UKULU WA MT. PETRO MTUME
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Lk.22:32
Bwana Yesu alimwambia Simoni Petro: Mimi nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.

UTUKUFU husemwa:

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, tunakuomba usiruhusu tutikiswe na mahangaiko yoyote, sisi ambao umetuimarisha katika mwamba wa ungamo la imani la mtume Petro. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: 1Pet.5:1-4
Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.23
1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
Hunihuisha nafsi yangu;

(K) Bwana ndiye Mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.

2. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya;
Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)

3. Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)

4. Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

SHANGILIO: Mt.16:18
Aleluya, aleluya!
Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu,
wala milango ya kuzimu haitalishinda.
Aleluya!

INJILI: Mt.16:13-19
Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

MAOMBI
Ndugu zangu wapendwa, Kwa maombezi ya Mitume tumwombe Kristo, Bwana wa Kanisa lake.

1. Uliwaweka mitume kuwa mashahidi wa ufufuko wako na kuwatuma duniani kote waitangaze habari hii ya furaha: Uwasaidie Baba Mtakatifu F. na maaskofu wote uliowachagua kuwa mahalifa wa mitume wako kuliongoza kanisa lako kwa busara na hekima.

2. Uliwaagiza mitume watangaze neno lako kati ya mataifa yote: Uwajaze Roho Mtakatifu wahubiri wote wa neno lako.

3. Uliweka kanisa lako juu ya msingi wa mitume: Ulifanye Kanisa lako kuwa alama ya umoja na ya amani kati ya mataifa.

4. Uliwaagiza mitume wawaondolee dhambi wale wote wanaotubu: Uwatie moyo mpya wote wanaoungama dhambi zao.

Bwana Yesu, unastahili kupokea heshima yote, upokee shukrani na sifa katika Kanisa lako pamoja na Baba na Roho Mtakatifu sasa na siku zote daima na milele. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba uzikubali sala na dhabihu za Kanisa lako, ili, kwa uchungaji wa mtakatifu Petro, Kanisa lako liufikie urithi wa milele, na, kwa mafundisho yake huyo, lishike imani kamili. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: Mitume, wachungaji wa taifa la Mungu.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Wewe, Mchungaji wa milele, huliachi kundi lako, bali walilinda na kulitunza siku zote kwa njia ya Mitume wenye heri, lipate kuongozwa na mawakili walewale wa Mwanao uliowaweka kulisimamia kama wachungaji.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wako tukisema kwa sauti ya unyenyekevu.

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,

ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.16:16,18
Petro akamjibu Yesu akasema: Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akamwambia: Wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu, wewe umetuhuisha kwa kushiriki mwili na damu ya Kristo, sisi tulioadhimisha sikukuu ya mtakatifu Petro, mtume. Tunakuomba, utujalie ili mabadilishano haya ya ukombozi yawe kwetu sakramenti ya umoja na amani. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.