Generic placeholder image

MTAKATIFU IRENEO Askofu na Mfiadini
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana ndiye mfalme wa wafiadini: njooni, tumwabudu (aleluya).

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.) Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyekfanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile , kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Wafiadini waishi
Pamoja na Kristo,
Kale walijaribiwa
Kwa maumivu makali,
Upendo wao mkubwa
Uchungu uliondoa
Hao walipotundikwa
Na kufa msalabani.

Karne hata karne
Twapata wafiadini,
Waja kwa mtiririko
Bila ya mabadiliko.
Mioyo mejaa pendo
Wala hawalalamiki,
Walidhihirisha pendo
Kimya bila ya vituko.

Hapana mtu ye yote
Aloupima upendo,
Au kwa yake mikono
Kakadiria uzito,
Bali Mungu ajuaye
Yalo moyoni mwa mtu
Ndiye anawapatia
Ile nchi ya ahadi.

Tukuzwe Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Nyie mnatuongoza
Salama katika giza
Tukizifuata njia
Zinazozipita nyota
Na kufika kwenye nuru,
Kwenye nuru ya milele.

ANT. I: Pendo lako lina thamani zaidi kuliko maisha yenyewe; midomo yangu itasimulia sifa yako (aleluya).

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Pendo lako lina thamani zaidi kuliko maisha yenyewe; midomo yangu itasimulia sifa yako (aleluya).

ANT. II: Wafiadini wa Bwana, mtukuzeni Bwana milele (aleluya).

WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

ANT. II: Wafiadini wa Bwana, mtukuzeni Bwana milele (aleluya).

ANT. III: Mtu atakayepata ushindi, nitamfanya awe nguzo katika hekalu langu, asema Bwana (aleluya).

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Mtu atakayepata ushindi, nitamfanya awe nguzo katika hekalu langu, asema Bwana (aleluya).

SOMO: 2Kor.1:3-5
Atukuzwe Mungu Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma, na Mungu mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyo hiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu. Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyo hiyo tunazidi kufarijiwa naye.

KIITIKIZANO
K. Bwana ni nguvu yangu. Nitamwimbia sifa. (W. Warudie)
K. Yeye ni wokovu wangu.
W. Nitamwimbia sifa.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Ye yote aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu, ataiokoa na kuipatia uzima wa milele.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Ye yote aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu, ataiokoa na kuipatia uzima wa milele.

MAOMBI
Kwa njia ya wafiadini, waliouawa kwa ajili ya neno la Mungu, tumtukuze Mwokozi wetu, shahidi mwaminifu na wa kweli.
W. Ulitukomboa kwa damu yako azizi.

Kwa njia ya wafiadini, waliotoa ushuhuda juu ya upendo wako,
- utufanye huru, tuweze kuishi kwa ajili yako. (W.)

Kwa njia ya wafiadini, waliotangaza kifo chako kiletacho wokovu,
- utupatie imani thabiti na ya kudumu. (W.)

Kwa njia ya wafiadini, waliouchukua msalaba wako,
- utujalie ujasiri kila tunapojaribiwa. (W.)

Kwa njia ya wafiadini, waliooshwa katika damu ya Mwana-Kondoo,
- utupatie neema tuweze kuushinda udhaifu wetu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, uliimarisha imani ya kweli na kuliletea Kanisa amani kwa kazi na maandishi ya Mtakatifu Ireneo. Kwa maombezi yake, fanyiza upya imani yetu na upendo wetu, ili daima tuweze kutafuta umoja na amani. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.