Juni 29

WAT. PETRO NA PAULO MITUME
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA:
Hawa ndio wale, ambao walipoishi, walipanda Kanisa kwa damu yao: walikunywa kikombe cha Bwana, wakawa rafiki zake Mungu.

Utukufu husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu, umetujalia tuifurahie siku hii takatifu na tukufu kwa sherehe ya watakatifu Petro na Paulo, mitume. Ulijalie Kanisa lako ili katika mambo yote lifuate maagizo yao, maana kwao limepokea mwanzo wa Ukristo. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Mdo.12:1-11
Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa Kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohane, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi, akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi Vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya Watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule Petro alikuwa amelala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:1-6(K)7
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

(K) Malaika wa Bwana hufanya kituo Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.

2. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote. (K)

3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

SOMO 2: 2Tim.4:6-8,17-18
Mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifikie ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina

SHANGILIO: Mt.16:18
Aleluya, aleluya!
Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.
Aleluya!

INJILI: Mt.16:13-19
Yesu akaenda pande za Kaisaria Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Baryona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba, sala ya mitume iandamane na dhabihu tunayokutolea ili itakaswe kwa jina lako; nayo sala itupe uchaji wako tunapokutolea sadaka hiyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: Utume wa Petro na Paulo katika Kanisa.
K.
Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Kwa maana mitume wako Petro na Paulo kwa mpango wako wanatujalia furaha. Petro alikuwa wa kwanza kukiri imani; na Paulo alieleza imani kwa ufasaha. Petro aliweka misingi ya Kanisa la kwanza kwa mabaki ya wana wa Israeli; Paulo aliitwa awe mwalimu wa Mataifa. Hivyo kwa karama zao mbalimbali waliiunda familia moja ya Kristo, wote wawili wakiheshimiwa duniani kote, wakashiriki taji lililo moja.
Kwa hiyo, sisi pamoja na watakatifu na Malaika Wote tunakutukuza, tukisema bila mwisho:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.16:16,18
Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kupokea sakramenti hii, utujalie tudumu katika Kanisa, ili, tukiendelea kuumega mkate na kuyashika mafundisho ya mitume, tuwe na moyo mmoja na roho moja, tukiimarishwa kwa upendo wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.