (K)

3. Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Naam, viinueni, enyi malango ya milele
Mfalme wa utukufu apate kuingia. (K)

4. Ni nani huyu Mfalme wa utukufu?
Bwana wa majeshi,
Yeye ndiye Mfalme wa utukufu. (K)

SOMO 2: Ebr.2:14-18
Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.

SHANGILIO: Lk.2:32
Aleluya, aleluya,
Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa,
Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.
Aleluya.

INJILI: Lk.2:22-40
Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, wazee wa Yesu walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Huwa wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mkononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, kwa amani, kama ulivyosema; kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa watu wote; nuru ya kuwa mwangaza wa mataifa, na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.

MAOMBI
Ndugu Wapenzi, Mkombozi alijionesha kwa watu hekaluni. Tumuombe, Ee Bwana Yesu Kristo, mwanga wa kuwaangazia mataifa yote.

1. Ulisaidie Kanisa lako kuwaelimisha na kuwatayarisha wachungaji, makatekista, masista na waumini kuwa wamisonari hodari wa kutangaza Habari Njema ya wokovu.

2. Uwaongoze mataifa kufikia mwanga na amani yako ili kuleta amani katika dunia yetu.

3. Uwaongoze watawala wa nchi kutunga sheria za kulinda usitawi na amani katika nchi zao.

4. Uwapelekee wazee wasaidizi ili wawatunze katika shida za afya na matatizo ya kijamii.

5. Utukusanye sisi sote katika hekalu tukufu la milele.

Ee Mungu, Mwana wako alipozaliwa na Bikira Maria, mwanga wake uliangaza dunia yetu na kulifukuza giza la udanganyifu. Utujalie sisi watumishi wako, tuufuate mwanga huo unaotuongoza katika njia ya kukufikia. Kwa Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba upendezwe na sadaka ya Kanisa lako linalofurahi, wewe uliyependa Mwanao pekee ajitoe mwenyewe kama Manakondoo asiye na doa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Anayeishi na kutawala milele na milele.

UTANGULIZI
Fumbo la kutolewa Bwana hekaluni
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu wmenyezi wa milele.
Kwa kuwa Mwanao wa milele ametolewa leo hekaluni na ametambulishwa na Roho Mtakatifu kuwa utukufu wa Israeli na mwanga wa Mataifa.
Kwa hiyo, sisi pia, tunaomwendea kwa furaha Mokozi huyo uliyemtuma kwetu, tunakusifu pamoja na Malaika na watakatifu, tukisema bila mwisho.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Lk.2:30-31
Macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa watu wote.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, kamilisha ndani yetu neema yako kwa sakramenti hii takatifu tuliyoipokea. Wewe ulimtimizia Simeoni tumaini lake, na hivi hakuona mauti kabla ya kumpokea Kristo. Vilevile utujalie na sisi, tunaoandamana kumlaki Bwana, tuupate uzima wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.