Generic placeholder image

Agosti 6
KUGEUKA SURA KWA BWANA
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. (Aleluya)

UTENZI
Wa kale kuliko ulimwengu,
Kuliko nyota ya asubuhi;
Vya kwanza kabla havijawa,
Wewe Muumba wa vyote upo.

Surayo ni Bwana wa uzima,
Ni Mwanao tokea milele;
Vya kuangamia ahuisha;
Vyote yeye huvipatanisha.

Kristo ulogeuka sura,
Mpendwa twakutumainia;
Tujalie kwa upendo wako
Yale tusiyopata kuona.

Ewe Baba na Mwana na Roho,
Kwa nyoyo zilogeuzwa nawe,
Fahari yako na tuisifu,
Na tuone surayo tukufu.

ANT. I: Yesu aliwachukua Petro, Yakobo, na Yohane nduguye Yakobo, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu. Huko, wakiwa wanamtazama, Yesu akageuka sura.

Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake (Kor.15:25)

Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,

Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."

Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"

Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Yesu aliwachukua Petro, Yakobo, na Yohane nduguye Yakobo, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu. Huko, wakiwa wanamtazama, Yesu akageuka sura.

ANT. II: Wingu jeupe likawafunika, nao wakasikia sauti ya Baba, ikisema, 'Huyu ni Mwanangu mpenzi, ambaye nimependezwa naye.'

Zab.121 Mungu kinga yetu
Ninatazama huko juu milimani;*
msaada wangu watoka wapi?

Msaada wangu watoka kwa Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.

Hatakuacha uanguke;*
mlinzi wako hasinzii.

Mlinzi wa Israeli*
hasinzii wala halali.

Mungu anakulinda na kukukinga;*
yuko pamoja nawe kukulinda.

Mchana jua halitakuumiza,*
wala mwezi wakati wa usiku.

Mungu anakukinga na majanga yote;*
anayalinda salama maisha yako.

Anakulinda ujapo na uendapo,*
sasa na hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Wingu jeupe likawafunika, nao wakasikia sauti ya Baba, ikisema, 'Huyu ni Mwanangu mpenzi, ambaye nimependezwa naye.'

ANT. III: Walipokuwa wanashuka kutoka mlimani, Yesu akawaonya, 'Msimwambie mtu mambo mliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka wafu,' aleluya.

WIMBO: 1Tim.3:16 Fumbo na utukufu wa Kristo

W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!

Alionekana katika umbo la kibinadamu,*
akathibitishwa na Roho kuwa ni mwadilifu.
W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!

Alionekana na malaika,*
akahubiriwa kati ya mataifa.
W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote.

Aliaminiwa po pote ulimwenguni,*
akachukuliwa juu mbinguni katika utukufu.
W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!

ANT. III: Walipokuwa wanashuka kutoka mlimani, Yesu akawaonya, 'Msimwambie mtu mambo mliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka wafu,' aleluya.

SOMO: Rom.8:16-17
Roho mwenyewe anajiunga na roho zetu, na kuthibitisha kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.

KIITIKIZANO
K. Enzi na nguvu ni vyake, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Heshima na fahari vimo katika makao yake matakatifu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Enzi...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Wanafunzi waliposikia, hofu iliwashika, wakaanguka kifudifudi. Lakini Yesu akawaendea, akawagusa akisema, 'Simameni, msiogope,' aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Wanafunzi waliposikia, hofu iliwashika, wakaanguka kifudifudi. Lakini Yesu akawaendea, akawagusa akisema, 'Simameni, msiogope,' aleluya.

MAOMBI
Siku ya leo tunamwomba Mwana wa Mungu, aliyejidhihirisha kwa rafiki zake akiwa katika utimilifu wa utukufu wake, tukisema:
W. Bwana, utuwezeshe kuona.

Ulibariki Kanisa lako zaidi na zaidi kwa hali yako ya ufufuko:
- ili ulimwengu uweze kuona katika Kanisa ukamilifu wa kazi yako. (W.)

Ulionekana pamoja na Eliya na Musa, ukapokea heshima za hao wawili:
- uuwezeshe ulimwengu kulipokea neno lako, na kuishi kadiri ya amri yako ya mapendo. (W.)

Hata kabla ya mateso yako, wanafunzi wako waliuona utukufu wa ufufuko wako:
- utuwezeshe kuwa tayari kupokea mateso na furaha. (W.)

Uliachana na utukufu wako, ukautangaza utawala wa Mungu, na watu wa taifa lako wakakataa kukupokea:
- utusaidie tuweze kukuona wewe katika maskini na wanaoonewa, na tuweze kuwapenda hao kwa sababu yako. (W.)

Uliwaonesha rafiki zako utukufu wa Mungu aliye hai:
- uwapokee kwako marehemu wote, na uwapatie utukufu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Baba, Mwanao wa Pekee alipogeuka sura katika utukufu, ulithibitisha ukweli wa mafumbo ya imani kwa ushuhuda walioutoa manabii Musa na Eliya juu ya Yesu. Hapo ulidokeza jinsi tutakavyokuwa utakapotufanya tuwe wanao kamili. Utujalie, kwa kuisikiliza sauti ya Yesu, tupate kuwa warithi pamoja naye, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.