Generic placeholder image

Julai, 11

MT. BENEDIKT ABATE
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya

UTENZI
Kw'ajili ya watakatifu wote
Wanaopumzika kisha kazi,
Ambao walikuungama wewe
Kwa imani mbele ya walimwengu,
Jina lako, E Yesu, litukuzwe
Milele. Aleluya! Aleluya!

Wewe ulikuwa ndo mwamba wao,
Ngome yao na pia nguvu yao;
Ulikuwa ndo kapiteni wao
Katika vita walivyofaulu;
Katika giza la huzuni, Bwana,
Ulikuwa Nuru yao ya kweli,
Angavu. Aleluya! Aleluya!

Laiti nao askari wako,
Waaminifu, wa kweli, shujaa,
Wangepiga vita kwa uungwana
Kama watakatifu wa zamani,
Na kupata, pamoja nao, taji,
Taji ya dhahabu ndo ya ushindi!
Fanaka! Aleluya! Aleluya!

Ee mwungano ulobarikiwa!
Ee ushirika mtakatifu!
Twapiga vita sawa kama wao,
Ndo chini ya ishara takatifu;
Katika wewe wote ni umoja,
Maana wote kabisa ni wako;
Umoja! Aleluya! Aleluya!

ANT. I: Mtu huyu alionekana hana hatia na ni mwaminifu; utukufu wa milele utakuwa wake (aleluya).

Zab.15 Rafiki ya Mungu
Ee Mungu, nani awezaye kukaa hemani mwako?*
Nani awezaye kukaa juu ya mlima wako mtakatifu?

Ni mtu anayeishi bila hatia,*
atendaye daima yaliyo sawa,

asemaye ukweli kutoka moyoni,*
na ambaye hasengenyi watu.

Ni mtu ambaye hamtendei ubaya mwenzake,*
wala hamfitini jirani yake.

Mtu huyo huwadharau wafisadi,/
lakini huwaheshimu wamchao Mungu.*
Hutimiza ahadi yake hata kama ikimtia hasara.

Hukopesha bila kutaka faida,/
wala hali rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia.*
Mtu mwenye sifa hizo, atakuwa imara milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Mtu huyu alionekana hana hatia na ni mwaminifu; utukufu wa milele utakuwa wake (aleluya).

ANT. II: Neema na huruma huwangojea wateule wa Mungu; Mungu huja kulisaidia taifa lake takatifu (aleluya).

Zab.112 Furaha ya mtu mwema
Heri mtu anayemcha Mungu,*
anayefurahia sana kutii amri zake.

Watoto wake watakuwa wenye enzi duniani;*
wazao wake watabarikiwa.

Jamaa yake itakuwa tajiri,*
naye atakuwa na fanaka daima.

Watu wema huangaziwa mwanga wa furaha,/
kama vile taa iangazayo gizani;*
naam, watu wenye huruma, wapole na waadilifu.

Heri mtu mkarimu, akopeshaye bila faida;*
aendeshaye shughuli zake kwa kutumia haki.

Mwadilifu hatashindwa kamwe,*
na atakumbukwa daima.

Akipata habari mbaya haogopi;*
moyo wake ni thabiti na humtumainia Mungu.

Hana wasiwasi, wala haogopi nyoka;*
ana hakika adui zake watashindwa.

Huwapa maskini kwa ukarimu;/
wema wake haubadiliki.*
Mtu wa namna hiyo atasifika daima.

Waovu huona hayo na kuudhika;/
husaga meno kwa chuki na kutoweka,*
mambo huenda kinyume cha matazamio yao.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Neema na huruma huwangojea wateule wa Mungu; Mungu huja kulisaidia taifa lake takatifu (aleluya).

ANT. III: Watakatifu wataimba wimbo mpya, mbele ya kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo; sauti zao zitaujaza ulimwengu mzima (aleluya).

WIMBO: Ufu.15:3-4
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!

Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!

Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako?*
Wewe peke yako ni Mtakatifu.

Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Watakatifu wataimba wimbo mpya, mbele ya kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo; sauti zao zitaujaza ulimwengu mzima (aleluya).

SOMO: Rom.8:28-30
Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kufuatana na kusudi lake. Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Basi, Mungu aliwaita wale aliokuwa amewateua; na hao aliowaita, aliwafanya pia wawe na uhusiano mwema naye; na hao aliowafanya wawe na uhusiano mwema naye, aliwashirikisha pia utukufu wake.

KIITIKIZANO
K. Bwana ni mwema; huyapenda matendo mema. (W. Warudie)
K. Uso wake ameuelekeza kwa mtu mwadilifu.
W. Huyapenda matendo mema.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Amebarikiwa na Bwana, na amezawadishwa na Mungu, mwokozi wake. Ndivyo wanavyokuwa wale wamtafutao Bwana.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Amebarikiwa na Bwana, na amezawadishwa na Mungu, mwokozi wake. Ndivyo wanavyokuwa wale wamtafutao Bwana.

MAOMBI
Tumwombe Baba atuongoze kwenye utakatifu, kwa maombezi na mfano wa watakatifu.
W. Utufanye tuwe watakatifu, kama wewe ulivyo mtakatifu.

Baba, ulitaka sisi tuitwe watoto wako, na ndivyo tulivyo.
- Uliwezeshe Kanisa lako duniani kote kuushuhudia uzuri wako. (W.)

Baba, umetupa mwito tutembee katika mwanga wako, na kila mara tufanye yale yanayokupendeza;
- maisha yetu yawe na utajiri wa kila kazi njema. (W.)

Baba, kwa njia ya Kristo umetupatanisha nawe;
- utudumishe katika kuliungama jina lako, ili sote tuweze kuwa na umoja. (W.)

Baba, umetualika kwenye sikukuu ya uzima wa milele;
- utufanye tuwe wakamilifu katika upendo wako, kwa njia ya mkate utokao mbinguni. (W.)

Baba, uwajalie wakosefu wote amani na msamaha;
- uwaruhusu marehemu kuishi katika mwanga wa uwepo wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, ulimteua Mtakatifu Benedikt awe mwalimu mwenye hekima wa wale waliotaka kujifunza kukutumikia. Utujalie tukupende wewe zaidi ya yote, na hivi tuzifuate amri zako kwa furaha. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.