MTAKATIFU YOSEFU MUME WA BIKIRA MARIA
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Lk.12:42
Huyu ndiye wakili mwaminifu na mwenye busara ambaye Bwana alimweka juu ya watumishi wake.
KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, umemkabidhi mtakatifu Yosefu kazi ya kutunza kiaminifu mwanzo wa mafumbo
ya wokovu wa binadamu. Tunakuomba, kwa maombezi yake, ulijalie Kanisa lako litumikie daima
kwa makini mafumbo hayo. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe
katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: 2Sam.7:4-5,12-14,16
Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu,
Daudi, Bwana asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Nawe siku zako zitakapotimia,
ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara
ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake
nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu
kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa
milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.89:1-4,26,28(K)36
1. Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.
(K) Wazao wake watadumu milele.
2. Nimefanya agano na mteule wangu,
Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele,
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)
3. Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
Hata milele nitamwekea fadhili zangu,
Na agano langu litafanyika amini kwake. (K)
SOMO 2: Rum.4:13,16-18,22
Ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria
bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani. Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema,
ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa
imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa
mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye
yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa,
ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Kwa hiyo
ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.
SHANGILIO: Mt.16:18
Aleluya, aleluya!
Heri wakaao nyumbani mwako, ee Bwana, wanakuhimidi daima.
Aleluya!
INJILI: Mt.1:16,18-21,24
Yakobo alimzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye Kristo. Kuzaliwa kwake Yesu Kristo
kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana
ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki,
asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika
wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo,
maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu,
maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi,
alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe;
Au,
Lk.2:41-51
Wazee wa Yesu huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake
miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza
siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa
hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa
wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta.
Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza
maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa,
na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta
kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?
Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii.
MAOMBI
Ee Mungu, ulipenda kumchagua Yosefu awe Mume wa Bikira Maria, ili kuitimiza ahadi ya Mkombozi kutoka katika ukoo
wa Daudi. Leo tunapofanya Sherehe yake, twakuomba.
1. Uwajalie Baba Mtakatifu F., Maaskofu na wote wenye Daraja takatifu neema ya
kuzidi kuyatunza kiaminifu mafumbo matakatifu uliyowaaminisha.
2. Watu wa mataifa yote wajaliwe kumkiri Mwanao kama Mungu na binadamu.
3. Uielekeze mioyo yetu kwenye ufalme wako na uwape watu wa ndoa mwamko wa kuishi kwa uaminifu,
upendo na mshikamano.
4. Mt. Yosefu aliliamini Neno lako; utujalie nasi imani thabiti kama hiyo hasa tunaposongwa na majaribu
makali.
5. Kwa maombezi ya Mtakatifu Yosefu, uwajalie wazazi wote fadhila ya mapendo kwa watoto wao na kwa wote
wanaohitaji msaada wao.
6. Kwa sala za Mtakatifu Yosefu, marehemu wetu wapokelewe katika ushirika wa watakatifu huko mbinguni.
Ee Mungu, Mtakatifu Yosefu alimpokea Maria kama mkewe na Yesu kama mwanawe na akawatunza kwa upendo usio na mipaka.
Utusaidie nasi kuyatimiza mapenzi yako kwa ndugu zetu wazima na wafu. Unayeishi na kutawala, daima na milele. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, mtakatifu Yosefu alimtumikia kwa moyo mkuu Mwanao pekee aliyezaliwa na Bikira Maria.
Tunakuomba utuwezeshe na sisi kuhudumia kwenye altare zako kwa moyo safi. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu.
UTANGULIZI
Utume wa Mt. Yosefu.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote,
ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, na kukusifu kwa mbiu inayokustahili,
na kukuhimidi na kukutangaza Wewe, katika adhimisho la sikukuu ya Yosefu mwenye heri.
Yeye alikuwa mtu mwenye haki, uliyependa awe Mume wake Bikira Maria Mama wa Mungu; na, kama mtumishi
mwaminifu na mwenye busara, ulimweka juu ya Familia yako takatifu awe baba mlinzi wa Mwanao mpenzi,
Yesu Kristo Bwana wetu, aliyetungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kwa njia yake Malaika husifu
adhama yako, Enzi hukuabudu, na Mamlaka hukupigia magoti wakitetemeka.
Mbingu na Nguvu za mbinguni, na Maserafi wenye heri, wakuadhimisha pamoja kwa shangwe.
Tunakusihi, utujalie tujiunge nao kwa wimbo wa sifa, tukisema kwa sauti ya unyenyekevu:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.25:21
Vema, mtumishi mwema na mwaminifu, ingia katika furaha ya Bwana wako.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, umetushibisha sisi familia yako kwa chakula cha altare hii, tukifurahia sherehe ya
mtakatifu Yosefu. Tunakuomba utuhifadhi kwa ulinzi wako wa daima na kulinda ndani yetu baraka
zako ulizotukirimia kwa hisani yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.