Generic placeholder image

Julai, 03

Mt. TOMA MTUME
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana ni Mfalme wa Mitume; njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.) Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyekfanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile , kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Enyi baba wa imani-
Yetu ya kale imani,
Pamoja na anga zote
Twaziimba sifa zenu
Ambao sauti zenu.
Lisikika duniani,
Kristo mkimtangaza,
Jina lake litukuza.

Maskini mliwapa
Habari Njema: Injili,
Neno la Mungu liwaka
Ndani mwenu lilimeta,
Na lahubiriwa tena
Siku hizi kwetu sisi,
Neno lisilozeeka,
Neno jipya siku zote.

Mlimtangaza Mungu
Alotufilia sisi,
Na akaacha mauti
Mshindi akafufuka,
Ukweli katupatia
Uliotufanya huru
Ndiye asobadilika
Karne hata karne.

Atukuzwe Baba, Mwana,
Na Roho Mtakatifu,
Katupatia imani,.
Imani isiyokufa:
Ni nuru katika giza
Tangu sasa hadi hapo
Nyota ile ya mchana
Ichomozapo nyoyoni.

ANT. I: Toma akasema, 'Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje, basi, kuijua hiyo njia?' Yesu akamjibu, 'Mimi ni njia, ukweli na uzima."

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua maikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Toma akasema, 'Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje, basi, kuijua hiyo njia?' Yesu akamjibu, 'Mimi ni njia, ukweli na uzima."

ANT. II: Toma, aitwaye Pacha, hakuwa pamoja nao wakati Yesu alipokuja. Basi, wale wanafunzi wengine wakamwambia, 'Tumemwona Bwana!' Aleluya.

WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

ANT. II: Toma, aitwaye Pacha, hakuwa pamoja nao wakati Yesu alipokuja. Basi, wale wanafunzi wengine wakamwambia, 'Tumemwona Bwana!' Aleluya.

ANT. III: Leta mikono yako hapa, na uyatazame matobo niliyotobolewa kwa misumari. Usiwe na shaka tena, bali uamini, aleluya.

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Leta mikono yako hapa, na uyatazame matobo niliyotobolewa kwa misumari. Usiwe na shaka tena, bali uamini, aleluya.

SOMO: Ef.2:19-22
Ninyi si wageni tena, wala si watu wa nje; ninyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu. Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi. Yeye ndiye mwenye kulitegemeza jengo lote, na kulikuza hata liwe hekalu takatifu kwa ajili ya Bwana. Katika kuungana naye, ninyi pia mnajengwa pamoja na wote Wengine, muwe makao ya Mungu kwa njia ya Roho wake.

KIITIKIZANO
K. Utawafanya wawe watawala katika nchi zote. (W. Warudie)
K. Jina lako, Bwana, litakumbukwa.
W. Katika nchi zote.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utawafanya...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Toma, unaamini kwa kuwa umeniona. Heri yao wale ambao hawajaona, lakini wameamini.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Toma, unaamini kwa kuwa umeniona. Heri yao wale ambao hawajaona, lakini wameamini.

MAOMBI
Kwa kuwa tumepokea kutoka kwa mitume urithi wetu wa mbinguni, tumshukuru Baba yetu kwa baraka zake zote.
W. Bwana, mitume waimba sifa zako.

Usifiwe, Bwana Mungu, kwa kutuzawadisha mwili na damu ya Kristo kwa njia ya mitume,
- ili tupate nguvu na uzima; (W.)

Kwa ajili ya neno lako, lililotangazwa na mitume,
- ili kutupatia mwanga na furaha; (W.)

Kwa ajili ya Kanisa takatifu, lililojengwa juu ya Mitume,
- ili kutufanya sisi sote tuwe mwili mmoja; (W.)

Kwa ajili ya utakaso tuupatao kwa njia ya ubatizo na kitubio, sakramenti walizokabidhiwa mitume,
- ili kuondoa dhambi mioyoni mwetu; (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Baba, adhimisho letu la sikukuu ya Mtakatifu Toma mtume litupatie daima msaada na ulinzi wake. Utujalie uzima wako kutokana na imani yetu kwa Mwanao, Yesu, ambaye Toma alimkiri kuwa ni Bwana na Mungu wake. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.