KUPASHWA HABARI MARIA YA KUZALIWA BWANA
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Ebr.10:5,7
Bwana ajapo ulimwenguni asema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako, Mungu.
UTUKUFU husemwa
KOLEKTA:
Ee Mungu umetaka Neno wako atwae mwili halisi wa kibinadamu tumboni mwa Bikira Maria. Tunakuomba
utujalie ili sisi pia, tunaoungama kwamba Mkombozi wetu ni Mungu na mtu, tustahili kushiriki umungu
wake. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho
Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Isa.7:10-14
Bwana alisema na Ahazi akinena, Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo
chini sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu
Bwana. Naye akasema, Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha
wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama,
bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.40:6-10(K)7,8
1. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja.
(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya mapenzi yako.
2. Katika gongo la chuo nimeandikiwa,
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
3. Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)
4. Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
Katika kusanyiko kubwa. (K)
SOMO 2: Ebr.10:4-10
Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema,
Dahabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka
za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa)
Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na
hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo
aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimaishe
la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
SHANGILIO: Yn.1:14
Aleluya, aleluya!
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake.
Aleluya!
INJILI: Lk.1:26-38
Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti,
kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake
bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani mwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja
nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?
Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba
na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu,
na bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele,
na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui
mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu
zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa
Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee
wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana
kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.
Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
NASADIKI husemwa: Wote hupiga magoni yasemwapo maneno "Akapata mwili...
akawa mwanadamu."
MAOMBI
Ndugu, tendo la Bikira Maria kupashwa habari ya kuzaliwa mtoto mwanaume atakayeitwa Immanueli ni uthibitisho
wa upendo wa Mungu kwetu sisi wakosefu na uaminifu wake katika ahadi zake. Basi, tumwombe: Ee Mungu Mwenyezi, kwa
Bikira Maria kupashwa habari ya kuzaliwa kwa Mwanao, twakuomba:
1. Upende kupokea dhabihu na sadaka wanazokutolea makuhani wetu kwa ajili ya Kanisa lako.
2. Utujalie wakombolewa wote kuyakataa mabaya na kuyapokea mema.
3. Utuongezee imani na utayari katika kuyapokea na kuyatimiza mapenzi yako, kama alivyofanya Bikira
Maria Mtakatifu.
4. Sisi sote tujaliwe kushiriki umungu wa Kristo aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu.
5. Utujalie uaminifu katika kuiishi miito yetu na kuyajali maongozi ya malaika wako watakatifu.
6. Uwapokee marehemu wetu katika ufalme wako huko mbinguni.
Ee Mungu, Neno wako alifanyika mwili kwa sababu unatupenda na ukamwashia Bikira Maria upendo huo hata
akakubali kumchukua mimba na kumtunza Mwanao. Uyapokee maombi yetu kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu mwenyezi, pokea kwa wema sadaka ya Kanisa lako. Kanisa linajua kwamba lilitokana na
kumwilishwa kwake Mwanao pekee. Ulijalie liadhimishe mafumbo yake kwa furaha katika sherehe
hii. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI
Fumbo la umwilisho wa Bwana.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daoma na
popote, ee Bwana, baba uliye mtakatifu, Mungu wmenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo, Bwana
wetu.
Ndiye aliyezaliwa kati ya watu na kwa ajili ya watu. Nidye yeye ambaye Bikira alipokea kwa
imani habari zake kwa malaika, na kwa upendo akamchukua mimba katika tumbo lake safi kwa
uwezo wa Roho Mtakatifu. Ndivyo ulivyokamilishwa ukweli wa ahadi walizopewa wana wa Isareli
na kujulishwa kuwa yatatimizwa matarajio ya mataifa.
Kwa njia yake majeshi ya Malaika husujudia adhama yako, wakifurahi daima na milele mbele ya
uso wako. Tunakusihi, utujalie tujiunge nao kwa wimbo wa sifu, tukishiriki kusema kwa shangwe:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ...
ANTIFONA YA KOMUNYO: Isa.7:14
Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakuomba uimarishe mioyoni mwetu mafumbo ya imani ya kweli. Tunaungama kwamba
yeye aliyechukuliwa mimba na Bikira ni Mungu kweli na mtu kweli. Kwa nguvu ya ufufuko wake
uletao wokovu, utujalie tustahili kuifikia furaha ya milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.