22 Julai

MT. MARIA MAGDALENA
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Yn.20:17
Yesu akamwambia Maria Magdalena, Enenda kwa ndugu zangu, ukawaambie: Ninapaa kwenda kwa Baba yangu, naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.

KOLEKTA:
Ee Mungu, Mwanao pekee alimjalia mtakatiu Maria Magdalena kuwa wa kwanza kutangaza furaha ya Pasaka. Tunaomba utujalie kwa maombezi na mfano wake tumtangaze Kristo aliye hai, na tumwone akitawala katika utukufu wako. Anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Wim.3:1-4
Usiku kitandani nalimtafuta mpendwa wa nafsi yangu, Nalimtafuta, nisimpate. Nikasema, Haya, niondoke nizunguke mjini, Katika njia zake na viwanjani, Nimtafute mpendwa wa nafsi yangu. Nikamtafuta, nisimpate. Walinzi wazungukao mjini waliniona; Je, mmemwona mpendwa wa nafsi yangu? Kitambo kidogo tu nikiisha kuwaondokea, Nikamwona mpendwa wa nafsi yangu.

Au, la kuchagua
2Kor.5:14-17

Upendo wa Kristo watubidisha; maana tumeukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote; tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao. Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena. Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! yamekuwa mapya.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.63:1-5,7-8(K)1
1. Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea kiu,
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.

(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.

2. Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai;
Midomo yangu itakusifu. (K)

3. Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai;
Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai
kama kushiba mafuta na vinono;
Kinywa changu kitakusifu
kwa midomo ya furaha. (K)

4. Maana wewe umekuwa msaada wangu,
Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
Nafsi yangu inakuandama sana;
Mkono wako wa kuume unanitegemeza. (K)

SHANGILIO: Yn.15:16
Aleluya, aleluya!
Maria tuambie: sema uliyoona njiani. Kaburi lilimfadhi Yule aliye Mzima; Niliona utukufu wa Kristo alipokuwa akifufuka.
Aleluya!

INJILI: Yn.20:1-2,11-18
Siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, hakafika kwa Simoni Petro na kwa Yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, Mama unalilia nini? Akawaambia, kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka, Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa. Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia: Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, upokee vipaji tunavyokutolea katika sikukuu ya mtakatifu Maria Magdalena, ambaye upendo wake ulipokelewa na Mwanao pekee kama zawadi yenye thamani kubwa. Anayeishi na kutawala milele na milele.

UTANGULIZI: Maria Magdalena mtume wa Mitume.
K.
Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukutangaze daima Wewe, Baba mwenyezi, ambaye huruma yako siyo ndogo kuliko uwezo, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye ndiye aliyejidhihirisha bustanini kwa Maria Magdalena, yule ambaye alimpenda alipokuwa hai, akamwona alipokufa msalabani, na kumtafuta alipokuwa amelala kaburini, na akawa wa kwanza kumwabudu baada ya kufufuka katika wafu, naye ndiye aliyempa heshima ya jukumu la kuwa mtume mbele ya mitume ili habari njema ya uzima mpya ifike hadi mipaka ya dunia.
Kwa hiyo, ee Bwana, sisi nasi pamoja na Malaika na Watakatifu wote, tunakusifu, tukisema kwa shangwe:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: 2Kor.5:14,15
Upendo wa Kristo watubidisha, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti yako takatifu tuliyopokea itujaze ule upendo wa kudumu, ambao kwao mtakatifu Maria Magdalena aliambatana bila kukoma na Kristo, mwalimu wake. Anayeishi na Kutawala milele na milele.