Generic placeholder image

Agosti 6
KUGEUKA SURA KWA BWANA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana ndiye Mfalme Mkuu wa utukufu; njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Wa kale kuliko ulimwengu,
Kuliko nyota ya asubuhi;
Vya kwanza kabla havijawa,
Wewe Muumba wa vyote upo.

Surayo ni Bwana wa uzima,
Ni Mwanao tokea milele;
Vya kuangamia ahuisha;
Vyote yeye huvipatanisha.

Kristo ulogeuka sura,
Mpendwa twakutumainia;
Tujalie kwa upendo wako
Yale tusiyopata kuona.

Ewe Baba na Mwana na Roho,
Kwa nyoyo zilogeuzwa nawe,
Fahari yako na tuisifu,
Na tuone surayo tukufu.

ANT. I: Leo Yesu Kristo aligeuka sura: uso wake ukang'aa kama jua, na mavazi yake yakawa meupe kama theluji.

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Leo Yesu Kristo aligeuka sura: uso wake ukang'aa kama jua, na mavazi yake yakawa meupe kama theluji.

ANT. II: Leo aligeuka sura, na sauti ya Baba ikamshuhudia; Musa na Eliya walionekana naye wakiwa katika hali ya utukufu, wakazungumza naye juu ya kifo, ambacho kingempata.

WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

ANT. II: Leo aligeuka sura, na sauti ya Baba ikamshuhudia; Musa na Eliya walionekana naye wakiwa katika hali ya utukufu, wakazungumza naye juu ya kifo, ambacho kingempata.

ANT. III: Musa alitangaza Sheria, na Eliya alikuwa nabii: hao wawili walionekana katika utukufu, waking'ara mlimani pamoja na Bwana.

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Musa alitangaza Sheria, na Eliya alikuwa nabii: hao wawili walionekana katika utukufu, waking'ara mlimani pamoja na Bwana.

SOMO: Ufu.21:10,23
Roho akanikumba, naye malaika akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionesha mji mtakatifu, yaani Yerusalemu, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuangazia, maana utukufu wa Mungu huuangazia, na taa yake ni yule Mwana-Kondoo.

KIITIKIZANO
K. Bwana, umemvika taji ya utukufu na heshima, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Ulimweka awe mwangalizi wa kazi za mikono yako.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Sauti ikasikika kutoka katika lile wingu: 'Huyu ni Mwanangu mpenzi, ambaye nimependezwa naye; msikilizeni,' aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Sauti ikasikika kutoka katika lile wingu: 'Huyu ni Mwanangu mpenzi, ambaye nimependezwa naye; msikilizeni,' aleluya.

MAOMBI
Tumwombe Kristo, kwa kuwa yu pamoja na Mungu Baba, na amepewa mamlaka yote, mbinguni na duniani.
W. Bwana, utuwezeshe kuona.

Utusaidie tuweze kufanya kazi vizuri leo:
- uigeuze mioyo yetu kwa uwepo wako. (W.)

Si kila mara tunahisi furaha na nguvu ya uwepo wako:
- tunapokuwa dhaifu na wachovu, utusaidie tuweze kuutazamia kwa matumaini utukufu ujao. (W.)

Uwakumbuke wote wanaoishi katika huzuni na taabu:
- uwapatie mwanga mpya, na matumaini yatokanayo na habari njema. (W.)

Tunakusifu, Bwana, na tunakushukuru kwa ajili ya ukuu wa utukufu wako:
- uwe pamoja nasi tunapoanza kuujenga ulimwengu wako mpya. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Baba, Mwanao wa Pekee alipogeuka sura katika utukufu, ulithibitisha ukweli wa mafumbo ya imani kwa ushuhuda walioutoa manabii Musa na Eliya juu ya Yesu. Hapo ulidokeza jinsi tutakavyokuwa utakapotufanya tuwe wanao kamili. Utujalie, kwa kuisikiliza sauti ya Yesu, tupate kuwa warithi pamoja naye, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.