Generic placeholder image

Juni 29

WAT. PETERO NA PAULO MITUME
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana ndiye mfalme wa mitume: njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.) Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyekfanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile , kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Nuru iangazayo zaidi
Kuushinda mwanga wa mchana,
Ni nuru gani angavu hii?
Kwa mkali zaidi mwangaza
Siku yang'ara kama dhahabu!
Wakuu wa Kanisa la Mungu
Hii siku inawaheshimu,
Ikiufanya uwe mwepesi
Mzigo wa wale wenye dhambi
Wanaoelekea mbinguni.

Paulo ndo aliwafundisha
Watu kanuni za dini yao,
Petro ndiye mlinzi mkuu
Wa lango la kwingilia mbingu.
Hao waanzishaji wa Roma,
Wanautiisha ulimwengu;
Paulo alikatwa upanga;
Na Petro kafa msalabani;
Enzi milele wafurahia,
Wakiwa wenye taji vichwani.

Furahi sana siku ya leo,
Ewe mji wa Roma, furahi!
Kutazo walitia alama
Kwa damu yao ya kifalme
Hao wawili ambao sasa
Washiriki utukufu wao.
Vazi la mji gani lameta
Kwa wekundu hasa kama wako?
Dunia ina uzuri gani
Uwezao nawe kulingana?

ANT. I: Najua ni nani ninayemtumainia, na nina hakika kwamba yeye, hakimu mwenye haki, atayaangalia kwa makini, yote niliyokuwa nimekabidhiwa mpaka Siku hiyo.

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua maikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Najua ni nani ninayemtumainia, na nina hakika kwamba yeye, hakimu mwenye haki, atayaangalia kwa makini, yote niliyokuwa nimekabidhiwa mpaka Siku hiyo.

ANT. II: Neema ya Mungu iliyo ndani yangu haijawa bure; bali neema yake ipo nami daima.

WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

ANT. II: Neema ya Mungu iliyo ndani yangu haijawa bure; bali neema yake ipo nami daima.

ANT. III: Nimeonesha ujasiri katika vita; safari nimeimaliza; imani nimeitunza.

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Nimeonesha ujasiri katika vita; safari nimeimaliza; imani nimeitunza.

SOMO: 1Pet.4:13-14
Furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo, ili mweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa. Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa juu yetu.

KIITIKIZANO
K. Waliutoa uhai wao kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo. (W. Warudie)
K. Walikwenda zao huku wanafurahi kwamba walikuwa wamestahili kuaibishwa.
W. Kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Waliutoa...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Simoni Petro akasema, 'Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno yaletayo uzima wa milele. Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu', aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Simoni Petro akasema, 'Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno yaletayo uzima wa milele. Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu', aleluya.

MAOMBI
Tunamwomba Kristo aliyelijenga Kanisa lake juu ya mwamba, na ambaye aliwatuma mitume wake wakatoe ushuhuda juu ya ushindi wake dhidi ya mauti.
W. Bwana, uwe pamoja na Kanisa lako.

Ulimwombea Petro ili imani yake isitetereke:
- uimarishe na kuidumisha imani ya Kanisa lako. (W.)

Baada ya kufufuka kwako ulimtokea Petro, na ukajionesha kwa Paulo:
- utusaidie tuweze kuishi kwa nguvu ya ufufuko wako. (W.)

Ulimchagua Paulo ili atangaze habari njema kwa mataifa:
- utuwezeshe kujitoa mhanga kueneza kweli za injili yako, kama alivyofanya Paulo. (W.)

Petro alikukana, lakini upendo wako ukamrudisha kwako:
- utuoneshe huruma na upendo wako, kwa makosa yetu yote. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, unatupatia furaha. kubwa ya kuadhimisha leo sikukuu ya mitume Petro na Paulo. Ulijalie Kanisa lako liweze kufuata mafundisho yao kikamilifu, kwa kuwa hao walikuwa ndio watu wa kwanza kutufundisha sisi kukuabudu wewe kwa njia ya Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.