Generic placeholder image
Julai, 25

MT. YAKOBO MTUME
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina, aleluya.

UTENZI
Wote walo duniani
Wapaze zao sauti
Wakimuimbia sifa
Za ushindi za mbinguni
Yeye alowapatia
Mitume wake neema
Ya kupiga mbio zao
Tukufu ulimwenguni.

Kwalo neno lako wewe
Waliichukua nuru
Ya ukweli wa injili
Hadi kwenye upagani;
Utupatie na sisi
Nuru hiyo ya mbinguni
Macho yetu yafurahi
Na nyoyo zichangamke.

Kwa matakwa yako wewe
Uwezo walijaliwa
Wa kufunga, kufungua
Duniani na mbinguni;
Fungua nyororo zetu,
Twondolee dhambi zetu,
Katika mioyo yetu
Tia upya ne'ma yako.

Na kwa nguvu yako wewe
Walilitamka neno
Lililoponya magonjwa
Na afiya kurudisha;
Endeleza kwetu huo
Uwezowe wa kuponya,
Saidia wadhaifu
Imarisha wenye nguvu.

ANT. I: Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika.

Zab.116:10-19 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Nilizidi kuamini hata niliposema:*
"Mimi naangamia.".

Hata niliposema kwa hofu,*
"Binadamu hawaaminiki."

Nimrudishie Mungu nini,*
kwa mema yote aliyonitendea?

Nitamtolea Mungu dhabihu ya kinywaji,*
nimheshimu kwa shukrani.

Nitamtimizia Mungu nadhiri zangu,*
mbele ya taifa lake lote.

Mungu huthamini kifo cha waaminifu wake.*
Ee Mungu, mimi ni mtumishi wako;

ni mtumishi wako kama alivyokuwa mama yangu,*
umeniweka huru.

Nitakutolea sadaka za shukrani,*
na kukupa heshima zangu.

Mbele ya taifa lako lote,/
ukumbini mwa Hekalu lako huko Yerusalemu,*
nitakutimizia yale niliyoahidi, Ee Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika.

ANT. II: Kisha akawaambia, 'Kesheni na kusali, ili msije mkaingia katika majaribu."

Zab.126 Kuomba nguvu mpya
Mungu alipoturudisha tena Sion,*
tulikuwa kama wanaoota ndoto!

Hapo tuliangua kicheko;*
tulishangilia kwa furaha.

Nao watu wa mataifa mengine walisema:*
“Mungu amewatendea mambo makubwa!”

Kweli Mungu alitutendea maajabu,*
tulifurahi kweli kweli!

Ee Mungu, urekebishe tena hali yetu/
kama mvua inavyotiririsha maji*
katika mabonde makavu.

Wanaopanda kwa machozi*
watavuna kwa shangwe;

wanaokwenda kupanda mbegu huku wakilia,*
watarudi kwa furaha huku wakichukua mavuno.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Kisha akawaambia, 'Kesheni na kusali, ili msije mkaingia katika majaribu."

ANT. III: Herode alianza kuwatesa baadhi ya Wakristo. Alimwua kwa upanga Yakobo, ndugu yake Yohane.

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake

katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Herode alianza kuwatesa baadhi ya Wakristo. Alimwua kwa upanga Yakobo, ndugu yake Yohane.

SOMO: Ef.4:11-13
Kristo ndiye aliyewapa watu zawadi: wengine aliwajalia wawe mitume, wengine manabii, wengine wawe waeneza injili, wengine wachungaji na walimu. Alifanya hivyo apate kuwatayarisha watu wote wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma ya Kikristo, ili kuujenga mwili wa Kristo, na hivyo sote tuufikie umoja wa imani, na kumjua Mwana wa Mungu; tuwe watu waliokomaa na kuufikia utimilifu wake Kristo mwenyewe.

KIITIKIZANO
K. Utangazeni utukufu wa Bwana kwa mataifa. (W. Warudie)
K. Simulieni maajabu yake kwa watu wote.
W. Yatangazeni kwa mataifa.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utangazeni...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Ye yote anayetaka kuwa mkuu kati yenu, lazima awe mtumishi wenu. Ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu, lazima awe mtumishi wa wote.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Ye yote anayetaka kuwa mkuu kati yenu, lazima awe mtumishi wenu. Ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu, lazima awe mtumishi wa wote.

MAOMBI
Kwa kuwa sisi ni sehemu ya jengo ambalo mitume ndio msingi wake, tumwombe Baba kwa ajili ya taifa lake.
W. Bwana, ulikumbuke Kanisa lako.

Baba, Mwanao alipofufuka kutoka wafu, ulimwonesha kwanza kwa mitume;
- utuwezeshe kumtangaza Mwanao kila mahali. (W.)

Ulimtuma Mwanao ulimwenguni apate kuwatangazia maskini habari njema;
- utujalie tuweze kuifikisha injili yake kwenye giza la maisha ya watu. (W.)

Ulimtuma Mwanao kupanda mioyoni mwa watu mbegu ya uzima usioharibika;
- utuwezeshe kupanda neno lake, na kuvuna furaha. (W.)

Ulimtuma Mwanao kuupatanisha ulimwengu nawe kwa kumwaga damu yake;
- utujalie tupate kushirikiana naye, katika kuurudisha urafiki kati yako na binadamu. (W.)

Ulimketisha Mwanao mkono wako wa kuume huko mbinguni;
- uwapokee marehemu, na kuwaingiza katika furaha ya utawala wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, uliipokea sadaka ya Mtakatifu Yakobo, wa kwanza miongoni mwa mitume wako kuutoa uhai wake kwa ajili yako. Ulijalie Kanisa lako lipate nguvu kwa kifo chake, na litegemezwe na sala zake za daima. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.