Generic placeholder image

Agosti 15
KUPALIZWA BIKIRA MARIA MBINGUNI
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Njooni, tumwabudu Mfalme wa wafalme: leo Mama yake, Bikira Maria, alipalizwa mbinguni.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Ewe safina takatifu
Iloteuliwa na Mungu
Ni safina ambayo Mungu
Zake neema kaijaza;
Safina imesha tulia
Katika hekalu la Mungu.

Safina tukufu zaidi
Kushinda hata Serafim,
Ni safina ichukuayo
Pendo la kimungu ndanimwe;
Dhambi haikukuchafua,
Mauti hayakukufunga.

E Mama mzazi wa Mungu,
Bikira asiye na doa,
Kwa uzuri wewe wang'aa
Mbinguni wanakutazama;
Taji ya nyota umevaa,
Ndiwe lango la Nuru, Mama.

Mtukufu Baba na Mwana,
Naye Roho Mtakatifu:
Mungu tumtolee sifa
Pamoja na Mama Maria,
Alo Malkia wa mbingu,
Daima milele tusifu.

ANT. I: Umebarikiwa, Ewe Maria, maana kwa njia yako wokovu ulifika ulimwenguni; sasa upo katika utukufu, na unafurahi mbele ya Bwana.

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Umebarikiwa, Ewe Maria, maana kwa njia yako wokovu ulifika ulimwenguni; sasa upo katika utukufu, na unafurahi mbele ya Bwana.

ANT. II: Bikira Maria amekwezwa juu zaidi kuliko makundi ya malaika; waamini wote na wafurahi, na kumtukuza Bwana.

WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

ANT. II: Bikira Maria amekwezwa juu zaidi kuliko makundi ya malaika; waamini wote na wafurahi, na kumtukuza Bwana.

ANT. III: Jina lako limetukuzwa hivi na Bwana, kwamba midomo ya watu haitaacha kamwe kukusifu.

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Jina lako limetukuzwa hivi na Bwana, kwamba midomo ya watu haitaacha kamwe kukusifu.

SOMO: Isa.61:10
Nafurahi sana katika BWANA, nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu amenifunika vazi la haki, kama bibi arusi aliyejipamba kwa vyombo vya dhahabu.

KIITIKIZANO
K. Leo Bikira Maria alipalizwa mbinguni. (W. Warudie)
K. Milele atashiriki ushindi wa Kristo.
W. Alipalizwa leo mbinguni.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Leo Bikira...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Utazame uzuri wa binti Yerusalemu, aliyepaa mbinguni kama jua lichomozalo alfajiri.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Utazame uzuri wa binti Yerusalemu, aliyepaa mbinguni kama jua lichomozalo alfajiri.

MAOMBI
Tutangaze ukuu wa Mwokozi wetu, aliyechagua kuzaliwa na Bikira Maria. Tukitumaini kwamba atatusikiliza, tuombe:
W. Usikilize maombezi ya mama yako.

Neno wa Milele, ulijipatia makao duniani katika mwili wa Mama Maria;
- ukae nasi milele katika mioyo yetu, isiyo na dhambi. (W.)

Kristo, Mkombozi wetu, ulimfanya Bikira Maria awe makao yako, na awe hekalu la Roho;
- utufanye tuwe makao ya Roho wako. (W.)

Neno wa Milele, ulimfundisha mama yako Maria kuchagua kilicho bora kabisa;
- utuwezeshe kufuata mfano wake, na kutafuta kwa bidii chakula kiletacho uzima wa milele. (W.)

Mfalme wa wafalme, ulimpaliza Maria mbinguni, ili awe pamoja nawe, mwili na roho;
- utuwezeshe kuyatafuta yaliyo ya juu, na kuyaelekeza maisha yetu kwako. (W.)

Mfalme wa mbingu na dunia, ulimketisha Mama Maria karibu nawe, ili awe malkia, atawale milele;
- utujalie furaha ya kushiriki utukufu wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, umempaliza, mwili na roho, Bikira Maria asiye na doa, mama ya Mwanao, na kumwingiza katika utukufu wa mbinguni. Uielekeze mioyo yetu mbinguni, ili, pamoja naye, tuweze kushiriki utukufu wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.