Generic placeholder image

Agosti 6
KUGEUKA SURA KWA BWANA
JUMANNE JUMA LA 18 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yesu aligeuka sura akiwa kati ya Musa na Eliya, ili yaliyoandikwa katika Sheria, na yale yaliyosemwa na Manabii, yapate kumshuhudia.

Adhuhuri
Ant.: Bwana Mungu, Mwokozi wetu, ametangaza uzima wa milele kwa njia ya injili yake.

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Wanafunzi waliposikia sauti ya Baba, hofu iliwashika, wakaanguka kifudifudi.

Zab.119:49-56 VII Kuwa na imani na sheria ya Mungu
Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mtumishi wako,*
ahadi ambayo imenipa matumaini.

Hata niwapo taabuni napata kitulizo,*
maana ahadi yako yanipa uhai.

Wenye kiburi hunidharau daima,*
lakini mimi sikiuki sheria yako.

Ninapoyakumbuka maagizo yako ya tangu kale,*
nafarijika, Ee Mungu.

Nashikwa na hasira kali,*
nionapo waovu wakivunja sheria zako.

Nikiwa huku ugenini,*
tenzi zangu ni juu ya amri zako.

Usiku ninakukumbuka, Ee Mungu,*
na kuzingatia sheria zako.

Hii ni baraka kubwa kwangu,*
kwamba nazishika amri zako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.53 Mtu asiyemcha Mungu
Watu wote wametenda dhambi, na wametindikiwa utukufu wa Mungu (Rom.3:23)

Wapumbavu hujisemea: "Hakuna Mungu!"/
Wote wamepotoka, wametenda mambo ya kuchukiza;*
hakuna hata mmoja atendaye jema.

Toka mbinguni Mungu awachungulia wanadamu,/
aone kama kuna yeyote mwenye busara,*
kama kuna mtu yeyote anayemcha Mungu.

Lakini wote wamepotoka,/
wote kwa pamoja wameharibika,*
hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja.

Mungu asema,“Je, hao watendao maovu hawana akili?"*
Wanawamaliza watu wangu,

kama kwamba wanakula mikate;*
tena hawamchi Mungu!"

Hapo, watetemeka kwa hofu,*
hofu ambayo hawajapata kuiona;

maana Mungu ataitawanya mifupa ya adui.*
Hao watashindwa, maana Mungu amewaacha.

Laiti ukombozi wa Israeli*
ungefika kutoka Sion!

Mungu atakapowafanikisha tena watu wake,*
Israeli atafurahi, na Yakobo atashangilia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.54:1-4,6-7 Sala ya kujikinga na maadui
Nabii anaomba ili kwa jina la Bwana aokolewe na uovu wa wale wanaomdhulumu (Kasiani)

Uniokoe, Ee Mungu, kwa jina lako;*
unisalimishe kwa enzi yako.

Uisikie, Ee Mungu, sala yangu;*
uyapokee maneno yangu.

Watu wenye kiburi wananishambulia;/
wakatili wanayawinda maisha yangu,*
watu wasiomjali kamwe Mungu.

Lakini Mungu ni msaada wangu,*
Bwana hutegemeza maisha yangu.

Kwa moyo radhi nitakutolea sadaka;*
nitalisifu jina lako kwa kuwa wewe ni mwema.

Maana umeniokoa katika taabu zangu zote,*
nami nimewaona adui zangu wameshindwa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yesu aligeuka sura akiwa kati ya Musa na Eliya, ili yaliyoandikwa katika Sheria, na yale yaliyosemwa na Manabii, yapate kumshuhudia.

Adhuhuri
Ant.: Bwana Mungu, Mwokozi wetu, ametangaza uzima wa milele kwa njia ya injili yake.

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Wanafunzi waliposikia sauti ya Baba, hofu iliwashika, wakaanguka kifudifudi.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Kut.19:9
BWANA akamwambia Musa: 'Tazama, mimi naja kwako katika wingu zito ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe hata milele."

K. U mzuri kuliko watoto wote wa wanadamu.
W. Midomo yako imeenea uzuri.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Kut.33:9,11
Ikawa Musa alipoingia humo hekaluni, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye BWANA akasema na Musa. BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake.

K. Elekezeni macho yenu kwake, na mtabasamu kwa furaha.
W. Wala msiinamishe tena vichwa vyenu kwa aibu.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 2Kor.3:18
Sisi sote ambao nyuso zetu hazikufunikwa, twaonesha, kama katika kioo, utukufu wa Bwana; na utukufu huo utokao kwa Bwana, ambaye ni Roho, watubadili tufanane zaidi na huo mfano wake kwa utukufu mwingi zaidi.

K. Bwana, wewe ndio chanzo cha uzima.
W. Kwa nuru yako tunaona mwanga.

SALA:
Tuombe: Baba, Mwanao wa Pekee alipogeuka sura katika utukufu, ulithibitisha ukweli wa mafumbo ya imani kwa ushuhuda walioutoa manabii Musa na Eliya juu ya Yesu. Hapo ulidokeza jinsi tutakavyokuwa utakapotufanya tuwe wanao kamili. Utujalie, kwa kuisikiliza sauti ya Yesu, tupate kuwa warithi pamoja naye, anayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.