Generic placeholder image

Julai, 22

MT. MARIA MAGDALENA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Kristo alikufa,
Kafufuka, aleluya;
Na kumbe hata mauti,
Kayachinja, aleluya.
Magdalena mcheshi
Haya sema, aleluya,
Uliona nini pale
Penye njia? aleluya,
Aleluya, aleluya.

"Nililiona kaburi
La mpenzi, aleluya;
Na mwenyewe nilimwona,
'Kamwabudu, aleluya.
Niliona kitambaa
Pia sanda, aleluya,
Vilofunga kichwa chake
Na miguu, aleluya;
Aleluya, aleluya.

"Walitoa malaika,
Ushahidi, aleluya,
'Yesu amesha fufuka,
Kaondoka, aleluya;
Kawambie wafuasi
Watamwona, aleluya,
Kweli Yeye watamwona
Galilaya, aleluya."
Aleluya, aleluya.

ANT. I: Yesu akamwuliza Maria, 'Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?'

Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Nilifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu.“

Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!

Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!

Humo ndimo makabila yanafika,/.
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.

Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.

Uombeeni Yerusalemu amani;*
“Wote wakupendao wafanikiwe!

Ukumbini mwako kuwe na amani,*
majumbani mwako kuweko usalama!“

Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
Ee Yerusalemu, nakutakia amani!

Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
ninakuombea upate fanaka!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Yesu akamwuliza Maria, 'Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?'

ANT. II: Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!

Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.

Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.

Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu.*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?

Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!

Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.

Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!

ANT. III: Yesu akamwambia, 'Maria!' Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, 'Rabboni!' yaani, Mwalimu!

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo

ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Yesu akamwambia, 'Maria!' Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, 'Rabboni!' yaani, Mwalimu!

SOMO: Rom.8:28-30
Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kufuatana na kusudi lake. Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Basi, Mungu aliwaita wale aliokuwa amewateua; na hao aliowaita, aliwafanya pia wawe na uhusiano mwema naye; na hao aliowafanya wawe na uhusiano mwema naye, aliwashirikisha pia utukufu wake.

KIITIKIZANO
K. Maria, usilie; Bwana amefufuka kutoka wafu. (W. Warudie)
K. Nenda kwa ndugu zangu, ukawaambie.
W. Bwana amefufuka kutoka wafu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Maria...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Maria aliwaendea wanafunzi, akawaambia kwamba alikuwa amemwona Bwana, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Maria aliwaendea wanafunzi, akawaambia kwamba alikuwa amemwona Bwana, aleluya.

MAOMBI
Pamoja na wanawake watakatifu wote, tumtukuze Mwokozi wetu, na tumwombe tukisema:
W. Njoo, Bwana Yesu.

Bwana Yesu, juu ya yule mwanamke mkosefu ulisema: 'Amesamehewa dhambi zake nyingi, kwa sababu ameonesha upendo mkubwa';
- utusamehe dhambi zetu, ambazo ni nyingi. (W.)

Bwana Yesu, wanawake walikupatia mahitaji yako katika safari zako;
- uyafungue macho yetu, ili tukuone wewe katika wale wanaohitaji msaada wetu. (W.)

Bwana na mwalimu, Maria alisikiliza mafundisho yako, na Marta alitumikia;
- utujalie, imani yetu ikue zaidi na zaidi, na mapendo yetu yawafikie wengine. (W.)

Bwana Yesu, wale wanaotekeleza matakwa ya Mungu, ndio kaka, dada na mama yako;
- utufundishe namna ya kuishi iwapasavyo watu wa familia yako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, Mwanao wa pekee, Yesu Kristo, alimfanya Maria Magdalena awe wa kwanza kutangaza furaha ya Pasaka. Utujalie, tukifuata mfano wake na kwa maombezi yake, tuweze kumtangaza, katika maisha haya, Kristo aliye hai, na hatimaye tupate kumwona akitawala nawe katika utukufu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.