Generic placeholder image
Juni 29

WAT. PETERO NA PAULO MITUME
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina (Aleluya).

UTENZI
Nuru iangazayo zaidi
Kuushinda mwanga wa mchana,
Ni nuru gani angavu hii?
Kwa mkali zaidi mwangaza
Siku yang'ara kama dhahabu!
Wakuu wa Kanisa la Mungu
Hii siku inawaheshimu,
Ikiufanya uwe mwepesi
Mzigo wa wale wenye dhambi
Wanaoelekea mbinguni.

Paulo ndo aliwafundisha
Watu kanuni za dini yao,
Petro ndiye mlinzi mkuu
Wa lango la kwingilia mbingu.
Hao waanzishaji wa Roma,
Wanautiisha ulimwengu;
Paulo alikatwa upanga,
Na Petro kafa msalabani;
Enzi milele wafurahia,
Wakiwa wenye taji vichwani.

Furahi sana siku ya leo,
Ewe mji wa Roma, furahi!
Kutazo walitia alama
Kwa damu yao ya kifalme
Hao wawili ambao sasa
Washiriki utukufu wao.
Vazi la mji gani lameta
Kwa wekundu hasa kama wako?
Dunia ina uzuri gani
Uwezao nawe kulingana?

ANT. I: Petro, mimi nimekuombea, ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako.

Zab.116:10-19 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Nilizidi kuamini hata niliposema:*
"Mimi naangamia.".

Hata niliposema kwa hofu,*
"Binadamu hawaaminiki."

Nimrudishie Mungu nini,*
kwa mema yote aliyonitendea?

Nitamtolea Mungu dhabihu ya kinywaji,*
nimheshimu kwa shukrani.

Nitamtimizia Mungu nadhiri zangu,*
mbele ya taifa lake lote.

Mungu huthamini kifo cha waaminifu wake.*
Ee Mungu, mimi ni mtumishi wako;

ni mtumishi wako kama alivyokuwa mama yangu,*
umeniweka huru.

Nitakutolea sadaka za shukrani,*
na kukupa heshima zangu.

Mbele ya taifa lako lote,/
ukumbini mwa Hekalu lako huko Yerusalemu,*
nitakutimizia yale niliyoahidi, Ee Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Petro, mimi nimekuombea, ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako.

ANT. II: Nipo radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu, ili uwezo wake Kristo ukae ndani yangu.

Zab.126 Kuomba nguvu mpya
Mungu alipoturudisha tena Sion,*
tulikuwa kama wanaoota ndoto!

Hapo tuliangua kicheko;*
tulishangilia kwa furaha.

Nao watu wa mataifa mengine walisema:*
“Mungu amewatendea mambo makubwa!”

Kweli Mungu alitutendea maajabu,*
tulifurahi kweli kweli!

Ee Mungu, urekebishe tena hali yetu/
kama mvua inavyotiririsha maji*
katika mabonde makavu.

Wanaopanda kwa machozi*
watavuna kwa shangwe;

wanaokwenda kupanda mbegu huku wakilia,*
watarudi kwa furaha huku wakichukua mavuno.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Nipo radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu, ili uwezo wake Kristo ukae ndani yangu.

ANT. III: Wewe ni mchungaji wa taifa la Mungu, ni mkuu wa mitume: ndiwe uliyepewa funguo za utawala wa mbinguni.

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake

katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Wewe ni mchungaji wa taifa la Mungu, ni mkuu wa mitume: ndiwe uliyepewa funguo za utawala wa mbinguni.

SOMO: 1Kor.15:3-5,8
Mimi niliwakabidhi ninyi mambo muhimu sana ambayo mimi niliyapokea: kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kufuatana na Maandiko matakatifu; kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kama ilivyoandikwa; kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili. Na baada ya hao wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama mtu aliyezaliwa kabla ya wakati.

KIITIKIZANO
K. Mitume walitangaza neno la Mungu, bila kumwogopa ye yote. (W. Warudie)
K. Walitoa ushuhuda juu ya ufufuko wa Yesu Kristo.
W. Bila kumwogopa ye yote.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mitume...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Petro, mtume, na Paulo, mwalimu wa mataifa, walitufundisha sheria zako, Bwana.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Petro, mtume, na Paulo, mwalimu wa mataifa, walitufundisha sheria zako, Bwana.

MAOMBI
Tunamwomba Kristo, aliyelijenga Kanisa lake juu ya msingi wa mitume na manabii.
W. Bwana, uwe pamoja na taifa lako.

Simoni, yule mvuvi wa samaki, aliitwa nawe ili awe mvuvi wa watu:
- uwaite wengine leo, ili washiriki hiyo kazi yake. (W.)

Wanafunzi wako walipohofu kuwa mashua yao itazama, wewe uliliamuru ziwa litulie, na kukawa shwari:
- ulilinde Kanisa lako linapokuwa katika matatizo, na ulijalie amani, ambayo ulimwengu hauwezi kulipatia. (W.)

Baada ya ufufuko wako, ulimpa Petro mamlaka ya kuliongoza Kanisa lako:
- uwaunganishe sasa watu wako wote katika umoja ule uliowaombea. (W.)

Ulimtuma Paulo awe mtume kwa watu wote:
- uiwezeshe habari yako njema kuhubiriwa siku hizi kwa viumbe vyote. (W.)

Ulilikabidhi Kanisa lako funguo za utawala wako:
- uwafungulie milango ya uzima wa milele marehemu waliokutumainia. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, unatupatia furaha kubwa ya kuadhimisha leo sikukuu ya mitume Petro na Paulo. Ulijalie Kanisa lako liweze kufuata mafundisho yao kikamilifu, kwa kuwa hao walikuwa ndio watu wa kwanza kutufundisha sisi kukuabudu wewe kwa njia ya Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.