Generic placeholder image

Julai, 26

WAT. YOAKIM NA ANNA
Wazazi wa Bikira Maria
IJUMAA JUMA LA 16 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bwana Mungu, shukrani twakupa
Kwa ajili ya watakatifu wako
Walofuata nyayo za miguu -
Nyayo zako zisizofuatika,
Waloushika mikononi mwao
Mkono wako usoonekana,
Na walioisikia sauti
Ile ilokuwa kimya kabisa.

Ewe Utatu Mtukufu sana
Milele usifiwe bila mwisho
Kwa ajili ya wote waloishi
Wakikunyenyekea wewe hivyo;
Watakatifu wako walopita
Vijia vyenye giza kwa imani
Sasa ndo wanashiriki furaha
Ya mwanga wako usiofifia.

ANT. I: Nitakutukuza siku zote, Ee Bwana, na nitasimulia matendo yako ya ajabu.

Zab.145 Wimbo wa kumsifu Mungu
Ewe Mtakatifu, Uliyeko na Uliyekuwako! Wewe ni mwenye haki (Ufu.16:5)

I
Nitakutukuza, Ee Mungu wangu na mfalme wangu;*
nitalitukuza jina lako daima na milele.

Nitakushukuru kila siku;*
nitalisifu jina lako daima na milele.

Mungu ni mkuu, astahili kusifiwa sana;*
ukuu wake hauwezi kuelezeka.

Matendo yako yatatukuzwa kizazi hata kizazi,*
watu watatangaza matendo yako ya enzi.

Watanena juu ya utukufu na fahari yako,*
nami nitatafakari matendo yako ya ajabu.

Watu watanena juu ya matendo yako ya kutisha,*
nami nitatangaza ukuu wako.

Watatangaza sifa za wema wako mwingi,*
na kuimba juu ya uadilifu wako.

Mungu ni mwema na mwenye huruma,*
hakasiriki ovyo, amejaa upendo mkuu.

Mungu ni mwema kwa wote,*
ni mwenye huruma kwa viumbe vyake vyote.

Ee Mungu, viumbe vyote vitakushukuru,*
nao waaminifu wako watakutukuza.

Watanena juu ya utukufu wa utawala wako,*
na kutangaza juu ya enzi yako kuu,

ili kila mtu ajue matendo yako makuu,*
na fahari tukufu ya utawala wako.

Utawala wako ni utawala wa milele;*
mamlaka yako yadumu vizazi vyote.

Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake zote,*
na kila kitu afanyacho ni chema.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nitakutukuza siku zote, Ee Bwana, na nitasimulia matendo yako ya ajabu.

ANT. II: Macho ya watu wote yakuelekea wewe, Bwana; u karibu na wote wanaokuita.

II
Mungu huwategemeza wote waangukao;*
huwainua wote waliokandamizwa.

Viumbe vyote vyakungojea kwa hamu,*
nawe wavipatia chakula chao kwa wakati wake.

Waufumbua mkono wako,*
na kwa ukarimu washibisha viumbe vyote.

Mungu ni mwenye haki katika njia zake zote;*
ni mwema katika matendo yake yote.

Mungu yuko karibu nao wote wamwitao,*
wote wale wanaomwita kwa moyo mnyofu.

Mungu huwapatia mahitaji yao wale wamchao;*
husikiliza kilio chao na kuwaokoa.

Mungu huwalinda wote wampendao;*
lakini atawaangamiza waovu wote.

Nitatangaza sifa za Mungu;/
viumbe vyote vilisifu jina lake takatifu,*
sasa na hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Macho ya watu wote yakuelekea wewe, Bwana; u karibu na wote wanaokuita.

ANT. III: Njia zako ni za kweli na za haki, Ee Mfalme wa milele.

WIMBO: Ufu.15:3-4 Utenzi Wa sifa
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!

Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!

Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako? *
Wewe peke yako ni Mtakatifu.

Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Njia zako ni za kweli na za haki, Ee Mfalme wa milele.

SOMO: Rom.9:4-5
Hao ndio watu wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu wake; aliagana nao, akawapa Sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake. Wao ni wajukuu wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina.

KIITIKIZANO
K. Amekuja kumsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake. (W. Warudie)
K. Kama alivyowaahidia wazee wetu.
W. Akikumbuka huruma yake.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Amekuja...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Tawi lilichipuka katika shina azizi la Yese; na ua zuri, lenye kunukia, likachanua katika tawi hilo.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Tawi lilichipuka katika shina azizi la Yese; na ua zuri, lenye kunukia, likachanua katika tawi hilo.

MAOMBI
Mungu alitufunulia upendo wake alipomtuma Mwanae wa pekee duniani, ili katika Mwana huyo tuwe na uzima. Tunaweza kumpenda Mungu kwa sababu yeye ametangulia kutupenda. Tuombe:
W. Bwana, utuwezeshe kukupenda wewe, na kupendana sisi kwa sisi.

Yesu alimsamehe dhambi yule mwanamke aliyetubu, kwa sababu huyo mwanamke alionesha upendo mwingi:
- utujalie tukupende kwa moyo wote, ili tupate kuponywa kwa nguvu zake Kristo. (W.)

Unawahurumia wapole na wanyenyekevu wa moyo:
- kwa wema wako, uielekeze mioyo yetu kwako, na utusaidie tuweze kutenda yaliyo mema. (W.)

Tunakiri kwamba tumesababisha madhara kwa wengine:
- twakuomba msamaha kwa uzembe wetu, na kutojali kwetu. (W.)

Tunaomba uwakumbuke jioni hii wale walio katika matatizo makubwa:
- uwajalie moyo mpya wale waliopoteza imani yao kwa watu na kwako wewe Mungu, na wale ambao wanautafuta ukweli lakini hawaupati. (W.)

Uwakumbuke wale wote waliokutumainia walipokuwa hai:
- kwa mateso na kifo cha Mwanao, uwajalie maondoleo ya dhambi zao zote. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, Mungu wa baba zetu, uliwajalia Watakatitifu Yoakim na Ana neema ya pekee ya kumzaa Maria, ambaye alimzaa Mwanao, Yesu Kristo. Kwa maombezi yao, utujalie tupate wokovu ule ulioliahidia taifa lako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.