Generic placeholder image

Julai, 11

MT. BENEDIKT ABATE
ALHAMISI JUMA LA 14 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina (Aleluya).

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Mtu ye yote akilitii neno la Kristo, upendo wa Mungu hukamilika ndani yake (aleluya).

Adhuhuri
Ant.: Mtu anayefanya atakavyo Baba yangu aliye mbinguni, ataingia katika ufalme wa mbinguni (aleluya).

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Wewe peke yako, Mungu, umeviona vitu ambavyo umewatayarishia wale wanaokutumainia (aleluya).

Zab.119:65-72 IX Umuhimu wa sheria ya Mungu
Umenitendea vema mimi mtumishi wako,*
kama ulivyoahidi, Ee Mungu.

Unipe hekima na maarifa,*
maana nina imani na amri zako.

Kabla ya kuniadhibu nilikosa,*
lakini sasa nashika agizo lako.

Wewe ni mwema na mfadhili;*
unifundishe kanuni zako.

Wenye kiburi wanasema uwongo juu yangu,*
lakini nashika amri zako kwa moyo wote.

Watu hao hawana akili,*
lakini mimi nafurahia sheria yako.

Nimefaidika kutokana na taabu yangu,*
maana imenifanya nijifunze amri zako.

Sheria uliyoweka ni muhimu zaidi kwangu*
kuliko mali zote za dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.56:1-6,8-13 Kumtumainia Mungu
Kristo ameoneshwa akiteseka (Mt. Jeromu)

Ee Mungu, unionee huruma,/
maana watu wananivamia.*
Wakati wote adui zangu wanizingira.

Mchana kutwa adui zangu wanishambulia;*
ni wengi mno hao wanaonipiga vita.

Ee Mungu, hofu inaponishika,*
mimi nakutumainia wewe.

Namtumainia Mungu, wala siogopi./
Ninamsifu kwa ajili ya ahadi yake.*
Binadamu watanifanya nini?

Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu;*
mawazo yao yote ni ya kunidhuru.

Wanakutana kupanga na kunivizia;/
wanachunguza yote nifanyayo;*
wananiotea kwa shabaha ya kuniua.

Ee Mungu, uwalipe kwa kadiri ya uovu wao,*
uwaangushe hao waovu kwa hasira yako.

Wewe wakujua kutangatanga kwangu;/.
umeweka kumbukumbu ya machozi yangu.*
Je, yote si yamo kitabuni mwako?

Kila mara ninapokuomba msaada wako,/
adui zangu wanarudishwa nyuma.*
Najua kwa hakika: Mungu yuko upande wangu.

Sheria uliyoweka ni muhimu zaidi kwangu*
kuliko mali zote za dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.57 Kuomba msaada
Zaburi hii yaeleza mateso ya Bwana (Mt. Augustino)

Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,*
kwako ninakimbilia usalama.

Kivulini mwa mabawa yako, napata usalama,*
hata hapo dhoruba kali itakapopita.

Namlilia Mungu Mkuu,*
Mungu anijaliaye kila kitu.

Atanisikiliza kutoka mbinguni na kuniokoa;/
atawashinda hao wenye kunidhulumu.*
Mungu atanionesha mapendo na uaminifu wake.

Adui wanizunguka kama simba wala watu;/
meno yao ni kama mikuki na mishale,*
ndimi zao ni kama panga kali.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu,*
utukufu wako uenee duniani kote.

Adui wamenitegea wavu waninase,*
nami nasononeka kwa huzuni.

wamenichimbia shimo njiani,*
lakini wao wenyewe wametumbukia humo.

Niko imara, Ee Mungu, niko imara;*
nitaimba na kukushangilia!

Amka, ee nafsi yangu!/
Amkeni, enyi zeze na kinubi!*
Nitayaamsha mapambazuko!

Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa;*
nitakuimbia sifa kati ya watu.

Upendo wako mkuu waenea hata mbinguni,*
uaminifu wako wafika hata mawinguni.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu;/
utukufu wako uenee duniani kote.*
Kinanda na kinubi, amkeni, nitaiamsha alfajiri.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Mtu ye yote akilitii neno la Kristo, upendo wa Mungu hukamilika ndani yake (aleluya).

Adhuhuri
Ant.: Mtu anayefanya atakavyo Baba yangu aliye mbinguni, ataingia katika ufalme wa mbinguni (aleluya).

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Wewe peke yako, Mungu, umeviona vitu ambavyo umewatayarishia wale wanaokutumainia (aleluya).

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Gal.6:8
Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uzima wa milele.

K. Bwana huwaongoza wanyenyekevu katika njia inayohusika (aleluya).
W. Huwafundisha maskini njia yake (aleluya).

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: 1Kor.9:26
Ndivyo, basi, ninavyopiga mbio nikiwa na nia ya kushinda; ndivyo ninavyopigana, na si kama bondia anayetupa ngumi zake hewani. Naupa mwili mazoezi magumu, na kuutia katika nidhamu kamili.

K. Bwana, ana heri mtu unayemfunza (aleluya).
W. Unamfundisha kwa sheria yako (aleluya).

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Filp.4:8,9
Ndugu zangu, jazeni fikra zenu kwa mambo mema na yanayostahili kusifiwa; mambo ya kweli, bora, ya haki, safi, ya kupendeza na ya heshima. Naye Mungu anayetujalia amani atakuwa pamoja nanyi.

K. Wale wanaokutumaini, na washangilie (aleluya).
W. Watafurahi milele; nawe utakaa kati yao (aleluya).

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, ulimteua Mtakatifu Benedikt awe mwalimu mwenye hekima wa wale waliotaka kujifunza kukutumikia. Utujalie tukupende wewe zaidi ya yote, na hivi tuzifuate amri zako kwa furaha. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.