Generic placeholder image

Julai, 29

MT. MARTA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Twamsifu mwanamke
Huyu ambaye, akiwa
Kajaliwa ujasiri
Wa hali ya juu sana,
Amejipatia sifa
Ambayo haitakoma,
Na mahali huko juu
Kati ya watakatifu.

Ulimwasha kifuani
Upendo mtakatifu
Hata hakulitafuta
Pumziko duniani,
Ila kwa saburi kubwa
Na kwa imani thabiti
Lipita njia nyembamba
Iongozayo kwa Mungu.

Alizuia tamaa
Yo yote isiyofaa
Kwa kujikania sana,
Kiungwana kujinyima;
Kwa sala aliilisha
Roho yake yenye njaa,
Na hivi kaenda kasi
Kwenye furaha za mbingu.

Ee Kristo, Bwana wetu,
Nguvu ya walo na nguvu,
Ambaye peke yako tu
Wafanya mambo makuu;
Kwa maombi ya daima
Yake huyu mwanamke,
Sikia kilio chetu,
Kwa huruma tusikize.

Sifa zote zimwendee
Mungu Baba mwenye enzi,
Sifa zote zikujie
Mwana wake wa milele,
Ambaye twakuabudu
Pamoja na Roho Mungu,
Siku zote na daima,
Milele yote. Amina.

ANT. I: Bwana, mtumishi wako anashangilia, kwa sababu umemwokoa, aleluya.

Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Nilifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu.“

Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!

Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!

Humo ndimo makabila yanafika,/.
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.

Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.

Uombeeni Yerusalemu amani;*
“Wote wakupendao wafanikiwe!

Ukumbini mwako kuwe na amani,*
majumbani mwako kuweko usalama!“

Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
Ee Yerusalemu, nakutakia amani!

Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
ninakuombea upate fanaka!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana, mtumishi wako anashangilia, kwa sababu umemwokoa, aleluya.

ANT. II: Sheria za Mungu katika moyo wa mwanamke mwema, ni kama misingi ya kudumu juu ya mwamba, aleluya.

Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.

Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.

Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu.*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?

Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!

Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.

Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Sheria za Mungu katika moyo wa mwanamke mwema, ni kama misingi ya kudumu juu ya mwamba, aleluya.

ANT. III: Mkono wa Mungu mwenyewe umempa nguvu; atabarikiwa milele, aleluya.

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo

ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mkono wa Mungu mwenyewe umempa nguvu; atabarikiwa milele, aleluya.

SOMO: Rom.8:28-30
Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kufuatana na kusudi lake. Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Basi, Mungu aliwaita wale aliokuwa amewateua; na hao aliowaita, aliwafanya pia wawe na uhusiano mwema naye; na hao aliowafanya wawe na uhusiano mwema naye, aliwashirikisha pia utukufu wake.

KIITIKIZANO
K. Mungu amemchagua yeye. Alimchagua kabla hajazaliwa. (W. Warudie)
K. Alimwingiza akae katika nyumba yake mwenyewe.
W. Alimchagua kabla hajazaliwa.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mungu...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Yesu aliwapenda Marta, Maria na Lazaro, ndugu wa familia moja.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Yesu aliwapenda Marta, Maria na Lazaro, ndugu wa familia moja.

MAOMBI
Kwa njia ya wanawake watakatifu, tumwombe Bwana kwa ajili ya mahitaji yote ya Kanisa lake.
W. Bwana, ulikumbuke Kanisa lako.

Kwa njia ya wafiadini wanawake, ambao walishinda mauti kwa ujasiri usiokoma,
- uliimarishe Kanisa lako wakati wa majaribu. (W.)

Kwa njia ya wanawake walioolewa, ambao waliyastawisha maisha ya jamii ya wanadamu,
- ulitie Kanisa moto mpya wa kuendeleza utume wake. (W.)

Kwa njia ya wajane wote, ambao waliutakatifuza upweke kwa sala na ukarimu,
- ulifanye Kanisa lako liwe ishara dhahiri ya upendo wako kwa ulimwengu mzima. (W.)

Kwa njia ya akina mama wote, ambao waliwaingiza watoto wao katika ufalme wa Mungu, na katika maisha ya kiutu kweli katika jumuiya,
- tunaomba Kanisa lako liwafikishe binadamu kwenye uzima wa milele na wokovu. (W.)

Kwa njia ya akina mama watakatifu wote, ambao wanaishi katika mwanga wa utukufu wako,
- uwajalie waamini marehemu waione furaha milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, Mwanao alikubali kukaribishwa katika nyumba ya Mtakatifu Marta. Kwa sala za Marta, utujalie tuweze kumtumikia Kristo kiaminifu kwa kuwahudumia ndugu zetu, na utukaribishe katika makao yako ya mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.