WAT. LAURENT SHEMASI NA SHAHIDI
MASOMO
SOMO: 2Kor.9:6-10
Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende
kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda
yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi,
mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama
ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, Haki yake yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu
mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza
mazao ya haki yenu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.112:1-2,4,9(K)5
1. Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
(K) Heri atendaye fadhali na kukopesha.
2. Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki. (K)
3. Amekirimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu. (K)
SHANGILIO: Yn.8:12
Aleluya, aleluya!
Yeye anifuataye, asema Bwana, hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya!
INJILI: Yn.12:24-26
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika
nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye
nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata
uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu
atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.