Generic placeholder image
Juni 29

WAT. PETERO NA PAULO MITUME
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina (Aleluya)

UTENZI
Wote walo duniani
Wapaze zao sauti
Wakimuimbia sifa
Za ushindi za mbinguni
Yeye alowapatia
Mitume wake neema
Ya kupiga mbio zao.
Tukufu ulimwenguni.

Kwalo neno lako wewe
Waliichukua nuru
Ya ukweli wa injili
Hadi kwenye upagani;
Utupatie na sisi
Nuru hiyo ya mbinguni
Macho yetu yafurahi
Na nyoyo zichangamke.

Kwa matakwa yako wewe
Uwezo walijaliwa
Wa kufunga, kufungua
Duniani na mbinguni;
Fungua nyororo zetu,
Twondelee dhambi zetu,
Katika mioyo yetu
Tia upya ne'ma yako.

Na kwa nguvu yako wewe
Walilitamka neno
Lililoponya magonjwa
Na afiya kurudisha;
Endeleza kwetu huo
Uwezowe wa kuponya,
Saidia wadhaifu,
Imarisha wenye nguvu.

ANT. I: 'Wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai'; 'Heri wewe Simoni, Mwana wa Yona."

Zab.117: Kumsifu Mungu
Enyi mataifa yote, msifuni Mungu!*
Enyi watu wote, msifuni!

Upendo wake mkuu kwetu ni thabiti;*
na uaminifu wake wadumu milele!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: 'Wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai'; 'Heri wewe Simoni, Mwana wa Yona."

ANT. II: Wewe ni mwamba, Petro, na juu ya Mwamba huu nitalijenga Kanisa langu.

Zab.147:12-20 Ni vizuri kumsifu Mungu
Ee Yerusalemu, umsifu Mungu!*
Umsifu Mungu wako, Ee Sion!

Maana ameiimarisha milango yako,*
amewabariki watu waliomo kwako.

Ameweka amani mipakani mwako;*
anakushibisha kwa ngano safi kabisa.

Yeye hupeleka amri yake duniani,*
na neno lake hutekelezwa upesi.

Hutandaza theluji kama pamba,*
hutawanya umande kama majivu.

Huleta mvua ya mawe/
vipande vikubwa vikubwa kama mkate*
na kwa ubaridi wake maji huganda.

Kisha hutoa amri, na maji hayo huyeyuka;*
huvumisha upepo wake, nayo hutiririka.

Humjulisha Yakobo ujumbe wake,*
na Israeli amri na maagizo yake.

Lakini watu wengine hakuwafanyia hayo;*
watu wengine hawayajui maagizo yake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Wewe ni mwamba, Petro, na juu ya Mwamba huu nitalijenga Kanisa langu.

ANT. III: Mtakatifu Paulo mtume, wewe ni chombo kiteule cha Mungu; mhubiri wa ukweli ulimwenguni kote.

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake

katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Mtakatifu Paulo mtume, wewe ni chombo kiteule cha Mungu; mhubiri wa ukweli ulimwenguni kote.

SOMO: Rom.1:1-2,7
Kutoka kwangu mimi Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, na mtume niliyeteuliwa na kuitwa kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema ya Mungu. Hapo kale Mungu aliwaahidia watu hii Habari Njema kwa njia ya manabii wake katika Maandiko Matakatifu. Basi, ninawaandikia ninyi nyote mlioko huko Roma ambao Mungu anawapenda, akawateua muwe watu wake. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.

KIITIKIZANO
K. Mitume walitangaza neno la Mungu, bila kumwogopa ye yote. (W. Warudie)
K. Walitoa ushuhuda juu ya ufufuko wa Yesu Kristo.
W. Bila kumwogopa ye yote.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mitume...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mitume wa Kristo wametukuzwa; walipendana hapa duniani; hawatengani baada ya kifo.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mitume wa Kristo wametukuzwa; walipendana hapa duniani; hawatengani baada ya kifo.

MAOMBI
Tunamwomba Kristo, aliyelijenga Kanisa lake juu ya msingi wa mitume na manabii.
W. Bwana, uwe pamoja na taifa lako.

Simoni, yule mvuvi wa samaki, aliitwa nawe ili awe mvuvi wa watu:
- uwaite wengine leo, ili washiriki hiyo kazi yake. (W.)

Wanafunzi wako walipohofu kuwa mashua yao itazama, wewe uliliamuru ziwa litulie, na kukawa shwari:
- ulilinde Kanisa lako linapokuwa katika matatizo, na ulijalie amani, ambayo ulimwengu hauwezi kulipatia. (W.)

Baada ya ufufuko wako, ulimpa Petro mamlaka ya kuliongoza Kanisa lako:
- uwaunganishe sasa watu wako wote katika umoja ule uliowaombea. (W.)

Ulimtuma Paulo awe mtume kwa watu wote:
- uiwezeshe habari yako njema kuhubiriwa siku hizi kwa viumbe vyote. (W.)

Ulilikabidhi Kanisa lako funguo za utawala wako:
- uwafungulie milango ya uzima wa milele marehemu waliokutumainia. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu wetu, tunaomba mitume wenye heri, Petro na Paulo, watutegemeze kwa sala zao. Kwa njia yao ulilifundisha Kanisa lako imani ya Kikristo kwa mara ya kwanza. Kwa maombezi yao, utujalie sasa tuweze kupata wokovu wetu wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.