Generic placeholder image

MTAKATIFU IRENEO Askofu na Mfiadini
IJUMAA JUMA LA 12 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

Ee Mungu, hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Bwana alimpatia ushindi baada ya mapambano makali, na akamfundisha kwamba hekima ni nguvu iliyo kuu kushinda nguvu zote (aleluya).

Adhuhuri
Ant.: Bwana alimpa taji ya heshima, na jina takatifu la utukufu (aleluya).

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Walikwenda huku wanalia, papo hapo wanapanda mbegu (aleluya).

Zab.119 XXI (161-168)
Wakuu wanidhulumu bila kisa,*
lakini mimi naziheshimu sheria zako kwa moyo wote.

Nafurahi kwa sababu ya ahadi yako,*
kama mtu aliyekuta kitu cha thamani.

Nachukia kabisa uwongo,*
lakini naipenda sheria yako.

Nakusifu mara saba kila siku,*
kwa sababu ya hukumu zako za haki.

Wapendao sheria yako wana amani kuu;*
hakuna kinachoweza kuwaangusha.

Ee Mungu, nakungojea uniokoe;*
natimiza amri zako.

Nashika mafundisho yako,*
nayapenda kwa moyo wote.

Natii amri na maagizo yako;*
wewe waona kila kitu nifanyacho.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.133 Uzuri wa umoja wa kidugu
Tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu (1Yoh.4:7)

Ni jambo zuri na la kupendeza mno*
ndugu kuishi pamoja kwa moyo mmoja.

Ni kama mafuta safi kabisa/
yatiririkayo kichwani na ndevuni mwa Aroni,*
hata mpaka katika vazi lake shingoni.

Ni kama umande wa mlima Hermoni,*
unaoanguka juu ya milima ya Sion.

Hapo ndipo Mungu alipoahidi baraka yake,*
uhai usio na mwisho.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.140:1-8,12-13 Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi (Mt.26:45)

Ee Mungu, uniokoe na watu wabaya,*
unikinge na watu wakatili.

Watu hao huwaza mabaya daima,*
huzusha magomvi kila siku.

Ndimi zao hatari kama nyoka wa sumu;*
maneno yao ni kama sumu ya joka.

Ee Mungu, unilinde na makucha ya wabaya;*
unikinge na wakatili wanaonuia kuniangusha.

Wenye kiburi wamenitegea mitego,/
wametandaza kamba kama wavu,*
wameficha mitego njiani wanikamate.

Namwambia Mungu, “Wewe ndiwe Mungu wangu."*
Usikilize, Ee Mungu, sauti ya ombi langu.

Ee Mungu, Bwana wangu, mwamba wa usalama wangu,*
umenikinga wakati wa vita.

Ee Mungu, usiwape waovu wanayotaka;*
wala mipango yao usiifanikishe.

Najua kwamba Mungu atamlinda mnyonge,*
na kuzitetea haki za mhitaji.

Hakika waadilifu watalisifu jina lako;*
wanyofu watakaa kwako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Bwana alimpatia ushindi baada ya mapambano makali, na akamfundisha kwamba hekima ni nguvu iliyo kuu kushinda nguvu zote (aleluya).

Adhuhuri
Ant.: Bwana alimpa taji ya heshima, na jina takatifu la utukufu (aleluya).

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Walikwenda huku wanalia, papo hapo wanapanda mbegu (aleluya).

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Pet.5:10-11
Mkisha teseka muda mfupi, Mungu aliye asili ya neema yote, na ambaye anawaiteni muushiriki utukufu wake wa milele katika kuungana na Kristo, yeye mwenyewe atawakamilisheni na kuwapeni uthabiti, nguvu na msingi imara. Kwake uwe uwezo milele! Amina.

K. Bwana alimpa joho la furaha (aleluya).
W. Aliweka taji ya utukufu juu ya kichwa chake (aleluya).

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Yak.1:12
Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili, atapewa tuzo la uzima ambalo Mungu aliwaahidia wale wanaompenda.

K. Nilimtumainia Bwana (aleluya).
W. Sitaogopa matendo ya wanadamu (aleluya).

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Hek.3:1-2a,3b
Roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa. Machoni pa watu walio wajinga walionekana kwamba wamekufa, bali wao wenyewe wamo katika amani.

K. Watarejea wakiwa wanaimba kwa furaha (aleluya).
W. Watarudi nyumbani wamechukua matita (aleluya).

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, uliimarisha imani ya kweli na kuliletea Kanisa amani kwa kazi na maandishi ya Mtakatifu Ireneo. Kwa maombezi yake, fanyiza upya imani yetu na upendo wetu, ili daima tuweze kutafuta umoja na amani. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.