Generic placeholder image

Julai, 22

MT. MARIA MAGDALENA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Jinsi Mungu alivyo wa ajabu miongoni mwa watakatifu wake! Njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.) Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Kristo alikufa,
Kafufuka, aleluya;
Na kumbe hata mauti,
Kayachinja, aleluya.
Magdalena mcheshi
Haya sema, aleluya,
Uliona nini pale
Penye njia? aleluya,
Aleluya, aleluya.

"Nililiona kaburi
La mpenzi, aleluya;
Na mwenyewe nilimwona,
'Kamwabudu, aleluya.
Niliona kitambaa
Pia sanda, aleluya,
Vilofunga kichwa chake
Na miguu, aleluya;
Aleluya, aleluya.

"Walitoa malaika,
Ushahidi, aleluya,
'Yesu amesha fufuka,
Kaondoka, aleluya;
Kawambie wafuasi
Watamwona, aleluya,
Kweli Yeye watamwona
Galilaya, aleluya."
Aleluya, aleluya.

ANT. I: Jumapili asubuhi sana, mara tu baada ya jua kuchomoza, Maria Magdalena alifika kaburini.

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua maikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Jumapili asubuhi sana, mara tu baada ya jua kuchomoza, Maria Magdalena alifika kaburini.

ANT. II: Moyo wangu unawaka; natamani kumwona Bwana wangu; namtafuta, lakini sijui walikomweka, aleluya.

WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

ANT. II: Moyo wangu unawaka; natamani kumwona Bwana wangu; namtafuta, lakini sijui walikomweka, aleluya.

ANT. III: Maria, huku analia, alichungulia ndani ya kaburi; akawaona malaika wawili, wamevaa mavazi meupe, aleluya.

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Maria, huku analia, alichungulia ndani ya kaburi; akawaona malaika wawili, wamevaa mavazi meupe, aleluya.

SOMO: Rom.12:1-2
Ndugu zangu, maadam Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: jitoleeni nafsi zenu kwa Mungu kama sadaka iliyo hai, takatifu na yenye kumpendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu. Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikra zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu, kutambua jambo hilo jema linalompendeza na kamilifu.

KIITIKIZANO
K. Maria, usilie; Bwana amefufuka kutoka wafu. (W. Warudie)
K. Nenda kwa ndugu zangu, ukawaambie.
W. Bwana amefufuka kutoka wafu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Maria...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Baada ya kufufuka kutoka wafu Jumapili asubuhi sana, Yesu alimtokea kwanza Maria Magdalena, ambaye kabla yake alikuwa amemtoa pepo saba.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Baada ya kufufuka kutoka wafu Jumapili asubuhi sana, Yesu alimtokea kwanza Maria Magdalena, ambaye kabla yake alikuwa amemtoa pepo saba.

MAOMBI
Pamoja na wanawake watakatifu wote, tumtukuze Mwokozi wetu, na tumwombe tukisema:
W. Njoo, Bwana Yesu.

Bwana Yesu, juu ya yule mwanamke mkosefu ulisema: 'Amesamehewa dhambi zake nyingi, kwa sababu ameonesha upendo mkubwa';
- utusamehe dhambi zetu, ambazo ni nyingi. (W.)

Bwana Yesu, wanawake walikupatia mahitaji yako katika safari zako;
- uyafungue macho yetu, ili tukuone wewe katika wale wanaohitaji msaada wetu. (W.)

Bwana na mwalimu, Maria alisikiliza mafundisho yako, na Marta alitumikia;
- utujalie, imani yetu ikue zaidi na zaidi, na mapendo yetu yawafikie wengine. (W.)

Bwana Yesu, wale wanaotekeleza matakwa ya Mungu, ndio kaka, dada na mama yako;
- utufundishe namna ya kuishi iwapasavyo watu wa familia yako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, Mwanao wa pekee, Yesu Kristo, alimfanya Maria Magdalena awe wa kwanza kutangaza furaha ya Pasaka. Utujalie, tukifuata mfano wake na kwa maombezi yake, tuweze kumtangaza, katika maisha haya, Kristo aliye hai, na hatimaye tupate kumwona akitawala nawe katika utukufu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.