Generic placeholder image
Julai, 25

MT. YAKOBO MTUME
ALHAMISI JUMA LA 16 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

Ee Mungu hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Nendeni, mkahubiri Habari Njema ya utawala: mlipata bure; toeni bure (aleluya).

Adhuhuri
Ant.: Nipo nanyi sikuzote, hata mwisho wa nyakati (aleluya).

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu (aleluya).

Zab.119:153-160 XX Kuomba msaada
Uangalie mateso yangu, uniokoe,*
kwa maana sikusahau sheria yako.

Unitetee na kunikomboa;*
unisalimishe kama ulivyoahidi.

Waovu hawataokolewa,*
maana hawazijali kanuni zako.

Huruma yako ni kubwa, Ee Mungu;*
Unijalie uhai kama ulivyoahidi.

Adui na wadhalimu wangu ni wengi,*
lakini mimi sikiuki maagizo yako.

Niwaonapo wahaini hao nachukizwa mno,*
kwa sababu hawazishiki amri zako.

Tazama, Ee Mungu, jinsi nizipendavyo amri zako!*
Unisalimishe kadiri ya upendo wako mkuu.

Kitovu cha sheria yako ni ukweli,*
hukumu zako za haki, zote ni za milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.128 Tuzo kwa jamaa imchayo Mungu
'Bwana akubariki kutoka Sion,' yaani kutoka Kanisa lake (Arnobius)

Heri wote wamchao Mungu,*
wanaoishi kufuatana na amri zake.

Kazi zako zitakupatia mahitaji yako,*
utaona furaha na kufanikiwa.

Mke wako atakuwa kama mzabibu*
wenye matunda mengi nyumbani mwako;

watoto wako watakuwa kama machipukizi*
ya mizeituni kuizunguka meza yako.

Naam, ndivyo atakavyobarikiwa*
mtu amchaye Mungu.

Mungu akubariki toka Sion!/
Uione fanaka ya Yerusalemu,*
siku zote za maisha yako.

Uishi na hata uwaone wajukuu wako!*
Amani iwe na Israeli!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.129 Sala dhidi ya adui za Israeli
Kanisa lasimulia mateso linayovumilia (Mt. Augustino)

Israeli anasema:/
"Mara nyingi adui wamenitesa,*
tangu ujana wangu!

Naam, wamenitesa tangu ujana wangu,*
lakini hawakuweza kunishinda.

Walinikatakata mgongoni mwangu,*
waliufanya kama shamba lililolimwa.

Lakini Mungu ni mwadilifu;*
amezikata kamba za hao waovu.“

Waaibishwe na kushindwa kabisa*.
wote wale wauchukiao mji wa Sion.

Wote wafanane na nyasi juu ya paa la nyumba,*
ambazo hunyauka kabla hazijakua;

hakuna anayejishughulisha kuzikusanya,*
wala kuzichukua kama matita.

Hakuna apitaye karibu atakayewaambia:/
"Mungu awabariki!*
Twawabariki kwa jina la Mungu.“

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Nendeni, mkahubiri Habari Njema ya utawala: mlipata bure; toeni bure (aleluya).

Adhuhuri
Ant.: Nipo nanyi sikuzote, hata mwisho wa nyakati (aleluya).

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu (aleluya).

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 2Kor.5:19b-20
Mungu ametupatia ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye. Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, patanishweni na Mungu.

K. Sauti yao imeenea duniani kote (aleluya).
W. Ujumbe wao umesikika kote ulimwenguni (aleluya.)

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Mate.5:12a,14
Mitume walifanya miujiza na maajabu mengi kati ya watu. Idadi ya watu waliomwamini Bwana, waume kwa wake, iliongezeka zaidi na zaidi.

K. Walifuata maagizo ya Mungu (aleluya).
W. Walishika amri zake (aleluya).

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Mate.5:41-42
Mitume wakatoka nje ya ule mkutano wa halmashauri, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu walistahili kuaibishwa kwa sababu ya jina la Yesu. Wakaendelea kila siku kufundisha na kuhubiri Habari Njema ya Kristo.

K. Furahini na shangilieni, Bwana alisema (aleluya).
W. Kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni (aleluya).

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, uliipokea sadaka ya Mtakatifu Yakobo, wa kwanza miongoni mwa mitume wako kuutoa uhai wake kwa ajili yako. Ulijalie Kanisa lako lipate nguvu kwa kifo chake, na litegemezwe na sala zake za daima. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.