Generic placeholder image

Julai, 22

MT. MARIA MAGDALENA
JUMATATU JUMA LA 16 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

Ee Mungu hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

ANT. I: Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako.

Zab.119:129-136 XVII Fikara juu ya neno la Mungu katika Torati
Kwa mapendo Sheria yote hutimizwa (Rom.13:10)

Mafundisho yako ni ya ajabu;*
kwa hiyo nayashika kwa moyo wote.

Maelezo ya mafundisho yako huleta mwanga;*
huwapa ufahamu wasiojua kitu.

Kinywa wazi ninahema,*
maana ninayo hamu ya amri zako.

Unigeukie na kunionea huruma,*
kama uwafanyiavyo wanaokupenda.

Uniimarishe kama ulivyoahidi;*
usikubali mimi nitawaliwe na uovu.

Uniokoe na udhalimu wa binadamu,*
ili nipate kuzishika kanuni zako.

Kuwako kwako kuniangazie,*
unifundishe kanuni zako.

Macho yangu yabubujika maji kama mto,*
kwa sababu watu hawaishiki sheria yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako.

ANT. II: Yupo hakimu na mtawala mmoja tu: wewe, basi, u nani hata umhukumu jirani yako?

Zab.82 Mungu mtawala mkuu
Basi, msihukumu kabla ya wakati wake, acheni mpaka Bwana atakapokuja (1Kor.4:5)

Mungu anaongoza baraza la mbinguni;*
anatoa hukumu katika kusanyiko la miungu:

"Acheni kuhukumu bila haki!*
Acheni kuwapendelea waovu!

Wateteeni wanyonge na yatima;*
wapeni haki maskini na fukara.

Waokoeni wanyonge na maskini,*
waopoeni katika makucha ya wadhalimu.

Lakini ninyi hamfahamu, hamna akili!*
Mmeharibu misingi ya haki duniani!

Nilisema: 'Ninyi ni miungu;*
nyote ni wana wa Mungu Mkuu!'

Hata hivyo, mtakufa kama watu wengine;*
maisha yenu yatakoma kama ya mkuu yeyote.”

Uje, Ee Mungu, uuhukumu ulimwengu;*
mataifa yote ni mali yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Yupo hakimu na mtawala mmoja tu: wewe, basi, u nani hata umhukumu jirani yako?

ANT. III: Niliita; Bwana akanisikia.

Zab.120 Kuomba msaada
Muwe na saburi katika shida; salini daima. (Rom.12:12)

Nilipokuwa katika taabu,*
nilimwita Mungu, naye akanisikiliza.

Ee Mungu, uniokoe*
na watu wadanganyifu na waongo.

Enyi watu wadanganyifu,*
mtapewa kitu gani?

Mtafanyiwa kitu gani zaidi?*
Mtaadhibiwa namna gani?

Kwa mishale mikali ya askari,*
kwa makaa ya moto!

Kukaa kati yenu ni balaa kama kukaa Mesheki*
au kama kukaa kati ya watu wa Kedari.

Nimeishi muda mrefu mno*
kati ya watu wanaochukia amani!

Mimi nataka amani;/
lakini nisemapo juu ya amani,*
wao hutaka vita.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Niliita; Bwana akanisikia.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Law.20:26
Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi BWANA ni mtakatifu, nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu.

K. Heri yao watu wale ambao Bwana ndiye Mungu wao.
W. Watu aliowachagua kuwa urithi wake.

Sala tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Hek.15:1,3
Wewe, Mungu wetu, U mwenye neema na kweli, mvumilivu, na katika rehema unaratibisha mambo yote. Kukufahamu Wewe ni haki tupu, na kuujua utawala wako ni shina la kuishi milele.

K. Wewe, Bwana, ni Mungu wa upendo na huruma.
W. Una saburi, umejaa rehema na kweli.

Sala tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Bar.4:21-22
Jipeni moyo, wanangu, mlilieni Mungu, Naye atawaponya katika nguvu na mkono wa adui. Maana nimemtumainia Aliye wa Milele awaokoe, Na furaha imenijia kutoka kwake Aliye Mtakatifu. Kwa sababu ya rehema itakayowajia upesi Kutoka kwake Mwokozi wenu wa milele.

K. Ee Bwana, ikumbuke huruma yako.
W. Usisahau upendo wako wa toka zamani.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi wa milele, Mwanao wa pekee, Yesu Kristo, alimfanya Maria Magdalena awe wa kwanza kutangaza furaha ya Pasaka. Utujalie, tukifuata mfano wake na kwa maombezi yake, tuweze kumtangaza, katika maisha haya, Kristo aliye hai, na hatimaye tupate kumwona akitawala nawe katika utukufu. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.